Mathayo 24: 24 “Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule".
Manabii wa uongo wa agano la kale ni kivuli cha manabii wa uongo katika agano jipya. Mfano wa yale yaliyokuwa wanayafanya agano lake ndio hayo hayo wanayoyafanya sasa katika agano jipya.
Waliwapoteza wale waliokuwa wachanga kiimani kadhalika walifanikiwa pia kuwapoteza hata baadhi ya wale waliokuwa wamesimama kiimani. Mfano wa manabii hao tunamwona mtu kama Hanania aliyetokea kipindi cha wafalme, wakati ambapo Mungu alisema Yerusalemu utateketezwa na watu wake kupelekwa utumwani Babeli, yeye alisimama kwa ujasiri mkubwa mbele ya mfalme na mbele ya makuhani wa Bwana na mbele ya watu wote na kusema Bwana anasema hivi haitatimia miaka miwili mpaka vile vyombo na vitu vyote Nebukadreza alivyovichukua kwenye ile awamu ya kwanza na kuvipeleka Babeli kurudishwa tena Israeli,.. Lakini kama tunavyosoma kumbe Mungu hakumtuma na unajua kwa namna ya kawaida mtu akitoa maneno ya faraja hata kama yawe ni ya uongo kiasi gani atapendwa tu!. Na ndio maana tunakuja kuona nabii kama Yeremia alipokuja kusema kuwa Yerusalemu utateketezwa na watu wake kuchukuliwa mateka alionekana kama ni mpinga-kristo, asiyeutakia mema Yerusalemu mji wa Mungu, hivyo mfalme na wale watu wakaamuru kwamba afungwe, katika vifungo vya mateso. Habari hizo tunazisoma katika kitabu cha Yeremia 28.
Kadhalika Walikuwepo na manabii wengine 400 enzi hizo hizo za wafalme wa Israeli waliokuwa wakimtabiria mfalme Ahabu siku zote, lakini ilipofika wakati ambapo Mungu amekusudia kuleta jambo baya juu ya mfalme Ahabu kutokana na maovu yake, ndipo likazuka jopo kubwa la manabii wa uongo wakaanza kumtabiria mfalme habari za kufanikiwa kwake atakapokwenda vitani. Lakini kulikuwa na nabii mmoja aliyeitwa Mikaya yeye hakupenda kusimamia upande wowote, lakini yeye kwa uaminifu kabisa alimwomba Mungu na kuuliza habari za mfalme Ahabu na ndipo Mungu akamwambia ni lazima Ahabu afe atakapokwenda vitani, lakini kwa kuwa mfalme aliona ni manabii wengi wanaomtabiria mafanikio yake zaidi ya uharibifu wake, na kwasababu yeye mwenyewe siku zote anapenda mambo ya faraja tu! hivyo akaamua kuwasikiliza wale wengi na kwenda vitani na kama tunavyosoma alipokwenda tu alikufa.(2Nyakati 18).
Sasa hawa wote ni mifano wa manabii wachache ambao hata sasa wapo kwenye agano jipya. Kadhalika lipo kundi lingine la manabii wa uongo lilikuwa kwenye agano la kale, Na hilo ndilo libaya zaidi kwasababu linatumika mahususi kuwaangusha wale wanaoonekana kusimama katika imani, hilo linaweza kuwaangusha hata walio manabii wa ukweli, na mfano wa kundi hilo tunaweza kulisoma habari yake katika kitabu cha 1Wafalme 13
Embu tusome pamoja na Bwana atatusaidia kupata kitu hapo:
1Wafalme 13:1-321 Na tazama, akatoka mtu wa Mungu katika Yuda kwa neno la Bwana, akafika Betheli. Naye Yeroboamu alikuwa akisimama penye madhabahu, afukize uvumba.2 Basi mtu huyo akapiga kelele juu ya madhabahu, kwa neno la Bwana akasema, Ee madhabahu, madhabahu, Bwana asema hivi, Angalia, mtoto atazaliwa katika nyumba ya Daudi, jina lake Yosia; na juu yako atawachinja makuhani wa mahali pa juu, wanaofukiza uvumba juu yako, na mifupa ya watu itateketezwa juu yako.3 Akatoa ishara siku ile ile, akasema, Hii ndiyo ishara aliyoinena Bwana, Tazama, madhabahu itapasuka, na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.4 Ikawa, mfalme Yeroboamu alipoyasikia maneno ya yule mtu wa Mungu, alipopiga kelele juu ya madhabahu huko Betheli, alinyosha mkono wake pale madhabahuni, akasema, Mkamateni. Basi ule mkono wake aliounyosha ukakatika, wala hakuweza kuurudisha kwake tena.5 Madhabahu ikapasuka, majivu ya madhabahuni yakamwagika, sawasawa na ishara aliyoitoa mtu wa Mungu kwa neno la Bwana.6 Mfalme akajibu, akamwambia yule mtu wa Mungu, Umsihi sasa Bwana, Mungu wako, ukaniombee, ili nirudishiwe mkono wangu tena. Yule mtu wa Mungu akamwomba Bwana mkono wa mfalme ukarudishwa tena, ukawa kama ulivyokuwa kwanza.7 Mfalme akamwambia mtu wa Mungu, Karibu nyumbani kwangu ujiburudishe, nami nitakupa thawabu.8 Mtu wa Mungu akamwambia mfalme, Ujaponipa nusu ya nyumba yako, sitaingia pamoja nawe, wala sitakula chakula, wala sitakunywa maji mahali hapa;9 maana ndivyo nilivyoagizwa kwa neno la Bwana, kusema, Usile chakula cho chote wala usinywe maji, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.10 Basi akaenda zake kwa njia nyingine, wala hakurudi kwa njia ile aliyoijia Betheli.11 Basi nabii mmoja mzee alikuwa akikaa katika Betheli; na wanawe wakamwendea wakamwambia kila neno alilolitenda yule mtu wa Mungu siku ile katika Betheli; na maneno aliyomwambia mfalme, hayo nayo walimwambia baba yao.12 Baba yao akawaambia, Amekwenda zake kwa njia ipi? Kwa maana wanawe walikuwa wameiona njia ile aliyoiendea yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda.13 Akawaambia wanawe, Nitandikieni punda. Wakamtandikia punda, naye akampanda.14 Akamfuata mtu wa Mungu, akamkuta ameketi chini ya mwaloni, akamwambia, Je! Wewe ndiwe yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda? Akamwambia, Mimi ndiye.15 Akamwambia, Karibu kwangu nyumbani, ule chakula.16 Naye akamwambia, Siwezi kurudi pamoja nawe, wala kuingia pamoja nawe; wala sili chakula wala sinywi maji pamoja nawe hapa;17 kwani nimeambiwa kwa neno la Bwana, Usile chakula wala usinywe maji huko, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.18 Akamwambia, Mimi nami ni nabii kama wewe, na malaika akaniambia kwa neno la Bwana, kusema, Mrudishe pamoja nawe nyumbani kwako, ale chakula, akanywe maji. Lakini alisema uongo.19 Basi mtu yule akarudi pamoja naye, akala chakula, akanywa maji nyumbani mwake.20 Hata ikawa, walipokuwa wameketi mezani, neno la Bwana likamjia nabii yule aliyemrudisha;21 akamlilia yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda, akinena, Bwana asema hivi, Kwa sababu umeiasi kauli ya Bwana, wala hukuishika amri ile aliyokuamuru Bwana, Mungu wako,22 bali umerudi, ukala chakula ukanywa maji, hapo alipokuambia, Usile chakula, wala usinywe maji; maiti yako haitaliingia kaburi la baba zako.23 Basi ikawa, alipokwisha kula chakula na kunywa maji, yule nabii aliyemrudisha akamtandikia punda.24 Na alipokuwa amekwenda zake, simba alimkuta njiani, akamwua. Maiti yake ikatupwa njiani, na yule punda akasimama karibu naye; na yule simba naye akasimama karibu na maiti.25 Na tazama, watu wakapita, wakauona mzoga umetupwa njiani, na yule simba akisimama karibu na mzoga, wakaenda, wakatoa habari katika mji ule alimokaa yule nabii mzee.26 Na yule nabii aliyemrudisha njiani alipopata habari, akasema; Ndiye yule mtu wa Mungu, aliyeiasi kauli ya Bwana; kwa hiyo Bwana amempambanisha na simba, simba akamrarua, akamwua, sawasawa na neno la Bwana alilomwambia.27 Akawaambia wanawe, akasema, Nitandikieni punda. Wakamtandikia.28 Akaenda, akamwona yule maiti ametupwa njiani, na punda na simba wamesimama karibu na maiti; yule simba alikuwa hakumla maiti, wala hakumrarua punda.29 Nabii yule akamtwaa maiti wa yule mtu wa Mungu, akamweka juu ya punda wake, akamrudisha; yule nabii mzee akaenda mjini mwake, kukaa matanga, na kumzika.30 Akamweka maiti katika kaburi lake mwenyewe; wakamlilia, wakisema, Aa! Ndugu yangu!31 Hata ikawa, alipokwisha kumzika, akawaambia wanawe, akasema, Nikifa mimi, nizikeni katika kaburi hili alimozikwa yule mtu wa Mungu; iwekeni mifupa yangu kando ya mifupa yake.32 Kwa maana neno hilo alilolia juu ya madhabahu katika Betheli, kwa neno la Bwana, na juu ya nyumba zote za mahali pa juu zilizo katika miji ya Samaria, hakika litatimizwa.Amen.
Ukifuatilia utaona huyu mtu wa Mungu, alikuwa amethibitika kabisa katika Imani kiasi kwamba hata mfalme Yerobohamu mwenyewe licha ya utajiri wake na fahari yake kuwa nyingi hakuweza kumshawishi kukaa na kuyaasi maagizo ya Mungu. Wala hakukuwa na mtu yeyote njiani aliyeweza kumshawishi ayatupilie mbali maagizo ya Mungu aliyompa. Lakini alipofika mbali kidogo na kukaribia kuimaliza safari yake, ndipo akazuka mmoja wa wale manabii wa uongo wale ambao kazi yao siku zote ni KUTAMKA MANENO YA FARAJA kinyume na maagizo ya Mungu.
Embu fikiria huyu mtu wa Mungu katika safari yake yote ya kuukatiza mji, bila kula wala kunywa, jua kali, uchovu mwingi, ni kweli angetamani hata apate mahali pa kustarehe kwa muda mfupi ili ale na kunywa apate nguvu kisha baada hata ya siku moja au mbili aende zake nyumbani, lakini Mungu hakuwambia afanye hivyo, Mungu hakutaka mtumishi wake aliyemtia mafuta mwaminifu akae au ashirikiane na watu waovu wanaoishi kwenye mji uliojaa sanamu uliojaa sanamu na machukizo. Mji uliojaa manabii vuguvugu, wanaopenda kutabiri mambo ya amani tu, siku zote, wanaopenda kutabiri mambo ya kuwafurahisha watu, yale mengine ya hukumu hawataki kuyazungumza. Lakini huyu mtu wa Mungu hakuisikia sauti ya Bwana ndipo nabii huyu mzee wa uongo ambaye kazi yake ni kutabiri mambo ya faraja akaja kumletea habari kwamba Bwana amemwambia arudi kwake ale, anywe..Kumbe hajui kuwa anakwenda kuiponza roho yake mwenyewe. Na mwisho wa siku kama tunavyosoma hakufika mbali simba akamuua.
Ndugu Hizi ni nyakati mbaya zile zilizobiriwa kuwa watatokea manabii wa uongo wapate kuwapoteza hata yamkini walio wateule. Inawezakana ikawa wewe ni mteule wa Mungu, inaweza ikawa hata wewe ni mtumishi mwaminifu wa Mungu na unatembea katika njia zilizonyooka za Yesu Kristo, mfano wa huyu mtu wa Mungu tuliyesoma habari zake. Lakini kumbuka dunia ya sasa inapumbaza sana, na wanaoipumbaza ni manabii wa uongo, hao ambao kazi yao kubwa ni kutabiri mambo ya Baraka tu, mambo malaini tu, mambo ya matumaini tu, kana kwamba Mungu wakati wote anapendezwa na dunia hii ya sasa iliyojaa dhuluma na uchafu kuliko hata ile ya sodoma na Gomora.
Hivyo kwa kuwa husikii tena ukikemewa dhambi au husikii tena habari za dhiki kuu ambayo inakaribia kuikumba hii dunia siku sio nyingi, kama ulivyokuwa unasikia hapo zamani, wewe unastarehe na kulegeza kamba zako za wokovu, na kuwa vuguvugu. Kwa kuwa husikii tena manabii hao wakizungumzia juu ya siku za mwisho wewe unaona kumbe mwisho bado sana, na wala uharibifu hautaikumba dunia leo wala kesho. Kwa kuwa hawagusii tena uvaaji wako, angali wewe hapo mwanzo ulikuwa ni mwanamke mtakatifu vimini huvai wala suruali, lakini sasa unaona watiwa mafuta wa Bwana hawakemei tena hivyo vitu wanakwambia vyote ni sawa na wewe unasikiliza uongo wao unaanza kuvaa vuguvugu tu kama wanawake wa kidunia. Hujui kuwa unachukuliwa na wimbi hilo la manabii wa uongo kukupoteza wewe. Uende kuzimu.
Ndugu usitazame ni jinsi gani wanaona maono ambayo ni sahihi kabisa, ni kweli hata wale wa agano la kale walikuwa vivyo hivyo, walikuwa wanaona maono ya ukweli na ndio maaana waliaminiwa na watu pamoja na wafalme kirahisi, lakini linapokuja suala la kutabiri juu ya uharibifu na hukumu za Mungu, na kiama hapo ndipo utakapoweza kuyatenga magugu na ngano. Kwasababu hilo kundi lingine halipendi kutabiri juu ya hayo, lenyewe ni maneno ya faraja tu siku zote, Unamwona huyu Nabii, aliyempotosha Nabii mwenzake aliwe na Simba alichofanya?? Baada ya kumfariji na kumdanganya kwamba Bwana kamwambia arudi ale pamoja na yeye, alijua kabisa Bwana hakumwambia lakini kamdanganya makusudi…
Yeremia 14: 14 “Ndipo Bwana akaniambia, Hao manabii wanatabiri uongo kwa jina langu mimi; mimi sikuwatuma, wala sikuwaamuru, wala sikusema nao; wanawapeni unabii wa maono ya uongo, na uaguzi, na neno la ubatili,” na hadaa ya mioyo yao. 15 Basi, kwa hiyo Bwana asema hivi, Kwa habari za manabii wanaotabiri kwa jina langu, wala mimi sikuwatuma, LAKINI HUSEMA, UPANGA NA NJAA HAVITAINGIA KATIKA NCHI HII; Kwa upanga na njaa manabii hao wataangamizwa. 16 Na watu hao, waliopewa unabii na wao, watatupwa nje katika njia kuu za Yerusalemu kwa sababu ya upanga na njaa; wala hawatakuwa na mtu wa kuwazika, wao na wake zao, na wana wao, na binti zao; maana nitamwaga uovu wao wenyewe juu yao”.
Unaona?. Huu si wakati wa kuziamini kila roho zinazokutakia mafanikio tu, na wala hazijali hatma ya maisha yako baada ya kifo, zichunguze sana, leo zitakutabiria utajifungua mapacha, kesho zitakutabiria utajenga jumba, mwezi ujao zitakutabiria faraja za ajabu, lakini hazitakutabiria madhara ya dhambi baada ya kifo, hazitakutabiria madhara ya sanamu ndani ya moyo wako, hazitakutabiria Neno la Yesu linalosema “ukiwa vuguvugu nitakutapika” Biblia inasema mbingu na nchi zitapita lakini maneno ya Mungu hayatapita kamwe, Bwana alisema dunia itaangamizwa, ni kweli itaangamizwa, alisema ufalme wa mbinguni umekaribia ni kweli umekaribia, alisema kutakuwa na dhiki kuu, ni kweli dhiki kuu lazima ije, alisema yupo mlangoni kurudi, ni kweli yupo mlangoni, alisema tujiepushe na hichi kizazi cha ukaidi kilichopotoka, na alisea pia “hakuna mtu atakayemwona yeye asipokuwa mtakatifu Waebrabia 12:14” Je! wewe leo umejiwekaje?. Ni matumaini yangu utaanza kuufanya wito wako na uteule wako imara kuanzia sasa, na kuacha kujitumainisha na mafundisho ya faraja ya hao wanabii wa uongo ambao wapo wengi duniani. Na kuanza pia kutazama siku za vilio ambazo nazo zinakuja mbeleni.
Bwana akubariki sana.
Tafadhali "Share" ujumbe huu kwa wengine na Bwana atakubariki.
No comments:
Post a Comment