"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, December 10, 2018

YESU MPONYAJI.

Zamani nilipokuwa mdogo nilikuwa ninasikia Yesu ni mponyaji! Yesu ni mponyaji! Lakini sikuwahi kufikiria kama angeweza kuja kuniponya mtu kama mimi. Nakumbuka ilikuwa ni mwaka 2004, siku moja nilipokaa na kufungua redio mida ya usiku mtumishi mmoja alikuwa anahubiri, na baada ya kumaliza mahubiri yake alisema ikiwa unaumwa na unataka uponyaji shika sehemu unayoumwa nami nitakuombea. Basi mimi kwa wakati huo nilikuwa ninasumbuliwa na sikio kwa muda mrefu, sikio lilikuwa linajaa mawimbi kama upepo unaovuma hivyo lilikuwa linanifanya nihisi maumivu mara kwa mara na kukosa raha. Lakini niliposikia yule mtumishi anasema shika mahali unapoumwa, ndipo na mimi nikashika sikio langu, nilifanya kama najaribu tu hivi nione kama nitaponywa sikuwahi kujua kama Yesu anaweza akawa karibu na mtu kiasi hicho.

Lakini cha ajabu alipomaliza kuomba, nilihisi kitu kama moto kimeshuka kwenye sikio, ukadumu kama kwa sekunde chache tu, kisha ukaisha, nikadhani labda utakuwa ni upepo wa joto umepitia tu, lakini niliposhika na kuweka kidole changu kwenye tundu la sikio na kutoa sikuhisi wimbi lolote wala maumivu yoyote kitu ambacho hapo kabla nilikuwa nikifanya hivyo ninahisi maumivu makali, nilipofanya kwa nguvu tena sikusikia chochote lilikuwa zima kama tu sikio lingine lilivyo kana kwamba halikuwahi kuwa na matatizo. Mpaka sasa ni miaka 14 imeshapita sifahamu tatizo lolote la masikio.Ndipo kuanzia huo wakati nikaanza kumtazama Kristo kwa jicho lingine sikujua kwamba kumbe anaweza kuwa karibu na mimi kiasi hicho..Na sio hilo tu alishawahi kuniponya namna hiyo hiyo mara kadhaa mbele.

Nimeandika huu ushuhuda wangu mwenyewe kukutia moyo wewe ambaye unayepitia katika hali za magonjwa na umekata tamaa kuona kuwa hakuna mtu yoyote anayeweza akaijali hali yako unayopitia sasa. Ndugu unaweza ukawa unaumwa kiasi cha kufa, unaweza ukawa sasahivi upo na ugonjwa uliokusumbua kwa muda mrefu, ambao umekugharimu pesa nyingi kutibiwa lakini haikuwezekana, bado tu unazidi kuwa katika hali ya kukosa matumaini, Unaweza ukasema Yesu hayajui matatizo yako, ni jinsi gani unavyopitia maumivu. Lakini nataka nikuambie Kama kuwa mgonjwa basi Kristo ilimgharimu awe mgonjwa zaidi yako ili wewe uwe mzima, kama ni kuwa mauti uti, basi Kristo alikuwa mauti uti mara nyingi zaidi yako kwa ajili yako ili kusudi kwamba aweze kuirudisha afya yako.

Kama ulikuwa na huzuni, Kristo alikuwa na huzuni kiasi cha kufa, Pengine Unasikia maumivu makali kutokana na majeraha makubwa yaliyo katika mwili wako, basi jua tu Kristo alipata maumivu ya namna yake mfano wake hakuna mwanadamu anayeweza akayapatia leo, ili kusudi kwamba wewe uwe mzima.

Hivyo usidhani kuwa YESU hajui unachokipitia, anafahamu sana kwasababu na yeye pia alishayapitia embu fikiria yale mapigo aliyokuwa anayapata siku ile, makovu, miiba kupenyezwa kwenye kichwa chake na kupondwa kwa fimbo, mijeledi ya visu 39, misumari mikononi na miguuni, na bado misumari hiyo hiyo ndiyo aliyoitegemea imning’inize msalabani, ni taabu kiasi gani mtu anaweza kupata, unategemea vipi mtu kama huyo asipatwe na mchanganyiko wa maumivu ya magonjwa unayoyajua wewe leo, alipata HOMA kali zaidi ya mtu yeyote aliyepata hapa duniani, aliugua, alikuwa mauti uti kwasasa tunaweza kusema hali aliyokuwepo Bwana Yesu ni zaidi ya mtu aliyeko ICU leo, mwili wote ulivimba hata usiweze kumtambua tena kwa ajili ya mapigo yale, wewe leo ugonjwa ulionao hauwezi kufikia hatua ya kuteseka kaisi hicho, lakini yeye alipata ugonjwa huo mkuu kwa ajili yako. Hivyo ndugu usiwe na hofu yeye BWANA anafahamu vizuri hali unayopitia, hauhitaji kumwadithia anaijua hali yako.
   
Sehemu mojawapo ya huduma iliyomleta Bwana duniani na aliyotiwa mafuta kwayo ndio hiyo ya kushughulika na madhaifu yetu.
Mathayo 8:14 “Hata Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwe wa Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani hawezi homa.
15 Akamgusa mkono, homa ikamwacha; naye akaondoka, akawatumikia.
16 Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya WOTE waliokuwa hawawezi,
17 ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, MWENYEWE ALIUTWAA UDHAIFU WETU, NA KUYACHUKUA MAGONJWA YETU.”
Unaona hapo?, YESU hakumponya mmoja au wawili, au watatu tu basi, hapana biblia inasema aliwaponya WOTE waliomwendea.Hivyo usiogope ikiwa ugonjwa ulionao hauponyeki, iwe ni cancer, iwe ni kisukari, iwe ni ukimwi, wowote ule, Usiogope unachopaswa kufanya ni kumkabidhi tu Kristo huo ugonjwa aushughulikie, wala hauhitaji mtumishi aje kukuwekea mikono, hata sauti hii unayoisikia inatosha kuinyanyua Imani yako na kupokea uponyaji wako. Unachopaswa kufanya ni mwamini tu YESU, na kama hujamkabidhi maisha yako, mkabidhi leo. kisha wewe mwenyewe zungumza naye mwambie unataka UPONE. Kisha kuanzia huo wakati anza kumshukuru kwasababu alishakusikia..usirudie rudie kumwambia wewe mshukuru tu! kwasababu yeye sio kama sisi wanadamu, jambo moja lazima tuambiwe mara sita sita ndipo tuelewe.

Anza pia kupenda kulitafakari Neno la Mungu kuanzia huo wakai, soma biblia shuhuda zote za matendo makuu ya Yesu aliyokuwa anawafanyia watu, pitia injili zote nne, hiyo itakusaidia kuiimarisha imani yako kwa YESU, tatizo linakuja ni pale mtu anamwomba leo Bwana YESU amponye, halafu anaendelea na mambo yake mengine, hana muda tena na habari za Mungu.

Unajua tatizo linakuja wapi kwa mtu wa namna hiyo?. Ni pale hata mfano Mungu akimponya ugonjwa wake, hatajua kuwa ni Mungu ndiye aliyemponya, hivyo hata uponyaji wake atakuwa na mashaka nao akidhani pengine ni Mungu au pengine kapona tu yeye mwenyewe, ataendelea kuwa hivyo kwasababu hakuwa na muda wala na Imani kwa aliyemtarajia amponye. Hivyo watu wa namna hiyo kupokea uponyaji wao inakuwa ni ngumu sana kwasababu ni rahisi sana kuingiwa na mashaka, na Imani ikishaingiwa na mashaka huwa haizai.

Lakini ukiwa ni mtafakariji mzuri wa Neno la Mungu, inakuwa ni ulinzi kwako, pale IMANI yako inapotaka kuyumba kidogo unakumbuka maandiko, au unayatafakari maandiko. Na mwisho wa siku Uponyaji wako unakufika.

Hivyo ndugu, YESU ni muweza mtwike yeye fadhaa zako kwasababu yeye anajishughulisha sana na mambo yako na kama haujamkabidhi maisha yako, fanya hivyo leo maadamu muda upo, kwasababu yeye anahitaji kuiponya roho yako zaidi ya mwili. Kwasababu anaweza akakuponya ukimwi leo ukawa mzima, lakini kesho ukaishia katika ziwa la moto, sasa hiyo inayo faida gani. Ni heri uponywe vyote, na ndicho anachokitaka yeye, Kwahiyo tubu ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako, ili ufanyike mtoto wa Mungu kwanza, Kisha hayo mengine atakuzidishia.

Ubarikiwe sana.

Pia washirikishe wengine habari za Uzima ulio katika damu ya YESU popote pale ulipo.

No comments:

Post a Comment