"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, January 12, 2019

IELEWE SAUTI YA MUNGU.

Shalom Mwana wa Mungu, karibu tujifunze kwa pamoja Neno la Mungu, na Leo tutajifunza moja ya njia ya kuielewa sauti ya Mungu inapozungumza nasi.

Kwanza ni muhimu kufahamu kuwa Mungu ni Mkuu, Upeo wake na mawazo yake yapo mbali sana, mahali ambapo hatuwezi kuyafikia…Kwahiyo kwa ukuu wake namna hiyo tunajua kabisa hakuna mwanadamu yoyote atakayeweza kumwelewa kama akitaka kuzungumza na sisi katika ukuu wake wote.

Kwahiyo kwasababu yeye ni mkuu na katuumba sisi watu wake katika hali ya udogo, hawezi akazungumza na sisi kwa lugha zake, bali atazungumza na sisi kwa lugha nyepesi na inayoeleweka, ili tuweze kumwelewa. Hata na sisi pia huwa tunapokuwa na mifugo yetu, hatuwezi kuzungumza nayo kama tunavyozungumza na wanadamu wenzetu, kama tukifanya hivyo ni wazi kuwa mifugo haitatuelewa ni sharti tutumie vitendo au sauti watakazozielewa kama miluzi au kutumia ishara fulani.
Kwasababu hiyo basi Mungu naye anazungumza na sisi kwa lugha za kibinadamu, kwa sauti za kibinadamu, kwa lafudhi za kibinadamu..Kwasababu mfano akizungumza na sisi kwa lugha za malaika hatutamwelewa, kwa lafudhi za kimbinguni hatutamsikia. Na endapo angejishusha zaidi na kuzungumza na sisi kwa ngurumo na radi na umeme, ndio kabisa tusingemwelewa, tungeishia kumwogopa badala ya kumpenda n.k.

Na ndio maana tunasoma Katika kitabu cha 1Samweli 3, Bwana akizungumza na Samweli kwa sauti inayofanana na ya Eli. Tunaona hakumwita kwa sauti ya mawimbi au radi, bali kwa sauti kama ya Baba yake wa kiroho. Mpaka Samweli akadhani ni Eli ndiye anayemwita. Na tunaona hakuishia kumwita mara moja bali alimwita kwa sauti ile ile mara nne.
1 Samweli 3:1-8 “Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya Eli. Na neno la Bwana lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri.
2 Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona),
3 na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu;
4 basi, wakati huo Bwana akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa.
5 Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena.
6 Bwana akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena.
7 Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake.
8 Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto.”
Umeona hapo? Ni mara nyingi tumekuwa tukitafuta kuisikia sauti ya Mungu kwa namna nyingi, lakini ni muhimu kujua kwamba sauti ya Mungu haipo mbinguni, sauti ya Mungu ipo pamoja nawe pale ulipo. Ipo karibu sana na wewe, ipo hapo ulipo moyoni mwako au pembeni kidogo chumba cha pili kinachofuata cha jirani yako aliye mkristo.

Kumbukumbu 30: 11 “Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali.
12 Si mbinguni, hata useme, Ni nani atakayetupandia mbinguni akatuletee, aje atuambie tusikie, tupate kuyafanya?
13 Wala si ng'ambo ya pili ya bahari, hata useme, Ni nani atakayetuvukia bahari, akatuletee, aje atuambie, tusikie, tupate kuyafanya?
14 Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya”.

Sauti ya Mungu haifanani na ya Malaika kwetu sisi, hapana sauti ya Mungu inafanana na sauti zetu sisi wanadamu, kiasi kwamba anapozungumza na sisi tusipokuwa makini tunaweza kudhani kuwa tunazungumza na wanadamu. Samweli pengine alifundishwa kuwa Mungu huwa anazungumza kutoka mbinguni, na akizungumza basi bahari na kuzimu, na mbingu na nchi zinatetemeka..Hiyo ni kweli, lakini hapa tunasoma sauti ya Mungu ilipoita ilisikika kama inatoka chumba kinachofuata, na ilifanana sana na sauti ya Baba yake wa kiroho aliyekuwa anamfundisha njia za wokovu.

Ndugu/Dada unayesoma ujumbe huu, mahali popote ulipo sauti ya Mungu ipo inazungumza na wewe, unaposikiliza Mahubiri au Mafundisho yanayohubiriwa na mtu fulani, yanayohusiana na wokovu wako, hiyo ni sauti ya Mungu inazungumza nawe..usijaribu hata kidogo kufikiri ni yule mtu ndiye anayezungumza na wewe la! Ni Mungu ndiye anayezungumza nawe, katika sauti ya Yule mtu.

Mahali popote usikiapo Mahubiri ya kutubu dhambi, ni sauti ya Mungu ikikukumbusha kile alichokiandika katika Neno lake (Biblia takatifu), kwamba wenye dhambi wote hawataurithi ufalme wa mbinguni, Mahali popote usikiapo habari za maonyo yahusuyo hukumu inayokuja hiyo ni sauti ya Mungu ikikukumbusha kile kilichoandikwa katika Biblia yake takatifu (juu ya hukumu itakayoijia ulimwengu mzima).
Kwahiyo usikiapo hiyo sauti usimkimbilie yule mtu anayekuhubiria na kudhani ni yeye ndiye anayezungumza na wewe kama Samweli alivyomkimbilia Eli, Kwasababu ukifanya hivyo basi anaacha kwanza kuzungumza na wewe, badala yake mkimbilie Mungu anayezungumza nawe moyoni mwako pale ulipo, Itii sauti yake na mgeukie yeye, Na kumwambia Bwana “ Zidi zungumza nami kwa kuwa mtumishi wako anakusikia, mwambie nibadilishe kwa kuwa mtumishi wako anakusikia” acha kuishi maisha ya dhambi kuanzi wakati huo na kuendelea, acha maisha ya ulevi, maisha ya uchawi, ya usengenyaji, ya uasherati,ya utazamaji pornography, ya ufanyaji masturbation, ya wizi,ya kamari, ya utukanaji, ya ulaji rushwa n.k n.K. Mtii Mungu na kuanza kuishi maisha yanayokubalika mbele zake, kwa kuacha kuvaa nguo zisizofaa; kama vimini, suruali,nguo zinazobana na upakaji wanja na lipstick..Jitenge na hivyo vyote kwasababu ndivyo vinavyowapeleka mamilioni ya watu kuzimu. Na sauti ya Bwana inakuonya leo uviache hivyo vyote.

Bwana Yesu alisema katika Yohana 3:3 “…Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.”. Unazaliwa mara ya pili kwa kumwamini Yesu Kristo kwamba alitumwa na Mungu, akaishi duniani maisha matakatifu yanayokubalika na Mungu akampendeza Mungu, akakushuhudiwa kuwa ndiye pekee ampendezaye Mungu, akasulibiwa kwa ajili ya dhambi zetu, akafa, akazikwa na siku ya tatu akafufuka, akapaa mbinguni, naye amewekwa kuwa mpatanishi wa sisi na Mungu na hakuna mwingine, na atarudi tena kuja kulinyakua kanisa lake kwenda nalo mbinguni.
Baada ya kumwamini hivyo..Hatua inayofuata ni kukusudia na kudhamiria kuacha maisha ya dhambi uliyokuwa unaishi huko nyuma maisha yote ya usengenyaji, maisha yote ya ulevi na uvutaji sigara, maisha yote ya kikahaba na utoaji mimba, maisha yote ya ulaji rushwa, utapeli na uwizi, maisha yote ya uashetari na uvaaji mbaya..Unasema kuanzia leo na kuendelea mimi ni hayo maisha ndio basii..!!

Ukishakusudia kufanya hivyo kwa vitendo na sio kwa mdomo tu, moja kwa moja bila kukawia nenda katafute ubatizo sahihi, huo utakuwa ni kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako,kulingana na Matendo 2:38, na kumbuka ubatizo sahihi sio wa kunyunyiziwa, bali ni wa maji mengi, wakuzamishwa mwili wote na ni kwa jina la Yesu Kristo.

Baada ya kufuata hatua hizo mbili rahisi, utakuwa umepiga hatua moja kubwa na ya muhimu katika maisha yako, ambayo hutajutia kamwe. Na baada ya hapo Bwana atayafanya yaliyosalia kwa kukupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu atakayekuwezesha kuishi maisha matakatifu na kukutia katika kuijua na kuielewa kweli yote ya Neno lake (Yaani Biblia takatifu). Nawe utakuwa umezaliwa mara ya pili, Mrithi wa Baraka za Mungu.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.
Mungu akubariki.

No comments:

Post a Comment