"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, March 14, 2019

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 57


SWALI 1: Mimi ninaye mchumba wangu ambaye tayari tumeshaweka mipango ya kuja kuoana baada ya mwezi mmoja,na mpaka sasa mipinga yote ipo tayari kilichobaki ni ndoa tu. Swali ni je! tukifanya sasa tendo la ndoa tunafanya dhambi mbele za Mungu?.
JIBU: Mpaka limeitwa tendo la ndoa, ni wazi kabisa linapaswa lifanyike ndani ya ndoa, na ndio maana halijaitwa tendo la uchumba au tendo la urafiki, haiwezekani mtu kurukia kula kokwa kabla hata hajayamenya maganda, ili kulifikia kokwa zipo kanuni za kufuata ambazo hizo hazikwepeki hata iweje. 
 
Mungu aliposema 13.4 “Ndoa na IHESHIMIWE NA WATU WOTE, na MALAZI YAWE SAFI; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu”…Alimaanisha kweli kweli kuwa jambo hili halipaswi kuingiliwa juu juu tu au kufanywa na watu ambao sio wanandoa.

Kumbuka hata mtu yeyote anayezini leo kitendo anachokifanya ni kile kile kifanywacho na wanandoa, lakini ni kwanini biblia inasema anafanya dhambi?, ni kwasababu Amefanya uasi, na kaasi nini? ameasi kanuni za Mungu alizoziweka kwa ajili ya tendo lile, 1Yohana 3.4 “Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.”

Kwa mfano embu jaribu kufikiria mtu anapokula chakula, tunajua hilo sio mbaya, ni jambo jema kabisa na Mungu anapenda kuona watu wakila, lakini mtu akipitisha ulaji wake kwa tamaa, mpaka mpaka kufikia hatua ya kuvimbiwa na kushindwa hata kukaa au kutembea,na kutapika ovyo mtu huyo tunasema ni mlafi na ULAFI biblia inasema ni dhambi?, Je tuseme ni kwasababu ya kula ndio katenda dhambi?, hapana bali katenda dhambi kwasababu moja tu, kuvuka mipaka iliyowekwa na Mungu ya mtu aiendee katika vyakula, alipaswa ale kwa kadiri yake, kwa kiasi, lakini yeye aliasi kanuni za Mungu na kula kwa ulafi. Na ndivyo ilivyo katika dhambi nyingine zote,

Hivyo ndoa yoyote ya kikristo, ili iitwe ndoa ni sharti iunganishwe, na anayeinganisha ni mmoja tu naye ni Mungu, na wala sio mwanadamu yoyote au mzazi, Hivyo hatua za awali watu wakishakutana, wakishakamilisha desturi zote za nyumbani kwao, ikiwemo kujitambulisha kwa wazazi na kutoa mahari, hatua inayofuata ni kumwendea huyu mpatanishi ambaye ni MUNGU ili yeye awape cheti kile cha ndoa kitokacho mbinguni.

Hapo ndipo unapolazimika kwenda katika kanisa, wengine wanasema kwani haiwezekani kufunga ndoa nje ya kanisa?, vile viapo tulivyoambiana mimi na mwenza wangu nyumbani si vinatosha tu Mungu kuikubali ndoa ile kuwa ni kama ndoa halali?..Nataka nikuambie ndugu ndoa sio jambo la siri, na pale Mungu aliposema ndoa na iheshimiwe alimaanisha kuwa ni lazima ipewe heshima yake, na watu wote, na watu watu baadhi tu, na sio kugeuzwa kama kazi ya malimao sokoni yananuliwa na kutumiwa tu bila gharama yoyote. …Jaribu kufikiri wewe ni mkristo na ghafla unaonekana unaishi ni mwanamke/mwanaume ndani ya nyumba yako, utaonekanaje katikati ya jamii ya watu wanaokuzunguka?,na tena kibaya zaidi mnafikia mpaka hatua ya kuzaa watoto, watu si watawaona kama ni wazinzi tu, na kusababisha jina la Mungu kutukanwa?..Unadhani kuna Baraka zozote kutoka kwa Mungu hapo?.

Hivyo tendo lijulikanalo kama tendo la ndoa likifanyika nje ya ndoa ni UASHERATI, na kama ukichunguza kwa makini utaona utoaji mimba mwingu unafanywa na watu wa namna hiyo, watoto kutelekezwa kunatokea kwa namna hiyo, watoto kubakia na mzazi mmoja mara nyingi huja kwa njia hizo..Migogoro mingi ihusuyo familia mpaka kuachana huja kwa namna hiyo..Kwasababu sio njia aliyoiridhia Mungu, na hivyo hakuna baraka za Mungu hapo, lakini ikiwa watu tayari wapo kwenye ndoa iliyounganishwa na Mungu kanisani, tazama mienendo ya ndoa hizo kama utaona mambo ya namna hiyo kwa wingi yakijitokeza, hiyo ni kwasababu wameiheshimu ndoa,kadhalika wamemuheshimu Mungu na Mungu pia amewaheshimu kwa kuwapa neema ya ziada. Na hiyo faida zake ni hizi,

KWANZA: Mungu anakuwa kama shahidi katikati yenu pale mnapobadilishana vile viapo vya kimaandiko mbele ya malaika na wanadamu(wakristo)..

PILI:anasimama kama mlinzi katikati yenu pindi ibilisi akitaka kuishambulia ndoa yenu..kwasababu tayari mlishamshirikisha katika maamuzi yenu basi anakuwa na wajibu wa kuitazama ndoa hiyo kwa jicho la ziada zaidi..

Na TATU anaachia Baraka za kindoa kwa wenzi wote. Na katika ulimwengu wa Roho, wapo malaika wanaachiwa vile vile ili kuhakikisha ndoa ile itakaa salama..hata kama kukitokea kutokulewana basi hiyo inaweza ikawa kwa muda tu, au Mungu akashughulika kumwadhibu Yule ambaye si mwaminifu katika ndoa..Faida hizo zote mtu anazipata endapo atamuheshimu Mungu kwa kumuhusisha katika nia yake ya kuoa au kuolewa. Lakini jaribu kufikiria kama Mungu hajahusishwa katika ndoa fulani unategemea nini?.Shetani anapowajaribu kunakuwa hakuna mtetezi, na ndio hapo ndoa kama hizo zinaishia mahali pabaya ikiwemo kuachana…

Hivyo ukifuata utaratibu wote wa Ki-Mungu ndipo ndoa yako itakapobarikiwa. Kama ulishazaa au ulishazini nje ya ndoa, nenda sasa mbele za Mungu tubu, uiweke ndoa yako mikononi mwake naye atakuangazia neema zake.

Ubarikiwe.

SWALI 2: Ndugu zangu hawa viumbe wa roho "MALAIKA" Hawa nao wanapumua[kuvuta na kutoa HEWA]kama sisi tunavyopumua?
JIBU: Shalom ndugu…Malaika ni viumbe wa rohoni, hivyo hawana miili kama sisi, na tunafahamu kuwa mwili ndio unaopumua na kuvuta oxygeni na sio roho….hivyo isichanganye kati ya UHAI na PUMZI, Roho zote zinapokea uhai kutoka kwa Mungu hivyo zinaweza kuishi hata nje ya mwili huu, lakini mwili pekee ndio unaopumua..Ukisoma pale mwanzo utaona baada ya mwanadamu kuumbwa, Mungu akampulizia PUMZI ya UHAI..Unaona hapo? Hakumpulizia Uhai, bali Pumzi ya Uhai, alikuwa tayari kashapewa uhai zamani Mungu alipomuumba siku ile alivyomfanya kwa sura yake na mfano wake(Mwanzo 1:27)..Lakini sasa tunakuja kuona mwili unatengenezwa tena katika mavumbi, (Mwanzo 2: 7 Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.) hivyo ili Mungu kuileta roho yenye uhai ikae katika mwili ndio hapo ilipaswa mwili upewe pumzi upumie.

Sasa Ukisoma Mwanzo 1:6 Inasema..“Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji.7 Mungu akalifanya anga, akayatenga yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo.8 Mungu akaliita lile anga Mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya pili.
 
kumbuka hapo hilo anga alilolifanya Mungu katikati ya maji ya juu na ya chini halikuwepo hapo kabla..alilifanya hilo mahususi kwa ajili ya mwili wa mwanadamu, kwa afya ya mwili wake, apate pumzi, na ndio huko huko oxygen inapotokea pamoja gesi zote tunazozifahamu sisi, ndipo upepo unapovumia, na hali zote za hewa unazozisikia, zote ni ndani ya hili anga ambalo Mungu alilifanya kati ya maji na maji..Na Hiyo yote ni kwa ajili ya kuutunza mwili huu wa nyama,,na ndio maana mtu akijaribu kwenda juu zaidi ya hii Anga (atmosphere), lililopo hapa juu, anakufa hakuna kwasababu hakuna hewa ya oxgen, Mungu aliliweka kwa sehemu fulani tu na sio kila mahali.. Hii yote ni kuupatia mwili pumzi na mazingira mazuri ya kuishi.

Hivyo mtu akifa leo, mwili wake unazikwa lakini roho yake inaendelea kuishi katika ulimwengu mwingine ambao hauna hivyo vitu.

Ubarikiwe.

 SWALI 3: Bibi yangu amenihadithia kuna Kaka yake mmoja alimuoa mke na akawa anamtesa na baadaye huyo kaka akaja kumkataa huyo mke baada ya kuzaa naye,Yule mke alipokuwa anarudi kwao Arusha alisema huyo Mume wake ataoa wake 1-12,kisha huyo wa 12 atakuwa kama fisi ammalize.Sasa baba huyo anaendelea kuoa leo mke huyu kesho yule kwasasa wameshafika takribani wake 6..Anaendelea..Swali je! Maneno yale ya yule mwanamke yanasimamiwa na Mungu au na Shetani?.
JIBU: Mtu yoyote akizungumza Neno kwa imani ni lazima litokee, uwezo huo Mungu amemuumbia mwanadamu ndani yake..Mwanadamu anaweza akaumba jambo lolote katika kinywa chake na likaenda kutokea kama lilivyo ikiwa atalifanya kwa imani.

Lakini Imani imegawanyika katika sehemu kuu tatu,..

1.Imani inayotokana na Mungu, hii inakuja kwa kumwamini Mungu, na Neno lake, kwa mfano mtu anaweza kuamrisha ugonjwa utoke kwa Jina la Yesu, na ugonjwa huo ukatii, anaweza akatamka uzima kwa maiti na maiti ile ikarudia uhai,.Sasa imani ya namna hii ni ile imani ya Ki-Mungu na hii haina mipaka.

2.Pili kuna imani inayotokana na shetani. Hii ni imani ile ambayo mtu anaweza akawa ni mchawi, au mshirikina au ana pepo fulani, kwa hiyo akizungumza Neno kwa imani, zile nguvu zilizopo ndani yake zinachanganyika na nguvu za giza kuhakikisha kuwa lile jambo linakwenda kutimia..kwa lugha ya sasa ndio unaweza ukasema mtu kalogwa au kafanyiwa jambo fulani la kichawi.

3.Na tatu kuna imani ya mtu binafsi..hiyo haitokani na shetani wala Mungu..bali inatokana na nia ya mtu mwenyewe..kwamfano unapounyanyua mkono wako juu, hiyo ni roho yako unaunyanyua huo mkono kwa Imani, mkono wako lazima utii na kunyanyuka juu, vinginevyo usingenyanyuka kama maagizo yasingetoka rohoni, unapotaka kupaa mpaka mawingu, mpaka mwezini, ni jambo ambalo haliwezekani kwa namna ya kawaida, japo sasa mwanadamu hana mabawa lakini aliposema ninataka kufika kule juu, alifika kwa imani yake..sio Mungu wala shetani anayefanya hivyo ni wewe(roho yako)..Sasa kwa namna hiyo hiyo pia roho ya mtu inaweza ikazungumza jambo na likatimia vilevile, kama Mungu hataingilia kati..

Mara nyingi Baraka za wazazi au laana za wazazi, huwa zinatokana na aina hii ya tatu ya imani, utakuta mzazi hamjui Mungu kabisa, wana hana habari yoyote na Mungu, lakini anaweza akambariki mtoto na mtoto anapata zile Baraka, au akamlaani na laana ile ikamfikia.

Kwahiyo kwa suala kama la huyo mwanamke kama sio Mkristo au kama hatumii nguvu za giza, basi inawezekana kaumizwa na tukio hilo sana na akaamua kuzungumza Neno lile la laana kwa Imani, na kama ni kama Mungu hatoliingilia kati basi ni lazima litimie.

Hivyo tuwe makini na sisi katika vinywa vyote, na ndio maana biblia inatushauri wakai wote tubariki wala tusilaani, maana hatujui maneno yetu tunayotoa yatakwenda kumuathiri yule kwa kiwango gani.(Warumi 12:14)

Ubarikiwe.

1 comment: