Ni nani aliyeidharau siku ya mambo
madogo?...Ni swali Bwana alilouliza.
Jina la Bwana Yesu Kristo,
libarikiwe, karibu katika kujifunza Neno la Mungu, Leo kwa Neema za Mungu,
tutajifunza namna ya kusimama imara siku
ya mambo madogo?.
Najua unajiuliza SIKU YA MAMBO
MADOGO NDIO NINI?...Lakini kabla ya kufikia huko kuelezea siku ya mambo madogo,
hebu tujikumbushe kidogo historia fupi ya Taifa la Israeli, ambapo kwa kupitia
hiyo tutaelewa kwa undani nini maana ya “siku ya mambo madogo”.
Kama wengi wetu tunavyojua Mungu
aliwatoa wana wa Israeli kutoka katika nchi ya Misri, na kuwaingiza katika nchi
ya ahadi, ambapo ndani ya nchi ile aliwaahidia kula mema yote endapo wataishi
kwa kuzishika amri zake, na kama ni msomaji mzuri wa biblia utagundua kuwa vipo
vizazi vilivyofanya vizuri kwa kwenda katika sheria za Mungu, ambavyo viliishi
kwa raha na kwa amani, na vipo pia vizazi vya wana wa Israeli ambavyo
havikufanya vizuri, vilikengeuka na kuacha kuyashika maagizo ya Mungu
waliyopewa na badala yake vikapitia
vipindi vya tabu sana.
Na utaona pia baada tu ya Israeli
kugawanyika na kuwa sehemu mbili yaani YUDA NA ISRAELI …ndio kipindi ambacho
wana wa Israeli walipozidi kukengengeuka
kwa viwango vya hali ya juu. Kuanzia kipindi cha Mfalme Yeroboamu mpaka kipindi
cha mfalme Hoshea wa Israeli kulikuwa hakuna unafuu kabisa, watu waliabudu
mabaali na sanamu wazi wazi na kuvukiza uvumba katika sehemu za juu. Na
kwasababu ya maasi kuwa mengi, Bwana alituma idadi kubwa sana ya manabii wake
katika kipindi hichi kuliko vipindi vyote vilivyotangulia ili kuwaonya wana wa
Israeli wageuke na kuacha njia zao mbovu, hivyo kuanzia huo wakati manabii
wengi sana walitokea kama wakina Eliya, Elisha, Nathani, Yona,
Habakuki,Sefania, Hosea, Mika, Yeremia,Isaya, Obadia,
Amosi,Nahumu,Ezekieli,Yoeli,Mika, Zekaria n.k Wote hawa walitokea ndani ya
kipindi cha wafalme wa Israeli..Lakini hawakusikia, kinyume chake waliwaua
wengine na kuwapiga kwa mawe.
Hivyo maovu yalipozidi hata kufikia
kikombe cha ghadhabu ya Mungu kujaa, kukawa hakuna tena kusamehe, Mungu
akaahidi kuwa watakwenda utumwani, na Miji yao yote itachomwa moto, na watu
wengi sana watauawa kwa upanga, na wengine watakufa kwa njaa, na wengine kwa Tauni. Na lile hekalu ambalo
mfalme Sulemani alilitengeneza kwa gharama nyingi litavunjwa na kuteketezwa
kabisa..Na kweli wakati ulipowadia Neno la Bwana lilitimia, Israeli
ilichukuliwa utumwani Ashuru na wale waliosalia wa Yusa ,Wakaldayo(yaani watu
wa Babeli)..walifika Yerusalemu wakauteketeza mji wao kwa moto, wakalivunja
lile hekalu kama Ilivyotabiriwa wakawaua watu wengi kwa upanga; wanawake, kwa
watoto na wachache waliobakia waliwachukua utumwani kwenda nao Babeli. Israeli Mji
ambao ulipata sifa na kuogopeka na mataifa yote ulimwenguni ukageuka kuwa kama
jalala.
Lakini Mungu ni wa rehema aliwaahidi
kuwa hawatakaa huko utumwani milele, bali watakaa huko wakimtumikia Mfalme wa
Babeli kwa miaka 70 tu! na baada ya hiyo miaka 70 kuisha watarejeshwa tena
kwao.
Sasa ndio tunaelekea kwenye kiini
cha somo letu, baada tu ya wana wa Israeli kutimiza ile miaka 70, wakiwa Babeli
Mungu aliwafungulia mlango wa kurudi tena nchini mwao, lakini waliporudi kule
walikuta tayari kuna watu wengine ambao walikuwa wanakaa pale, ambao sio
waisraeli, ambao mfalme wa Uajemi aliwaweka wakae kule…Lakini Hao watu
walipoona wana wa Israeli wamerudi tena nchini mwao wakaanza kuwapiga vita.
Wakati wana wa Israeli wanapanga
kumjengea tena Mungu Hekalu lingine jipya baada ya lile la kwanza kuharibiwa na
Mfalme wa Babeli miaka 70 iliyopita, wanakutana tena na changamoto nyingine ya
kusumbuliwa…hivyo kwasababu ya hao watu iliwafanya waishiwe nguvu kabisa ya
kuijenga tena nyumba ya Mungu, kwasababu pia kwa idadi yao waliorudi Israeli
walikuwa ni wachache sana.
Lakini ulipofika wakati Mungu
aliwanyanyua manabii wake wawili HAGAI na ZEKARIA kuwatabiria wana wa Israeli
kwamba wasimame imara waijenge nyumba ya Mungu wasiogope changamoto zilizopo
mbele yao, ijapokuwa hawana fedha wala utajiri lakini Bwana atakuwa nao katika
UDOGO WAO. Bwana akamwambia Hagai maneno haya awaambie wana wa Israeli.
Hegai 2: 1 “Katika mwezi wa saba, siku ya ishirini na moja ya mwezi, neno la Bwana lilikuja kwa kinywa cha Hagai nabii, kusema,2 Sema sasa na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, na hayo mabaki ya watu, ukisema,3 Miongoni mwenu amebaki nani aliyeiona nyumba hii katika utukufu wake wa kwanza? Nanyi mnaionaje sasa? Je! Mbele ya macho yenu, siyo kama si kitu?4 Lakini sasa uwe hodari, Ee Zerubabeli, asema Bwana; nawe uwe hodari, Ee Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, nanyi iweni hodari, enyi watu wote wa nchi hii, asema Bwana; MKAFANYE KAZI, kwa kuwa mimi ni pamoja nanyi, asema Bwana wa majeshi;5 KAMA NENO LILE NILILOAGANA NANYI MLIPOTOKA KATIKA NCHI YA MISRI; NA ROHO YANGU INAKAA KATI YENU; MSIOGOPE.6 Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, Mara moja tena, ni kitambo kidogo tu, nami nitazitikisa hizo mbingu, na hii nchi, na bahari, na nchi kavu;7 nami nitatikisa mataifa yote, na vitu vinavyotamaniwa na mataifa yote vitakuja; nami nitaijaza nyumba hii utukufu, asema Bwana wa majeshi.8 FEDHA NI MALI YANGU, NA DHAHABU NI MALI YANGU, asema Bwana wa majeshi.9 Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema Bwana wa majeshi; na katika mahali hapa nitawapa amani, asema Bwana wa majeshi”.
Unaona maneno hayo?..Bwana anawatia
moyo wana wa Israeli kuwa WASIOGOPE! Utukufu wa hekalu la pili utakuwa mkubwa
kuliko utukufu wa lile Hekalu la Kwanza. Hivyo wasonge mbele, wakafanye kazi,
wasiangalie umaskini walio nao, wala shida waliyo nayo wasonge mbele kwasababu
utukufu wa nyumba ya pili utakuwa ni mkubwa kuliko utukufu wa nyumba ya kwanza,
na FEDHA NA DHAHABU NI MALI ya Bwana.. haleluya!! Haleluya!!.
Zaidi ya hayo wakati wana waisraeli
wakiongozwa na kiongozi wao aliyeitwa ZERUBABELI wanatazama kuwa kujenga nyumba
na uchache wao, na umaskini wao, pamoja na wingi wa maadui uliowazunguka ni
jambo lisilowezekana, ni kama mlima mkubwa umewekwa mbele yao halafu
uusawazishe kwa beleshi..Lakini jicho la Mungu lilikuwa linaona tofauti..Na
ndio Bwana akampa nabii Zekaria maono mengine miezi miwili baada ya yale maono
ya Hagai na kusema..
Zekaria 4: 5 “Ndipo malaika aliyesema nami akajibu, akaniambia, Hujui vitu hivi ni nini? Nikasema, La, Bwana wangu.6 Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, SI KWA UWEZO, WALA SI KWA NGUVU, BALI NI KWA ROHO YANGU, ASEMA BWANA WA MAJESHI.7 NANI WEWE, EE MLIMA MKUBWA? MBELE YA ZERUBABELI UTAKUWA NCHI TAMBARARE; NAYE ATALILETA LILE JIWE LA KUWEKWA JUU KABISA PAMOJA NA VIGELEGELE VYA, NEEMA, NEEMA, ILIKALIE.8 Tena neno la Bwana likanijia, kusema,9 Mikono yake Zerubabeli imeiweka misingi ya nyumba hii, na mikono yake ndiyo itakayoimaliza; nawe utajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma kwenu10 MAANA NI NANI ALIYEIDHARAU SIKU YA MAMBO MADOGO? Kwa kuwa watafurahi, nao wataiona timazi katika mkono wa Zerubabeli…..”
Unaona hapo anasema NANI WEWE, EE
MLIMA MKUBWA? MBELE YA ZERUBABELI UTAKUWA NCHI TAMBARARE, Mbele ya changamoto
zote zinazoonekana kama ni milima, mbele za masihi wa Bwana zitakuwa ni nchi
tambarare…na sio kwa uwezo wa Zerubabeli wala kwa nguvu zao bali kwa roho yake
Bwana ndio watausawazisha huo mlima.
Na zaidi ya yote Bwana anamwambia
Zerubabeli.. “MAANA NI NANI ALIYEIDHARAU SIKU YA MAMBO MADOGO”…
Sasa siku ya mambo madogo ndio
ipi?..Ndio hiyo siku ambayo walikuwa hawana chochote, siku ambayo walikuwa
wanaona hakuna chochote kinachoweza kufanyika, siku ambayo walikuwa wanaona
ndio kwanza mambo bado hata hayajaanza, siku ambazo nguvu zao ni chache, hizo
ndio siku za mambo madogo?..Na Bwana anawauliza ni nani anayezidharau siku
hizo??...Ni nani anayesema kwamba jambo hilo la kuisimamisha nyumba yenye
utukufu mwingi halitafanikiwa?..Ni nani anayesema kuwa katika udhaifu huo
hakuna chochote kinachoweza kufanyika?!...sentensi hiyo huwa inamuhuzunisha
Mungu sana.
Ndugu somo hili ni la kukutia moyo
tu! wewe ambaye upo katika safari ya kwenda mbinguni, kuwa USIIDHARAU SIKU YA
MAMBO MADOGO.
Kama ndio kwanza unaanza kumtafuta
Mungu, usizidharau siku hizi ambazo unajiona huwezi kuitenda kazi ya Mungu,
siku inafika utakayoleta matunda mengi kwa Kristo, endapo hutazimia unachopaswa
kufanya ni kuendelea kusonga mbele kwa bidii zote bila kukata tamaa,…Mtaji
ulionao moyoni mwako uzalishe, kwasababu ni kama mbegu ndogo, na itakapokuwa
itakuletea faida nyingi sana mbeleni. Mwingine aliniambia jana siwezi kumgeukia
Mungu kwasasa sina kazi,..ndugu hata ukipata bilioni 100 leo bado utajiona tu
hujafika, anza leo na Bwana.
Na pia katika maisha ya kawaida ya
kujitafutia rizki,ikiwa wewe ni mkristo na kwanza ndio shughuli uzifanyazo zinaanza kuchipuka, upo kama fukara tu! au una mtaji kidogo, au kazi
yako ni ya hadhi ya chini sana, na ukiangalia mbele unaona milima mikubwa, hiyo
milima isikuogopeshe, ITAKUWA NCHI TAMBARARE…. Usidharau siku ya mambo madogo
nenda kakifanyie kazi hicho kidogo, kakizalishe!! Usimvunjie Mungu heshima kwa
kutomwamini endelea kutenda haki katika utakatifu wote kwa sababu fedha na
dhahabu ni mali yake, mwisho wa siku atakunyanyua tu! kama alivyomnyanyua
Zerubabeli na haitakuwa kwa nguvu zako wala kwa uwezo wako bali kwa ROHO WA
MUNGU,…NI NANI WEWE UNAYEIDHARAU SIKU YA MAMBO MADOGO! Mungu mwenyewe haidharau
wewe ni nani uidharau na mtu mwingine yoyote yeye ni nani hata aidharau siku ya
mambo yako madogo!!..Hata kama unauza mchicha usizidharau hizo siku.
Na mwisho kabisa tunaona baada ya
Zerubabeli kupata unabii ule kutoka kwa Bwana, kwa vinywa vya Hagai na Zekaria
Manabii wa Bwana, alipata nguvu mpya yeye pamoja na Yoshua na wana wa Israeli wote
na kwenda kuijenga nyumba ya Mungu, na baada tu ya kutia nia ya kwenda kuijenga
nyumba, wakati huo huo vibali vikaanza kufunguka, mara mfalme anatoa amri
wapewe ruhusa ya kujenga pasipo kusumbuliwa,mara mfalme anasema wapewe fedha na
wasilipishwe kodi yoyote na fursa nyingi na upendeleo mwingi waliupata kutoka
kwa watu na mfalme, nyumba ya Mungu ilipatikana na dhahabu nyingi na fedha
nyingi, na ikamalizika chini ya mikono ya Zerubabeli salama sawasawa na unabii
Bwana alioutoa.
Hivyo ndugu, Bwana ndiye
anayenyanyua na ndiye anayeshusha, kama alikushusha chini wakati mwingine ni
kwasababu ya maovu yako (ingawa sio kila kushushwa chini ni kwasababu ya
maovu,nyingine ni kwa utukufu wa Mungu kama Ayubu), kama ilivyo tu kufanikiwa,
sio mafanikio yanatoka kwa Mungu…lakini kama maisha yako yalikuwa hayampendezi
Mungu huko nyuma na akakushusha ni kwasababu anakupenda anataka akupe tumaini
tena, kama alivyowashusha wana wa Israeli kukaa Babeli miaka 70, na walipotubu
aliwarudisha tena katika nchi yao na kuwapa faraja kubwa kama hiyo, na
kuwanyanyua tena! Kwanini na wewe asikufanyie hivyo endapo utatubu kabisa kwa
kumaanisha kuziacha dhambi zako na kumgeukia yeye. Na kumbuka USITUBU!
Kwasababu tu unataka KUPATA UTAJIRI WA ULIMWENGU HUU, tubu kwasababu unataka
kwanza kupata UTAJIRI WA ULIMWENGU UNAOKUJA!.....Huo ukiupata hata huu wa
ulimwengu hauhitaji kuuhangaikia, Bwana alisema TUTAZIDISHIWA, kuzidishiwa sio
kusumbukia, kitu cha kutafuta ni Ufalme wa Mungu, huo ndio tumeambiwa tuutafute
kwa bidii zote …“ Mathayo 6:33..utafute kwanza ufalme wake na haki yake, na
hayo mengine mtazidishiwa”.
Hivyo Kama hujampa Bwana maisha
yako, huu ndio wakati wako wa kufanya hivyo, kabla mlango wa Neema haujafungwa,
Roho wa Mungu anataka utii thabiti kutoka ndani ya moyo wako na sio
kulazimishwa, anataka utubu kabisa kwa kudhamiria KUACHA, sio KUPUMZIKA, hapana
bali kuacha dhambi, unakusudia kuacha kwa vitendo usengenyaji, uasherati,
rushwa, utukanaji, ulevi, uvaaji usio na heshima(vimini na suruali kwa
wanawake), unakusudia kuacha anasa zote za ulimwengu, na ukisha tubu hatua
inayofuata ni ubatizo sahihi, na ubatizo sahihi ni wa maji Mengi na kwa Jina la
Yesu Kristo, kulingana na Matendo 2:38, na kisha baada ya ubatizo Bwana
mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu atakayekusaidia kushinda
dhambi. Na hapo utakuwa umezaliwa mara ya pili kwa maji na kwa Roho.
Mungu akubariki sana.
No comments:
Post a Comment