"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, March 20, 2019

NI NANI ANAYEUFUNGA MLANGO WA MAARIFA?.


Wakati nikiwa shule ya msingi, kuna mwalimu mmoja aliyetufundisha somo lijulikanalo kama “stadi za kazi”, mwalimu huyu wanafunzi wote tulimpenda sana kwasababu alikuwa tofauti kidogo na walimu wengine, kwani yeye kila alipokuwa akija darasani, alituambia watoto tumchangie hela ya karanga atutoe nje michezoni (lakini kiukweli hakuitumia kwa karanga bali alikwenda kununulia pombe).Na kama unavyojua watoto wanavyopenda michezo,hawapendi kukaa muda wote darasani kufundishwa, hivyo suala la kujitolea kila mtu sh.5 au sh.10 halikuwa ni jambo kubwa sana kulinganisha na raha tuliyokwenda kuipata kwenye michezo!.

Hiyo ndio ilikuwa desturi yake, na walimu wengine walipokuwa wanaona watoto wanacheza nje muda wa masomo, walipoulizwa mnafanya nini nje muda huu, wote wanajibu ni sehemu ya somo mwalimu ametutoa nje!, na ni kweli katika somo la stadi za kazi michezo inayo nafasi yake. Lakini baadaye likaja kuleta madhara mengine.

Hiyo ikapelekea watoto kupoteza hamu ya kufundishwa darasani somo lile, na hivyo kutokuwa na maarifa ya mambo mengine muhimu yahusuyo stadi za kazi, mfano ujenzi, ususi, uchongaji, ufugaji, ukulima, ushonaji n.k. wakabakia kufikiri stadi za kazi ni michezo tu ya kuruka ruka nje. Na mwisho wa siku mtihani wa mwisho ukifika watoto wanafeli. Kwasababu wanakuwa wamekosa maarifa ya kutosha juu ya somo lile…Unaona hapo tatizo mama lipo kwa yule mwalimu ambaye angepaswa atimize wajibu wake wa kuwafungulia wanafunzi wake mlango wa maarifa kwa kuwafundisha mambo yote katika uwiano, badala yake yeye ndiye anayekuwa wa kwanza kuufunga mlango huo kwa faida zake mwenyewe.

Jambo la namna hiyo lipo hata katika kanisa la Mungu, biblia inasema katika.

Luka 11:52 “Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa MMEUONDOA UFUNGUO WA MAARIFA; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia”.

Unaona, Mungu alishaweka ufunguo mlangoni, kilichokuwa kimebaki ni kufunguliwa tu na kuingia katika maarifa ya kumjua Mungu kwa mapana na marefu yake na sio kuhangaika hangaika tena, lakini hapa tunaona wana-sheria (yaani watu waliobobea katika kuisoma sheria/torati), au kwasasa tunaweza kusema waalimu wa biblia, wachungaji, maaskofu,manabii n.k. wao ambao ndio wangepaswa wawe wa kwanza kuuzungusha ule ufunguo ili waingie katika maarifa ya kumjua Mungu pamoja na watu wao, badala yake wao ndio wanaokuwa wakwanza kuundoa ule ufunguo na wanafanya hivyo kwa makusudi kabisa,…na mtu akishautoka ufunguo ni nani awezaye kuingia tena?.

Viongozi hawa wanajua kabisa watu wengi hawapendi, kufundishwa maneno ya Mungu katika mapana yake na marefu yake, kwasababu ni wachanga hawajui umuhimu wake kwasasa, na wao bila hata ya kuwahurumia, wanawalazimisha hivyo hivyo wajifunze na hayo mengine hata kama hawataki kwa usalama wa maisha yao,..Wao wanawafundisha yale ambayo watu wanataka tu kusikia, watu wanapenda tu, na kibaya zaidi pale wanapoona matoleo yanaongezeka kwa injili kama hizo, ndipo wanapoamua kutia nanga na kufundisha hizo hizo tu siku zote, na kuacha mambo ya msingi.

Viongozi hawa wanafahamu kuwa injili za mafanikio zinapendwa na watu wengi, lakini kwa makusudi kabisa huku wakijua kabisa hakuna mlevi yoyote atayeurithi ufalme wa mbinguni, wala mtu yoyote ambaye sio mtakatifu atakayemwona Mungu, (Waebrania 12:14), wala wazinzi, wala muabudu sanamu, lakini wao hawana muda wa kugusia mambo hayo…

Viongozi hawa wanafahamu kabisa kuwa wale watu ni wachanga, na kama ni wachanga ni lazima watapenda vitu vilaini laini tu, na yeye kama mwalimu badala azingatie kuwa mchezo peke yake haitoshi kumpa mtu maarifa yote ya kufaulia mtihani bali achanganye na maarifa mengine yote..Yeye hilo halizingatii na matokeo yake mwisho wa siku watoto wote wanafeli, na ndio huko watu wanaishia shimo la kuzimu.

Ndugu jiulize injili unazozisikia mara kwa mara, JE! ZINAKUJENGA PANDE ZOTE AU UPANDE MMOJA TU WA MAFANIKIO YA KIMWILI?...Unafahamu kuwa haya maisha yatakuwa na mwisho?..ulishawahi kulitafakari hilo?, kama unyakuo hautakukuta basi ujue siku yoyote unaweza ukaondoka hapa duniani, na huko uendako je! utakuwa mgeni wa nani? Huko uendako umejiwekea hazina gani?..BWANA YESU ANASEMA ITAKUFAIDIA NINI UUPATE ULIMWENGU MZIMA, NA HUKU UMEPATA HASARA YA NAFSI YAKO?, upate nyumba nzuri, upate gari, upate umaarufu, upate ukubwa na kila kitu na huku unapata hasara ya nafsi yako kwa kumkosa Kristo moyoni mwako??

Siku ile utakapokufa utasema laiti ningejiwekea huku hazina, nisingekuwa mahali hapa pa taabu, Leo hii unafurahia injili ya kuburudishwa na vichekezo na comedy kwenye madhabahu, na huku unajua kabisa umefarakana na Mungu moyoni mwako, na hata ukifa leo unakwenda kuzimu, hujui kuwa kizazi unachoishi ndio kizazi kilicho katika hatari kubwa sana kuliko vyote vilivyotangulia, ni kizazi kilicho katika hatari ya kuuona uharibifu utakaoijilia dunia nzima, hujui kuwa kulingana na kalenda ya kimbinguni tunaishi katika lile kanisa la Mwisho lijulikanalo kama Laodikia ambalo ndilo litakaloshuhudia kurudi kwa pili kwa Kristo?. Hufahamu kuwa hatua za Unyakuo zimeshakwisha anza, na wewe huna habari, haujui kuwa kazi za mpinga-kristo sasa zipo dhahiri na kiti chake kinajulikana sasa mahali kilipo, wewe upo buzy kukimbilia injili za vichekesho, na kufarijiwa, na huku unadhani upo sawa…Kaa mbali na hao viongozi! Na hizo injili ambazo zimekosa uwiano.
 

Tunaonywa tuwe makini, huu ni wakati wa kutafuta kwa bidii mahusiano yetu binafsi na Mungu, kupata maarifa ya kina juu ya mapenzi yake kwetu sisi wanadamu, na maarifa haya yanakuja kwa kulitafakari na kuliishi Neno la Mungu.
2Petro 1:4 “Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa WASHIRIKA WA TABIA YA UUNGU, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa.
5 Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu MAARIFA”,
Hivyo ni maombi yangu, tutaanza mwanzo mpya sasa, ikiwa tulishampa Bwana maisha yetu, embu tuongezee na maarifa ya kumjua Mungu na uweza wake..Tutafakari zaidi mambo ya mbinguni kwasababu mtihani mkubwa sana upo mbele yetu,na tusipokuwa na maarifa ya kutoka ya kuyajua mapenzi ya Mungu, basi tujue kufeli kupo mbele yetu, na kufeli kwenyewe ni kuishia kuzimu..Lakini tukiwa na maarifa ya kutosha kuhusu Mungu wetu, hiyo itatusaidia kuishi maisha ya uangalifu sasa katika huu ulimwengu kama wapitaji hapa duniani na mwisho wake tutafauli ni kuishia Mbinguni milele.

Kama hujampa Bwana maisha yako kihakika, au unasita sita katika mambo mawili, au umezamishwa katika hizi injili za mafanikio zisizokuwa na uwiano za kuchuja mbu na kumeza ngamia, hebu tenga muda jaribu kuweka mambo yote kwenye mizani, jaribu kulitilia mkazo lile lenye uzito mkubwa zaidi na hayo mengine yafuate baadaye.

Mathayo 23:23 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache.24 Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia”.

Hivyo tuwe tayari kuzisikia habari zote, za ufalme wa mbinguni, kwa uwiano wote, na Mungu atatusaidia, La kwanza liwe ufalme wa mbinguni, na hayo mengine yafuate.

Wakolosai 1.9 “Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ILI MJAZWE MAARIFA YA MAPENZI YAKE KATIKA HEKIMA YOTE NA UFAHAMU WA ROHONI;
10 mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu;”

Mungu akubariki.

No comments:

Post a Comment