Mithali 20:14 “Haifai kitu, haifai kitu, asema mnunuzi; Lakini akiisha kwenda zake hujisifu.”
Ni wazi kabisa kwa jinsi tunavyozidi kuwa hapa duniani kuna mambo ambayo hayakwepeki, mfano kama hatutakuwa wauzaji, basi tutakuwa wanunuzi wa vitu fulani, Mungu karuhusu iwe hivyo ili kutufudhisha sisi kwa nadharia mambo yanayoendelea rohoni, na kama tunavyofahamu siku zote ile lugha ya biashara, muuzaji atataka kupandisha thamani ya ile bidhaa yake juu kidogo kwa kiwango ambacho si chake, ili kusudi kwamba ikitokea mnunuzi ataitaka bidhaa ile kwa gharama ya chini kidogo, basi asimpoteze mteja wake atampunguzia mpaka kwenye kiwango cha thamani halisi aliyokusudia kuiuza hapo mwanzo, Na hivyo yule mteja atakapoona amepunguziwa bei basi hiyo itamfanya aridhike na kununua bidhaa ile, pasipo kujua kuwa kile alichokitoa ndio thamani halisi ya bidhaa ile.
Hali kadhalika na mnunuzi naye, anataka kwenda kwa muuzaji tayari kichwani ameshajipanga kuwa atakapofika kwa muuzaji ni lazima ashushe kidogo thamani ya kile kitu, hata kama anajua thamani yake inaweza ikawa ni ile ile iliyowekwa na muuzaji, lakini ni lazima afanye hivyo, hiyo ni ili tu aipate ile bidhaa kwa bei ya unafuu kidogo, na mwisho wa siku anaipata, hivyo hayo ni mambo ya kawaida kabisa na yapo siku zote masokoni…Ili biashara ifanyike ni lazima kuwe na mapambano ya bei.
Vile vile na Sisi (mimi na wewe) kama wahubiri tunafanya biashara, na biashara tunayoifanya ni ya kuuza Wokovu kwa watu wenye dhambi, ili tumpatie Kristo faida za watu, ikiwa tutauweka sokoni wokovu wetu katika thamani ya chini, basi tujue kuwa wale watakaovutiwa na kuja kuununua watautaka kuunua kwa thamani ya chini zaidi ya hiyo unayouza, haiwezekani waupokee kwa mara ya kwanza kwa gharama zile zile unazozitaka wewe, kwa viwango vile vile unavyovitaka wewe,..ni hatua kwa hatua..
Sasa injili zetu na mafundisho yetu, yakiwa ni manyonge, mtu unamvuta kwa Kristo leo, halafu unamwambia kuvaa suruali ni sawa, kuweka makucha ya bandia mfano wa mnyama kenge ni sawa, kuimba miziki ya kidunia ni sawa wala hakuna shida yoyote, hatukemei dhambi, hatumuhubirii mtu utakatifu, ambao pasipo huo tunajua kabisa hakuna mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao biblia inasema hivyo katika (Waebrania 12:14) muda wote sisi tunamfundisha mafundisho ya jinsi ya kufanikiwa hapa duniani, huku tunapuuzia mafanikio ya Roho yake ambayo ni kwa kumjua Kristo na wokovu wake kamili..anachokifamu tu tangu siku ile tumemvuta kwa Kristo ni “pokea kwa jina la YESU”, Anafahamu tu shuhuda za kichawi zaidi kuliko shuhuda za Yesu, hajui hata baada ya kifo ni nini kinafuata, hajui unyakuo ni kitu gani, hajua maandiko, yeye tunachomuhubiria tu ni kwamba “watapigana nawe lakini hawatashinda”.....
Ni kweli kabisa hapo tumefanikiwa kuwavuta, ni sawa na tunawaudhia bidhaa zetu za wokovu tulizopewa na Kristo, lakini tunategemea vipi watu kama hao wataununua kwa gharama ile ile unayoitazamia wewe, kwamba wawe watakatifu kama wewe au kuliko wewe, hilo haliwezekani kinyume chake wataupokea wokovu wako kwa thamani ya chini kidogo, na ndio hapo utakuta japo ulimleta mtu kwa Kristo lakini maisha yake yapo mbali na Kristo, utasikia ni mzinzi, ni mlevi, utasema mbona nilimhubiria mimi akaokoka?..Ndio ulimhubiria lakini ulimpa viwango hafifu vya wokovu, na hivyo kama ilivyo desturi ya mnunuzi si jambo la kushangaza kuinunua bidhaa yako kwa kiwango cha chini kidogo, na matokeo yake ndio akawa kama alivyo, mtukanaji, mzinzi, mvaaji vimini barabarani, msengenyaji, anajulikana mtaani kwa utapeli, n.k…
Ndugu, biblia inasema kazi ya kila mtu itapimwa, usifurahie watu wengi kukimbilia bidhaa zako, zilizo hafifu za bei ya chini, (mfano wa bidhaa za kichina) zinazotengenezwa na majani tu, ambazo hata jua haziwezi kustahimili, ni kweli utaziuza nyingi kwa wakati mmoja lakini faida yake itakuja kidogo, tofauti na mtu Yule anayefanya biashara ya DHAHABU, atapata mteja mara moja kwa mwezi lakini faida yake ni mara 1000 ya zaidi ya Yule wa mchicha.
1Wakorintho 3: 11 “Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo.12 Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedhaau mawe ya thamani, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri.13 Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani.14 Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu.15 Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa moto”.
Unaona hapo?..Tunapaswa tujitathimini ni wokovu upo tunawapelekea wenye dhambi, ili siku ile tusije tukajikuta wote tunaangukia katika hasara na majuto, na kazi zetu na taabu zetu zikaonekana kuwa ni bure…Tuupe wokovu thamani yake, tuwafundishe watu UTAKATIFU na NENO la Mungu, na TOBA! tusiwafiche juu ya hukumu inayokuja, tuwaambie ukweli njia inayokwenda UZIMANI ni nyembamba nayo imesonga nao wanayoina ni wachache, na inayoenda mautini NI PANA, tuwaambie kulingana na maandiko wanawake kuvaa vimini, suruali, mapambo, ni dhambi na vinapeleka wengi kuzimu. Ni kweli mambo kama hayo hayapendwi lakini mnunuzi atakayekuja kuununua wokovu wa namna hiyo..Atakuwa ni wa uhakika, na ndio hao biblia inasema mbingu nzima na malaika juu mbinguni wanawafurahia wakitubu..Lakini sio wokovu tu mwepesi ambao huo kila mtu anasema anao lakini roho yake ipo mbali ni Kristo.Hatupaswi kuhubiri vile watu wanavyovitaka, bali kile Kristo anachokitaka, hilo ndio jukumu letu.
Naamini, utakuwa umeongeza kitu katika vile ulivyojaliwa kuvijua, Bwana akubariki na atuongezee Neema yako sote tuzidi kumjua yeye.
Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, litukuzwe daima.
Shukran sana
ReplyDelete