"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Sunday, April 7, 2019

KWA MUNGU ASIYEJULIKANA.


Tunasoma katika Matendo 17 Mtume Paulo, alipofika Athene mji mkuu wa Ukigiriki, mji ambao ulikuwa umejaa wasomi wengi ambao hata sasa historia ya dunia inarekodi sehemu kubwa ya Elimu na Sayansi tuliyonayo leo hii chimbuko lake lilikuwa ni huko Ugiriki, Wanafalsafa maarufu ambao wanafahamika kwa akili zao na hekima zao nyingi walizowahi kuzionyesha duniani mfano Aristotle, Xenophon, Plato,Pythagoras,Socrates,Plotemy, n.k. wote hao Walitokea huko huko Ugiriki, hivyo tangu zamani hawa watu walijulikana kama ni watafiti wakubwa (Great thinkers), na wagunduzi wa vitu vingi, na hivyo hawakuwa watu wa kubabaishwa tu na habari zinazovuma au maneno ya kutungwa yasiyoweza kuthibitishwa uhalisia wake yanayokuja katika jamii zao...

Na ndio hapa tunaona Mtume Paulo anaingia Athene sasa baada ya kuzunguka mataifa mengi na nchi nyingi kuhubiri, nchi hii kwake ilikuwa ni ya tofauti kidogo Kama Biblia inavyotuleza watu hawa wa Athene walikuwa hawana muda wa kufanya mambo mengine yoyote isipokuwa kutoa habari tu na kusikiliza juu ya taarifa mpya zinazowafikia (Soma Matendo 17:21), hii inaonyesha ni jinsi gani walivyokuwa wamejikita katika masuala ya utafiti na usomi ili kujua nini maana ya mambo yote na uhalisia wake zaidi ya kuganda katika mambo yale yale wanayoyaona kila siku..

Hivyo mtume Paulo alipoingia katika mji ule alianza kuupeleleza ili aone ni mambo gani yanayoendelea kule, lakini alipokuwa akizunguka huko na kule alikutana na madhahabu kubwa sana, iliyoandikwa maneno haya KWA MUNGU ASIYEJULIKANA..Hilo likateka sana fikra zake kupelekea kutaka kufahamu ni kwanini waandike vile, ni kwanini watengeneze madhabahu kwa Mungu wasiyemjua,

Kumbuka kama tulivyoona hapo mwanzo Wagiriki hawakuwa kama watu wa mataifa mengine mfano wa warumi au wamedi, hapana hawa ni watu waliokuwa wanafikiria sana, na wadadisi na wachunguzi wa kina wa mambo yote, hivyo kuandika vile sio kwamba walijisikia tu kuandika au walibuni wazo hilo kisha watengeneze madhabahu ya Mungu asiyejulikana kisha waabudu juu yake, hapana badala yake, ni kweli walitazama mambo yote,na kutathimini kwa kina na kwa utaratibu wakagundua kuwa katikati ya vitu vyote vilivyopo duniani na vinavyoabudiwa hakuna hata kimoja kinachoweza kuleta ufasaha wa mambo yao yote, isipokuwa kwa Mungu asiyejulikana asifanya vikao na wanadamu. hii ikiwa na maana japo kulikuwa na miungu mingi ugiriki watu wanayoiabudu wakati ule, lakini hakuna hata mmoja aliyefikia viwango vya kustahili kupokea Ibada zote za kiungu kwa kazi zake zote zinazoonekana ulimwenguni kote..

Walijua kabisa kipo kitu kingine zaidi ya wao wanavyoweza kukifikiri au kikitafsiri kiitwacho Mungu au vinginevyo, kinachoendesha shughuli zote za ulimwenguni, na wanadamu na kitu hicho hawawezi kuwasiliana nacho kwa njia za kawaida kwasababu ni kikuu sana, zaidi ya upeo wa kufikiri wa wanadamu, ni cha elimu ya juu sana, hakijulikani kama kipo mbali na sisi au karibu na sisi, ni kwamba tu hakina ushirika na wanadamu, wala hakielezeki, wala hakifananishwi, njia zake hazieleweki hali kadhalika hazichunguziki na makao yake hayafahamiki, na hivyo wakaona ili kufanya habari zake kuwa fupi basi wakaweka madhabahu yake mahali pa juu sana kuliko madhabahu nyingine zote na kuanza kumwabudu hivyo hivyo tu pasipo maarifa yoyote kumuhusu yeye..Ila walichokuwa wanajua ni kwamba ni kwa Mungu huyo anayeishi na ni mkuu kuliko vitu vyote.
Matendo 17:22 “Paulo akasimama katikati ya Areopago, akasema, Enyi watu wa Athene, katika mambo yote naona ya kuwa ninyi ni watu wa kutafakari sana mambo ya dini.
23 Kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua.
24 Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono;
25 wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote.
26 Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao;
27 ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu.
28 Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wenu, mtunga mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazao wake.
29 Basi, kwa kuwa sisi tu wazao wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu.
30 Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu.
31 Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu.
32 Basi waliposikia habari za ufufuo wa wafu wengine walifanya dhihaka; wengine wakasema, Tutakusikiliza tena katika habari hiyo.
33 Basi hivi Paulo akaondoka akawaacha.
34 Baadhi ya watu wakashikamana naye, wakaamini; katika hao alikuwamo Dionisio, Mwareopago, na mwanamke mmoja jina lake Damari, na watu wengine pamoja na hao”.
Kama tunavyosoma tunaona mtume Paulo alifika na kuanza moja kwa moja kuwafunulia kwa utaratibu habari za Mungu huyo ambaye wanamwabudu pasipo wao kumjua, Mungu asiyejulikana. Na hivyo waliposikia habari za jambo hilo jipya masikioni mwao wengi wao walikaa chini na kumsikiliza.

Ndugu, hao watu walikuwa wapo sahihi kabisa kuenenda katika hali hiyo ni kweli kumwelewa ni kazi sana,au tunaweza kusema haiwezekani kabisa kumwelewa yeye au kumjua yeye kama hatutajua njia fasaha ya kumwendea…

Mambo hayo hayo ya Athene yanajirudia hata leo hii, Wanasayansi sio kwamba hawaamini kuwa hakuna nguvu ya kimiujiza (Supreme being) inayouongoza huu ulimwengu hapana wanaamini kabisa isipokuwa wao wanamtambua kwa jina lingine (nature) na hiyo inawafanya wasiamwamini kabisa Mungu tunayemwamini sisi, hawaamini kama huyo (nature) ambaye sisi tunamwita Mungu anaweza akawa dhaifu namna hiyo etu ajishughulishe na wanadamu na kutazama dhambi zao ili awaadhibu, angali yeye tunamfahamu anayo mambo makubwa sana yasiyokuwa na mwisho huko angani na ulimwengui kote yasiyoweza kuelezeka kwa fikra za kibinadamu iweje leo, eti udhaifu wa mtu umuudhi, huyo sio Mungu…Unaona? Ndivyo wanavyowaza na kuamini.

Mwanasayansi mmoja maarufu wa kizazi chetu ajulikanaye kama ALBERT EINSTEIN,ambaye dunia sasa inamwona kama mtu wa karne kwa mapinduzi yake makubwa aliyoyaleta katika ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia, yeye anasema hivi …..“Mimi naamini katika Mungu, lakini sio katika Mungu huyu watu wanaomwita wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo ambaye yeye msingi wake ni kujishughulisha na vitu vidhaifu vya wanadamu, kama dhambi, na kuadhibu watu, huyu hawezi akawa ni Mungu ninayemfahamu: anaendelea kusema: mimi anasema naamini katika Mungu ambaye ni mkuu zaidi ya upeo wa kibinadamu muumba wa UNIVERSE, ambaye akili za kibinadamu hazijitoshelezi kumwelezea tabia zake”.. Yaani kwa ufupi anaamini kwa Mungu asiyeweza kufikiwa.

Unaona? Hali kadhalika jambo kama hilo tunaliona kwa ndugu zetu waislamu, wanasema Mungu tunayemwabudu ni Mungu mkuu sana (Allah), hajazaa, wala hajazaliwa, wala hana mtoto, wala hana USHIRIKA na mwanadamu yeyote wala kiumbe chochote, si mwanaume, wala si mwanamke, na hivyo mtu yeyote anayemwita Mungu baba, au mfalme wake anatenda dhambi kubwa sana ya kumshusha Mungu hadhi ya kumfananisha na Mwanadamu ambayo ni sawa na dhambi ya kukufuru…

Sasa hawa wote sio kwamba wanakosea kuamini hivyo, hapana, walichokiona kuhusu Mungu ni kweli kabisa, na ndivyo Mungu alivyo katika uhalisia wake, lakini kumbuka jambo hilo ndio kama lile lile lililowakuta watu wa Athene wao walitengeneza madhahaba na kumwabudu Mungu ndani yake lakini madhahabahu hiyo ilikuwa na jina la “KWA MUNGU ASIYEJULIKANA.”

Unaona? Walimwabudu Mungu asiyejulikana, walimwabudu Mungu wasiyemjua, Sasa madhara yanayokuja kujitokeza kwa watu wa namna hiyo ni kwamba maisha yao yote wataishia kutokumwelewa muumba wao kabisa mpaka kufa kwao, pia hawatakaa wanufaike na chochote kutoka kwa muumba wao, Na mwisho wa siku wanaishi akutokumwelewa hata pale Mungu atakapotaka kusema nao hawatamwelewa na hivyo kupotea kabisa katika dira ya Mungu. angalia kwa makini utaona, watu na namna hiyo wanaishia kumwogopa, na kuwa na wasiwasi, na kumwendea kwa hofu zisizokuwa na maana yoyote, kwasababu wametaka kumwona yeye katika uhalisia wa ukuu wake lakini sio katika njia ambayo amewapangia wanadamu wote wamwone yeye.

Ndugu yangu Mungu kumleta Yesu Kristo duniani kulikuwa na manufaa sana, kwangu mimi na kwako wewe, ni kutufanya sisi tumwelewe yeye vizuri katika utimilifu wote, biblia inasema “Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili.”(Wakolosai 2:9), Unaona pale ambapo tulikwama pasipo kumwelewa Mungu sasa tunamwelewa kwa kupitia mwana wake YESU KRISTO.

Na ndicho Paulo alichokifanya mara moja kwa wale watu wa Athene, Aliwahubiria Kristo, Mwana wa Mungu, ambaye kwa huyo sisi tunahama moja kwa moja kutoka kuwa viumbe tu vya kawaida vya mwenyezi Mungu, na kufanyika kuwa WANA WA MUNGU aliye hai kama yeye alivyokuwa.. Na kwa kumwamini yeye basi tunakuwa na uwezo wa kumwelewa Mungu na mapenzi yake katika maisha yetu kwa urahisi kabisa, tunakuwa na uwezo wa kusimama mbele ya madhabahu ya Mungu mbinguni na kuzungumza naye bila kutaabika kama wengine walivyo sasa hivi…

Na ndio maana alisema… (Yohana 14.6…”Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.)..Na pia alisema… Aliyeniona mimi amemwona Baba;….Hatuwezi kumjua Mungu kwa njia yoyote ile isipokuwa kwa kupitia mwana wake YESU KRISTO. Huo ni ukweli ndugu wala usihangaike pengine”
Waebrania 1:1”Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi,

2 mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.
3Yeye kwa kuwa ni mng'ao wautukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;
4amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao”.
Tuchulie Mfano ulio hai ni sawa na leo hii unataka kuwasiliana na mimi bila kutegemea hicho kioo kilichopachikwa mbele ya simu yako, ni kweli kabisa Simu sio hicho kioo ambacho unakipangusa,na kuandika namba juu yake, …Simu ni ni kitu kingine cha ndani kilichojawa na Commands tofauti tofauti ili kufanya kifaa hicho kiweze kutumika kwa mawasiliano, sasa ikiwa utaondoa hicho kioo cha juu na ukataka kuwasiliana nami, basi jiandae kukukutana huko nambo ambayo hujayazoea maneno huko kama Galllery, au Contacts, au SMS, usitazamie utayakuta huko wala kidole hakitahitajika huko kufanya mawasiliano yaende.., ni wazi kuwa utakutana na vitu kama chips, cards,modems,processors,circuit board, na vinginevyo ambavyo hata kwa lugha ya Kiswahili havina tafsiri, ambavyo wewe kwa akili yako ya kawaida hutaelewa chochote isipokuwa yule mtaalamu wa hivyo vitu, yeye pekee ndiye anayeweza kupiga simu pasipo kioo kile, kwa vifaa na ujuzi alionao ..


Lakini sasa kwanini kile kioo kimewekwa, ni kwa faida yako wewe usiyejua hayo mambo magumu yaliyopo ndani ya hiyo simu, ili kufanya simu ionekane kuwa na maana kwako ndio hapo ukawekewa hicho kioo kizuri kwa nje chenye mpangilio mzuri wa mafile, kazi yako wewe ni kubofya tu au kupangusa, na moja kwa moja taarifa zako zinapelekwa ndani ya simu, na hivyo simu inafahamu kuwa ulimaanisha nini, na saa hiyo hiyo simu inapigwa kwenye minara kuungwa na mimi mahali nilipo kuwasiliana na wewe, Unaona hapo? jambo ambalo lingepaswa lifanywe na wataalamu wa hali ya juu, kuamrisha hizo code za simu lakini sasa linafanywa na wewe kirahisi tu kupitia kidole chako juu ya kile kioo.

Hivyo hivyo YESU ndiye kioo chetu kwa Mungu, ili tuweze kunufaika na Muumba wetu aliye mkuu sana, asiyechunguzika njia zake, asiyeelezeka kwa namna ya kibinadamu, asiyekuwa na mwanzo, aliye mwanadamu hatuna budi kumtumia yeye kama kirahisi chetu vinginevyo hatutakaa tumjue Mungu kwa kumchunguza.. Kwa kumwamini yeye na maneno yake,na sasa yale mambo yote ambayo tunayaona ni magumu kwetu, kumfikia Mungu wetu basi yanafanyika kuwa marahisi kabisa, embu fikiria kwa kuiamini tu damu ya Yesu unakuwa na nafasi ya moja kwa moja kusimama mbele za Muumba wa mbingu na nchi na kupata rehema ya kujibiwa maombi yako mambo ambayo watu wa agano la kale waliyatafuta kwa kafara nyingi lakini wasiweze kabisa kufikia hatua ya kuondolewa dhambi zao, au kusimama mbele ya madhabahu ya Mungu mbinguni...Unadhani hilo ni jambo dogo au rahisi, ukiwa nje ya Kristo hilo haliwezekani kabisa ndugu na ndio maana utaona hao wengine wanateseka huko nje, ni haki yao,kuwa hivyo japo wanamuheshimu Mungu kwa hofu lakini upendeleo huo hawataweza kuupata mpaka watakapoingia ndani ya KRISTO..

Wanamwamini Mungu lakini sio katika maarifa, wanamfahamu kuwa ni muweza wa yote lakini uweza wake hauna matunda yoyote ndani ya maisha yao, magonjwa yao hayaponywi, hawawezi kufunguliwa katika vifungo vya giza, hawawezi kupata faraha ya kudumu na amani ambayo ni YESU KRISTO tu pekee ndio anayeitoa, hawana uzima wa milele ndani yao, hawawezi kumwomba chochote kwasababu yeye huwa hajishughulishi na mambo ya wanadamu…Hana mshirika, ..Kwasababu hanawa ushirika naye kama wanavyosema…kwao ni Mungu asiyejulikana! Na asiyefanya vikao na wanadamu,..Lakini kwetu tuliomwamini Kristo Yesu, Mungu anafanya vikao na sisi, na anakuwa ni Mungu tunayemfahamu, tunakuwa ni watu wa Milki ya Mungu, ukuhani wa kifalme, uzao mteule haleluya!!

Hivyo ndugu yangu, ikiwa bado upo nje ya Kristo, wakati ndio huu, wewe mkristo-jina, wewe ni mwislamu, wewe ni asiye-na-dini mkabidhi leo maisha yako, utubu dhambi zako kabisa kwa kumaanisha kuziacha, kisha fanya hima ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na uwe ni kwa jina la YESU KRISTO, hapo ndipo utakapopokea uwezo wa kuwa mwana wa Mungu, na kuhesabiwa kuwa mtu wa kimbunguni kwasababu Roho wa Mungu atashuka ndani yako kuanzia huo wakati , kukusaidia wewe kumkaribia Mungu..na kumwelewa Mungu, Kwasababu atayatwaa yaliyo ya Kristo na kukupasha wewe habari.

Wakolosai 1:15 “naye (KRISTO) ni mfano wa Mungu asiyeonekana , mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.

Lakini ikiwa utaendelea kubakia nje ya wokovu ufahamu kuwa hutakaa umfikie Mungu, wala kumjua wala maombi yako hayatakaa yamfikie yeye kama mwana, utakufa katika dhambi, utakufa katika kukosa maarifa ya kumjua Mungu hiyo haijalishi unaonyesha heshima nyingi kwake kiasi gani, utafanana na wale watu wa ATHENE wanamwabudu Mungu wasiyemjua.. na mwisho wake utaishia katika lile ziwa la Moto.Wakati ndio huu, fanya bidii uje kwa Kristo. Na Bwana atakusaidia.

Tafadhali “shiriki ” neema hii kwa wengine, ili nao waponywe na Neno la Mungu, na Bwana atakubariki.

Ikiwa utapenda kujifunza masomo mengine, yapo katika website yetu. |www wingulamashahidi org|, ingia pale utajifunza mengi.

Maran Atha.

No comments:

Post a Comment