"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, April 1, 2019

MADHAIFU:


Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe.
 
Mambo mengi yanayoendelea katika ulimwengu wa mwili ni ufunuo wa mambo yanayoendelea katika ulimwengu wa roho..Uhusiano wa Baba na mtoto..ni ufunuo wa Uhusiano wa Baba yetu wa mbinguni na sisi watoto wake tuliopo hapa duniani…Kama Baba mzazi asivyoweza kumdharau mwanawe hata kama afanye jambo la kitoto kiasi gani ndivyo Baba yetu wa mbinguni asivyoweza kutudharau sisi watoto wake katika uchanga wetu. Na watoto wa Mungu ni wapi? Watoto wa Mungu ni wale waliomwamini Mwanawe mpendwa Yesu Kristo, hao ndio watoto wa Mungu…
Yohana 1: 11 “Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika WATOTO WA MUNGU, NDIO WALE WALIAMINIO JINA LAKE”

Kauli hiyo Ikiwa na maana kuwa kama mtu hajampokea bado Yesu Kristo bado hajapewa huo uwezo wa kufanyika kuwa mtoto wa Mungu, Hivyo sio mtoto wa Mungu bali anakuwa kama mtu tu au kiumbe cha Mwenyezi Mungu.
 
Upo usemi unasema “mtoto hakui kwa mzazi wake”…Na ndivyo ilivyo kwa Baba yetu wa mbinguni..sisi ni watoto wake na tutabaki kuwa watoto wake tu milele…na Mungu hana wajukuu (wote sisi ni watoto wake).

Wapo watu wanapitia vita vya kiakili sana wanapokwenda kumwomba Mungu, kwasababu wanajiangalia ni jinsi gani wana madhaifu mengi, wanajiona hawajui kupangilia maneno wanaposali, wanakosa mtiririko mzuri wa maneno, Ningependa nikuambie kuwa Baba yetu haangalii wingi wa maneno au mpangilio mzuri wa Maneno tulionao mbele zake, bali anaiangalia nia yetu ya ndani, tamaa yenu au kusudi letu la ndani…kwasababu yeye mwenyewe alishasema anajua haja za mioyo yetu hata kabla ya sisi kwenda kumwomba. (Mathayo 6:8).

Mzazi anao uwezo wa kujua kuwa mwanawe anahitaji chakula na maji…kabla hata huyo mtoto hajajua kuzungumza wala kujua nini maana ya chakula wala maji..kwasababu upeo wake ni mkubwa zaidi ya huyo mtoto, ameishi muda mrefu na hivyo anafahamu mambo yote mtoto anapaswa ayapate hata kama hatazungumza..Ndivyo ilivyo kwa Baba wa mbinguni. Na pia Mungu hana kinyongo wala hatukinai. Madhaifu yetu hayamfanyi Baba yetu wa mbinguni atuchukie..kama tu madhaifu ya vichanga vyetu hayatufanyi tuwachukie…zaidi sana ndio tunawapenda, na kuwatengenezea njia kila siku ya wao kukua ili baadaye waachane na hayo madhahifu, hilo lipo wazi hakuna mzazi katika hali ya kawaida anamchukia mtoto wake mchanga..tena zaidi ya yote ndio anampenda zaidi.

Mathayo 7:11 “Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?”

Lakini tatizo kubwa linakuja ni wengi kutokuelewa tofauti kati ya MADHAIFU na DHAMBI. Mungu hachukizwi na madhaifu yetu lakini anachukizwa na dhambi…Kwasababu madhaifu ni kitu kinachotokana na uchanga au kukosa ufahamu, lakini dhambi ni kitu kingine…Wengi wanabadili dhambi kuwa madhaifu…Labda utasikia mtu ni mwasherati halafu atakwambia ni udhaifu wangu tu!, mtu anatukana halafu anakuambia ni udhaifu wetu wanadamu tumeumbiwa hayo kwahiyo Baba anaelewa, mtu ni mwizi au mlevi halafu anasema huo ni udhaifu wake..Ndugu huo sio udhaifu unaozungumziwa katika maandiko Hizo ni Dhambi na zinamchukiza Mungu, ambazo mshahara wake ni mauti. Hebu wewe mwenyewe tafakari mtoto wako akiwa mwizi au mtukanaji unaweza kwenda mbele za watu na kuwaambia walimwengu kuwa mwanangu anaudhaifu wa utukanaji au uzinzi?..kuna mtu atakuelewa kweli..Ni wazi kuwa watu wote watakuambia umfunze mwanao aache hizo tabia.

LAKINI NINI MAANA YA UDHAIFU?.

Udhaifu ni kitu mtu anakifanya kisivyopaswa, kwa kutokujua..lakini endapo akijua usahihi wa jambo hilo basi anajirekebisha mara…Kwamfano mtu aliyempa Kristo maisha yake kwa mara ya kwanza (Yaani kasikia injili na kuchomwa moyoni na kumwamini kuwa Yesu Kristo ni Kweli) anaweza kuwa na madhaifu mengi…anaweza akawa bado anatabia Fulani za kiulimwengu ambazo anakuwa anazionyesha..tabia za ubishi ubishi, wakati mwingine ugomvi, tabia za kupenda baadhi ya vitu vya kiulimwengu, vijitabia vya kutokujali n.k na hiyo yote ni kwasababu bado hajasikia mahali popote na wala hajasoma maandiko na kuelewa kuwa mambo hayo mtu aliyempa Bwana maisha yake hapaswi kuyafanya…Na inapotokea anausikia ukweli kuwa mambo hayo sio sahihi aliyokuwa anayafanya, haraka sana anakuwa ni mwepesi kugeuka…

Sasa mtu wa namna hiyo Mbele za Baba wa mbinguni alikuwa anaonekana kama ni mtoto tu! Mwenye madhaifu ambayo baadaye atakapokuja kujua ukweli atabadilika. Na hata angekufa katika ile hali ya madhaifu bado angeokoka kwasababu alikuwa anafanya mambo ambayo alikuwa hajui kama ni makosa…Na alikuwa hafanyi vile kwa makusudi…bali ni kwasababu alikuwa hajui! Ni sawa na mtoto wako mchanga anapojisaidia kwenye nguo zake za ndani..huwezi kumpiga au kumwadhibu kwa kosa lile au anapochukua kikombe na kukirusha kule? utamwekea kinyongo?…kwasababu unajua amefanya vile kwa uchanga wake wa akili…endapo angekuwa mtu mzima asingefanya vile. Na Baba wa mbinguni ni zaidi ya hayo, yeye anaangalia kwa jicho la ndani zaidi kuliko hata sisi tunavyoona.
 
 
Lakini sasa endapo mtu kashaujua ukweli kuwa uasherati ni dhambi, uzinzi ni dhambi, ulevi ni dhambi, rushwa ni dhambi, wizi ni dhambi, utazamaji pornography na utoaji mimba ni dhambi, ufanyaji masturbation ni dhambi,uvaaji mbovu ni dhambi..halafu bado anaendelea kufanya hivyo kwa makusudi, pengine kaujua kwa kusoma maandiko au kuhubiriwa….huyo mtu mbele za Mungu sio mdhaifu bali ni muasi na atahukumiwa..
 
Biblia inatuonya sana kuhusu dhambi za makusudi…ni hatari sana hizo…
Waebrania 10:26 “Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, HAIBAKI TENA DHABIHU KWA AJILI YA DHAMBI;
27 bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao.
28 Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu.
29 Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?”
Shetani amedanganya wengi kuwa uasherati ni madhaifu yetu sisi wanadamu, kwahiyo mtu anakwenda kufanya uzinzi akiamini moyoni mwake kuwa Bwana anaelewa, …akiamini kuwa huo ni udhaifu Mungu aliomwekea kila mwanadamu ndani yake..usidanganyike ndugu yangu hiyo ni tiketi ya kwenda kuzimu moja kwa moja…shetani anakushawishi kukuambia ufanyaji wa masturbation ni udhaifu, usidanganyike ndugu, huo ni muhuri wa kukupeleka kuzimu..Shetani anakushawishi kuamini kuwa utukanaji, chuki, kutokusamehe na vinyongo ni udhaifu na huku unajua kabisa ndani ya moyo wako mambo hayo ni machukizo mbele za Mungu..usidanganyike ndugu yangu mambo hayo ni njia panda ya Jehanamu ya moto..

Na moja ya dhambi kubwa inayowapeleka watu wengi kuzimu ni UASHERATI na nyingine ni KUTOKUSAMEHE…Uasherati ndio inayoshika namba moja na kutokusamehe inafuata hapo nyuma…Watu wengi wanakimbilia kuomba toba wasamehewe dhambi zao, lakini maandiko yanasema…
Mathayo 6: 14 “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, WALA BABA YENU HATAWASAMEHE NINYI MAKOSA YENU,”..
Na unafikiri madhara ya kutokusamehewa na Bwana dhambi zako ni nini??..Ni ZIWA LA MOTO!!!..Kwahiyo ndugu kutokusamehe sio udhaifu bali ni dhambi..Kwaufupi jambo lolote unalolifanya huku unajua kabisa sio sahihi kimaandiko, jambo hilo ni dhambi.

Ni matumaini yangu kuwa utakuwa umeongeza kitu juu ya vile unavyovijua, na Kama hujampa Bwana maisha yako, mlango upo wazi leo, fanya hivyo leo kabla nyakati za hatari hazijafika..

Bwana akubariki sana, pia nakukaribisha kutembelea tovuti yetu hii, kwa masomo mengine ya ziada /www wingulamashahidi org/, Pia naomba ushiriki ujumbe huu kwa wengine na Bwana akubariki.

No comments:

Post a Comment