"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, May 17, 2019

MAANA YA KUISHI NA MKE KWA AKILI.


Shalom. Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.
 
Neno la Kristo linasema:
1 Petro 3:7 “Kadhalika ninyi waume, KAENI NA WAKE ZENU KWA AKILI; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.”
Agizo hilo biblia iliyotoa linawahusu wanaume waliooa , na si kila mwanamume tu!..kwasababu utasikia mtu ambaye anaishi na mwanamke ambaye hawajaoana, au anaishi na mwanamke ambaye si mke wake, bali ni mke wa mtu mwingine…. anakwambia… “Biblia imetuambia tuishi na wake zetu kwa akili”… nataka nikuambia ndugu hapo utakuwa huishi kwa akili, bali kwa kukosa akili…kwasababu mtakuwa mnafanya uzinzi na uasherati! Utasema hilo lipo wapi katika maandiko
Mithali 6: 32 “Mtu aziniye na MWANAMKE HANA AKILI KABISA; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake. 33 Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika”.
Umeona? Akili inayozungumziwa hapo?..sio akili ya kuwa beberu ndani ya nyumba, au kuchepuka.. Ikiwa na maana kuwa moja wapo ya akili anazotakiwa mwanamume awe nazo anapoishi na mke wake ndio hiyo… “ KUWA MWAMINIFU KATIKA NDOA YAKE KWA KUJIEPUSHA NA ZINAA NJE YA NDOA YAKE”.

Kwasababu biblia inasema mtu aziniye na mwanamke atapata jeraha na kujivunjiwa heshima yake..itakufaidia nini unafanya zinaa nje ya ndoa yako halafu siku moja unafumaniwa na watu wanaanza kukunyooshea kidole?..hapo utakuwa umefanya jambo la kipumbavu, na biblia inasema fedheha yako haitafutika..Ni doa la daima.

Na hiyo AKILI ya kushinda, uasherati inakuja kwa kumwamini Yesu Kristo tu!, na kuoshwa dhambi zako kwa damu yake na kufanyika kiumbe kipya…haiji kwa kuongeza mke wa pili au watatu…Yesu pekee ndiye atakayeweza kukuondolea kiu ya mambo yote machafu ya ulimwengu huu.

⏩Maana nyingine ya kuishi na mke kwa akili, ni kumpenda na kumjali, upendo husitiri mambo mengi sana..Na hakuna mtu anayechukia kupendwa, kwahiyo upendo wa kweli na wa dhati ukiwepo hakuna matatizo yoyote yatakayojitokeza katika maisha ya ndoa..kutakuwa siku zote ni furaha, hiyo nayo ni akili.
⏩Maana nyingine ya kuishi na mke kwa akili, ni kugundua kasoro zake, na mapungufu yake, na kujua namna ya kuyatatua hayo ki BIBLIA!..Zingatia hilo neno KI BIBLIA! Sio kwa kutumia hekima za waswahili, au wasanii,au mila, au marafiki hapana! Bali biblia…epuka sana kutafuta suluhisho la “wahenga walisema”..au “wazee wazamani walisema” au “watu wanasemaga”…badala yake ni lazima IJIFUNZE kutafuta suluhisho kutoka kwenye Biblia(Maandiko matakatifu). Hekima za watu wa ulimwengu huu, zinafaa kwa baadhi ya mambo lakini si yote! Asilimia kubwa ya hekima za dunia hii zinazoshauri kuhusu masuala ya ndoa zinapotosha nyingi ni za Yule adui.

Kwahiyo hapo, ni lazima MWANAMUME ulijue NENO LA MUNGU kwa wingi ndani yako, hiyo ndio AKILI ya kuishi na mke wako?.

⏩Na maana ya mwisho ya kuishi kwa akili ni kuishi kwa Malengo Fulani ya kimaisha, ambayo hayakinzani na Neno la Mungu, hapa ndio linakuja suala la kupanga maisha na namna ya kujiongezea kipato kwa kazi zinazompa Mungu utukufu na mambo yote yanayofanana na hayo kwa ajili ya maisha mazuri ya familia.

⏩Lakini pia kumbuka Neno la Mungu halijamzuia pia mwanamke kuishi na mwanamume kwa akili, kwasababu na yeye kapewa akili vile vile, nanapaswa na yeye pia aishi na mume wake kwa akili, Kwa kujiepusha na zinaa na mambo yote tuliyojifunza hapo juu.
Pia wewe kama mwanamke soma vifungu hivi vitakusaidi kujua mwanamke mwenye akili kibiblia ni yupi..si yule wa kukaa vibarazani na kuwasema watu.
Mithali 31: 10 Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani.
11 Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato.
12 Humtendea mema wala si mabaya, Siku zote za maisha yake.
13 Hutafuta sufu na kitani; Hufanya kazi yake ya mikono kwa moyo.
14 Afanana na merikebu za biashara; Huleta chakula chake kutoka mbali.
15 Tena huamka, kabla haujaisha usiku; Huwapa watu wa nyumbani mwake chakula; Na wajakazi wake sehemu zao.
16 Huangalia shamba, akalinunua; Kwa mapato ya mikono yake hupanda mizabibu.
17 Hujifunga nguvu viunoni kama mshipi; Hutia mikono yake nguvu.
18 Huona kama bidhaa yake ina faida; Taa yake haizimiki usiku.
19 Hutia mikono yake katika kusokota; Na mikono yake huishika pia.
20 Huwakunjulia maskini mikono yake; Naam, huwanyoshea wahitaji mikono yake.
21 Hawahofii theluji watu wa nyumbani mwake; Maana wote wa nyumbani mwake huvikwa nguo nyekundu.
22 Hujifanyia mazulia ya urembo; Mavazi yake ni kitani safi na urujuani.
23 Mume wake hujulikana malangoni; Aketipo pamoja na wazee wa nchi.
24 Hufanya nguo za kitani na kuziuza; Huwapa wafanya biashara mishipi.
25 Nguvu na hadhi ndiyo mavazi yake; Anaucheka wakati ujao.
26 Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema i katika ulimi wake.
27 Huangalia sana njia za watu wa nyumbani mwake; Wala hali chakula cha uvivu.
28 Wanawe huondoka na kumwita heri; Mumewe naye humsifu, na kusema,
29 Binti za watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote.
30 Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa. 31 Mpe mapato ya mikono yake, Na matendo yake yamsifu malangoni.
Bwana akubariki.

No comments:

Post a Comment