"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, May 24, 2019

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 3


 
Karibu tujifunze Neno la Mungu,Biblia takatifu..Kama tunavyojua vitabu hivi vya biblia pamoja na kwamba vimeandikwa wakati mwingine kwa mfumo wa Hadithi, lakini vimebeba ufunuo mkubwa sana ndani yake. Ndio maana tunapaswa tujifunze Biblia na sio tuisome tu!...kwasababu kuna tofauti kubwa kati ya kujifunza na kusoma.

Tumekwisha kuvipitia kwa ufupi vitabu 8 vya kwanza, ambapo cha Mwisho kilikuwa ni kitabu cha RUTHU ambacho kilikuwa kinaelezea chimbuko la Mfalme Daudi lilipotokea, tulimwona mwanamke huyu Ruthu, ambaye hakuwa hata myahudi (alikuwa mtu wa mataifa)kwa Imani aliweza kubeba uzao wa Kifalme ndani yake, kama vile Rahabu kwa imani alivyohesabiwa miongoni mwa wayahudi japo hakuwa myahudi ..na tuliona pia kitabu hiki kiliandikwa na Nabii Samweli ambaye ndiye aliyekuwa mwamuzi wa mwisho kabisa wa Taifa la Israeli.

Na sasa kitabu kinachofuata ni kitabu cha SAMWELI wa Kwanza..Kitabu hichi kiliandikwa na Nabii Samweli mwenyewe kama jina la kitabu lilivyo, sehemu za mwisho wa kitabu baada ya Samweli kufa ziliandikwa na Nabii Gadi na Nabii Nathani ambao tutakuja kuona habari zao huko mbeleni.
 
Kitabu hichi cha SAMWELI WA KWANZA (au 1 Samweli). Ni kitabu kinachoelezea mabadiliko makubwa ya Taifa la Israeli. Ni kitabu kinachoelezea mabadiliko ya nyakati. Kumbuka wakati wana wa Israeli wanatoka Misri hawakuwa na Mfalme na haukuwa mpango wa Mungu fulani mmoja atawale juu ya wengine…

wangekuwepo viongozi lakini sio Mfalme, kuwepo kwa mfalme ndani ya Taifa la Israeli haukuwa mpango kabisa wa Mungu…kwani kwa kupitia mfumo wa kifalme ndio uliowatesa wao wakiwa Misri, walitumikishwa vikali kwa amri ya Mfalme wa Misri, kwahiyo Bwana alipowaweka Huru mbali na hiyo kamba hakutaka tena watoto wake wafungwe au wajifunge katika katika mfumo huo kwasababu alijua madhara yake…Na sio tu kuwa na mfalme bali hata hakutaka watwae watumwa miongoni mwa ndugu zao na kuwatumikisha kama walivyotumikishwa walipokuwa Misri.
Walawi 25: 38 “Mimi ndimi Bwana, Mungu wako, niliyewatoa katika nchi ya Misri ili niwape nchi ya Kanaani, nipate kuwa Mungu wenu.
39 Tena kwamba nduguyo amekuwa maskini pamoja nawe, akajiuza kwako; usimtumikishe mfano wa mtumwa;
40 kwako wewe atakuwa mfano wa mtumishi aliyeajiriwa, au mfano wa msafiri; naye atatumika kwako hata mwaka wa yubile;
41 ndipo atakapotoka kwako aende zake, yeye na wanawe pamoja naye, naye atairejea jamaa yake mwenyewe, tena atairejea milki ya baba zake.
42 KWA KUWA HAO NI WATUMISHI WANGU, NILIOWALETA WATOKE NCHI YA MISRI; WASIUZWE MFANO WA WATUMWA.
43 Usitawale juu yake kwa nguvu; ila umche Mungu wako.
44 Tena katika habari za watumwa wako na wajakazi wako, utakaokuwa nao; mataifa walio kando-kando yenu, katika hao mtanunua watumwa na wajakazi.
45 Tena katika wana wa wageni wakaao kati yenu mtajinunulia, na katika jamaa zao walio pamoja nanyi, waliowazaa katika nchi yenu; wao watakuwa milki yenu.
46 Nanyi mtawafanya kuwa urithi kwa watoto wenu baada yenu, wawe milki yao; siku zote mtatwaa watumwa wenu katika hao; LAKINI MSITAWALE KWA NGUVU JUU YA NDUGU ZENU, HAO WANA WA ISRAELI, WENYEWE KWA WENYEWE”.
Umeona! Kwahiyo Mungu, alikataza watoto wake wasiwe watumwa katika hiyo nchi waliyoahidiwa…Na zaidi ya yote ukiendelea kusoma utaona Bwana hakuwaruhusu hata pia kutozana RIBA wao kwa wao.

Lakini tunaona wana wa Israeli baada ya miaka mingi kupita walisahau hilo agizo..wakatamani utawala wa kishupavu kama wa Mataifa yaliyowazunguka..Ndipo ukafika wakati waisraeli wote wakakusanyana wakamwendea Nabii Samweli ambaye ndiye alikuwa mwamuzi wa kipindi hicho wakamwambia wanataka mfalme juu yao ili wafanane na mataifa mengine ya Duniani.

Jambo lile likamchukiza sana Samweli na Mungu, na Mungu akawapa mfalme kama walivyotaka, na Bwana akamwongoza Nabii Samweli aandike kitabu cha mambo hayo ili iwe kumbukumbu kwa vizazi vinavyokuja mbele yao na iwe fundisho kwetu sisi watu wa zamani hizi…Kwahiyo sehemu ya Mwanzo wa kitabu hichi inaelezea historia ya Samweli, kuzaliwa kwake na ukuhani katika hema ya Mungu, pamoja na Eli kuhani..Na kuanzia sura ya 8 na kuendelea ndipo tunaona wana wa Israeli wakitaka mabadiliko. Na sehemu iliyobakia inaelezea maisha na matendo ya Mfalme wa Kwanza wa Israeli (Sauli) mwanzo wake na mwisho wake.

1 Samweli 8:4 “Ndipo wazee wote wa Israeli wakakutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama;
5 wakamwambia, Angalia, wewe umekuwa mzee, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tufanyie mfalme atuamue, mfano wa mataifa yote.
6 Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba Bwana.
7 Bwana akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao.
8 Kwa kadiri ya matendo yote waliyonitenda tokea siku ile nilipowatoa katika Misri hata leo, kwa kuniacha mimi, na kwa kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokutenda wewe.
9 Basi sasa, isikilize sauti yao; walakini, uwaonye sana, na kuwaonyesha desturi ya mfalme atakayewamiliki.
10 Naye Samweli akawaambia wale watu waliotaka mfalme maneno yote ya Bwana.
11 Akasema, Mfalme atakayewamiliki ninyi atakuwa na desturi hii; atatwaa wana wenu na kuwaweka kwake, kwa magari yake, na kuwa wapanda farasi wake; nao watapiga mbio mbele ya magari yake.
12 Naye atawaweka kwake kuwa maakida juu ya elfu, na maakida juu ya hamsini; na wengine atawaweka walime shamba lake, na kuvuna mavuno yake, na kufanyiza zana zake za vita, na vyombo vya magari yake.
13 Na binti zenu atawatwaa kuwa wafanyaji wa marhamu, na wapishi, na waokaji.
14 Atatwaa makonde yenu, na mashamba yenu ya mizabibu, na ya mizeituni, yale yaliyo mazuri sana, ili awape watumishi wake.
15 Naye atawatoza ushuru wa mbegu zenu na wa mizabibu yenu, awape maakida wake, na watumishi Wake.
16 Atawatwaa watumishi wenu na wajakazi wenu, na ng'ombe zenu walio wazuri sana, na punda zenu, naye atawatia katika kazi zake mwenyewe”.
17 Atawatoza fungu la kumi la makundi yenu; nanyi mtakuwa watumwa wake.
18 NANYI MTALIA SIKU ILE KWA SABABU YA MFALME WENU MLIYEJICHAGULIA; BWANA ASIWAJIBU SIKU ILE.
19 Walakini hao watu wakakataa kuisikiliza sauti ya Samweli; wakasema, Sivyo hivyo; lakini tunataka kuwa na mfalme juu yetu;"
Kwa ufupi mwanzo wa matatizo makubwa yaliyowakumba wana wa Israeli yalianzia wakati huu walipojitakia mfalme….huko mbeleni utakuja kuona Wafalme ndio waliowakosesha sana wana wa Israeli na kuwasababisha waingie utumwani na kutapanywa katika mataifa yote duniani.

Na zaidi ya yote utaona Bwana aliwaonya hapo juu, kuwa Mfalme wanayemtaka atawafanya wana wao na binti zao kuwa watumwa, watatumikishwa kwa utumishi mkali..Na watalipishwa ushuru kwa kila kitu, desturi ambayo hapo mwanza hawakuwa nayo, na wataiona hiyo nchi ya Kaanani Bwana aliyowapa ni chungu! Wataona hakuna tofauti na kule Misri walipotoka..Na Bwana akawaambia siku hiyo baada ya mateso hayo wataomba msaada kwa Bwana lakini Bwana hatawasikia……. Lakini hawakuelewa kama biblia inavyosema! Wakapewa mfalme kama walivyotaka…Na Neno la Bwana likaja kutimia juu yao kama lilivyo miaka kadhaa mbeleni: walitumikishwa kwa utumishi mkali mpaka siku moja wakakusanyika kuomba wapunguziwe makali ya utumishi baada ya Mfalme Sulemani kufa…Tunayasoma hayo katika..

2 Nyakati 10:2 “Ikawa Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia, (maana alikuwako Misri, ambako amekimbilia mbele ya mfalme Sulemani), Yeroboamu akarudi kutoka Misri.
3 Wakapeleka ujumbe, wakamwita, Yeroboamu akaja na Israeli wote, wakamwambia Rehoboamu, wakasema,
4 Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa upunguze utumwa mgumu wa baba yako, na kongwa lake zito alilotutwika, nasi tutakutumikia.
5 Akawaambia, Mnirudie baada ya siku tatu. Watu wakaenda zao…………………..

9 Akawaambia, Je! Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa, waliosema nami, wakisema, Utufanyie jepesi kongwa alilotutwika baba yako.
10 Na wale vijana waliokua pamoja naye wakamwambia, wakasema, Uwaambie hivi watu wale waliosema nawe, wakinena, Baba yako alilifanya zito kongwa letu, lakini wewe tufanyie jepesi; uwaambie hivi, KIDOLE CHANGU CHA MWISHO NI KINENE KULIKO KIUNO CHA BABA YANGU.
11 Basi kama baba yangu aliwatwika kongwa zito, mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu AKIWAPIGA KWA MIJELEDI, LAKINI MIMI NITAWAPIGA KWA NGE.
12 Basi Yeroboamu na watu wote wakamjia Rehoboamu siku ya tatu, kama mfalme alivyoamuru, akisema, Mnirudie siku ya tatu.
13 Mfalme akawajibu kwa ukali; mfalme Rehoboamu akaliacha shauri la wazee, akasema nao kwa shauri la vijana,
14 akinena, Baba yangu aliwafanyia kongwa zito, NAMI NITAWAONGEZEA; BABA YANGU ALIWAPIGA KWA MIJELEDI, LAKINI MIMI NITAWAPIGA KWA NGE.
15 Basi mfalme hakuwasikia wale watu; MAANA JAMBO HILI LILITOKA KWA MUNGU, ili alithibitishe neno lake alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati kwa mkono wa Ahiya Mshiloni.”

Umeona? Wafalme wote wa Israeli waliwatumikisha wana wa Israeli kama watumwa, hata Mfalme Sulemani naye, aliwatumikisha wana wa Israeli kupita kiasi…jambo ambalo Mungu hakulitaka.

Kwahiyo kitabu hichi kinaelezea mabadiliko ya Utawala wa wana wa Israeli, kutoka kutawaliwa na Mungu mbinguni mpaka kujitakia mfalme wa kidunia awatawale..Hivyo kina mafunuo mengi sana ndani yake na siri nyingi ni vizuri kama hujakisoma ukisome peke yake, Bwana atakufunulia mambo mengi sana yanayohusiana na wakati huu tunaoishi…lakini jambo moja la kipekee ambalo tunaweza kujifunza juu ya kitabu hiki ni juu ya UBAYA WA KUIGA WATU WA ULIMWENGU HUU..Hekima ya Mungu ni kuu kuliko hekima ya ulimwengu huu, wana wa Israeli walitazama kwa nje jinsi utawala wa kifalme unavyopendeza, hawakujua ndani yake jinsi ulivyo mbaya, mpaka walivyoingia…

Na sisi katika safari yetu ya ukristo tunajifunza, Mambo ya ulimwengu huu, ustaarabu wa ulimwengu huu kwa nje yanaweza kuonekana ni mazuri, yanavutia lakini ndani yake yanamadhara makubwa, Mungu anapotuonya tukae mbali na ulimwengu si kwasababu anatuonea wivu, hapana ni kwa faida yetu wenyewe…anajua madhara tutakayoyapata huko mbeleni endapo tukiuiga ulimwengu, endapo tukienenda kama ulimwengu unavyoenenda…Endapo tukianza kutamani na sisi kuvaa vimini na suruali kama watu wa ulimwengu wanavyovaa, kujipamba kama watu wa ulimwengu wanavyojipamba,..Tutaingia kwenye mtego ambao mwisho wa siku tutaomba Mungu atutoe na Mungu hatatusikia siku hiyo, kama alivyowaambia wana wa Israeli kuwa “18 NANYI MTALIA SIKU ILE KWA SABABU YA MFALME WENU MLIYEJICHAGULIA; BWANA ASIWAJIBU SIKU ILE”.

Tunapoonywa sasa ni wakati wa kusikia, utakapozama kwenye uchawi utafika wakati utalia na Bwana asikujibu!..utakapozama kwenye anasa kupindukia na hali sasa unasikia maonyo hutaki kugeuka itafika wakati utalia na Bwana asikujibu…utakapozama kwenye uasherati na kila siku Bwana anakuonya kwa maonyo haya hutaki kusikia…utafika wakati utalia na Bwana asikujibu!...Unapozama kwenye kuacha uongozi wa Mungu na kufuata uongozi wa mwanadamu, Bwana anakwambia hivi, wewe unasema vile, Bwana anakwambia geuka huku hii ndio njia, lakini wewe unasema dini yangu haisemi hivyo wala watu wote hawasemi hivyo…ndugu yangu utafika wakati utalia na kuomboleza na Bwana hatakusikia!...Unyakuo utakapopita na utakapoachwa utalia na Bwana asikusikie…

Unajua ni kwanini watu wengi wenye magonjwa ya kutisha(japo si wote), Hawaponi? Watu wanaoingia kwenye mitego ya Ibilisi hawanasuki?...Ni kwasababu ya kushupaza shingo wakati wanaonywa..
Mithali 1:29 “Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa.”

Na imefika wakati wameshazama kwenye matatizo ndipo wanamlilia Mungu,..wengi wanasamehewa makosa yao lakini mauti inakuwa ipo pale pale…sasa hasara zote hizo za nini? Kwanini leo usifanye uteule wako na wito wako imara kama biblia inavyosema katika 2 Petro 1: 10 “Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe.
11 Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo”.

Kama hujampa Bwana maisha yako, saa ya wokovu ni sasa, unachotakiwa kufanya sasahivi na hapo ulipo kutubu dhambi zako zote ulizozifanya hapo kabla, na unazozifanya sasahivi…unamwambia Bwana hutaki kuzifanya tena, na wewe mwenyewe ukidhamiria kweli kweli kutokuzifanya tena, kama ulikuwa unakula rushwa unaacha, kama ulikuwa unafanya uasherati unaacha, kama ulikuwa mshirikina unaacha unakwenda kuchoma vifaa vyote vya kishirikina, kama ulikuwa ni mtukanaji, msagaji, mlawiti, shoga, mtoaji mimba, mfanyaji masturbation, mtazamaji pornography, mvaaji vibaya nk. Vyote unaviacha unaanza maisha mapya ndani ya Kristo na Bwana mwenyewe atakusamehe na kukupa maisha mapya ndani yake…Na kama madhara yalikuwa makubwa na ulikuwa hujui kwa mapana madhara yake pia atakuponya ugonjwa wako, atakurejeshea uzima, ila jambo la kwanza ni kutubu kwa kumaanisha kutokufanya tena.

Bwana akuabariki.

🔜 Usikose mwendelezo wa kitabu kinachofuata cha Samweli wa pili na vinginevyo. Pia naomba share kwa wengine, kwa utukufu wa Mungu. Nakukaribisha pia kutembelea website yetu kwa masomo mengine mengi ya ziada../www wingulamashahidi org/

AMEN.

No comments:

Post a Comment