Yohana 2:13 ‘’Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu.14 Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng'ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi.15 Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng'ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao;16 akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara.17 Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako utanila.18 Basi Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Ni ishara gani utuonyeshayo, kwamba unafanya haya? 19 Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha.20 Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu?21 Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake.22 Basi alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa alisema hivi, wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu.’’
Tukisoma kisa hichi ni rahisi kuwahukumu Makuhani na Mafarisayo na Wayahudi kuwa walikuwa watu wasiofikiri…watu wanaoona miujiza lakini hawaamini…ni kweli kuna mambo ya kulaumiwa lakini si yote…. hebu leo kwa sehemu tuchunguze kama ni kweli walikuwa hawafikiri wakati wote..
Jaribu kuchukua mfano wewe ni mtumishi wa Serikali, labda unatumika kwenye shirika fulani la Umma..halafu siku moja anatokea mtu usiyemjua anaingia mahali mnapofanyia kazi na kuanza kuvuruga vuruga nyaraka na hati muhimu..huku anawapazia sauti na kuwaambia…msigeuze serikali ya Raisi wangu kuwa pango la mafisadi….na mnapojaribu kumzuia na kumwuliza yeye ni nani na nani kamtuma kufanya vile, anawajibu…jiuzuluni wote na mwachie ngazi leo na baada ya siku tatu nitalinyanyua hili shirika upya.
Unafikiri ni kitu gani..kitagonga kwenye akili…Moja kwa moja aidha utajua huyo mtu karukwa na akili..Na pili jambo litakalofuata ni kutafuta njia ya kwenda kumshitaki haraka…Kwasababu anakuja kuharibu kazi na kuzungumza vitu visivyoeleweka…eti atalinyanyua shirika ndani ya siku tatu!!...Shirika hili mpaka kulifikisha hapa tumetumia miaka Zaidi ya 20 wewe unataka kulinyanyua ndani ya siku tatu!..
Hebu fikiria huyo mtu hata akienda mahakamani atashindaje kesi?..kwasababu amesikiwa na watu wote kwa kinywa chake akisema atalinyanyua shirika kwa siku tatu.
Na ndivyo ilivyokuwa kwa Bwana Yesu mahali Fulani, alipowakuta wayahudi wanafanya biashara kule Hekaluni,aliwaambia wasigeuze nyumba ya Baba yake kuwa pango la wanyang’anyi lakini walipomuhoji kwa ishara gani unafanya haya? Akawaambia libomoeni hekalu hili na ndani ya siku tatu nitalisimamisha.
Sasa wayahudi walidhani wamemsikia vizuri na kumwelewa…kumbe hawajamwelewa ingawa wamemsikia,..ndio maana Neno linasema ‘kusikia mtasikia lakini hamtaelewa..Kutazama mtatazama lakini hamtaona (Mathayo 13:14)’…Walidhani hekalu litakalobomolewa na kusimamishwa ndani ya siku tatu ni hilo la mawe wanaloliona mbele yao..kumbe kulikuwa na hekalu lingine ambalo lilikuwa ni mwili wa Bwana Yesu.
Na waliendelea na huo upofu mpaka siku ya mwisho, pale walipomsulibisha
Walisema maneno haya:
Mathayo 27:40 ‘’Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani’’.
Lakini tunaona waliokuja kumwelewa ni wanafanzi wake tu! Tena dakika za mwisho, Wale waliokuwa wanatembea naye kila siku. Ndio waliopewa neema ya kumwelewa Bwana Yesu alikuwa anamaanisha nini katika maneno yake. Sio kila mtu tu alikuwa anamwelewa Bwana Yesu.
Ndugu huo upofu mpaka leo upo! Unaendelea kwa watu wengi wasio wanafunzi wa Yesu Kristo..Bwana hana wanafunzi 12..alianza na wanafunzi 12, lakini sasa anao wanafunzi wengi…Na hao ndio anaowafunua macho ya kuyaelewa maneno yake…wengine walio nje maneno ya Yesu yatakuwa ni mafumbo kwao…wataona wanamwelewa sana Bwana Yesu lakini kumbe hawamwelewi..
Watadhani kwasababu Bwana aliyageuza maji kuwa divai basi alihalalisha unywaji wa pombe, lakini hawaelewi kuwa Pia kitendo cha Bwana kula na makahaba na wenye dhambi lengo lake halikuwa kuhalalalisha ukahaba wao wala dhambi zao…Alifanya vile ili kutafuta njia ya kuwavuta watubu kwa upendo wake….Na watu walipomwita kuwa mlevi haikumaanisha kuwa yeye kweli ni mlevi..wewe unaweza kuitwa mlevi na maadui zako lakini isiwe ni mlevi kweli…kadhalika walipomwita yeye ni mlafi haikumaanisha Bwana Yesu alikuwa ni mlafi kweli…
Alipomwita Herode Mbweha!..hakumaanisha kumtukana!!…ingekuwa ndio hivyo, basi yeye mwenyewe amejitukana sana…alipokuwa anajiita mwanakondoo?..au anapowafananisha watu wake na kondoo..kwa wale wafugaji wanaelewa ni afadhali mtu akuite mbwa kuliko kondoo.
Kadhalika aliposema mkawabatize watu wote kwa jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu hakumaanisha hivyo vyeo bali alimaanisha ni jina moja ambalo ndio la Baba, na ndio hilo hilo la Mwana na ndio hilo hilo la Roho Mtakatifu na hilo sio lingine Zaidi ya Jina la YESU (Matendo 2:38).
Na aliposema…’’aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele’’..hakumaanisha tukamkamate na kumchinjwa na kunywa damu yake kama simba…bali alimaanisha kuula katika roho na kuinywa damu yake katika roho..Na chakula cha Roho zetu ni Maneno tunayosikia…Yakiwa ni Maneno ya Mungu, basi ni chakula bora cha uzima wa milele, na yakiwa maneno ya yule mwovu basi ni chakula kisichofaa cha mauti.
Kwahiyo Biblia inatufundisha tuwe na masikio yanayosikia, na macho yanayoona..ili kwamba tunaposoma Biblia tuielewe…Na hayo tutayapata kwa kuwa wanafunzi wa Yesu tu!..kwasababu hao ndio Bwana alikuwa anawapa kuelewa maneno yake…
Na vigezo vya kuwa mwanafunzi ni hivi..
Luka 14:25 ‘’Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia,26 Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.27 MTU YE YOTE ASIYEUCHUKUA MSALABA WAKE NA KUJA NYUMA YANGU, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.28 Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?29 Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki,30 wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.31 Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini?32 Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali.33 Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu’’.
Je! Umeuchukua msalaba wako?..je! umewachukia ndugu zako, baba yako na mama yako?...kuchukia kunakozungumziwa hapo sio kuchukia mtu kwa hasira au chuki ya moyo…hapana! Bali ni kitendo cha kuyakataa na kuyachukia maamuzi ya wazazi wako au ndugu zako yanayopingana na mapenzi ya Mungu kwako, na kuamua kuyafuata yale mapenzi ya Mungu tu!..Huko ndio kuwachukia kunakozungumziwa hapo juu!!...kama baba yako ni mlevi na anakutaka na wewe uwe kama yeye…hapo unayachukia hayo maamuzi na kusema hapana!..kama ni msengenyaji hivyo hivyo..kama ni mlarushwa na wewe anataka uwe kama yeye unasema No! kama ni mchawi au Mwenda kwa waganga..na anataka kukufundisha na wewe uwe kama yeye..hapo unasema hapana! N.k.
Na pia ili uwe mwanafunzi biblia inasema unapiga gharama!! Ukristo sio jambo la kujaribu na kutoka! Biblia inasema utachekwa….Ukiamua kumfuata Bwana Yesu, hesabu kuwa kuna kuonekana mpumbavu, kuonekana mshamba…wakati mwingine kuonekana umerukwa na akili…Na pia ukristo sio mteremko muda wote…piga hesabu kuwa kuna wakati Bwana anaweza kukuacha kwa kipindi Fulani kirefu pasipo kuzungumza na wewe kwa njia unayotaka! Je! Utaendelea kuwa naye!...utakapopitia shida, dhiki na wakati mwingine misiba utamwacha?
Pia piga gharama! Je asipokupa vile vitu unavyohitaji! Utaendelea kuwa naye?.
Na mwisho anasema ‘mtu yeyote asiyeacha vyote alivyo navyo hawezi kuwa mwanafunzi wangu’..Kuacha vyote ulivyonavyo ni mfano wa wakina Petro…waliacha vyote walivyo navyo na kumfuata Bwana…Kuacha vyote ulivyo navyo sio lazima kwenda kuuza mali zako au hazina yako…bali ni kuishi kana kwamba hivyo vitu sio vya kwako…kiasi kwamba hata ikitokea kimepotea hakipo kwenye akili yako…umeshakiacha siku nyingi…akili yako imetawaliwa na kutenda mapenzi ya Mungu na kuyaishi…hakina chochote katika moyo wako…kiwepo au kisiwepo vyote kwako ni sawa sawa tu.
Ukishapiga hizo gharama, na kujitwika msalaba wako, biblia inasema umekuwa mwanafunzi wake…ambao wamepewa Neema ya kuzijua siri za ufalme wa mbinguni…
Hivyo kama hujampa Kristo Yesu Maisha yako, ni vizuri ukafanya hivyo leo… Na ili uwe mwanafunzi wake piga gharama za kumfuata…na Bwana akusaidie katika hilo.
Mungu akubariki sana.
Tembelea /www wingulamashahidi org/ kwa masomo Zaidi.
No comments:
Post a Comment