"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, June 17, 2019

LILE TUMAINI LILILO NDANI YETU LINAPOULIZIWA.


Jina la mwokozi wetu YESU KRISTO lisifiwe daima, Nakukaribisha ndugu mpendwa tujifunze maandiko, Leo tutangazia kwa sehemu kitabu cha waraka wa kwanza wa Petro tutaona Neno kuu la msingi ambalo mtume Petro aliwasihi ndugu wote katika Bwana ambao walikuwa wanaishi kama wageni katika mataifa mengi, Ikumbukwe kuwa wakati ule dhiki kuu ilipotokea Yerusalemu, wakristo wakiyahudi walipokuwa wakitafutwa wafungwe na kuuawa, wengi wao waliondoka Yerusalemu, na kukimbilia katika mataifa mengine ya mbali, vile vile na kule katika mataifa wale wakristo waliopokea injili nao pia hawakuwa katika hali ya usalama, nao pia shetani alikuwa anawawinda na hivyo walikuwa wanahama hama. Na ndio maana ukisoma nyaraka zote za mitume utaona wakristo wote walikuwa wanajulikana kama wasafiri, wageni na wapitaji katika dunia.

Na ndio maana tunaona waraka huu wa kwanza wa Petro, anauandika kwa watu wote(wakristo wa-kimataifa na wa-kiyahudi). Walio katika UTAWANYIKO, yaani kwenye mataifa mengine ya kigeni, Tunasoma hayo katika :
1Petro 1:1 “Petro, mtume wa Yesu Kristo, kwa wateule wa Utawanyiko, wakaao hali ya ugeni katika Ponto, na Galatia, na Kapadokia, na Asia, na Bithinia;
2 kama vile Mungu Baba alivyotangulia kuwajua katika kutakaswa na Roho, hata mkapata kutii na kununyiziwa damu ya Yesu Kristo. Neema na amani na ziongezwe kwenu.”
Unaona sasa ukisoma waraka huu utaona Petro akiwasihi wawaheshimu watu wote, wawe na mwenendo mzuri, watii mamlaka, waheshimiane wao kwa wao, wasaidiane, wapendane, na wasishitakiwe kwa jambo lolote ovu, ili kusudi kwamba watu wa mataifa wasiomjua Mungu wao wasipate Neno la kuwashitaki. Aliwasihi pia wakristo wote waliopo huko wavumilie, na zaidi ya yote wafurahie pale wanapoteswa kwa ajili ya Kristo.
1Petro 4:13 Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.
14 Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia.
15 Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya, au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine.
16 Lakini ikiwa kwa sababu ni Mkristo asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo.”
Unaona?, Huko katika mataifa ya ugenini, walikuwa ni kama kioo, na matamasha,watu wote wanawaangalia..Lakini mwisho wa siku Mtume Petro akawaambia maneno haya:

“Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.” (1Petro 3:15)

Hii ikiwa na maana kuwa itafika wakati wale watu wanaowazunguka watavutiwa kujua nini hasa sababu ya wao kuwa hivyo.Japo kuwa ni wageni, japokuwa wanapitia dhiki na mateso na shida lakini bado wapo na msimamo wao..Nini hasaa hawa watu wanakitazamia?.. Ndio hapo mtume Petro anawaasa sasa wawe tayari kuwaeleza habari za TUMAINI lililo ndani yao..
Kwamba ule uzuri waliowekewa mbele yao, na ufalme ambao upo karibuni kufunuliwa na wao wakiwa kama wafalme na makuhani,Taifa takatifu la Mungu pamoja na kiongozi wao mkuu Yesu KRISTO,kama MFALME wa Wafalme, ndio sababu inayowafanya waishi kama walivyo, wakae mbali na dhambi na matendo yote ya giza, wasione kama hizo dhiki na mateso ni kitu kikubwa katika maisha yao kulinganisha na tumaini lilipo mbele yao.(1Petro 2:9)

Embu jaribu kufikiria huyo mtu akisikia hivyo ataachaje kubadilika. Na sisi vivyo hivyo tunapaswa tuishi kama wapitaji, kama wageni wasafiriji, huku tukiwa na TUMAINI la amani na furaha, ili siku moja nasi tuulizwe na watu wasiomjua Mungu, watu wenye mahangaiko, wenye hofu ya maisha na mizigo ya dhambih watuulize je! Mbona nyinyi mpo hivi na bado maisha yenu ni ya amani.. Nasi ndipo tuwaeleze TUMAINI lililo ndani yetu habari za YESU KRISTO...kwa upole na hofu, sio kwa kuwatisha hapana bali kwa upole na hofu biblia inatuambia hivyo. Na mwisho tutajikuta wengi wanavutiwa na TUMAINI hilo..Lililo la kweli.
Wafilipi 3:1 “Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika Bwana….”
4 Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini.
5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. BWANA YU KARIBU.
6 Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.
7 Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.(Wafilipi 4:4-7)
Amen.

1 comment: