"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, June 12, 2019

MADHARA YA KUUPIZIA MAAGIZO YA MSINGI MUNGU ANAYOKUPA.


Jina la Bwana wetu Yesu Kristo lisifiwe, nakukaribisha mtu wa Mungu tujifunze Maneno ya uzima, na leo tutajifunza ni kwanini Mungu alitaka kumuua Musa mwanzoni kabisa mwa huduma yake japokuwa yeye mwenyewe ndio aliyemuita na kumthibitishia kuwa atakuwa pamoja naye. Tukilifahamu hilo kwa undani itatusaidia na sisi kuielewa tabia ya Mungu, na hivyo kuchukua hatua stahiki tusije tukajikuta tunaangamia kwa uzembe fulani.

Tunafahamu sababu kubwa iliyomfanya Musa akimbie kule Misri ni ile hali ya yeye kutetea chimbuko lake (yaani la Kiebrania), tunaona alipomuua Yule Mmisri aliyekuwa anapigana na Mwebrania alikimbilia nyikani kwa Wamidiani na hakurudi tena Misri mpaka miaka 40 ilipoishia, sasa huo wakati wote alipokuwa katika Ardhi ile ni wakati ambao Mungu alikuwa anampitisha Musa katika madarasa ya kimaisha afahamu vizuri chimbuko lake, Mungu “alimtweza”, hicho kipindi chote, hivyo akafahamu vizuri asili yake, huku akisaidiwa na mkwewe Yethro, ambaye ndiye alimpa binti yake aliyeitwa Sipora awe mkewe, Wote hawa walikuwa ni wazao wa Ibrahimu isipokuwa kwa mama tofauti, Waisraeli walitoka kwa Sara, lakini Wamidiani (yaani wakina Yethro mkwewe Musa), walitokea kwa mke mdogo aliyeitwa Ketura ambaye Ibrahimu alimtwaa baada ya Sara kufa.

Hivyo wote walikuwa ni ndugu, na wote walimwabudu Mungu mmoja, sasa kumbuka wakati huo Torati ilikuwa bado haijafika, kwani Torati ilikuja kutolewa na Musa, lakini lilikuwepo agizo moja KUU ambalo Ibrahimu alipewa na Mungu kwa wazao wake wote, kama dalili ya agano aliloingia yeye na Ibrahimu, na agizo hilo lilikuwa ni TOHARA kwamba wazao wake wote watahiriwe, Hivyo mtoto yoyote anayezaliwa bila kupoteza muda siku ya 8 anapaswa atahiriwe kisha apewe jina..Na kwa kufanya hivyo atakuwa tayari kashahesabika kuwa ni mazao wa Ibrahimu mrithi wa Baraka zote Mungu alizomwahidia Ibrahimu na uzao wake.

Hivyo watoto wote wa Ibrahimu walitahiriwa, haikujalisha ni wa mke yupi ni wa kijakazi Hajira, au wa Sara au wa Ketura…haikujalisha hiyo, wote walitahiriwa kufuata maagizo waliyopewa.. Hivyo ilikuwa ni jambo la ajabu na la kushangaza itokee mzao yoyote mpaka amefikia mtu mzima hajatahiriwa,kwanza ulikuwa unaonekana ni kafiri, na unatengwa na jamii yote, Kama tu walikuwa hawashirikiani kwa chochote na mataifa ambayo hawajatahiriwa unadhani ukiitwa mzao wa Ibrahimu halafu hujatahiriwa utachukuliwaje?. Sio tu wazao wa Ibrahimu watakukataa bali pia Mungu mwenyewe atakukataa.

Sasa Musa alilifahamu hilo, mpaka akazaa watoto, lakini hakuliweka akilini kuwa kila mzao wa Ibrahimu wa kiume anapaswa atahiriwe, yeye alipuuzia, alilichukulia kiwepesi wepesi tu, kama jambo lisilokuwa na umuhimu mkubwa kwenye mambo ya rohoni na hivyo mpaka akazaa mtoto,akakua mkubwa, siku ya 8 ikipita, mwezi ukapita, miaka ikapata yupo naye tu…

Wakati huo wote Mungu hakumsemesha chochote, mpaka ikafikia wakati Mungu alipomwita kule mlimani, na kumpa maelekezo ya kwenda kuwaokoa wana wa Israeli, Mungu akamthibitishia kuwa atakuwa naye, kwa miujiza na ishara kubwa..

Na ndivyo ilivyo leo hii watu wanaona Mungu akitembea nao kwa ishara kubwa na miujiza wanapumbazika wakidhani kuwa hiyo yote ni kwasababu Mungu amependezwa nao.

Lakini angalia kilichomtokea Musa, kumbe huku nyuma Mungu alikuwa amepanga kumuua, kabla hata hajafika mbali, akiwa njiani usiku, Yule malaika ambaye alienda kuwaua wazaliwa wa kwanza wa Wamisri alikuwa ameshaandaliwa kumamliza Musa habari yake iwe imeishia pale pale.

Lakini mke wake Sipora kuona vile aligundua kuwa ni lile kosa la mume wake kuwa mzembe kutotimiza maagizo ya Mungu kwa mwanae, hivyo alichofanya haraka, alidhubutu kwenda kinyume cha taratibu akachukua jiwe kali akakata govi la mwanae, japo Sipora hakupendezwa na kitendo kile na ndio maana akamwambia Musa “Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi.” Hayo tunayasoma katika kitabu cha Kutoka:
Kutoka 4:24 “Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa kulala, Bwana akakutana naye akataka kumwua.
25 Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi.
26 Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri.”
Unaona, Musa alipata neema tu kwa Mungu pamoja maono yake makubwa ya kwenda kuwaokoa wana wa Israeli lakini asingefika mbali. Mambo kama hayo hayo yalimtokea Balaamu, aliambiwa asiwalaani Israeli lakini yeye akakang’ang’ania kwenda kule kwa Balaki ambako Mungu amemwambia asiende….lakini yeye akakazana kung’ang’ania kwenda mwishowe Mungu akamruhusu aende na kumpa maagizo ya kufanya huko aendako…. lakini kumbe njiani Mungu a alikuwa amepanga kumuua, Ni Punda tu ndio aliyemsaidia vinginevyo safari yake ingeishia pale (Hesabu 22).

Ndugu, Ni vizuri tukaitambua tabia ya Mungu ili na sisi yasitukute kama hayo, Leo hii Sipora wala Punda hawapo. Kumbuka wakati ule Tohara ya mwili ilikuwa ni muhimu mpaka Mungu alitaka kumuua Musa kwa uzembe wa Tohara ambayo si ya kwake, itakuwaje wewe ambaye sasahivi unaipuuzia tohara ya Roho yako ambayo hiyo inanguvu mara nyingi sana kuliko ile ya mwilini.

Biblia inasema:
Warumi 2:28 “Maana yeye si Myahudi aliye Myahudi kwa nje tu, wala tohara siyo ile ya nje tu katika mwili;
29 bali yeye ni Myahudi aliye Myahudi kwa ndani, na tohara ni ya moyo, katika roho, si katika andiko; ambaye sifa yake haitoki kwa wanadamu bali kwa Mungu”.
Utasema, mbona Mungu huwa ananionyeshaga maono?, mbona huwa kila siku ananishuhudia kwenye ndoto mimi ni mteule wake, Mbona huwa ananitumia kutenda miujiza na maajabu, mbona huwa anajibu maombi yangu, mbona huwa ananipigania katika biashara zangu na shughuli zangu na mambo yangu yote, ..Lakini nataka nikuambie kama hujatolewa govi katika moyo wako, KIFO KITOKACHO KWA BWANA KIPO MBELE KINAKUNGOJA.

Sasa swali TOHARA hii YA ROHO ZETU INAFANYIKAJE?
Wakolosai 2:11 "Katika yeye [YESU KRISTO] mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya Kristo.
12 Mkazikwa pamoja naye katika UBATIZO; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu."
Unaona hapo, tohara iliyosahihi baada ya kuamini kwa mkristo, kwa kuyaacha maisha yake ya kale, ni KUBATIZWA, kama ishara ya kwamba umekufa pamoja naye na kufufuka pamoja naye. Watu wengi wanapuuzia haya maagizo marahisi wanayaweka kando halafu wanataka kwenda kumtumikia Mungu..
Wanapumbazika pale wanapoona ishara zikifuatana nao, lakini kumbe Mungu kaweka kifo mbele yao, ndugu weka kwanza msingi wako imara ndipo nyumba itasimama, utawahubiria nini watu wamfuate Kristo wakati wewe mwenyewe huamini katika tohara ya Roho yako na katika ubatizo ambao Bwana wako alikuwa ni mkamilifu aliuendea wewe ni nani usifanye?…

Ikiwa wewe ulishamwamini Kristo, au ndio unampokea leo hii, usikawie kwenda kubatizwa ipasavyo ili kutimiliza haki yote. Na kumbuka pia ubatizo sahihi ni ule wa kuzamwishwa katika maji mengi na uwe ni katika JINA LA YESU KRISTO ambalo ndilo jina la Baba na mwana na Roho Mtakatifu..sawasawa na mitume walivyobatiza (katika Matendo 2:38, 8:16, 10:48, 19:5).

Hivyo Ikiwa unajiiona wewe ni nabii mkuu zaidi ya Musa, au mtu wa rohoni, basi uyatumbue ya kuwa hayo ni maagizo ya Mungu.

Bwana akubariki sana.

No comments:

Post a Comment