SWALI: Maandiko yanasema Eliya aliomba kwa bidii hadi akasimamisha mvua kunyesha kwa MUDA wa miaka 3 na nusu.(Yakobo5:17) Je! kuomba kwa bidii ni kuomba kwa namna gani?
JIBU: Tukisoma:Yakobo 5:17 “Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita.18 Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake.”Kwakuwa habari hii inamzungumzia Eliya hivyo ili kuelewa vizuri hiyo bidii aliyokuwa nayo ni vizuri tukarejea kwenye tukio halisi lenyewe ili tuone ni jinsi gani aliomba. Sasa ukiangalia vizuri utaona biblia haijatoa maelezo mengi juu ya maombi aliyoyaomba siku ile alipozuia mvua. Inaonyesha tu Eliya akitokea kwenye tukio na kuzungumza maneno yale na kuondoka,1Wafalme 17:1 "Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu.2 Neno la Bwana likamjia, kusema,3 Ondoka hapa, geuka, uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordani."Lakini siku ile anarudi, ili kuifungua tena mbingu kwa Neno la Mungu, tunaona halikuwa ni jambo la kutamka na kuondoka tu kuna vitu viliendelea pale embu Tusome:1Wafalme 18:41 “Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele.42 Basi Ahabu akainuka ili ale na kunywa. Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu kifudifudi, akainama uso mpaka magotini.43 Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Enenda tena mara saba.44 Ikawa mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Enenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie.45 Ikawa, muda si muda, mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua nyingi. Ahabu akapanda garini, akaenda zake Yezreeli.”Hapo unaweza ukajifunza mambo kadhaa, cha kwanza Eliya kabla hata hajamwomba Mungu, alishaamini kuwa mvua inakwenda kunyesha siku hiyo katika nchi, na ndio maana alikuwa na ujasiri wa kumwambia Mfalme Ahabu inuka unywe kwani pana sauti ya mvua tele. Pili alipoonenda magotini sasa ili kumwomba Mungu jibu lake halikuja ndani ya wakati alioutazamia pengine aliomba lisaa la kwanza, akitazamia kabla hata hajamaliza juu kutakuwa kumeshafunga, lakini Yule mtumishi wake alipoenda alirudisha repoti kuwa juu hakuna dalili yoyote ya mvua kunyesha, lakini aliendelea kukaa uweponi mwa Bwana akimshukuru kwa matendo yake makuu, lisaa lingine likapita akamwambia mtumishi wake haya nenda katazame tena, akarudi akasema hakuna kitu, ikaendelea hivyo hivyo lisaa la tatu, la nne, mpaka lisaa la 7 pengine, akamwambia nenda katazame usichoke, ndipo Yule mtumishi wake akarudi akasema ninaona kawingu kadogo kama cha mkono wa mtoto mchanga,Ndipo Eliya alipoacha kuomba akijua kuwa tayari imekwisha kuwa..Na kama ingetokea hakuna kitu chochote kilichotokea ni wazi kuwa angeendelea hivyo hivyo hata mara 20 au 50, au 100 kwa nguvu ile ile akijua kuwa Mungu ameshamsikia..Huko ndiko kuomba kwa BIDII ambapo hata sisi tunapashwa tuwe nako, Ni rahisi kumwamini Mungu tunapompelekea mahitaji yetu lakini kudumu uweponi Mwake hatuwezi pale tunapoona majibu yanachelewa kidogo, hayajaja ndani ya wakati tuliotuzamia..Tunaanza kumtilia Mungu mashaka pengine hajatusikia. Lakini tukiendelea kushikilia na kumwamini Mungu kuwa ameshatenda, hata kama itapita siku, wiki, mwezi, miaka, ukizidi kushikilia nakwambia milango yote itafunguka mbele yetu.Hivyo kwa ufupi kuomba kwa bidii kunakozungumziwa hapo ni Kukaza kumwamini Mungu mpaka majibu yanapotokea.
Ubarikiwe sana.
SWALI: Ninachanganyikiwa sana katika suala ya kunena kwa lugha mpya, Je! hizi lugha ni zipi, na je! ni lazima kila mkristo aliyepokea Roho Mtakatifu anene kwa lugha mpya?.
JIBU: Hili ni moja ya jambo linalowachanganya wengi sana, Na nilinichanganya hata mimi pia kwa muda mrefu, na lingine linalofanana na hili ni juu ya uthibitisho halisi wa mtu kuwa amepokea Roho Mtakatifu ni upi?..Lakini napenda ufahamu kuwa tukiweza kutofautisha kati ya hivi vitu viwili yaani “vipawa vya Roho Mtakatifu” na “Roho Mtakatifu” mwenyewe tutaweza kuondoa huu utata kwa sehemu kubwa sana..Biblia inasema Kunena kwa lugha ni moja ya karama ya Roho Mtakatifu kama zilivyokarama nyingine, mfano Unabii, miujiza, uponyaji, ualimu, uinjilisti n.k. Lakini hatutaenda sana huko turudi kwenye msingi wa swali letu linalouliza juu ya Kunena kwa Lugha.Tukirudi nyuma kidogo kabla siku ile Bwana Yesu kupaa, aliorodhesha baadhi ya ishara ambazo zitaambata na wale wote waliomwamini na mojawapo ya ishara hizo alisema watanena kwa lugha mpya. Marko 16:17 “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; 18watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya”.Sasa Neno “Lugha mpya”, ni Neno lisilo na mipaka (Halifungiki), yaani kwa ufupi Lugha yoyote usiyoijua wewe ukiinena kwako ni Lugha mpya, iwe ni ile iliyopo katika nchi yako, au nje ya nchi yako, au iwe ya ulimwengu huu au sio ya ulimwengu huu maadamu hauitambui bado kwako ni Lugha mpya.Hivyo ukisoma maandiko utaona ulikuwa ni mpango wa Roho Mtakatifu tangu zamani, kuwa utafika wakati atazungumza na watu wote wa ulimwenguni kwa lugha tofauti, unabii huo unaweza kuusoma katika Isaya 28: 11 “La, bali kwa midomo ya watu wageni, na kwa lugha nyingine atasema na watu hawa;”Sasa utagundua kumbe lengo la kwanza Roho Mtakatifu kusema kwa lugha gheni katikati ya watu ni ili kuwavuta kwake wamwamini. Hapa ni lazima atumie lugha za kibinadamu, Mfano dhahiri ni kile kilichotokea Siku ile ya Pentekoste, Walijikuta wote wanazungumza Lugha za mataifa mengine ya mbali na wale waliokuwa wanasikia wote walishikwa na butwaa na kusema hakika haya matendo makuu ya Mungu..Na kwa kitendo kile tu maelfu ya watu walivutwa Kwa Kristo. Na jambo hili liliendelea kwa muda mrefu sana.Na pia kusudi la pili la lugha hizi Roho Mtakatifu kuziachia duniani ni ili kudhihirisha uwepo wake katikati ya waaminio, Hapa ndipo mtu anajikuta ananena lugha asiyoifahamu kwa uweza wa Roho wa Mungu..kuna Lugha za kimbinguni pia, ambazo hizo hazina matunda yoyote kwa watu wasioamini, na ndio maana Mtume Paulo alionya akasema ikiwa mtu atajikuta katika hali kama hii basi na anyamaze na anene na nafsi yake mwenyewe na Mungu wake kwa jinsi anavyojaliwa, vinginevyo ataonekana kama mwendawazimu kama akifanya hivyo katikati ya watu wasioamini, na Mungu sikuzote ni Mungu wa utaratibu.(1Wakorintho 14:28). Fikiri mtu asiyeujua kabisa Ukristo, anaingia kanisani ghafla anashangaa watu wanaanza kuzungumza lugha zisizoeleweka…moja kwa moja atahisi amekutana na watu pengine ni wendawazimu au wanaabudu miungu..lakini akiingia na kusikia lugha yake pale inaongelewa katika ufasaha wote na anayeiongea sio hata wa jamii ya watu wake..Na maneno anayoongea ni ya kumtukuza Mungu..atashangaa sana na kuogopa kusema huu ni muujiza?..na hivyo atajua mahali pale kuna uwepo Fulani wa kiMungu na hivyo atatubu na kumgeukia Mungu.Na kusema kuwa kila mwaminio ni lazima anene kwa lugha mpya, kauli hiyo inapingana kabisa na maandiko. Kumbuka kuwa mtu haneni lugha kama apendavyo yeye, au ajisikiavyo yeye bali ni kama vile Roho ANAVYOMJALIA MTU KUTAMKA (Soma Mdo 2:4), kama tu vile mtu asivyoamua kuona maono mpaka Mungu amwonyeshe na lugha ndio ziko hivyo hivyo..Vinginevyo mtu utakuwa ananena tu kwa akili zake, na ndivyo watu wengi walivyofanya leo hii, ambayo yanafanya tunaonekana kama watu waliorukwa na akili..Kunena kwa lugha ni kipawa cha Mungu na Mungu anakigawa kwa jinsi apendavyo yeye mwenyewe, mmoja atampa lugha mpya, mwingine unabii, mwingine tena uponyaji, mwingine uongozi, wingine matendo ya miujiza, mwingine kufundisha n.k..lakini wote hatuwezi kuwa manabii, au wote waalimu au wote wenye kufanya matendo ya miujiza au wote wenye kunena kwa lugha au wote wachungaji.1Wakorintho 12.27 "Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake.28 Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha.29 Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza?30 Wote wana karama za kuponya wagonjwa? WOTE WANENA KWA LUGHA? Wote wafasiri?."Na jambo lingine la muhimu la kufahamu ni kuwa mtu anaweza kuwa na ananena kwa lugha mpya lakini bado asiwe na Roho Mtakatifu ndani yake, kama tu vile mtu anaweza akawa ni nabii, akaona maono yote duniani, na asiwe nabii wa kweli, kama tu vile mtu anaweza akaponya magonjwa kwa karama Mungu aliyompa na kufanya miujiza mingi isiyokuwa ya kawaida na bado Kristo asimtambue.(Mathayo 7:21).Hivyo usijisifie karama, kwasababu Roho Mtakatifu sio karama yeye ni zaidi ya hicho, ikiwa utapenda kupata maelezo marefu juu ya uthibitisho fasaa unaomtambulisha mtu kuwa amepokea Roho Mtakatifu atanitumia ujumbe inbox, nikutumie somo lake.Hivyo kwa kumalizia ikiwa wewe ni mmojawapo wa waliokirimiwa kipawa hichi Unaponena kwa lugha mwombe pia Mungu akupe kutafsiri, Sehemu hii inaonekana kwa wachache katika kanisa lakini ndio inayofaa zaidi, kuliko kunena tu maneno yasiyojulikana kanisani mbele ya watu, kwasababu hilo linaweza kuwa na manufaa tu kwako mwenyewe lakini lisiwe na msaada wowote kwa wengine.Lakini kama litaambatana na tafsiri hilo linafaa sana na lina nguvu kwasababu linalijenga kanisa la Kristo kwa ujumla.1Wakorintho 14:27 “Kama mtu akinena kwa lugha, wanene wawili au watatu, si zaidi, tena zamu kwa zamu, na mmoja na afasiri.14.28 Lakini asipokuwapo mwenye kufasiri na anyamaze katika kanisa; aseme na nafsi yake tena na Mungu.”Jivunie karama yako ikiwa inalijenga kanisa la Kristo, na sio kwa kujionyeshea kuwa ni hodari wa kunena, Mtume Paulo alijisifia zaidi ya mtu yoyote, lakini alisema ni heri anene maneno matano lakini yanalifaa kanisa kuliko kunena maneno Elfu kwa lugha.
Bwana akabariki.
SWALI: Kwanini Bwana Yesu alisema pale msalabani naona kiu?
JIBU: Kulikuwa na sababu kuu mbili kwanini Bwana Yesu kuzungumza maneno yale, Sababu ya kwanza ilikuwa ni ili kutimiza maandiko kama Yohana alivyoandika katika Injili yake.Yohana 19:28 “Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu.”Unaona hapo?. Ikumbukwe kuwa sehemu kuwa ya unabii aliomuhusu Yesu katika agano la kale ulitimia ndani ya wakati huu wa Mateso ya Bwana Yesu. Yaani matukio mengi sana yaliyokuwa yanatendeka na kutokea ndani ya kile kipindi kifupi cha wiki moja ya mwisho yalikuwa ni mfulilizo wa matukio ya kinabii..Jaribu kifikiria kitendo kama kile cha Yesu tu kupigwa kofi (Yohana 18:22), tayari kilishatabiriwa kitafanyika (soma Ayubu 16:18),kutemewa mate(Ayubu 30:10),kusalitiwa,vazi lake kupigwa kura, kudhihakiwa. (zab 22)n.k...Vivyo hivyo na kusema hili nina KIU tayari lilishatabiriwa kama tu vile yale maneno mengine kama“Eloi Eloi Lama sabakthani” yalivyotabiriwa kwahiyo alisema maneno yale ili kutimiza maandiko.Pia Ikumbukwe kuwa Bwana Yesu alikaa msalabani muda wa saa 6, licha ya mahangaisho yale ya huku na kule kubebeshwa misalaba na jana yake na pamoja usiku uliopita alikuwa akikesha katika majonzi mengi na kupigwa bila kula wala kuonja chochote, ni wazi kuwa Kiu kilimshika sana Tunasoma katika…hakuna mwanadamu wa kawaida ahangaishe hivyo halafu asisikie kiu..haiwezekani…Na unabii wa kuchoka kwake ulitabiriwa pia katika Biblia kitabu cha zaburi.Zab 22:15 ‘Nguvu zangu zimekauka kama gae, Ulimi wangu waambatana na taya zangu; Unaniweka katika mavumbi ya mauti”…Unaona hii ni kuonyesha kuwa mwili wake alikaukiwa na maji mpaka mdomo wake ukawa mkavu kiasi cha ulimi wake kuganda kwenye taya zake.. Na ndio maana akasema nasikia kiu.Lakini pia sababu nyingine ya pili ambayo ni ya rohoni, ilikuwa ni kuonyesha kuwa sasa shughuli yote imekwisha, ni wakati sasa wa kunywa, maadui wamekwisha shindwa. Sikuzote kiu huwa kinakuja baada ya kufanya kazi Fulani ngumu ya kuchosha,au mazoezi n.k.. na ndio maana tunamwona Samsoni Siku ile wayahudi walipomfunga kamba na kumpeleka kwa wafilisti kwa usalama wa nchi yao,waliona ni heri wampoteze mtu mmoja ili taifa letu zima lisiangamie mikononi mwa wafilisti, kama tu vile wayahudi walivyomfunga Bwana Yesu na kumpeleka kwa watu wa mataifa wamsulibishe,walisema ni heri mmoja afe ili taifa zima lisiangamie mikononi mwa Warumi. Lakini tunajua ni kitu gani kilitokea pale mara baada ya vita kuisha pale Samsoni alipowapiga wale wafilisti 1000 kwa taya ile moja ya Punda, Tunasoma Samsoni aliona KIU sana.Waamuzi 15:15 “Naye akaona mfupa mbichi wa taya ya punda, akautwaa, akapiga watu elfu kwa mfupa huo;16 Samsoni akasema, Kwa taya ya punda chungu juu ya chungu, Kwa taya ya punda nimepiga watu elfu.17 Ikawa, alipokuwa amekwisha kunena akautupa ule mfupa wa taya mkononi mwake; na mahali pale pakaitwa Ramath-lehi.18 Kisha akaona kiu sana, akamwita Bwana akasema, Wewe umetupa wokovu huu kwa mkono wa mtumishi wako; na sasa nitakufa kwa kiu, na kuanguka katika mikono ya watu wasiotahiriwa.19 Lakini Mungu akapasua mahali penye shimo palipo katika Lehi, pakatoka maji; naye alipokwisha kunywa, roho yake ikamrudia, akaburudika; kwa hiyo jina la mahali pale likaitwa Enhakore, napo pa katika Lehi hata hivi leo.20 Naye akawa mwamuzi wa Israeli: katika siku za Wafilisti muda wa miaka ishirini.”Hivyo kitendo cha Yesu kutoa kauli ile ilikuwa ni ishara ya rohoni kuonyesha kuwa tayari shetani kashashindwa vita..Na ndio maana maneno yaliyofuata baada ya pale yalikuwa ni haya IMEKWISHA!.(Yohana 19:30).
Ubarikiwe.
SWALI: Shalom! Nisaidie mistari hii mwandishi alikuwa na ufunuo gani, Mhubiri 7 :15-18
JIBU: Shalom,Tukianza na mstari wa 15 anasema: “Mambo hayo yote nimeyaona mimi katika siku za ubatili wangu, yuko mwenye haki apoteaye katika haki yake, yuko na mtu mwovu azidishaye maisha yake katika udhalimu wake.Huyu ni Sulemani akizungumza maneno hayo, anasema akiwa katika siku za UBATILI wake, yaani akiwa katika siku za masumbuko yake ya kutafuata jumla ya mambo yote, alikutana na Fumbo moja ambalo lilimtatiza sana, na Fumbo lenyewe ndio hili “yuko mwenye haki apoteaye katika haki yake, yuko na mtu mwovu azidishaye maisha yake katika udhalimu wake”. Au kwa lugha nyingine iliyorahisi ni kusema wenye haki wengi hawaishi muda mrefu, lakini wale waovu ndio wanakuwa na maisha marefu. Aligundua Kumbe haki haipimwi kwa kipimo cha umri mrefu mtu anaoishi.Fumbo hili linafanana na lile lingine alilolisema katika Mhubiri 9: 11 “Nikarudi, na kuona chini ya jua, ya kwamba si wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo; lakini wakati na bahati huwapata wote.”Hata wewe mambo haya yatagon kwenye kichwa chako lakini huo ndio uhalisi, Ni mara ngapi unasikia na kutazama wale watu ambao hawana elimu,wala hawana ujuzi tena kama wamefika mbali sana, wengine labda ni darasa la 7 lakini hao ndio wanaokuwa matajiri sana? . Hili ni funzo kwako ikiwa utatafuta ujuzi au elimu kwa kigezo cha kuwa bilionea, utavunjika moyo , vilevile ikiwa unautafuta ufalme wa mbinguni ili uje upate utajiri kwa sadaka, kadhalika utavunjika moyo sana! Au leo hii unaokoka ili mambo yako ya kiuchumi yakae vizuri, yaani hiyo ndio sababu ya wewe kuokoka.. unajeweka katika hatari kubwa ya kuvunjika moyo huko mbeleni...Hekima na wokovu havina ushirika na pesa kabisa..Tukiendelea na mistari unaofuata anasema ..Mhubiri 7: 16 "Usiwe na haki kupita kiasi; Wala usijiongezee hekima mno; Kwani kujiangamiza mwenyewe?17 Usiwe mwovu kupita kiasi; Wala usiwe mpumbavu; Kwani ufe kabla ya wakati wako?18 Ni vizuri kwamba ulishike neno hilo; naam, hata kwa neno hilo tena usiuondoe mkono wako; kwa kuwa mtu yule amchaye Mungu atatoka katika hayo yote.”Kuna mambo mawili hapo la kwanza usiwe na haki kupita kiasi na pili usiwe mwovu kupita kiasi, yote haya yanaweza kukusababishia kifo ambacho hakijafikia umri wake. Lakini nataka upigie mstari jambo moja hapo la msingi hasemi usiwe na haki au usiwe na hekima, hapana bali anasema usiwe na haki KUPITA KIASI wala usiwe na HEKIMA KUPITA KIASI, hii inafunua tabia ya kujikweza, kujionyesha kuwa wewe ni kitu Fulani, wewe ni mtakatifu kuliko wengine, mifano dhahiri ya matukio kama haya tunayo, tunaweza kuyaona si kwa wengine zaidi ya waandishi na mafarisayo..Ukisoma Luka 18:10 utaona Bwana Yesu alitoa mfano huu…. “Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru.11 Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.13 Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.14 Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.Unaona, walijihesabia haki kupita kiasi, kufunga kwao, kutoa kwao zaka,kutokuzini kwako, ndio kulikowapa kiburi wajione wao ni kundi fulani maalumu mbele za Mungu na hiyo iligeuka kuwa hasara kwao kwa kuupoteza wokovu ambao wao ndio wangetakiwa waupate wakwanza..Hivyo kama tukiangalia maudhui ya huyu mhubiri hasaa yalikuwa ni kutaka kuonyesha kuwa, sio mwenye haki, sio mwovu, sio mwenye hekima kupita kiasi sio mpumbavu anaweza kujiongeza maisha kwasababu ya mwenendo wake.Na ndio maana anahitimisha kwa maneno haya “18 Ni vizuri kwamba ulishike neno hilo; naam, hata kwa neno hilo tena usiuondoe mkono wako; KWA KUWA MTU YULE AMCHAYE MUNGU ATATOKA KATIKA HAYO YOTE.””Unaona, ukimcha Bwana utaepukana na hayo yote, Kumcha Bwana ni kujinyenyekeza mbele za Mungu kwa kuitii injili yake na maagizo yake yote anayokupa kwa kufanya hivyo basi utapata hekima iliyo sahihi ya kumwendea mbele zake..Ndio mhubiri maana huyo huyo anasema kumcha Bwana ndio chanzo cha hekima na maarifa, Na sio hekima ndio chanzo cha kumcha Bwana.hivyo leo hii mtu Yule atakayekubali kumtii Kristo na kuyaishi maneno yote aliyoyasema atakuwa na uhakika kuwa amesimama upande ulio salama.Lakini ukiwa mtu wa dini(kama mafarisayo na waandishi, ambao wao wanajiona wao tu ndio wanao Mungu wengine wote ni waovu, Na hiyo inawafanya hata hatawaki kusikia jambo lingine lolote, mfano tu leo, hata mtu umwelezeje kwamba biblia inasema hivi, maadamu tu dhehebu lake au dini yake halifundishi hivyo au haliamini hivyo basi hakusikilizi,..huko ni kujihesabia haki kupita kiasi biblia inakokukataza), Na ukiwa pia mwovu, mambo hayo mawili basi jua utakumbana na mauti (rohoni na mwilini).Ubarikiwe.
No comments:
Post a Comment