Shalom Mtu wa Mungu, karibu tujifunza Maandiko..Leo kwa Neema za Bwana tutajifunza kwa ufupi juu ya HASIRA YA KIMUNGU…Tusome Mstari ufuatao kabla ya kuendelea ambao utatusaidia kuelewa kiini cha somo letu.
Waefeso 4:26 ‘Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka;’’
Ukisoma mstari huu kwa haraka haraka ni rahisi Kuchanganyikiwa na kufikiri biblia imehalalisha mambo baadhi maovu..Lakini leo tutajifunza kwa ufupi tafsiri ya mfano huo, ambapo tukishaelewa itatusaidia na sisi kuenenda kama maandiko yanavyotaka tuenende.
Sasa ukiusoma kwa utaratibu mstari huo, unaona biblia inasema mwe na hasira ILA MSITENDE DHAMBI!...Haijasema tu mwe na hasira basi halafu ikaishia hapo, bali imesema mwe na hasira ila msitende dhambi…ikiwa na maana kuwa hasira inayozungumziwa hapo sio ile hasira inayozaa dhambi…
Mfano wa hasira inayozaa dhambi ni kama ile mtu anatukanwa na anakasirika na matokeo ya ile hasira ni kumwekea kinyongo yule aliyemtukana, au kumchukia, au kutafuta kisasi au kutokumsamehe…sasa hizo ni hasira zinazozaa dhambi ambazo sio zilizozungumziwa hapo kwenye Waefeso 4:26.…kwasababu kinyongo, kutokusamehe, kisasi, chuki, wivu nk hivyo vyote ni dhambi.
Sasa swali linakuja ni hasira gani inayozungumziwa hapo?...Ili kuielewa hiyo hasira inayozungumziwa hapo ambayo haizai dhambi tusome tena mstari ufuatao wa mwisho…tutapata majibu.
Marko 3: 1 ‘Akaingia tena katika sinagogi; na palikuwako huko mtu mwenye mkono uliopooza;2 wakamvizia ili kuona kama atamponya siku ya sabato; wapate kumshitaki.3 Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, Simama katikati.4 Akawauliza, Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya? Kuponya roho au kuiua? Wakanyamaza.5 Akawakazia macho pande zote kwa HASIRA, AKIONA HUZUNI KWA AJILI YA UGUMU WA MIOYO YAO, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Naye akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena’.
Umeona hapo Hata Bwana Yesu alikuwa na HASIRA, lakini hasira yake haikuwa hasira yenye hatima ya dhambi bali hatima ya HUZUNI kwa ajili upofu wao..Na hiyo ndio hasira Mtume Paulo aliyokuwa anaizungumzia katika Waefeso 4:26 kuwa ‘Mwe na hasira, ila msitende dhambi’…Hasira aliyokuwa anaizungumzia hapo ni hasira ya kutamani mtu Fulani apone na sio hasira ya kumwangamiza mtu. Kama Bwana Yesu alivyofanya hapo! Alikasirika kwa huzuni, aliona kwanini hawa watu wanaona miujiza yote hii lakini mioyo yao bado migumu? Ikamfanya akasirike huku akiwahuzunikia.
Ili tuweze kuelewa tena vizuri jaribu kuutafakari mfano huu , imetokea mwanao kafanya jambo Fulani baya sana, labda amekutukana wewe kama mzazi wake, na ulishamwonya mara nyingi awe na tabia njema…bila shaka utakasirika lakini hasira hiyo sio ya kumchukia au kumwekea kinyongo mwanao bali ya kumhuzunikia!...utakasirika huku unahuzunika, huzuni hiyo ni ya kutamani abadilike, sio afe.
Na sisi hasira zetu zinapaswa ziwe hivyo hivyo, unapotukanwa na mtu, au unapoaibishwa, au unapodhihakiwa na kuudhiwa kwa sababu ya jambo Fulani au kwasababu ya njia unayoiendea ya haki…hasira inaweza kuja wakati mwingine lakini hasira hiyo inapaswa isiwe kwa kutenda dhambi, bali kwa kuwahuzunikia kwa wanayoyafanya, kuudhiwa kama mkristo kupo kwa namna moja au nyingine, na kama haujakutana nako leo ipo siku utakutana nako
1 Timotheo 3:12 ‘Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu WATAUDHIWA.’
Sasa siku wanapokufanyia mambo yasiyostahili, sio wakati wa kuwaombea na wenyewe wapatwe na yaliyokukuta wewe, badala yake ni kuwahurumia ukijua si wao bali ni shetani anafanya kazi ndani yao..
Utaudhiwa kila mahali unapokwenda, utakutana na watu ambao hawatakuelewa kwa chochote utakachowaambia, kama ilivyokuwa kwa Bwana hakueleweka kwa baadhi ya watu mpaka jambo hilo likawa linamkasirisha. Walikuwa wanatoa maneno ya kumkera sana, na ndio siku ile kabla ya kuondoka kwake akawaambia mitume wake.
Yohana 15: 20 ‘Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi;…’’.
Bwana akubariki sana, naamini utakuwa umepata kitu…
Ukiwa bado hujampa BWANA YESU Maisha yako, basi jua Upo kwenye hatari kubwa kuliko hata hatari ya kupata ajali yoyote ile…Bwana Yesu ndio Njia, na kweli na Uzima..Mtu hafiki mbinguni bila njia yake yeye..Hivyo nakushauri ufanye maamuzi sahihi leo ya kumkaribisha moyoni mwako..atakusamehe bure pasipo gharama yoyote na atakufanya kuwa kiumbe kipya, kwasababu ndicho anachokitaka kwako..
Hivyo unachopaswa kufanya hapo ulipo, ni kujitenga kwa muda mchache na kutubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kutozifanya tena…unakusudia kuacha uasherati moja kwa moja, ulevi moja kwa moja, anasa na mambo yote mabaya ya ulimwengu huu…na ukishakusudia kufanya hivyo…Bwana ataona umemaanisha kumfuata kwa moyo..hivyo atakuandalia zawadi ya Roho wake Mtakatifu ambaye atauzika kabisa ule utu wako wa kale ambao ulikuwa unakufanya ushindwe kuishinda dhambi, na atakuvika utu upya ambao katika huo utaweza kuishinda dhambi kiurahisi kabisa..Lakini hilo ni mpaka umekusudia kweli kweli kumfuata yeye.
Hivyo mkaribishe leo, moyoni mwako kabla mlango wa Neema haujafungwa..
Maran atha!
No comments:
Post a Comment