"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, July 23, 2019

MLINZI, NI HABARI GANI ZA USIKU?


 
Licha ya kulinda, jukumu lingine kuu mlinzi alilonayo ni kuhisi hatari kutoka mbali, Na ndio maana utaona mnyama ambaye Mungu alimuumba kutulinda sisi (Mbwa), licha tu ya kupewa ukali, lakini pia amepewa uwezo wa kunusa mbali,na kusikia, na ndio maana wakati wa usiku utaona mbwa wanabweka sana, hiyo ni kutokana na kuwasikia na kunusa vitu vilivyo mbali sana visivyo vya kawaida, ambavyo hata wewe huwezi kuvihisi au kuvisikia, ule wakati ambao unaouna ni wa utulivu na salama lakini kwa Mbwa ni machafuko.

Vivyo hivyo na mlinzi yoyote, hana jukumu la kulinda tu pale adui anapokuja, bali pia anajukumu la kuhisi hatari, na hiyo inakuja kwa kupepeleza, kuchunguza, kutafiti na kutazama, na wakati mwingine kufanya doria, itakayomsaidia kuhisi tatizo kabla halijatokea.. na thamani ya mlinzi sikuzote ipo usiku n.k…
Isaya 21:11 “Ufunuo juu ya Duma. Mtu ananililia toka Seiri, Ee mlinzi, habari gani za usiku? Ee mlinzi, habari gani za usiku?
12 Mlinzi akasema, Mchana unakuja na usiku pia; mkitaka kuuliza, ulizeni; njoni tena.”
Ukisoma hata katika agano la kale utaona walinzi wa miji walikuwa wanakaa katika minara mirefu, ili kuwasaidia kuona kitu kinachokuja kutoka mbali, na wakiona hatari basi bila kuchelewa tarumbeta lilikuwa linapigwa na mji wote kujiweka tayari kwa vita.

Ezekieli 33:1 “Neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, sema na wana wa watu wako, uwaambie, Hapo nitakapoleta upanga juu ya nchi, watu wa nchi hiyo wakimtwaa mtu mmoja miongoni mwao, na kumweka AWE MLINZI WAO;
3 ikiwa, aonapo upanga unakuja juu ya nchi hiyo, apiga tarumbeta na kuwaonya watu;
4 basi mtu awaye yote aisikiaye sauti ya tarumbeta, wala haonywi, upanga ukija na kumwondoa, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe.
5 Aliisikia sauti ya tarumbeta, wala hakuonywa; damu yake itakuwa juu yake; lakini kama angalionywa, angalijiokoa roho yake.”

Lakini kama mji utakosa walinzi, au watazamaji, ni dhahiri kuwa utakuwa katika hatari ya kuvamiwa na maadui wakati wowote, na siku maadui watakapokuja watakuja ghafla wenyeji hawatajua chochote kwasababu hawakuwa na waonaji wanaoona mbele yao.

Ndivyo Bwana alivyotabiri jinsi itakavyokuwa katika hizi siku za mwisho, kuja kwake kutakuwa kwa ghafla, kama mwivi usiku wa manane.
(Ufunuo 16:15 “Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake”.)
vile vile mwisho wa dunia utawajia watu kwa ghafla,

(2Petro 3:10 “Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea”.)

na hiyo yote ni kwasababu wamekosa MLINZI katika mioyo yao.

Na ndio maana jambo kuu na la muhimu sana ambalo Bwana Yesu alituachia siku ile aliyokuwa anaondoka, alikuwa ni ROHO MTAKATIFU, akamwita ni msaidizi wetu, kwa namna nyingine ni mlinzi wetu, alijua kabisa, wakati wa giza utapita duniani, na sikuzote giza linaleta usingizi, hivyo kama hatakuwepo mtu wa kuwasaidia kukesha nao, watasinzia na uharibifu utawapata kwa ghafla…

Hivyo akatugawia Roho Mtakatifu, ambaye ndio tupo naye sasa, wote waliompokea kila siku anawashuhudia ndani ya mioyo yao hatari iliyopo duniani sasahivi na jinsi ya kuwa waangalifu. Anawataarifu kila iitwapo leo habari za mwisho wa dunia na kuja kwa Kristo. Na hawa ndio wale hata siku ile ya unyakuo itakapokaribia sana kufika wataifahamu, kwasababu mlinzi wa kuwapasha habari yupo mioyoni mwao.

1 Wathesalonike 5 :1 “Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.
2 Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.
3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.
4 Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi”.
 
Unaona, wale waliojazwa Roho Mtakatifu ndio siku hiyo hajitawapa kama mwivi kwasababu, atakuwepo kuwapasha habari juu ya mambo yote yanayokuja. Watajua kabisa wakati wa kuondoka umefika, kama wanavyoshuhudiwa hata sasa, itakapofika kipindi kifupi sana kabla ya unyakuo, mlio wa kengele utazidi kuongezeka ndani ya mioyo yao.

Yohana 16:13 “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, NA MAMBO YAJAYO ATAWAPASHA HABARI YAKE”.

Lakini wale wengine, ambao hawana ROHO MTAKATIFU sasa, ndio wale hata wakisikia kuwa tunaishi siku za mwisho hawashtuki,mioyoni mwao hakuna mabadiliko yoyote, macho yao yamefumbwa, ukiwaambia Yesu Kristo yupo mlangoni kurudi, wanakudhihaki, Na wengine tayari walishampa Bwana maisha yao, zamani walikuwa wanaishi kama wana wa mbinguni lakini baada ya muda na wao wamegueka wakafanana na watu wengine wa kidunia, hao ndio wale ambao wamemzimisha ROHO MTAKATIFU ndani yao, Yule mlinzi anayewalinda amelala, na hivyo hawezi tena kuwapasha habari ya mambo yanayokuja na hatari iliyopo mbele yake.
Mtunzi wa Zaburi aliandika hivi, kwa wachao Mungu..

Zaburi 121:3 “Asiuache mguu wako usogezwe; ASISINZIE AKULINDAYE;
4 Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli.
5 BWANA NDIYE MLINZI WAKO; Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume.”

Wapo ambao, awalindaye amesinzia, na hao ndio wale wanawali wapumbavu wanaozungumziwa katika Mathayo 25. Ambao kwa pamoja na wenzako (wale wanawali werevu) walikuwa wanamngoja Bwana wao, lakini kwasababu hawa hawakuwa na mafuta ya ziada katika chupa zao, wakarudi baadaye wakakuta mlango umeshafungwa, kule kuishiwa na mafuta ndio kumzimisha Roho..Kwasababu mwanzoni walikuwa nayo lakini baadaye yaliwaishia..Na mafuta siku zote katika biblia yanamwakilisha ROHO MTAKATIFU.

Ndugu yangu nataka nikuambue tunaishi katika siku za mwisho, hakuna mtu asiyejua kuwa Dalili zote zimeshatimia, Jiulize Kristo akirudi leo kulichukua kanisa lake, utaufichia wapi uso wako wewe ambaye bado unasuasua, kwa injili ulizokuwa unahubiriwa kila kukicha lakini bado hutaki kugeuka?. Roho Mtakatifu kila siku anagonga katika mlango wa moyo wako lakini hutaki kufungua. Biblia ipo wazi inasema na mtu yoyote asiyekuwa na Roho wa Kristo huyo sio wake (Warumi 8:9).

Ni maombi yangu utamruhusu huyu mlinzi ayaongoze maisha yako kuanzia sasa katika hichi kipindi kifupi tulichobakiwa nacho kabla ya hii dunia kuisha..Kama ulikuwa umepoa, au umemzimisha Roho Mtakatifu ndani yako, ni wakati wa kutengeneza mambo yako upya sasa. Na kama hujamkabidhi Bwana maisha yako, unachopaswa kufanya ni kutubu kwa kudhamiria kabisa kuacha dhambi, kisha kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi,kwa jina la YESU KRISTO, kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako. Na ukishatii maagizo hayo mepesi Bwana mwenyewe atamshusha Roho wake Mtakatifu ndani yako, kuanzia huo wakati na kuendelea naye atakuongoza na kukupasha habari ya mambo yote yahusiyo saa tunayoishi na siku za mwisho, na hatimaye siku ile haijakujia kama mwivi.

Bwana akubariki sana.
www.wingulamashahidi.org

No comments:

Post a Comment