"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, July 3, 2019

MUUNGANO WA DINI NA MADHEHEBU YOTE, UMEKARIBIA.


Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze biblia.

Bwana Yesu alituonya katika Mathayo 24:3 “Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia?
4 Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye.
5 Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi”
Sentensi hi ina maana watatokea watu katika siku za mwisho, ambao watasema wao ni makristo, kumbuka tafsiri ya Kristo sio Yesu, Tafsiri ya Kristo ni “ni mtiwa mafuta”..kwahiyo hapo aliposema watatokea wengi kwa jina lake na kusema mimi ni Kristo maana yake watatokea wengi wakisema wao ni watiwa mafuta wa Mungu..na watatumia Jina la Yesu, lakini ni watiwa mafuta wa uongo. Hivyo tumeonywa tuangalie wasitudanganye.

Kitu kimoja kikubwa ambacho wengi hawajui ni kwamba shetani sasahivi anafanya kazi yake ya kupotosha kwa kutumia biblia..Hicho ndio kitabu chake kikubwa anachotumia kupotosha ukweli…wala hatumii vitabu vya kichawi au vitabu vya wa-uddha “pali canon” au vya wahindu “the vadas” au qurani cha waislamu, hapana! Hatumii hivyo, anatumia kitabu cha ukweli kuupotosha ukweli…. anahakikisha watu hawaielewi biblia, ili kila mmoja atoke na uelewa wake na tafsiri yake ya maandiko, na akishafanikiwa kufanya hivyo anawagawanya watu katika makundi makundi, yenye itikadi tofauti tofauti, jambo ambalo halikuwa mpango wa Mungu …kama Bwana alivyosema… “mwapotea kwakuwa hamyajui maandiko” ….Na Roho ya Mpinga-Kristo ndiyo inafanya kazi kwa njia hii, kuhakikisha inatenga watu katika vikundi vikundi…Na ikishawatenga baadaye inavikusanya hivi vikundi pamoja na kuviunganisha tena…Kumbuka hii roho haiunganishi watu! Wala haitafuti hicho, yenyewe inatafuta kuunganisha vikundi ambavyo vimewatenga watu. Ambayo ni roho mbaya sana hiyo.

Ili kuelewa vizuri hebu tafakari huu mfano…wanandoa wawili ambao walikuwa wameoana ndoa ya kikristo kabisa na kuishi Maisha ya furaha, halafu akatokea mtu akapandikiza fitna katikati yao wakaachana…na kila mmoja akaenda kuoa na kuolewa na mtu mwingine…na huko walikokwenda kila mmoja akapata Watoto na kutengeneza familia nyingine…halafu huyu mtu aliyewatenganisha baadaye anakuja kutumia bidii na nguvu kuzileta pamoja hizo familia mbili…zikae pamoja kwa amani na upendo, zishirikiane pamoja katika masuala ya kijamii na maendeleo..Hatafuti kuwarejesha pamoja hao walioachana kwamba warudiane, bali anatafuta kuzileta pamoja familia zao…kwamba kila mmoja abaki na mume wake au mke wake lakini wawe na umoja!. Bila shaka unaweza ukaona huyo mtu ni mnafiki na mbaya kiasi gani!!
Na ndio Roho ya Mpinga-Kristo inavyotenda kazi sasahivi, inawatoa watu katika umoja wa Roho ambao ndio Mungu anaoukusudia, inawavunja na kuwapeleka kwenye madhehebu mengi mengi…kila mmoja lina itikadi zake…Na mwisho sasa inataka kuyaleta haya madhehebu pamoja! Na huku kila moja likiwa katika itakadi yake, Haitawaleta watu pamoja hapana bali madhehebu!..

Ndugu huu ni wakati wa kuwa macho sana! Sio kila umoja ni Umoja wa kiMungu, na sio kila muungano ni muungano wa kiMungu..Mfumo wa madhehebu ni wa Ibilisi, inaumiza kusikia hivi lakini huo ndio ukweli…Kristo hajawahi kuanzisha dhehebu lolote na wala Kristo hajagawanyika kama Paulo alivyosema katika…
1 Wakoritho 1:10 “Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja.
11 Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu.
12 Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu kusema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo.
13 Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo”
Mpaka kufikia sasa kuna Zaidi ya madhehebu 41,000 duniani..na kila siku yanazidi kuzaliwa mengine mengi…Na hivi karibuni yatakwenda kuungana…hayataungana kiimani bali kiitikadi…kwamba kila mmoja awe na dhehebu lake lakini tuwe na katiba Fulani moja ya kutuweka pamoja ambayo yeyote atakayeikiuka basi ataadhibiwa kisheria..
Dhehebu la kwanza kutengenezwa na shetani lilikuwa ni Katoliki, yakafuata mengine kama Lutherani,anglikani, mennomites, Baptist, SDA, Mormon, n.k..Kwahiyo katoliki ndio mama wa madhehebu yote unayoyaona leo…Ndio kitovu cha machafuko yote, na ndio makao makuu ya Mpinga-Kristo aliyetabiriwa..

Itafika wakati Siasa ya ulimwengu italemewa katika kutatafuta Amani ya dunia ambayo inaharibiwa na mvurugano wa kidini na vikundi vya kigaini kama ISI, anti-BALAKA, LRA, Boko Haramu, Alshabaab,Alqaeda, Hizbola, Taliban n.k itakiri imeshindwa hivyo suluhisho lingine la haraka litatafutwa, ambalo hilo litakuwa ni la mchanganyiko wa dini na siasa…

Atatafutwa kiongozi mkubwa ambaye ni wakidini na hapohapo ni wa kisiasa, ambaye atasaidia kuirejesha amani ya dunia..Na kiongozi pekee atakayeonekana hapo si mwingine bali atakuwa ni Papa, hivyo atapewa nguvu na mataifa yote duniani…kuwa aamue juu ya amani ya dunia..Na Papa atakachokifanya kwasababu ndani yake ni roho ya mpinga-kristo yenyewe inatenda kazi, atauambia ulimwengu kuwa chanzo cha matatizo yote ni kwasababu hatuna UMOJA! Hivyo atakuja na agenda ya kuyaunganisha kwanza madhehebu yote ya kikristo na kuyawekea katiba moja! Hatayalazimisha kama inavyodhaniwa na wengi…hapana bali atayashawishi kwa kuyadanganya…ataitisha kikao cha viongozi wote wa madhehebu na kuweka chini mada kadhaa, na hivyo wale viongozi watadanganyika na kuwamwini Papa, na hivyo kutia muhuri maneno atakayoyasema, tunavyozungumza sasa hivi ni kuwa mikakati hiyo inaendelea kuzungumziwa mara kwa mara katika baraza la EKUMENE… Na Papa hataishia tu kuyaunganisha madhehebu yote ya kikristo bali atayaunganisha na madhehebu ya kiislamu na kuyawekea katiba yake inayohusiana na uislamu, na dini nyingine zote zitakazosalia atakazokaa nazo vikao.

Na katiba hiyo itakapokamilika itakuwa na sheria Fulani mpya, na utaratibu Fulani mpya..hivyo utaanza UTARATIBU MPYA WA ULIMWENGU..Zitakuja sheria kwamba mtu yeyote asiyekuwa mshirika wa dhehebu lolote au dini yoyote ambayo halijasajiliwa katika umoja huo, atakamatwa na kupelekwa kwenye magereza Fulani maalumu, lengo ni kuwakamata watu wa ovu ili kuleta umoja kwenye jamii..Na hayo magereza kwa nje yataonekana ya kawaida lakini ndani yatakuwa ni ya mateso Makali sana ya siri. Kadhalika kila mtu itampasa akahakiki taarifa zake za muhimu kama vile benki, hospitali, Bima, usajili wa shule na vituo vya kazi, TIN na moja ya taarifa hizo pia itakuwa ni DHEHEBU UNALOABUDIA..kama dhehebu lako sio mshirika wa huo umoja, basi uhakiki wako hautakamilika…..Na wote wasiofanya hivyo unajua ni kitu gani kitafuata…hawataweza kununua chochote kwasababu kadi zao za benki zitakuwa zimefungwa kwa kutokuhakikiwa taarifa zao, hawataweza pia kusafiri kwa sababu passport zao zitakuwa zimefungiwa, hawataweza pia kuuza kwasababu TIN zao za biashara hazijahakikiwa upya kwa mfumo huo mpya hivyo zitafungwa, kadhalika hawataweza kununua kwasababu hawatakuwa na pesa yoyote ya kununulia kutokana na hivyo vikwazo, vya kushindwa kufanya kazi..

Hivyo ndivyo chapa ya mnyama itakavyofanya kazi…kutakuwa hakuna kimbizana huko barabarani kupigwa stika Fulani kwenye mkono au uso, huko ni kufikira kidhaifu.
Ndugu tunaishi katika siku za mwisho sana, siku si nyingi unyakuo utapita..na hayo mambo yataanza kufanyika..sasahivi mambo hayo yameshaanza kujiandaa kutokea ndio maana unasikia hapa na pale, Papa ameunganisha dhehebu hili na lile, utasikia sheria za kutaka usajili wa madhehebu ufanyike zinapitishwa n.k

Kristo anatuambia.. “Tokeni huko enyi watu wangu Ufu.18:4” maana ya kutoka kwenye madhehebu ni kurudi kwenye umoja wa Roho ambao ndio Mungu alioukusudia tangu mwanzo, yaani kurudi kwenye NENO LA MUNGU. Ukiulizwa kwanini unafanya hivi au kwanini hufanyi vile unasema ni kwasababu Neno la Mungu linasema hivyo, na sio kwasababu dhehebu linasema hivyo, ukiulizwa wewe ni dini gani au dhehebu gani, jibu ni rahisi tu wewe ni MKRISTO. Yanayozidi hapo yamehasisiwa na ile roho ya Mpinga-Kristo (roho ya udhehebu), ambayo inawapumbaza watu wasiuone ukweli. …

Kipindi Madhehebu ya mafarisayo na masadukayo yalipopatana na wanasiasa Herode na Pilato kupata ndipo wakati wa Bwana kuondoka ulikuwa umekaribia kadhalika Unapoona huu muunganiko huu unajiandaa kutokea ni wakati wa kuwa macho sana, unyakuo umekaribia, ukombozi wetu pia umekaribia.

Bwana akubariki sana.

No comments:

Post a Comment