Tukisoma katika biblia mahali pengine Bwana alijitambulisha kama ALFA na OMEGA.
Ufunuo 22: 12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho”.
Hapo kuna vitu vitatu…1) Yeye ni Alfa na Omega…2) Yeye ni mwanzo na mwisho….3) Yeye ni wa kwanza na wa mwisho.
Hizo ni sentensi tatu zinazoelezea maumbile ya Mungu. Hebu tuzitame kwa ufupi moja baada ya nyingine.
ALFA NA OMEGA:
Tafsiri ya Alfa na Omega sio mwanzo na mwisho, kama inavyofahamika na wengi…ingekuwa ndiyo tafsiri yake hiyo, visingetenganishwa vitu vitatu hapo juu…Sasa Afla ni herufi ya kwanza kwenye alfabeti za Kingiriki..yenye alama hii (α) Na Omega ni herufi ya mwisho ya kwenye alfabeti za lugha ya kigiriki yenye alama hii (ω)…Kwenye alfabeti zetu sisi herufi ya kwanza ni (A) na ya mwisho ni (Z)….kwa kigiriki ya kwanza ndiyo hiyo alfa na ya mwisho ni omega.
Kwahiyo katika mstari huo aliposema yeye ni alfa na omega, alikuwa anajitambulisha uungu wake katika umbo la NENO. (Kumbuka hapo mwanzo kulikuwako Neno….naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa ni Mungu,…Vitu vyote vilifanyika kwa huyo wala pasipo yeye hakuna chochote kilichofanyika Yohana 1:1).
Kwahiyo akiwa katika Neno, yeye ndiye Neno la Kwanza na ndiye Neno la Mwisho, kwahiyo ili lijitambulishe lazima litumie Herufi kujitambulisha, (herufi ya kwanza na ya mwisho, alfa na Omega)… Kwanini hakutumia herufi ya A na Z?..ni kwasababu lugha zinazotumia alfabeti hizi kama vile kiingereza zilikuwa hazijazaliwa bado, na hata kama zingekuwa zimeshazaliwa bado zilikuwa ni lugha changa, kwani wakati Yohana anapewa haya maono lugha iliyokuwa kuu na uliyozungumzwa sehemu kubwa ya dunia ilikuwa ni kigiriki, hata lugha iliyotumika kuandika vitabu vingi vya agano jipya ni lugha hii, ndio maana yakatumika maneno ya kigiriki.
Yeye ni MWANZO NA MWISHO:
Sifa ya pili, Hapa Mungu anajitambulisha kwa umbo la MUDA….
Kama alivyosema mahali Fulani yeye ni UPENDO, na sio yeye ana upendo…kadhalika hapa, anajitambulisha kuwa yeye ni MWANZO na sio yeye ana mwanzo!..halikadhalika yeye ndiye MWISHO, na sio yeye mwenye mwisho…yeye hana mwanzo na wala hana mwisho, kwasababu yeye ndio mwanzo wenyewe na ndio mwisho wenyewe.
Ili uelewe vizuri hebu tafakari jambo hili: umewahi kuchunguza mwanzo wa magharibi ni upi? Au mwisho wa magharibi ni upi?...au mwanzo wa mashariki ni upi na mwisho wake ni upi?..utakuja kugundua kuwa mashariki haina mwanzo wake wala mwisho wake, vivyo hivyo na magharibi haina mwanzo wala haina mwisho,kwasababu mahali ulipo tayari panaweza kuwa ni mashariki ya mbali sana kwa sehemu nyingine halikadhalika panaweza kuwa ni magharibi ya mbali sana kutoka sehemu nyingine…kwahiyo hapo ulipo tayari ni ni mwanzo na mwisho wa magharibi na mashariki. Kuna mstari wanaouita kitaalamu IDL huo ndio wanasema umetenganisha mashariki na magharibi lakini kiuhalisia hakuna mstari pale…Wamebuni tu, ili kuwarahisishia kutimiza matakwa yao ya kijeografia, lakini hakuna mwanzo wa mashariki wala magharibi, ingawa kuna mashariki na magharibi..
Na ndio Mungu yupo hivyo hivyo, ingawa kuna kitu kinaitwa MWANZO na Mwisho, lakini yeye hana mwanzo, wala hana mwisho……kwasababu yeye pale alipo ndio mwanzo na ndio mwisho….Na kama vile tunavyozidi kuelekea sana mwisho wa mashariki ndivyo tunavyojikuta tunatokea mwanzo wa mashariki hiyo hiyo…kadhalika na Mungu…tunapodhani tunamjua sana na hivyo tumefika karibia na mwisho wa kumjua yeye…kumbe ndio tupo mwanzo wa kumjua yeye….Na pale tunapodhani yupo mbali sana na sisi kumbe ndio yupo karibu sana na sisi, na pale tudhaniapo kuwa tumemkaribia sana, kumbe bado sana tumfikie..Kwasababu yeye ndio mwanzo na ndio mwisho, akili zake hazichunguziki, wala hakuna mtu anayeweza kumwelezea asilimia mia na kusema sasa nimemjua Mungu.
Isaya 40:28 “Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki.”
Yeye ni WAKWANZA NA WAMWISHO:
Sifa ya tatu na ya mwisho, Hapa Mungu anajifunua na kujitambulisha katika umbo la mtu…Lile Neno lililojitambulisha kwa herufi alfa na Omega, sasa linavaa mwili na kujitambulisha kama Mtu, na kusema Yeye ni wa Kwanza na wa Mwisho.
Hapa anaelezea Uungu wake kabla ya vitu vyote..Yeye alikuwepo kabla ya kiumbe chochote kile…kabla ya Malaika na kitu kingine chochote…ndiye wa Kwanza, akaitoa sehemu ya roho yake akatuumba sisi wanadamu na malaika…Na hivyo sisi wote tumetoka kwake…Na mwisho wa siku tutarudi kwake..kwasababu yote yametoka kwake..
Mungu wetu hakuna linalomshinda, wala hakuna asilolijua, utasemaje leo hakujui, wala hajui unayopitia?..huyu mwanzo na mwisho utasemaje kakusahau?..hajakusahau alisema “hata nywele za vichwa vyetu zimehesabiwa zote (Luka 12:7)”….kama anajishughulisha na mambo madogo sana ya nywele zetu atashindwaje kujishughulisha na mambo makubwa ya Maisha yetu, Hivyo kuna baraka nyingi sana katika kumwamini huyu Mungu.
Lakini pia huyu Mungu ni alfa na Omega, maneno yake ndio mwanzo na mwisho, akisema Neno lake ni lazima litimie, na halirekebishwi wala halina marekebisho…limehakikiwa na limejitosheleza, akisema roho itendayo dhambi itakufa…ni kweli itakufa, akisema mtu asipozaliwa mara ya pili hawezi kuurithi ufalme wa mbinguni…maneno yake hayo ni alfa na Omega..yatatimia kama yalivyo, akisema atakuja ni kweli atakuja..
Hivyo mpaka sasa bado anawaalika watu karamuni, je! Wewe ni mmoja wao wa walioalikwa?..kama bado unasubiri nini, usigeuke leo na kutubu? Siku ile utakuwa mgeni wa nani utakapojikuta upo kuzimu?..kumbuka hakuna nafasi ya pili kwa mtu yeyote atakayekufa katika dhambi leo,..wengi wanajifariji kuwa mbele ya kiti cha hukumu watakuwa na hoja za kujitetea, nataka nikuambie siku ile kutakuwa hakuna kujitetea…Kwasababu hakuna yeyote awezaye kumtega wala kumkamata Mungu kwa maneno.
Bwana akubariki sana.
Sawa kabisa Mungu akubariki
ReplyDeleteThanks ffor a great read
ReplyDelete