"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, July 25, 2019

SIKU YA TAABU YA YAKOBO.


Yeremia 30:7 “Ole! Maana siku ile ni kuu, hata hapana inayofanana nayo, maana ni wakati wa taabu yake Yakobo; lakini ataokolewa nayo.”
Biblia inasema ni siku ambayo haiwezi kufananishwa na siku yoyote katika historia ya siku zote za dunia ambazo zilishawahi kuwepo mambo ambayo yataenda kulikuta Taifa la Israeli, Hicho ndio kipindi cha taabu kuu ambacho Danieli alionyeshwa;
Danieli 12: 1 “ Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na wakati huo watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile”.
Na Bwana wetu Yesu Kristo alikuzingumzia pia, kuweka msisitizo wa uzito wa dhiki hiyo ..
Mathayo 24:21 “Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe.
22 Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo.”
Na cha kuzingatia ziadi ni kuwa dhiki hii haitakuja wakati wowote isipokuwa wakati ambapo Israeli imesharudi na kuwa kitu kimoja kama zamani za kale za mfalme Daudi na Sulemani.
Yeremia 30:1 “Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema,
2 Bwana Mungu wa Israeli, asema hivi, ya kwamba, Uyaandike kitabuni maneno hayo yote niliyokuambia.
3 Kwa maana, tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapowarejeza watu wangu wa Israeli na Yuda waliofungwa, asema Bwana; nami nitawarudisha hata nchi niliyowapa baba zao, nao wataimiliki…………
7 “Ole! Maana siku ile ni kuu, hata hapana inayofanana nayo, maana ni wakati wa taabu yake Yakobo; lakini ataokolewa nayo.”
Na jambo hilo lilitimia mwaka 1948, baada ya kukaa zaidi ya miaka 2500 bila kuwa taifa huru, Israeli sasa ni taifa huru, na sisi ni mashahidi kuwa tumeshaanza kuona mwanzo wa utungu wa mambo hayo, kipindi cha vita ya pili vya dunia jinsi wayahudi walivyouliwa kikatili na Dikteta wa kijerumani Adolf Hitler bila sababu yoyote, tafakari jinsi wanawake na watoto walivyokuwa wanachukuliwa uchi, na kudanganywa kuwa wanaenda kuogeshwa kumbe wanafungiwa kwenye mabafu ya gesi za sumu (Gas chambers), na huko ndani kwenye vyumba hivyo,vya giza inatupwa gesi moja kali ijulikanayo kama Zyklon B, inawaua watu kama kuku waliochinjwa, huku damu zikitoka midomoni na puani, ndani ya dakika 4 tu zinakuwa ni maiti zilizolala chini. Na mauaji mengine ya kikatili ukifuatilia katika historia utayaona. Wayahudi zaidi ya milioni 6 waliuliwa kwa namna kama hizo kikatili.

Sasa huo ni mfano mdogo sana,(mwanzo wa utungu) kwa hiyo dhiki itakayokuja huko mbeleni. Mambo yatakuwa mabaya zaidi, kutakuwa kuna mateso ya ajabu ambayo hayajawahi kufanyika popote, kama tu wakati wa Hitler watu walikuwa wanachukuliwa kwa marika tofautitofauti na wanawekwa kwenye barafu wakiwa uchi na wanaangaliwa mpaka wafe, huku wengine wakichukua data, kuchunguza ni rika lipi linawahi kufa katika hali ya ubaridi (na hiyo biblia inaiita tu ni mwanzo wa utungu)…unadhani itakuaje utungu wenyewe ukianza?....pengine watu watalishwa nyama za miili yao wenyewe wangali wakiwa hai….Dhiki hii Mungu atairuhusu kwa watu wake Israeli, na watu wa mataifa wachache ambao walibaki kwenye unyakuo….na hiyo yote Mungu ameruhusu kwa makosa ya Israeli ukiendelea kusoma mistari inayofuata ya hiyo Yeremia 30 utaona, na atakayetekeleza hilo zoezi ni mpinga-Kristo, Wayahudi (Waisraeli) wataadhibiwa hivyo lakini baadaye Mungu atawaokoa..

Lakini mpaka hayo yote yatokee, Kanisa la Kristo litakuwa limeshanyakuliwa,mbinguni, Bibi-Arusi sikuzote haandaliwi kupitia dhiki bali anaandaliwa kwa ajili ya sherehe, na ndivyo itakavyokuwa kwa Bibi-arusi wa Kristo, wakati wote huu ambao yupo duniani sasa anaandaliwa kwa ajali ya karamu ya mwana-kondoo, ambayo Kristo amekuwa akituandalia mbinguni kwa miaka 2000 sasa, Siku watakapoisikia paraparanda ya Mungu ikiwaita, muda huo huo watageuzwa kufumba na kufumbua na kuwa na miili ya utukufu ya kimbinguni, wataungana na wale watakatifu waliolala,kisha kwa pamoja watapaa zao mbinguni, kumfurahia Bwana wao. Hivyo watakaopitia hii dhiki ni wale wanawali wapumbavu, ambao hawakujiweka tayari kwa ajili ya kumlaki Bwana wao akiwa hapa duniani….Hao ndio watakaojumuika na wayahudi,
Mathayo 25:6 “Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki.
7 Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao.
8 Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika.
9 Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.
10 Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa.
11 Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie.
12 Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi.
13 Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa.”
Utajisikiaje, siku ile unaona wenzako wapo juu mbinguni karamuni, halafu wewe umeachwa?, umetengwa na uso wa Mungu milele,Ikiwa neema unaichezea leo, usidhani itakuwepo kipindi kile, wakati huo neema ya Mungu itakuwa kwa wayahudi watu wake, kupigwa kwao upofu leo ni ili wewe na mimi tutubu tumgeukie Mungu, (soma Warumi 11:8-36 )wakati ule ukifika Mungu hatakuwa na habari tena na :wewe, au mtu yoyote wa mataifa, bali watu wake, wateule wake wayahudi. Na hao ndio Bwana atakaowakoa.

Hizi ni nyakati za mwisho ndugu, usipumbazwe na huu ulimwengu unaopita, angalia ni faida gani unakuahidia maisha baada ya hapa?, majira yanabadilika haya, matukio yanayotokea duniani, ni kuonyesha kuwa dunia imeshafika OMEGA. Acha kusuasua kwenye njia mbili, huu sio wakati wa kuhubiriwa injili ya kubembelezwa tena, mkabidhi Kristo maisha yako leo, tubu kabisa na umaanishe kumfuata, na yeye ni mwaminifu na mwenye huruma, hata kama dhambi zako ni nyingi kiasi gani ataziweka mbali na wewe. Tubu ukabatizwe, Upokee Roho Mtakatifu.

Bwana akubariki.Tafadhali “Share” Ujumbe huu kwa wengine. 

No comments:

Post a Comment