"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, July 9, 2019

USIPIGE MATEKE MCHOKOO!


Karibu tujifunze Biblia, leo tutajifunza juu ya kukaa katika kusudi la Mungu.

Tukizidi kujifunza juu ya wito wa Mtume Paulo, tunaweza kupata mambo mengi sana ambayo yataweza kutusaidia sisi katika kuongeza maarifa yetu ya kumjua Mungu. Tukisoma kitabu cha Matendo ya mitume mlango wa 26, biblia inasema…
Matendo26:14 “Tukaanguka nchi sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? NI VIGUMU KWAKO KUUPIGA MATEKE MCHOKOO. 15 Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi”.
Tunaona Mtume Paulo, alipokuwa anaelekea Dameski kuwakamata na kuwafunga wakristo ndipo akatokewa na Bwana njiani! Na Neno la kwanza kuambiwa ni “ Sauli Sauli mbona waniudhi?”… Hilo ni swali lisilokuwa na jibu..Ni kama vile Bwana alishawahi kumwonya mara nyingi lakini akawa hasikii…Maana ni ngumu mtu usiyemjua kuja kwako ghafla tu na kukwambia mbona unaniudhi?...Ni wazi kuwa huyo mtu mtakuwa mnajuana kwa namna moja au nyingine.

Kadhalika Paulo sio kwamba alikuwa hamjui kabisa Bwana Yesu, alikuwa anamjua na alishawahi kumsikia kipindi Bwana anaishi duniani, na alishaisikia injili ya kumvuta kwa Kristo hapo kabla…Kwasababu asingeweza kuanza kuwashika wakristo kama hakusikia kitu walichokuwa wanakihubiri, hivyo Roho Mtakatifu alikuwa anamvuta tangu zamani ndani ya moyo wake na kumshuhudia kabisa kuwa Kristo ndiye njia ya kweli lakini alikuwa anashupaza shingo, anaikataa ile sauti ndani yake, anashindana na agizo la Mungu. Ndio maana utaona hata wakati wa kifo cha Stefano alikuwepo pale akisikiliza Stefano alivyokuwa anahubiri…
Matendo 7:53 “ninyi mlioipokea torati kwa agizo la malaika msiishike.
54 Basi WALIPOSIKIA MANENO HAYA, WAKACHOMWA MIOYO, wakamsagia meno.
55 Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu.
56 Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu.
57 Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja,
58 wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli.
59 Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu.
60 Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. NA SAULI ALIKUWA AKIONA VEMA KWA KUUAWA KWAKE”.
Biblia inasema hapo waliposikia yale mahubiri ya Stefano “wakachomwa mioyo yao”…Maana ya kuchomwa mioyo hapo… “ni kufahamu kuwa kinachozungumziwa ni ukweli”…hakuna mtu anaweza kuchomwa moyo kama kitu kinachozungumzwa ni cha uongo hakuna! Ukweli ndio unaochoma watu mioyo….hivyo kwa wivu wakataka kumwua Stefano na Sauli naye (ambaye ndiye Paulo) naye alikuwepo pale pale akichomwa moyo akijua kabisa stafano anachozungumza ni kweli. Na kinachochoma watu mioyo ni Neno la Mungu ambalo ndilo KWELI yenyewe.

Kuna wengine ambao wakisikia Neno la Mungu wanachomwa mioyo na kukusudia kutubu au kuacha njia zao mbaya kama ilivyokuwa wakati wa Pentekoste kama tunavyosoma katika:
Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? 
38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu”..
Na kuna wengine wanaposikia Neno la Mungu linawachoma ndani wanaifanya mioyo yao kuwa migumu zaidi na kuipinga na kukusudia kumzimisha Roho ndio kama hawa wakina Sauli, walichomwa mioyo yao, lakini hawakutaka kutubu badala yake walimwua Stefano.

Kwahiyo Paulo alikuwa anajua kabisa kuwa Kristo ni mwana wa Daudi, na ni kweli alikufa na akafufuka.. moyoni alikuwa anashuhudiwa kabisa kuwa huo ndio kweli, na si yeye peke yake bali hata na baadhi ya makuhani na mafarisayo na wakuu, walikuwa wanajua kabisa Yesu ndiye Kristo lakini kwa kuwa wana wivu…wakawa wanampinga (Matendo 5:17, Marko 12:14).
Yohana 12:42 “Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi.
 43 Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu”.
Lakini kwasababu Sauli alikuwa anaipenda DINI kuliko kuyafuata mapenzi ya Mungu, akawa anashindana na agizo la Mungu, na kwa kuendelea kuwaua watumishi wa Kristo na hiyo ndio ikawa sababu ya Bwana kumtokea na kumwambia mbona waniudhi?...Na alipotokewa na Bwana jambo la kwanza kumwuliza ni nani wewe? Bwana?...anauliza swali na hapo hapo analo jibu!...alijua kabisa ni Bwana Yesu.

Sasa utaona baada ya Bwana kumwambia tu Sauli mbona waniudhi, kuna sentensi nyingine inayofuata hapo mbele yake…alisema “NI VIGUMU KWAKO KUUPIGA MATEKE MCHOKOO”

Sasa swali la kujiuliza mchokoo ni Nini?

Mchokoo ni fimbo Fulani yenye ncha ya chuma kwa mbele iliyokuwa inatengenezwa kwa mfano wa mkuki Fulani hivi, ambao wakulima wa zamani walikuwa wanaitumia kuwaongozea ng’ombe wakati wa kulima…Wakati wa kulima kulikuwa kuna ng’ombe baadhi waliokuwa na kiburi, hawataki kutembea mbele, wanaweza kuanza vizuri lakini wakifika katikati ya safari, ukijaribu kuwalazimisha tu kwenda mbele wanarusha mateke hivyo kazi inakuwa haiendi.....hivyo fimbo ya kawaida ilikuwa haiwezi kuwaongoza kwahiyo zamani ndio walikuwa wanatengeneza hiyo fimbo maalumu yenye ncha kwa mbele na kuiweka nyuma ya ng’ombe wakati wa kulima…endapo ng’ombe akikataa kusonga mbele na kurusha mateke anakutana na hiyo fimbo yenye ncha! Na inamchoma na kumwumiza, hivyo anajikuta anafanya kazi bila shuruti!..

Sasa ndio hapa Bwana anamwambia Paulo “Ni vigumu kwako kupiga mateke mchokoo”…Au kwa lugha nyepesi ni sawa na kusema “ni vigumu kwako kushindana na agizo la Mungu utakuwa unajiumiza mwenyewe”….

Bwana Yesu alimwona Paulo alikuwa anashindana na kusudi lake, na hivyo akamwambia atakuwa anajiumiza mwenyewe kwa wivu wake na hasira zake na chuki zake na kiburi chake juu ya kazi ya Mungu…Wakati anafikiria kuwaua watakatifu ndio kuwakomoa hakujua kuwa ndio anajitafutia mabaya mwenyewe, ndivyo anavyozidi kujiangamiza mwenyewe kama vile kujichomaa kwa mchokoo…….Na kama sio Bwana kumtokea njiani pengine huko alikokuwa anakwenda ndio kungekuwa mwisho wake asingerudi tena.…Kama tu Balaamu, wakati anafikiria kwenda kuwalaani Israeli wakati Bwana ameshamwonya kwa nguvu asiende, yeye akazidi kushindana na agizo la Mungu na kukusudia kwenda…kumbe njiani wakati anakwenda Bwana alikuwa ameshamkusudia mauti! Bwana alikuwa amemwandaa tayari malaika wake kumwangamiza…kama sio Punda kuzungumza naye, habari ya Balaamu leo isingekuwepo kwenye biblia.
Na hata leo, kuna watu pia wanashindana na kusudi la Mungu, Bwana anasema hivi? Wao wanasema hivi na kuwafundisha watu upotofu na hali wanajua kabisa wanachokifanya sio sahihi….huko ni kushindana na agizo la Mungu, ni kupiga mateke mchokoo hivyo utajiumiza mwenyewe? Usijaribu kushindana na kusudi la Mungu kwa namna yoyote ile, ni kujihatarishia Maisha..Unaona mahali injili inahubiriwa unakwenda kusumbua au kuvuruga, au kuweka kikwazo chochote isiendelee mbele, kwasababu tu ya hasira zako binafsi, au chuki zako au wivu wako…usifanye hivyo tena…

Unapojaribu kudhoofisha kazi ya Mungu kwa namna yoyote ile ni kupiga mateke mchokoo..ni kujitafutia shari badala ya heri..kwajinsi unavyoiharibu, ule uharibifu ni kama mkuki kwako, unapenya kwenye maisha yako kwa nguvu ile ile utakayoitumia kuharibu kazi ya Mungu…kama vile mchokoo unavyopenya kwenye nyama ya ng’ombe… Paulo na Balaamu walipata Neema tu! Ya kuonyeshwa hatari waliyokuwa wanaiendea mbeleni lakini inaweza isiwe hivyo kwetu (mimi na wewe)… Usiingilie kabisa kazi za Mungu kwa ubaya kwa namna yoyote ile..utakuwa unashindana na Mungu mwenyewe na si mwanadamu..KAA CHONJO!

Ubarikiwe sana.
www.wingulamashahidi.org

No comments:

Post a Comment