Karibu katika mwendelezo wa vitabu vya Biblia, leo tutaendele na vitabu 4 vya mbele, yaani Wafalme wa kwanza (1Wafalme), na Wafalme wa Pili (2Wafalme), Mambo ya nyakati wa kwanza (1Nyakati) na Mambo ya nyakati wa pili(2 Nyakati).. Tumekwisha pitia vitabu 10 vya kwanza, hivyo ni vizuri kama hujapitia maelezo ya vitabu vilivyopita, ukavipitia kwanza ili tuende pamoja katika hivi vitabu vinavyofuata.
Kitabu cha Wafalme wa kwanza na Wafalme wa Pili, kilikuwa ni kitabu kimoja, isipokuwa kiligawanywa katika sehemu mbili…Na mwandishi wa kitabu hichi alikuwa ni Nabii Yeremia. Ingawa Nabii Yeremia alizaliwa mwishoni kabisa mwa enzi za Wafalme lakini aliweza kukusanya rekodi zote za habari za Wafalme, kwani habari za kila mfalme na matendo yake zilikuwa zinarekodiwa na kuhifadhiwa kwenye vitabu maalumu vinavyojulikana kama vitabu vya Tarehe.
Lakini kwa ufupi Kitabu hivi viwili vya wafalme kama jina lake lilivyo, vinazungumzia Utawala wa wafalme wa Israeli, Na vitabu viwili vinavyofuata vya (1 Nyakati na 2 Nyakati) Ni marudio ya habari hizo hizo za Wafalme isipokuwa yana habari chache chache sana ambazo hazikurekodiwa katika kitabu cha wafalme…Ni sawa na injili iliyoandikwa na Mathayo na Luka ni vitabu viwili vilivyoandikwa na waandishi wawili tofauti lakini vyote vinazungumzia habari moja..ndivyo ilivyo kitabu cha Wafalme na Mambo ya nyakati, vyote vinaelezea habari moja za Wafalme wa Israeli…isipokuwa hichi cha mambo ya nyakati kimeanzia nyuma kidogo, kwa mfalme Daudi. Na mwandishi wa kitabu cha Mambo ya Nyakati alikuwa ni EZRA..ambaye ndiye aliyekiandika kitabu cha Ezra pia..Huyu alikuwa ni mwandishi..ambaye habari zake tutakuja kuziona tutakapofika katika kitabu cha Ezra..
Sasa tukirudi katika habari za Wafalme..kumbuka haukuwa mpango wa Mungu, Israeli wawe na Mfalme juu yao tangu mwanzo, lakini kwasababu ndio ilikuwa nia yao kukataa uongozi wa Mungu, usiohusisha mwanadamu, Mungu akawapa haja ya mioyo yao, lakini pamoja na hayo hakuwaacha…tofauti na sisi wanadamu, mtu asipofanya tunavyotaka tunamtupa moja kwa moja, hatutaki hata kumsikia tena, lakini kwa Mungu haipo hivyo, hakuwatupa Israeli watu wake moja kwa moja ingawa walimuasi…Hivyo Mungu akatengeneza njia ya kuwaokoa kwa kupitia hao hao wafalme waliowataka…
Kwahiyo kitabu cha Wafalme wa Kwanza, kinaanza na Mfalme Sulemani, ambaye alikuwa ni mfalme wa tatu wa Israeli akituanguliwa na Sauli na Daudi ambao habari zao utazipata katika vitabu vya Samweli. Sulemani alikuwa ni mwana wa Daudi, na mama yake alikuwa ni yule mke wa Uria, ambaye Daudi aliyemtamani..Hivyo baadaye Mungu alikuja kumfanyia wema mwanamke yule na kumfanya mwanawe kuwa mfalme juu ya Israeli, Sulemani alitawala miaka 40 katika Israeli, alianza vizuri lakini hakumaliza vizuri, kwani pamoja na Hekima yote na ufahari wote aliopewa na Mungu alikuja kukengeuka dakika za mwisho, na kwenda kuoa wanawake wa kigeni, ambao Mungu alimkataza asioe, (Nehemia 13:25-26 )na hao wanawake wakamgeuza moyo akaenda kutengenezea maashera hiyo miungu migeni, ambayo ni machafuko makubwa sana mbele za Mungu, Ingawa alikuja kutubu dakika za mwisho, na Bwana alimsamehe lakini tayari alikuwa ameshaisababishia Israeli madhara makubwa sana..
Sasa kabla ya kwenda kwenye madhara aliyoisababishia Israeli, tutazame jambo moja jema na kuu alilolifanya.; Tunaona baada ya kufa baba yake, yeye ndiye aliyekuwa na dhamana ya kumtengenezea Mungu nyumba, biblia inasema Mungu hakai kwenye nyumba zilizotengenezwa na mikono, lakini pamoja na Daudi kulifahamu hilo bado alilazimisha kumjengea Mungu nyumba hivyo hivyo, na Mungu akaliona hilo akapendezwa naye na kumbariki, na kuuchagua mji wake na kabila lake kuwa makao makuu ya kuweka jina lake, japo Mungu alimzuia Daudi asimjengee kwasababu alimwaga damu nyingi, hivyo mwanawe ambaye ni Sulemani ndiye atakayejenga HEKALU kwa niaba yake. Na wakati ulipowadia Sulemani wakati ulipowadia, alitumia akili nyingi, na hekima nyingi kuijenga ile nyumba…
Alikwenda kutafuta miti maalum na ya thamani kutoka nchi za mbali, na vito maalumu kutoka kila kona ya dunia, na kuileta Israeli, Zaidi alikwenda kutafuta watu wenye akili nyingi, kutoka mataifa mengine kusaidia kuongeza ujuzi katika ujenzi, kwahiyo Hekalu lilijengwa kwa gharama kubwa na kwa ujuzi wa hali ya juu, kulikuwa hakuna mfano wake duniani kote. Na lilitengenezwa Yerusalemu, katika mji wa kabila la Yuda, hakukusikika kelele yoyote wakati wa ujenzi, hivyo ilipunguza hata kasi ya maadui,kuvamia kwasababu hakuna mtu aliyekuwa anaelewa kitu kinachoendelea ndani..wengi walidhani kazi imesimama tu!..lakini ilikuwa inaendelea ndani kwa ndani…ghafla wanakuja kushangaa nyumba hii hapa imekamilika!..Sasa inawekwa wakfu kwa Mungu.
Mungu akalibariki Taifa la Israeli na Mfalme, kwa jambo hilo, na kukawa na amani kwa Zaidi ya miaka 40, lakini Sulemani alipokuwa mzee akakengeuka, na hivyo Mungu hakupendezwa naye tena, hakumwua lakini alimnyang’anya sehemu ya Ufalme wake, kwani hapo kwanza alikuwa anatawala makabila yote 12, kama Sauli na Daudi walivyokuwa wanatawala, lakini matokeo yake akapokonywa 10 akabakiwa na mawili tu, yaani kabila la Benyamini pamoja na kabila lake mwenyewe Yuda…lakini hakunyakang’anywa kwenye utawala wake bali wa mwanae.
1 Wafalme 11:1 “Mfalme Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti,2 na wa mataifa Bwana aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda.3 Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo.4 Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.5 Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni na Milkomu, chukizo la Waamoni. 6 Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, wala hakumfuata Bwana kwa utimilifu, kama Daudi baba yake.7 Sulemani akamjengea Kemoshi, chukizo la Wamoabi, mahali pa juu, katika mlima uliokabili Yerusalemu, na Moleki, chukizo la wana wa Amoni.8 Na kadhalika ndivyo alivyowafanyia wake zake wa nchi za kigeni, waliofukiza uvumba, wakawatolea miungu yao dhabihu.9 Basi Bwana akamghadhibikia Sulemani kwa sababu moyo wake umegeuka, naye amemwacha Bwana, Mungu wa Israeli, aliyemtokea mara mbili,10 akamwamuru katika habari ya jambo lilo hilo asifuate miungu mingine; lakini yeye hakuyashika aliyoyaamuru Bwana.11 Kwa hiyo Bwana akamwambia Sulemani, Kwa kuwa umefanya hayo, wala hukuyashika maagano yangu, na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitampa mtumishi wako.12 Walakini katika siku zako sitafanya haya, kwa ajili ya Daudi baba yako; nitaurarua utoke katika mkono wa mwana wako.13 Lakini sitauondoa ufalme wote pia; nitampa mwana wako kabila moja, kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, na kwa ajili ya Yerusalemu niliouchagua”
Hivyo hayo yote yalitokea wakati wa utawala wa mtoto wake Rehoboamu, na kuanzia huo wakati Israeli ikagawanyika sehemu mbili, kaskazini na kusini, upande wa kusini ndio huo uliokuwa na makabila mawaili (yaani Yuda na Benyamini) na upande wa kaskazini (makabila 10 yaliyosalia). Hivyo kaskazini wakawa na mfalme wao na Kusini wakawa na Mfalme wao…
Kaskazini PAKAITWA ISRAELI na kusini PAKAITWA YUDA. Hivyo Israeli ambayo hapo kwanza ilikuwa ni taifa moja ikagawanyika na kuwa mataifa mawili ndani ya Taifa moja…kutokana na dhambi ya Sulemani.
Hayo ndio madhara ya dhambi aliyoyaleta Sulemani, na ndio madhara ya dhambi, unaweza ukasema nikitenda dhambi fulani itaniathiri mimi peke yangu, haitawahusu wengine, nataka nikuambie ndugu, ukiwa mwamini ukifanya dhambi yoyote ya makusudi haitakuathiri wewe peke yako bali itaathiri na wengine na Zaidi ya yote itaathiri kazi ya Mungu, kwasababu jina la Mungu litatukanwa kwa ajili yako.
Baada tu ya Israeli kugawanyika katika sehemu hizo mbili, hapo ndio ikawa sehemu nyingine ya chanzo cha machafuko, watu waliokuwa wanakaa kaskazini (yaani yale makabila 10) yakaacha kabisa kumcha Mungu wa Israeli kama hapo kwanza kwasababu mfalme wao wa kwanza anayeitwa Yeroboamu aliwatengenezea sanamu ya ndama, waiabudu kama Mungu wao badala ya Mungu wa Israeli..hivyo ikawa ni machafuko makubwa zaidi, wakawa hawana tofauti na watu wa Mataifa.
Na yale makabila mawili yaliyosalia ambayo yalikuwa kusini angalau kidogo watu waliokuwa wanakaa kule walikuwa wanamwogopa Mungu ingawa si sana, na walikuwa wanamcha Mungu kwasababu tu Hekalu la Mungu lilikuwa huko nchini kwao Yuda, hiyo kidogo ikawafanya wawe na hofu ya Mungu. Lakini na wao pia wakaja kukengeuka baaye…Hivyo mataifa haya mawili ndani Taifa moja yakawa na kila moja na mfalme wake, na itikadi zake, ingawa walikuwa wanatambuana kama ndugu, na hakukuwa na Mfalme mmoja kwa mataifa yote mawili, hapana kila moja lilikuwa na mfalme wake kuanzia huo wakati na kuendelea.
Walipita Wafalme karibia 20 katika Israeli ( yaani upande wa kaskazini)…lakini wote walifanya machukizo mbele za Mungu, kila aliyekuja alikuwa anafanya mabaya kuliko aliyemtangulia…Na miongoni mwa wafalme waliofanya mabaya sana ni Mfalme Ahabu ambaye alikuwa na mke wake aliyemtoa nchi za mataifa, ambaye alikuwa ni mchawi, aliyeitwa Yezebeli, hawa waliichafua Israelli kwa kiwango cha juu sana…Mpaka ikafika kipindi Bwana akaileta huduma ya Eliya duniani, na lengo la huduma ya Eliya ilikuwa ni KUWAREJESHA WANA WA ISRAELI WAMRUDIE MUNGU WAO. Mungu alitumia ishara nyingi katika huduma ya Eliya ili kuwarejesha wamgeukie yeye…(kwa maelezo marefu juu ya huduma hii ya Eliya tutumie ujumbe inbox tukutumie )…wachache wakawa wanatii na kugeuka lakini wengi wakawa hawatii..
Na katika Yuda pia walikuwa wanatumiwa manabii wengi, lakini angalau Yuda kidogo watu walikuwa si wagumu kama Israeli..Kwani kulikuwa kuna Wafalme katika Yuda ambao walikuwa wanamtii Mungu na kumheshimu kama alivyofanya Daudi, mfano wa wafalme hao alikuwepo mfalme Hezekia, na Mfalme Yosia hawa walikwenda katika njia za Mungu katika ukamilifu wote, hivyo katika vipindi vya utawala wao Mungu aliwabariki na kuwaepushia madhara,… Manabii wote tunaowasoma katika Biblia, kuanzia Eliya, Elisha, Habakuki, Isaya, Hosea, Nahumu, Yona, Amosi, Yeremia, Obadia,Habakuki, Mika n.k wote hawa walitokea kipindi hichi cha Wafalme kasoro nabii Danieli, Hegai, zekaria pamoja na Malaki hawa walitokea baada ya Isreali kutawanyishwa…
lakini hao wengine Walikuwa wanatumwa kuwaonya wana wa Israeli na wana wa Yuda pamoja na wafalme wao wamgeukie Mungu…Unapopitia kitabu hichi ili upate picha vizuri, ni vyema ukapitia pia vitabu vya manabii, uone Bwana alivyokuwa anawaonya Israeli kwa nguvu, na jinsi gani alivyokuwa anawatabiria kuwa watakwenda utumwani Babeli wasipotubu..Kwa muda wako soma kitabu cha Yeremia, Hosea, Nahumu, Isaya utayaona mambo hayo kwa urefu, …
Kwa miaka mingi Zaidi ya 400, walikuwa wanatumiwa manabii wa kuwarejesha lakini ni wachache tu ndio waliokuwa wanatii na kugeuka, hivyo uvumilivu wa Mungu ukafika kikomo, kukawa hakuna tena msamaha, Mungu akaamua kuwatoa Waisraeli wote kutoka katika nchi yao waliyopewa na Mungu, waliokuwa wanakaa upande wa kaskazini, yaani Israeli (yale makabila 10)..yalichukuliwa utumwani kwenda nchi inayoitwa ASHURU, na wale waliokuwa wanakaa kusini (yaani Yuda) baada ya miaka 125 mbeleni nao pia walichukuliwa na kupelekwa utumwani BABELI,..wao hawakuchukuliwa kipindi kimoja na Israeli kwasababu angalau kwao kulikuwa na hofu ya Mungu kuliko Israeli, lakini baadaye nao pia wakakengeuka kama Israeli na kuchukuliwa mpaka Babeli…Nchi ya Ahadi ikabaki nyeupe!! Wakaletwa makafiri wakaishi huko kwa niaba yao, nchi ya Israeli ikakaliwa na makafiri. Yuda Wakapelekwa utumwani miaka 70..
2 Nyakati 36:14 “Na zaidi ya hayo wakuu wote wa makuhani, na watu, wakakosa mno sawasawa na machukizo yote ya mataifa; wakainajisi nyumba ya Bwana aliyoitakasa katika Yerusalemu.15 Naye Bwana, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu ALIWAHURUMIA WATU WAKE, NA MAKAO YAKE;16 lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, HATA ILIPOZIDI GHADHABU YA BWANA JUU YA WATU WAKE, HATA KUSIWE NA KUPONYA.17 Kwa hiyo akaleta juu yao mfalme wa Wakaldayo, aliyewaua vijana wao kwa upanga nyumbani mwa patakatifu pao, asiwahurumie kijana wala mwanamwali, mzee wala mkongwe; akawatia wote mkononi mwake.18 Na vyombo vyote vya nyumba ya Mungu, vikubwa kwa vidogo, na hazina za nyumba ya Bwana, na hazina za mfalme, na za wakuu wake; vyote pia akavileta Babeli.19 Wakaiteketeza nyumba ya Mungu, wakaubomoa ukuta wa Yerusalemu, wakayateketeza kwa moto majumba yake yote, wakaviharibu vyombo vyake vyote vya thamani.20 Na wale waliookoka na upanga akawachukua mpaka Babeli; wakamtumikia yeye na wanawe hata kulipoingia milki ya Uajemi;21 ili kulitimiza neno la Bwana kwa kinywa cha Yeremia, hata nchi itakapofurahia sabato zake; kwa maana siku zote ilipokaa ukiwa ilishika sabato, kutimiza miaka sabini.”
Mstari wa 16, unasema “lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, HATA ILIPOZIDI GHADHABU YA BWANA JUU YA WATU WAKE, HATA KUSIWE NA KUPONYA”.
Ndugu katika vitabu hivi tunajifunza kuwa..kuna wakati unafika ghadhabu ya Mungu, itajaa hata kusiwe na kuponya, wewe unayesema Mungu anakawia, wewe unayedharau na kuidhihaki na kuicheka injili leo, na kuwacheka na kuwafanyia mizaha watu wa Mungu, siku inakuja ambapo utalia na kutakuwa hakuna msaada, siku ya ghadhabu ya Mungu inakuja! Usidanganywe na watu wanaosema kuwa Mungu hawezi kuangamiza dunia, au hakuna mwisho wa dunia, ndugu watu wa kipindi cha Nuhu ndio walikuwa wanasema hivyo hivyo…lakini ghafla tu walishangaa siku moja mbingu zimefunga, zimekuwa nyuesi……Jiepushe na ghadhabu ya Mungu, Uvumilivu wa Mungu ni kukufanya wewe utubu, umgeukie Mungu, tubia uasherati wako, rushwa zako, utukanaji wako, usengenyaji wako, na kutokusamehe kwako…Wema wa Mungu unakuvuta leo kwasababu hataki upotee soma tena mstari wa 15 unasema…
“15 Naye Bwana, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu ALIWAHURUMIA WATU WAKE, NA MAKAO YAKE; ”
Ni mara ngapi asubuhi na mapema umekutana na mahubiri, kwenye redio, kwenye Tv, mitandaoni, mitaani au hata sehemu zako za kazi?..Usipuuze unaposikia injili unayopewa bure pasipo hata kulipia hata sh. Moja..siku ile utakosa cha kujitetea..
Kuna wakati mlango wa rehema utafungwa, ambapo utatamani kutubu utashindwa: Wana wa Israeli walilia na kuomboleza, siku ile wanapochukuliwa mateka,lakini Mungu hakusikia chochote. Ndivyo itakavyokuwa kwa wale wanaochezea neema sasa.
Luka 13:24 “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.25 Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako;26 ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu.27 Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.28 Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno,mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje.”
Hivyo unachopaswa kufanya ni kutubu hapo ulipo kwa kudhamiria kuacha dhambi zako, na kwenda kutafuta ubatizo sahihi kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako, ubatizo sahihi ni wa kuzamishwa mwili wote na kwa jina la Yesu Kristo kulingana na Matendo 2:38, na Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu.
Hakikisha unakisoma vitabu hivi mwenyewe, usiache kipengele hata kimoja, kwasababu ni habari zinazoeleweka na zimewekwa katika mfumo mrahisi wa kueleweka, haihitaji ufafanuzi sana kukielewa. Hapa tunajaribu kukupa picha tu, ili kukusaidia wewe mwenyewe kuvisoma vitabu hivyo kiurahisi, Hivyo tumia muda wako mwingi kuvisoma peke yako, Na Mungu atakufunulia mengi zaidi…
Usikose mwendelezo, na Pia washirikishe wengine habari njema..
Bwana akubariki.
No comments:
Post a Comment