Jina la Bwana Yesu Kristo, libarikiwe…
pamoja na kazi nyingine nyingi anazozifanya Roho Mtakatifu juu ya mtu aliyemwamini Yesu Kristo, nyingine ni kumwongoza katika kuijua kweli yote…Hilo tunalisoma katika..
Yohana 16:13“ Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake”
Neno kuongoza halina tofauti sana na kuelekeza, yaani mtu anayekuelekeza jambo Fulani hatua kwa hatua, mpaka kufikia hitimisho analotaka yeye ufikie, hana tofauti na mwongozaji…na kazi ya mwelekezaji au mwongozaji, sio tu kuonesha njia pekee bali hata kurekebisha baadhi ya makosa..Kwamfano mtu anapotaka kukuongoza kufika mahali Fulani, halafu wewe unampa mashauri yako ya njia ya kuipitia, ni wazi kuwa kama hayo mashauri yako sio sahihi basi atakurekebisha kwa nia ya kukuelekeza njia iliyo bora zaidi.
Na ndivyo ilivyo kwa Roho Mtakatifu, yeye ni mwongozaji wetu, na Roho Mtakatifu ndio jambo la kwanza kabisa mtu aliyemwamini Kristo anapaswa kuwa naye…Biblia inasema mtu asiye na Roho Mtakatifu huyo sio wake (Warumi 8:9) Ikiwa na maana kuwa mtu asiye na Roho Mtakatifu, hakuna uongozi wowote wa KiMungu unaoendelea juu ya Maisha yake..Ni kupotea tu!.
Hivyo mtu aliyeamini, katika hatua za awali kabisa, anakuwa hajui vitu vingi, hiyo ni kawaida kabisa, anakuwa kama mtoto mdogo aliyezaliwa, ambaye hajui chochote katika maisha haya, na vivyo hivyo mtu aliyezaliwa mara ya pili anakuwa ni mdhaifu katika roho. Lakini pamoja na udhaifu huo kunakuwa na kitu ndani yake kinachomfanya aelewe mambo mengi kwa muda mfupi kwasababu anakuwa na moyo wa unyenyekevu wa kutaka kujua au kufahamu Zaidi kuhusu Mungu, kama mtoto mchanga… hiyo Kiu ni ambayo Roho Mtakatifu kaiweka mwenyewe ndani ya mtu, ili itumike katika mstari wa kuwa chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu.
Roho Mtakatifu anaanza kumvuta, kidogo kidogo na kumtoa hatua moja hadi nyingine, aielekee njia ya utakatifu, ndio hapo mtu ataanza kutoka katika ulimwengu na kuona sababu ya kutafuta kanisa Fulani ambalo angalau ataweza kuipooza ile kiu iliyopo ndani yake ya kutaka kumjua Mungu…Atatoka kwenye dhambi na hatimaye kujiunga kanisa Fulani, atapata vitu ndani ya lile kanisa ambavyo vitamsisimua sana na kumfanya kukua kiroho kwa kiwango Fulani..na atakapofika mahali na kuona hali yake ya kiroho ipo pale pale, baada ya kukaa muda mrefu, kuna kitu kitamwambia hapo ulipo bado unahitaji kuwa na Mungu zaidi…..hiyo nguvu itamsukuma kutafuta hazina mpya ya chakula cha kiroho kwa hali na mali, utaona anazidi kutafuta mahali ambapo atapata chakula kilichobora zaidi…lengo lake sio kuhama kanisa au dhehebu hapana!.
Bali lengo lake ni kupata kuweka sawa hatima ya Maisha yake ya kiroho…Tofauti na wengi wanaohama makanisa sasahivi ni kwasababu tu wamesengenywa kidogo, au kwasababu wanahitilafiana na mchungaji wake kwa masuala ambayo hata sio ya kiimani, au kwasababu wanakemewa waache dhambi, au kwasababu wanataka kuolewa au kuoa, au kwasababu wamechoka tu kukaa pale na hivyo wanajaribu ladha mpya n.k...
Aliye na Roho Mtakatifu kweli haondoki mahali kwasababu kama hizo…Kinachomwondoa sehemu moja hadi nyingine ni ile kiu iliyopo ndani yake ya kutaka kumjua Mungu Zaidi, na anakuwa hana kiburi…Mahali alipokuwa anakaa hapo kwanza walikuwa hawana utaratibu wa maombi ya mfungo, hivyo anaona kuna kitu ndani ya roho yake kimepunguka anahitaji kuwa mwombaji zaidi na msomaji wa maandiko zaidi, kwahiyo anatafuta mahali ambapo atakuwa mwombaji Zaidi…Au mahali alipo kuna mchanganyiko wa Neno la Mungu na mambo ya ulimwengu huu hivyo anaondoka kwenda kutafuta mahali atakapoishibisha roho yake na Neno lisilochanganywa.
Au pengine mahali alipokuwa anakaa hakukuwa na desturi za kwenda kufanya uinjilishaji, na yeye anaona kuna kiu ndani yake ya kwenda kuwahubiria wengine habari njema popote pale, na hivyo mahali alipo haiwezekani kufanya hivyo, kwahiyo anaondoka kwenda mahali ambapo atatimiza agizo hilo la Bwana Yesu la kwenda kuhubiri injili kwa kila kiumbe..
Au pengine mahali alipokuwepo kunafanyika ibada za sanamu, na baada ya kuyachunguza maandiko vizuri anaona si sawa kufanya jambo hilo, na hivyo anaondoka kwenda kutafuta mahali ambapo hataabudu sanamu tena n.k.
Sasa katika hatua zote hizo utaona mtu huyu wa Mungu anaweza akawa ameshatembea sehemu nyingi zote akitafuta kukaa mahali salama….Na anavyozidi kusogea mbele ndivyo anavyozidi kuwa bora zaidi katika Imani. Na mtu anayekua kutoka sehemu moja hadi nyingine anakuwa hatamani tena kurudia yale ya nyuma…kwamfano mahali alipokuwepo ni mahali ambapo palikuwa hakuna utaratibu wa kusali au kuomba, wala palikuwa hakuna msisitizo wa kuishi maisha matakatifu akishatoka hapo hawezi tena kutamani kurudia hapo..
Sasa jambo hilo la kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa lengo la kutafuta Usalama wa maisha yako ya kiroho, na si sababu nyingine tofauti na hizo…sio dhambi! Bali ni kazi ya Roho Mtakatifu katika kukuongoza na kukuweka katika kweli yote…
Hiyo ndio kazi ya Roho Mtakatifu kutuhakikisha hatukwami sehemu moja kila siku bali tunakuwa kuufikia utimilifu,
Kosa moja linalofanyika na watu wengi, ni kujaribu kutafuta dhehebu Fulani la kuhamia na kutafuta lililobora zaidi ya lingine kwa kuangalia watu wengi wanakwenda wapi, au kwa kusikiliza ushauri wa watu, au kwa kuangalia uzuri wa kanisa….lakini hawasikilizi msukumo wa Roho Mtakatifu ndani yao, ambaye huyo ndiye angewaongoza katika kuwatia kwenye kweli yote…
Binafsi nimekutana na watu wengi, wakiniuliza nimeamini sasa nihame hapa niende kanisa gani?...Binafsi huwa nakosa jibu la hili swali..kwasababu Mungu hakuanzisha madhehebu, na Roho Mtakatifu hamwongozi mtu kwenda kwenye dhehebu lolote bali anamwongoza katika kuijua kweli…..Hiyo njaa na kiu ya Neno la Mungu ndio inayomsukuma mtu kutoka sehemu moja hadi nyingine kutafuta chakula, hivyo hata kama akikutana na chakula kilichochacha mbele yake atakula tu kwa huo muda ilimradi aweze kuishi..
Kanisa sio suluhisho la kuishi katika mapenzi ya Mungu, bali Roho Mtakatifu ndio suluhisho, unapokaa chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu kwa kuyasoma maandiko ndivyo unavyompa nafasi Roho Mtakatifu kukuonesha ni wapi ulikuwa unakosea, na ni wapi unapaswa urekebishe na ni wapi pa kukaa palipo salama…lakini sio kutafuta ushauri kutoka kwa watu, au kwa kuangalia ni wapi wengi wanakwenda. Wengi wanaofanya hivyo hakuna chochote katika maisha yao kitakachobadilika kwasababu ni sawa na wamehama dini moja na kujiunga na nyingine…huko wanakokwenda wanakwenda kuwa washirika wa dini tu na si wakristo halisi, na kuvamiwa na roho ya udhehebu ambayo ndiyo roho ya mpingakristo….roho ya kusema dini yangu inafundisha hivi, au dhehebu halisemi hivyo n.k Kumbuka madhehebu ya Mafarisayo na Masadukayo ndiyo yaliyoongoza kumpinga Bwana Yesu katika huduma yake…sasa roho hiyo hiyo ndiyo iliyopo katika madhehebu (yaani watu walioacha uongozi wa Roho Mtakatifu na kuwa washirika au washabiki wa dini)..Bwana alipokuwa anawaambia Mafarisayo hivi wenyewe wakawa wanasema Musa hakutufundisha hivyo, kwahiyo ikawafanya kuwa mbali na Mungu kuliko hata watu wa Ulimwengu wasio mjua Mungu, hiyo yote ni kutokana na Udhehebu na Udini uliokuwa ndani yao.
Ndio maana Biblia inatuambia tutoke huko (Ufu.18:4), Tunapomgeukia Roho Mtakatifu na kufuata uongozi wake ndio kutoka kwenyewe kunakozungumziwa hapo…yeye ndiye kiongozi wetu ambaye kila siku anarekebisha makosa yetu kulingana na Biblia na kutuweka katika mstari.
Usianze kutafuta kanisa la kwenda sasa, anza kutafuta maandiko yanasemaje kwanza…ndipo Roho atapokuongoza pa kwenda, Roho Mtakatifu anawaongoza watu wanaosoma maandiko sio wanaotafuta makanisa…
Bwana akubariki sana!
No comments:
Post a Comment