Waebrania 6:11 “Nasi twataka sana kila mmoja wenu aidhihirishe bidii ile ile, kwa utimilifu wa matumaini hata mwisho;12 ili msiwe wavivu, bali mkawe wafuasi wa hao wazirithio ahadi kwa imani na uvumilivu. 13 Kwa maana Mungu, alipompa Ibrahimu ahadi, kwa sababu alikuwa hana mkubwa kuliko yeye mwenyewe wa kumwapa, aliapa kwa nafsi yake, 14 akisema, Hakika yangu kubariki nitakubariki, na kuongeza nitakuongeza. 15 Na hivyo kwa kuvumilia akaipata ile ahadi”.Neno uvumilivu siku zote limekuwa sehemu ya Mungu, na sisi vivyo hivyo tunapaswa liwe sehemu ya maisha yetu, Kama Mungu asingekuwa mvumilivu ni wazi kuwa mimi na wewe tungekuwa tumeshapotea siku nyingi, kwani wakati tu tuliposikia injili kwa mara ya kwanza, siku hiyo hiyo Mungu alitazamia tubadilike lakini wengi wetu tulikuwa wakaidi, ndio tukazidi kuwa watenda dhambi hata zaidi ya hapo mwanzo miezi ikapita, miaka ikapita, japo tulikuwa tunasikia kila siku mahubiri yanahubiriwa lakini hatukuzingatia, Sasa kama ingekuwa Mungu ni mtu wa kukataa tamaa mapema, sio mvumilivu, sidhani kama mpaka leo hii tungekuwa tunaishi,..
Lakini uvumilivu wake, umekuwa neema kwetu na umemzalia matunda si yeye tu, bali sisi pia. Mimi binafsi ninayo kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kuwa mvumilivu kwangu, kwa maana maovu mengi niliyoyafanya huko nyuma nilidhani nilishamkufuru Mungu siku nyingi. Na ni kwanini Mungu anakuwa mvumilivu kwetu?..Jibu ni ili kutuvuta tufikie TOBA halisi.
Warumi 2:4 “Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu?”Zaburi 86: 15 “Lakini Wewe, Bwana, U Mungu wa rehema na neema, Mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli”
Vivyo hivyo na sisi tulio katika imani, Uvumilivu ni moja ya nguzo muhimu sana. Katika mbio hizi zilizo mbele yetu, japo tumewekewa thawabu kubwa huko mwisho mwa safari lakini ukweli ni kwamba milima na mabonde ya ibilisi hayakwepeki, majaribu na masumbufu, na wakati mwingine dhiki tutakutana nazo hapa duniani, na Bwana Yesu alishatueleza kabisa kuwa mambo hayo tutakuwatana yao wala hakutuficha,(Yohana 16:33)..Hivyo ni safari inayohitaji uvumilivu.
Lakini Swali ni Je! uvumilivu wa aina gani huo unaohitajika kwetu?
Kuna mwingine anaweza akawa labda anapitia matatizo yake binafsi, labda uchumi wake umeyumba, au amekumbana na matatizo ya kifamilia, au magonjwa n.k..na huku nyuma hata hana habari na Mungu, sasa mtu wa namna hii, anaweza akatiwa moyo kibinadamu awe mvumilivu katika hali ngumu anayoipitia kwa huo muda..Lakini huo sio uvumilivu unaozungumziwa katika maandiko.
Uvumilivu unaozungumziwa ni uvumilivu unaolenga Imani. Yaani kutokukatishwa tamaa na hali unayopitia sasa hivi ambayo inaweza kukusababishia kupoteza thawabu yako uliyoandaliwa mwisho wa safari..kwamfano wakati mwingine unaweza ukaona unapitia katika hali Fulani ngumu ambayo sababu yake tu ni uliamua kutokukifanya hicho kitu ambacho ni kinyume na mapenzi ya Mungu, unaweza ukawa unatengwa au unachukiwa kwasababu tu umeacha kufanya dhambi, mwanzoni ulikuwa unakunywa pombe na marafiki zako lakini sasa hunywi tena, mwanzoni ulikuwa unakwenda disco lakini sasa huendi tena, mwanzoni ulikuwa msengenyaji lakini sasa husengenyi tena, na matokeo yake kumetokea kundi la watu wanakutengenezea visa tu, wanakuwekea vikwazo,wanakusema vibaya..wakati mwingine ndugu, hata kazini kwako n.k.
Hapo ndipo unapopaswa uvumilie, biblia inasema katika Mhubiri 7: 8 “Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake, Na mvumilivu rohoni kuliko mwenye roho ya kiburi.
9 Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu”…...
Pasipo uvumilivu hatuwezi kumzaliwa Mungu matunda..Kama vile Bwana alivyotoa ule mfano wa mpanzi, akasema mbegu nyingine ziliangukia pembezoni mwa barabara nyingine zikaangukia kwenye miamba nyingine zikaangukia kwenye miiba,..nyingine kwenye udongo mzuri, hapo Bwana alikuwa anafunua aina tatu ya vipingamizi mtu atakavyokutana navyo kabla ya kuufikia mwisho mzuri wa safari yake, awali ya yote shetani atataka kumpokonya kile alichokisikia, itafika tena wakati ataudhiwa kwa ajili ya hilo Neno aliloendelea kulishika, baadaye tena baadhi ya mambo yatataka kumsonga asizae, na shughuli za ulimwengu huu na anasa, na tamaa ya mambo mengi …
Lakini Yule ambaye atazaa 30, mwingine 60 mwingine 100 Biblia inasema, hakuifikia hiyo hatua hivi hivi tu, bali aliifikia kwa KUVUMILIA vipingamizi vyote.
www.wingulamashahidi.org
Lakini Yule ambaye atazaa 30, mwingine 60 mwingine 100 Biblia inasema, hakuifikia hiyo hatua hivi hivi tu, bali aliifikia kwa KUVUMILIA vipingamizi vyote.
Luka 8:11 “Na huo mfano, maana yake ni hii; Mbegu ni neno la Mungu. 12 Wale wa karibu na njia ndio wasikiao, kisha huja Ibilisi akaliondoa hilo neno mioyoni mwao, wasije wakaamini na kuokoka. 13 Na wale penye mwamba ndio wale ambao wasikiapo hulipokea lile neno kwa furaha; nao hawana mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa hujitenga.14 Na zilizoanguka penye miiba ni wale waliosikia, na katika kuenenda kwao husongwa na shughuli na mali, na anasa za maisha haya, wasiivishe lo lote. 15 Na zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda KWA KUVUMILIA.’’Hivyo ndugu, tunapaswa tuilinde Imani Mungu aliyotupa mara moja tu, Na hiyo tutailinda kwa kuvumilia mabaya yote shetani atakayojaribu kutulea mbele yetu yatakayotufanya tuuache wokovu au turudi nyuma….Iwe ni magonjwa, iwe shida ya fedha, iwe ni kukosa mavazi, iwe ni kuwa yatima, iwe ni kuwa mjane, iwe ni kuwa tasa, iwe ni kupigwa au kutengwa au wakati mwingine kufungwa, vyovyote vile yasitufanye sisi kukosa uvumilivu wa kuyaongojea tuliyoandaliwa mbele. Tuige mfano wa Ibrahimu.
Ufunuo 2:3 “tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka.”Bwana akubariki sana.
www.wingulamashahidi.org
No comments:
Post a Comment