"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, August 7, 2019

MAVAZI YA NDANI NA YA NJE.

Madhabahu zote wana wa Israeli walizomjengea Mungu ilikuwa ni lazima wazijenge katika mahali pa juu, hivyo ndivyo walivyoagizwa na Mungu, mahali ambapo pameinuka, au waiinue madhabahu yenyewe juu,..kwasababu maana ya neno lenyewe madhabahu ni ‘”palipo inuka”, hakukuwa na nama yoyote madhabahu ikajengwa bondeni, au shimoni na Mungu alifanya hivyo makusudi kufunua mambo makubwa kiroho, jambo hilo hilo hata wapagani baadaye walikuja kuliiga, nao pia madhabahu zao wakawa wanazijenga sehemu za juu, au wanazinyanyua juu, na ndio maana utasoma kwenye biblia sehemu nyingi wakati wa enzi za wafalme, Bwana anawakemea wayahudi kwa makosa yao ya kutokuziondoa sehemu za juu,..akiwa na maana ya madhabahu zao za sanamu walizozijijengea kwa uchawi wao, Shetani siku zote ni mwigaji, hakuna jambo jipya alilowahi kulibuni yeye mwenyewe, alipomuona Mungu anawaagiza wana wa Israeli watoe kafara za wanyama kwa ajili ya upatanisho wa dhambi zao, yeye naye akaiga mambo hayo hayo, na ndivyo ilivyokuwa hata katika madhabahu zake.

Sasa wakati madhabahu ilipojengwa na kunyanyuliwa juu, mtu yeyote atakayeiendea ambaye ni kuhani alipewa masharti ya kuiendea na mavazi rasmi ya kuvaa. Kuhani mkuu au kuhani yoyote ilikuwa ni lazima avae mavazi ya kumsitiri mwili wake wote, hivyo ziliandaliwa kanzu nzuri za kitani, ndefu, ambazo mtu akivaa hizo zilimsitiri mwili wake wote, lakini hiyo peke yake haikutosha kumsitiri mtu maeneo yote, kwani wakati wa kuiendea madhabahu ambayo imenyanyuliwa ni lazima utapandisha ngazi ili kuifikia juu, na hivyo kanzu kwa upande wa chini huwa haisitiri, kunakuwa wazi, na ilikuwa mfano uchi wao ukionekana tu madhabahuni pa Mungu ilikuwa ni mauti, Mungu mwenyewe anakuua.
Kutoka 20:26 “Tena hutapanda kwenda madhabahuni kwangu kwa daraja, uchi wako usidhihirike juu yake.”
Hivyo kutatua tatizo hilo, Bwana akawapa makuhani wake wote amri kuwa watengenezewe suruali ambazo watazivaa kwa ndani ili kusudi kwamba watakapopanda kwenda madhabahuni, uchi wao usionekane kwa chini, wawe salama.

Kutoka 28:39 “Na hiyo kanzu utaifuma ya kitani nzuri ya kazi ya urembo, ufanye na kilemba cha nguo ya kitani nzuri, nawe utafanya mshipi wa kazi ya mwenye kutia taraza. 40 Kisha utafanya kanzu kwa ajili ya wana wa Haruni, nawe wafanyie mishipi, wafanyie na kofia kwa utukufu na uzuri. 41 Nawe mvike huyo nduguyo Haruni na wanawe nao mavazi hayo; nawe watie mafuta, na kuwaweka kwa kazi takatifu, na kuwatakasa, ili wapate kunitumikia mimi katika kazi ya ukuhani. 42 Nawe wafanyie suruali za nguo ya kitani, ili kufunika tupu ya miili yao; suruali hizo zitafika tangu kiunoni hata mapajani;43 na Haruni na wanawe watazivaa, hapo watakapoingia katika hema ya kukutania, au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike katika mahali patakatifu; wasije wakachukua uovu, wakafa; hii itakuwa ni amri ya milele kwake yeye, na kwa wazao wake.”
Lakini tunapaswa tujiulize mambo haya yanafunua nini katika agano jipya?. Jambo la kwanza ni kwamba Madhabahu ya Mungu tunayomwabudia katika Roho imenyanyuka sana tena imenyanyuka juu kuliko hata ya akina Haruni nayo ipo mbinguni na sadaka yake juu yake, ambayo ni Bwana wetu Yesu Kristo, Vyote hivi vipo mbinguni.

Hivyo tunapokwenda mbele ya madhabahu hii, kupeleka mahitaji yetu, au kumfanyia Mungu ibada, tunapaswa tuwe makini sana, kwanza tunapaswa tuwe tumesitiriwa sio tu kwa mavazi ya nje, bali pia na kwa yale ya ndani vinginevyo tunaweza tukajiona tupo sawa lakini kumbe tunajitafutia kifo, badala ya uzima.

Mavazi ya nje ni yapi?. Ni mwonekano wako wote wa nje kwa ujumla,.Ikiwa leo hii unaweza kutembea barabarani na vimini wewe kama mwanamke na suruali na nguo zinazochora maungo yako..na kibaya Zaidi huoni hata aibu kuingia nazo katika nyumba ya ibada, madhabahuni pa Mungu na mavazi hayo ni dalili kubwa ya kujichumilia mauti. Vile vile unakuwa mlevi, na bado unakwenda mbele za Mungu, huko ni kujitafutia kifo ndugu, kama umeamua kuwa baridi ni heri ukawa baridi kwelikweli, kuliko kuwa vuguvugu.

Mtume Petro wakati anavua akiwa nusu uchi, Bwana alipotokea alijitupa kwenye maji kuficha uchi wake, kwasababu ya kumheshimu Bwana, na yeye alikuwa ni mwanamume…

itakuwaje kwako wewe mwanamke! Mbele ya Bwana? Unafikiri unapaswa ujisitiri kiasi gani?

Vilevile mavazi ya ndani, ni mambo yaliyo moyoni mwako, mambo ambayo kwa nje hayawezi kuonekana lakini kwa ndani hayaelezeki kwa jinsi yalivyo mabaya, mfano wa wale mafarisayo na waandishi Bwana Yesu aliowazungumzia..
Mathayo 23:28 “Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi”.
Ndani unayo chuki na watu, unao wivu, ndani umewawekea wengine vinyongo na vikwazo, ndani umeweka kisasi halafu bado unapanda madhabahuni pa Mungu kwenda kumwomba, au kumfanyia ibada, hapo ni sawa na kuhani aliyevaa kitani nzuri ndefu ambayo kwa nje unaonekana kweli wewe ni mwema lakini mbele za Mungu upo uchi..

Hiyo ni mbaya sana, unatazama pornography kwa siri, unazini kwa siri kwasababu wanakwaya wenzako hawajakuona unadhani pia Mungu hakuoni, unakwenda disco kisirisiri, lakini huku nyuma unakwenda kumwimbia Mungu na kumwabudu..Nataka nikuambie ni heri usifanye kabisa au utubu uamue kumwishia Mungu.

Fahamu kuwa kanisa hili tunaloishi ndilo kanisa la saba lijulikanalo kama kanisa la Laodikia, na ndio la mwisho, na kama huufahamu ujumbe wa kanisa hilo unaweza kusoma katika Ufunuo 3:14-21 uone kama tabia zinazozungumziwa pale haziendani na ukristo uliopo sasa?. Hili ni kanisa vuguvugu, ambalo linajiona kuwa Tajiri lakini ni uchi, maskini na dhaifu..
Ufunuo 3:14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu. 15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. 16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. 17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi. 18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona. 19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu. 20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. 
21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi. 
22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”

Unaona hapo? Bwana anatupa shauri tununue kwake mavazi meupe aibu ya uchi wetu isipate kuonekana, “kumbuka huo ni ushauri sio lazima”..na mavazi hayo anayoyazungumzia ni yale ya nje na ya ndani. Ndugu usipumbazwe na mambo mengi maovu unayoyaona sasahivi ulimwenguni. Yalitabiriwa yatakuwa hivyo na kuzidi kuongozeka katika siku za mwisho,. Lakini pia Bwana alituahidia sisi wa kanisa la Mwisho la Laodikia thawabu kubwa kuliko makanisa mengine yote yaliyotutangulia ikiwa tutashinda.

Tafakari aliposema tutaketi pamoja naye Mfalme wa wafalme, Bwana wa Mabwana Yesu Kristo katika Enzi yake, hilo sio jambo dogo. Hivyo kwa mtu yoyote mwenye akili timamu atayahesabia Maisha haya ya kitambo tu kuwa si kitu cha kulinganisha na thawabu hizo zinazokuja.
Hivyo ndugu, ikiwa bado upo nje ya Kristo, Usiipuzie hii neema iliyopo sasa. Tubu kwa kumaanisha kabisa kuacha dhambi, kisha uende ukabatizwe kulingana na maandiko kwa kuzamishwa katika maji mengi kwa jina la BWANA YESU ukapate ondoleo la dhambi zako, na Bwana atakupa kipawa cha Roho mtakatifu (Matendo 2:38).

Bwana yupo mlangoni kurudi, naye mwenyewe anasema anakuja upesi! Na wala hatakawia.

Ubarikiwe sana. 

1 comment: