"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, August 8, 2019

MWISHO WA HAO WAMSAHAUO MUNGU.


Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima, karibu tujifunze maneno ya uzima, Kama tunavyofahamu tunaishi ukingoni kabisa mwa wakati, siku zile ambazo Bwana Yesu alisema upendo wa wengi utapoa duniani kwasababu ya kuongezeka kwa maasi (Mathayo 24:12) Ndizo tunazoishi sasa.

Sasa Upendo unaozungumziwa hapo sio tu upendo wa ndugu, bali pia upendo wa kumpenda Bwana utapoa ndani ya watu wengi.

Unakuta mtu alianza vizuri na Bwana, mwanzoni, alikuwa amesimama vizuri, anamtafuta Mungu kwa bidii, anasali, anajilinda na ulimwengu, anavaa mavazi ya heshima, na Zaidi ya yote anawahubiria wengine habari njema.. lakini kwasababu ulimwengu wasasa umebadilika, na yeye anabadilika nao, hapo mwanzo alikuwa haendi disco lakini sasa ameanza kuwa muhudhuriaji mzuri, hapo mwanzo alikuwa havai suruali na vimini lakini sasa ni mvaaji hodari, hapo mwanzo alikuwa ni mwombaji mzuri lakini sasa kasongwa na kampani za watu wa kidunia, mizunguko ya huku na kule kila kukicha haiishi, na kwasababu smartphone zimekuja sasa, utamkuta ule muda ambao angepaswa awe analiafakari Neno la Mungu nyumbani kwake na familia yake, utamkuta ana chat kwenye mitandao na katika magroup ya whatsapp hata 50 yasiyokuwa na maana, na kutazama mambo yasiyostahili mitandaoni, na pornograph.

Na hali hiyo inaendelea hivyo hivyo mpaka baadaye anajikuta kamsahau Mungu kabisa ambaye alishamwokoa zamani, anaona sasa wokovu hauna maana tena, hauna faida yoyote, ni kujinyima tu bure kusikokuwa na sababu za msingi, na hivyo anaamua kuishi maisha ya kidunia huku akidhani kuwa ndio kayapenda maisha yake kumbe ndio ameyaangamiza…Biblia inasema:
Ayubu 8:8 “Basi, uwaulize, tafadhali, vizazi vya zamani, Ujitie kuyaangalia yale baba zao waliyoyatafuta;
9 (Kwani sisi tu wa jana tu, wala hatujui neno, Kwa kuwa siku zetu duniani ni kivuli tu;)
10 Je! Hawatakufunza wao, na kukueleza, Na kutamka maneno yatokayo mioyoni mwao?
11 Je! Hayo MAFUNJO yamea pasipo matope Na MAKANGAGA kumea pasipo maji?
12 Yakiwa yakali mabichi bado, wala hayakukatwa, Hunyauka mbele ya majani mengine.
13 NDIVYO ULIVYO MWISHO WA HAO WAMSAHAUO MUNGU; Na matumaini yake huyo mbaya huangamia;
14 Uthabiti wake utavunjika, Na matumaini yake huwa ni nyuzi za buibui.
15 Ataitegemea nyumba yake, isisimame; Atashikamana nayo, isidumu.
16 Yeye huwa mti mbichi mbele ya jua, Nayo machipukizi yake huenea katika bustani yake.
17 Mizizi yake huzonga-zonga chuguu, Huangalia mahali penye mawe.
18 Lakini, aking'olewa mahali pake, Ndipo patamkana, na kusema, Mimi sikukuona.
19 Tazama, furaha ya njia yake ni hii, Na wengine watachipuka kutoka katika nchi.”
Unaona hapo mwandishi anasema, Sisi ni wa juzi tu, tuwaulize watu walitutangulia zamani, tuwaulize wakina Sulemani, n.k. je! MAFUNJO yamea pasipo matope Na MAKANGAGA kumea pasipo maji?. Mafunjo na makangaga ni aina ya mime mirefu ambayo hiyo huwa inaota sehemu za mabwawa au maziwa, sehemu zenye maji mengi, mahali pengine popote palipo na upungufu wa maji haziwezi kuota, ni sawa tu na yale magugu maji,…Na ndio hapo anauliza je! Mimea hiyo inaweza kuota katika nchi kame kama vile katani iotavyo jangwani,?...Jibu ni La!, anasema ndivyo ilivyo kwa watu wale wamsahauo Muumba wao.
Mpaka mtu amsahau Mungu, ni wazi kuwa hapo nyuma alikuwa ameshafahamiana naye, huwezi kumsahau mtu ambaye humfahamu, vivyo hivyo wanaozungumziwa hapo ni wakristo wale ambao hapo nyuma walikuwa sawa na Mungu lakini sasa wamepoa, hapo kabla walikuwa moto kwa Mungu lakini sasa wamevutwa na ulimwengu. Wala hawazungumziwi watu wasiomjua Mungu kabisa..

Mwandishi anaendelea kusema.. “Yeye huwa mti mbichi mbele ya jua,”. Ikiwa na maana kuwa mpaka huo mti umekuwa mbichi ni wazi kuwa ulishawahi kuwepo pembezoni mwa mito ya maji, lakini ghafla haupo tena katika mito bali upo mbele ya jua.. Unatazamia vipi mti huo utakuwa na maisha marefu?. Vivyo hivyo na sisi tunapomsahau Mungu katika dunia hii mbovu inayopita, siku za mwanzoni tunaweza tusione matokeo yoyote, hiyo ni kwasababu ule ubichi bado upo ndani yetu, lakini siku chache mbeleni, tutakapo kauka ghafla ndipo tutakapojua kuwa kumbe tulikosea na tutakapotaka kugeuka tumrudie yeye hatutaweza tena kwasababu tayari tulishakatwa siku nyingi.. Hata leo hii ukiuta mti mkubwa, huwezi kuona matokeo ya kukauka majani yake siku hiyo hiyo, lakini nenda rudi baada ya siku mbili, tatu ndipo uakapoona tofauti.
Zaburi 50:22 “Yafahamuni hayo, Ninyi mnaomsahau Mungu, Nisije nikawararueni, Asipatikane mwenye kuwaponya.”
Katika nyakati hizi za hatari njia pekee ya kuishi maisha ya kutokumsahau Mungu ni kuhakikisha, kwanza kila siku unalitafakari Neno la Mungu, sio kusoma tu, hapana bali kutenga muda wa kutosha kulitafakari Neno, wengi wanaishia katika kusoma tu kama vile kitabu halafu basi, hiyo haikuongezei chochote, ni sawa na umetengewa sahani ya ugali, lakini ule ugali wote hauwezi kwenda tumboni moja kwa moja kama usipopitia kinywani, utafunwe, uvunjwe vunjwe na meno kisha uingie kidogo kidogo mpaka wote uishe, vivyo hivyo, ukiwa na pupa ya kulisoma Neno la Mungu kama kitabu tu ama gazeti, kama kutumiza wajibu Fulani ulioambiwa na mhubiri Fulani…

kisha kwenda kulala, litakuboa tu, na hutapata jambo jipya ndani yake, utaona kuna mambo magumu, haieleweki, lakini kwanza ukichukua muda kusali na kumwomba Roho Mtakatifu akusaidie, kisha ukatafakari lile unalolisoma hata kama ni mstari mmoja kwa muda mrefu ukililinganisha na maisha yako kisha, ukaweka mipango ya kulitendea kazi, basi lile Neno la Mungu litakuwa na manufaa makubwa sana kwako. Hatuhesabiwi haki kwa kumaliza kuisoma biblia yote, bali kwa kuielewa..
Kumbukumbu 8:11 “Jihadhari, usije ukamsahau Bwana, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo”.
Pili, jenga desturi ya kuhudhuria ibadani, ukutane na waaminio wenzako, kaa na ndugu ambao ni wakristo wenzako wenyewe nia ya kwenda mbinguni pamoja na wewe, tafuta marafiki wenye faida za kimbinguni..Chuma hunoa chuma, lakini kama muda wako wote utakaa na marafiki wa kidunia ambao hao wakati wote hata habari na Mungu hawana, na wewe uliyempokea Kristo unaendelea kukaa nao, ipo dalili kubwa sana ya kumsahau Mungu.

Na mwisho kuwa mtu wa maombi. Ukizingatia vigezo hivyo ni ngumu kujikuta umerudi nyuma kwa sababu yoyote ile. Kumbuka nyakati hizi ndio zile nyakati za hatari sana ambazo zilitabiriwa kuwa watu watakuwa wa kupenda sana anasa kuliko kumpenda Mungu..Hivyo tunaaswa kuwa makini sana katika safari yetu ya wokovu.
Waefeso 5:15 “Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima;
16 mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu.
17 Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana.
18 Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho;
19 mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu;
20 na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo;
21 hali mnanyenyekeana katika kicho cha Kristo.”
Bwana akubariki sana. Tafadhali “Share” Ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki.

2 comments:

  1. Amina,Mungu aendelee kukutia nguvu kwa utumishi mwema unaoutoa kwa sababu najikuta napata hofu ya kiMungu ndani yangu nisomapo jumbe hizi unazozitoa.

    ReplyDelete