Kuna watu wanasema sasa tunaishi katika agano jipya hivyo Mungu hatazami tena Taifa, wala mtu wala jinsia bali wote ni sawa kulingana na Wagalatia 3:28. Na hivyo wanadai kuwa hakuna kitu kama hicho taifa la Israeli kurudiwa na Mungu tena na Mungu kutembea nao kama ilivyokuwa katika agano la kale, sisi wote ni sawa na Kristo hivyo hakuna haja ya kutazama kinachoendelea Israeli, lile ni kwasasa ni taifa tu kama mataifa mengine. Ni kweli kabisa mbele za Kristo hakuna hivyo viambazi, wote ni sawa hakuna myahudi wala myunani, wala mke au mume, lakini katika kanuni ya utendaji kazi wake, ameweka mipango, mipaka, na kanuni na taratibu, na muda..
Kwamfano ilimpasa Mungu awapige upofu kwanza wayahudi(yaani Waisraeli) ili sisi, yaani mimi na wewe tuipokee neema, Mungu aliwafanya wawe vile kwa makusudi kabisa kwa ajili yetu na laiti asingefanya vile, leo hii sisi tusingemjua Kristo. Wokovu huu ungebakia kuwa ni wa wayahudi tu biblia inasema hivyo…Vile vile kama pia ukitazama kwa ukaribu utaona Neema ilipokuja kwa mataifa, haikuja na kukaa kila mahali kwa wakati mmoja japo kweli ilisikika ulimwenguni kote,lakini neema haikukaa kila mahali, ilikuwa inazunguka ukisoma maandiko na historia utoana ilianza bara la Asia, baadaye ikaja kuenea bara la Ulaya, baadaye ikafika Marekani, na mwisho wa siku sasa ipo kwetu huku Afrika..Na ndio maana utaona kuna mwitikio mkubwa wa watu kumtafuta Kristo huku kuliko mabara mengine yote duniani, lakini mfano kama ungekuja kipindi cha karne ya 19 huku Afrika, ungekutana na uchawi na ushirikina tu, wakati ulaya ndio ulikuwepo uamsho mkuu wa Roho.
Hivyo neema hii inatabia ya kutembea, na sasa inakaribia kuondoka na kurejea Israeli ilipoanzia, Na Bwana aliahidi kabla haijarudi atarudisha watu wake Israeli katika Taifa lao nao watakaa salama, kisha baadaye atawaletea uamsho. Jambo hilo tumeliona likitimia mwaka 1948, baada ya kukaa zaidi ya miaka 2500, ugenini kwenye mataifa mengine.Tofauti na wale wanaosema kuwa Israeli hawatarudiwa tena..Biblia ilitabiri kuwa watarudi nchini kwao.
Yeremia 34:23 “Kisha neno la Bwana likamjia Yeremia, kusema,24 Je! Hufikiri neno hili walilolisema watu hawa, wakinena, Jamaa zile mbili alizozichagua Bwana amezitupilia mbali? Hivyo ndivyo wanavyowadharau watu wangu, ili wasiwe taifa tena mbele yao.25 Bwana asema hivi, Ikiwa agano langu la mchana na usiku halikai imara, ikiwa mimi sikuziamuru kawaida za mbingu na dunia;26 ndipo nitawatupilia mbali wazao wa Yakobo, na Daudi, mtumishi wangu, hata nisitwae wazao wake watawale juu ya wazao wa Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; kwa maana nitawarudisha wafungwa wao, nami nitawarehemu.”
Unaona hapo Bwana anasema kama vile agano lake la mchana na usiku likivunjika, yaani siku moja ipite kusiwe mchana, au kusiwe usiku basi na atawatupilia mbali watu wake wayahudi, lakini kama halijawahi kutanguka, basi kwame hatakaa awasahau wayahudi.
Nataka nikuambie ndugu Uamsho wao utakuwa wa kipekee sana, ni ule Mtume Paulo alisemea juu ya mzeituni halisi uliokatwa na kurudishwa kwenye shina lake halisi, unategemea vipi matunda yasitoke halisi zaidi, ikiwa sisi tuliokuwa mizeituni mwitu tukapachikwa kwenye mzeituni halisi na tukatoa matunda halisi, je si zaidi hao waliokuwa halisi wenyewe, watatoa kilicho bora zaidi..
Warumi 11:15 “Maana ikiwa kutupwa kwao kumeleta upatanisho kwa ulimwengu, je! Kukubaliwa kwao kutakuwa nini kama si uhai baada ya kufa?16 Tena malimbuko yakiwa matakatifu, kadhalika na donge lote; na shina likiwa takatifu, matawi nayo kadhalika.17 Lakini iwapo matawi mengine yamekatwa, na wewe mzeituni mwitu ulipandikizwa kati yao, ukawa mshirika wa shina la mzeituni na unono wake,18 usijisifu juu ya matawi yale; au ikiwa wajisifu, si wewe ulichukuaye shina, bali ni shina likuchukualo wewe.19 Basi utasema, Matawi yale yalikatwa kusudi ili nipandikizwe mimi.20 Vema. Yalikatwa kwa kutokuamini kwao, na wewe wasimama kwa imani yako. Usijivune, bali uogope.21 Kwa maana ikiwa Mungu hakuyaachia matawi ya asili, wala hatakuachia wewe.22 Tazama, basi, wema na ukali wa Mungu; kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, ukikaa katika wema huo; kama sivyo, wewe nawe utakatiliwa mbali.23 Na hao pia, wasipokaa katika kutokuamini kwao, watapandikizwa; kwa kuwa Mungu aweza kuwapandikiza tena.24 Kwa maana ikiwa wewe ulikatwa ukatolewa katika mzeituni, ulio mzeituni mwitu kwa asili yake, kisha ukapandikizwa, kinyume cha asili, katika mzeituni ulio mwema, si zaidi sana wale walio wa asili kuweza kupandikizwa katika mzeituni wao wenyewe?25 Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili.26 Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake.27 Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao.”
Ndugu yangu kuna wakati unafika hii neema inayochezewa na watu itarudi makao yake makuu (Israeli), na hawa wayahudi ambao unawaona sasa hawana habari na Yesu, wapo vuguvugu, hawaeleweki, biblia inasema ndani ya siku moja Mungu atawamwagia Roho ya neema, nao watatubu kwa kumaanisha kabisa, yaani mji mzima wa Yerusalemu utakuwa unaomboleza siku hiyo , wakimwombolezea Bwana Yesu ambaye walikuwa wakimpinga tangu zamani.
Zekaria 12:10 “Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.11 Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido.12 Nayo nchi itaomboleza, kila jamaa peke yake; jamaa ya nyumba ya Daudi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Nathani peke yao, na wake zao peke yao;13 jamaa ya nyumba ya Lawi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Shimei peke yao, na wake zao peke yao.14 Jamaa zote zilizosalia, kila jamaa peke yake, na wake zao peke yao”.
Wakati huo, neema itakuwa imeshaondoka kwenye mataifa yote dunia, hapo ndipo Mungu ataitumia Israeli kuwa fimbo kwa mataifa yote, usitamani wakati huo ukukute..Leo hii tumeshaanza kuona dalili ndogo ndogo, jiulize kwanini taifa la Israeli ni dogo kuliko hata mkoa wa Songwe, halina kitu chochote cha kuvutia wala haina teknolojia ya kutisha sana kama mataifa ya mashariki na Magharibi lakini kila mtu anaizungumzia, isitoshe bado wanaigopa, na hapo hata Mungu hajatia mguu wake kutembea nao, jiulize wakati huo ukifika itakuwaje?.
Ndugu ni mambo mengi ya kutisha yapo mbele yetu ambayo hata sisi wenyewe hatuyajui vizuri, ni heri tukabakia katika upande salama, Vita ya Harmagedoni ambayo itakuja kupigwana kipindi kifupi baada ya unyakuo itapiganiwa pale pale Israeli…( ukihitaji maelezo marefu juu ya vita hii, nitumie ujumbe inbox nitakutumia somo lake..)
Huu ni wakati wa kuweka mambo yetu sawa, ikiwa bado hujatubu, mgeukie muumba wako sasa, na ikiwa bado upo nusu nusu, vuguvugu, uimarishe wito wako sasa, kabla nyakati za hatari hazijafika.
Bwana akubariki. Tafadhali “Share” Ujumbe huu kwa wengine.
Ikiwa utapenda kujifunza masomo haya katika mpangilio mzuri usiache kutembelea website yetu hii?>> www.wingulamashahidi.org
No comments:
Post a Comment