"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, August 28, 2019

SEHEMU ISIYO NA MAJI.


Maji yanawakilisha uhai, mahali ambapo hapana maji hapana uhai hiyo inajulikana na watu wote….Sayari zilizopo huko juu hazina maji, na ndio moja wapo ya sababu inazozifanya zisiwe na uhai…Hivyo hata hii dunia tunayoishi iliumbwa kutoka katika maji.
2Petro 3: 5 “Maana hufumba macho yao wasione neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu;
6 kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia”.
Mwanzo 1: 1 “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. 2 Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji”.

Kwahiyo sehemu yoyote isiyo na maji ni makazi ya kifo…Kadhalika katika roho, yapo maji ya rohoni, ambayo hayo mtu yeyote asiyekuwa nayo, moyo wake unakuwa ni nchi kavu, au nchi kame, makao ya kifo… Na hivyo Roho Mtakatifu hawezi kushuka mahali palipo pakame, yeye anashuka mahali penye maji, kama alivyotua wakati wa kuitengeneza upya dunia ya kwanza, alitua juu ya uso wa vilindi vya maji, ndipo akaanza uumbaji….Maji na Roho vinakwenda pamoja, (1 Yohana 5:9

“Kisha wako watatu washuhudiao duniani], Roho, na maji, na damu; na watatu hawa hupatana kwa habari moja.) ndio maana kuna umuhimu sana wa kubatizwa ubatizo wa maji mengi na si wa kunyunyiziwa ndipo Roho aingie ndani ya mtu, kwasababu dunia ya kwanza biblia inasema Roho Mtakatifu hakutua juu ya chemchemi, au juu ya unyevunyevu bali juu ya uso wa vilindi, ikiwa namaana kuwa ni dunia yote ilikuwa imejaa maji sio sehemu baadhi tu! hapana Bali yote..ndipo uumbaji ukaanza.

Mtu aliyempa Kristo Maisha yake kwa kudhamiria kabisa kuacha dhambi, na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi, na kwa jina la Yesu Kristo, hapo mtu huyo ni sawa na anaujaza moyo wake na maji ya uzima..Moyo wake unakuwa umejaa maji mpaka juu kabisa, vilindi vya maji ya uhai vinakuwa juu yake, na hivyo tayari Roho Mtakatifu kushuka juu yake na kuanza uumbaji, anakuwa amezaliwa mara ya pili na kuwa kiumbe kipya. Roho Mtakatifu anaanza kusema na iwe Nuru juu yake, na inakuwa hivyo, Roho Mtakatifu anaanza kutenga maji na maji,na kutengeneza ndani yake mito, chemichemi, na vipindi vya mvua, na kuchipusha kile ki-kijani ndani yake n.k

Bwana Yesu alisema katika 
Yohana 7: 38 “Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake. 39 Na neno hilo alilisema katika habari ya Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa”.
Sasa tumeshaona ni namna gani Roho ya mtu aliyezaliwa mara ya pili mbele za Mungu inaonekana kama ni mahali penye maji, penye uhai na mahali ambapo ni makazi ya Roho Mtakatifu, na tumeshaona kuwa Ili Roho Mtakatifu akae ndani ya mtu ni lazima ubatizo sahihi wa kimaandiko wa maji mengi uhusike..Kama Ilivyokuwa katika uumbaji.

Vivyo hivyo mtu yeyote ambaye hajamwamini Yesu Kristo, wala hajabatizwa inavyopaswa wala hajapokea Roho Mtakatifu, moyoni mwake ni nchi kavu..Na hakuna namna yoyote ile ambayo Roho Mtakatifu atatua juu yake…Na kama Roho Mtakatifu hatatua juu yake basi ni Dhahiri kuna roho nyingine zitatua juu yake…Na hizo si zaidi ya roho chafu za Mapepo…Roho za Mapepo ndizo zinazotafuta sehemu kavu isiyo na maji na kushuka juu yake..Tusome..
Mathayo 12:43 “Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika, asipate.
44 Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa.
45 Mara huenda, akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya”.
Unaona hapo?..Biblia inasema anapitia sehemu isiyo na maji, na hiyo si nyingine Zaidi ya mtu ambaye hajamwamini Kristo, na hajabatizwa na kupokea Roho Mtakatifu.Kitu kimoja watu wengi wasichokijua ni kwamba shetani sasa hayupo kuzimu...wala haungui moto sasahivi…shetani yupo hapa hapa duniani na baadhi ya mapepo yake, yapo mapepo baadhi biblia imesema kuwa ndio yapo kuzimu sasa kwenye vifungo, lakini sio yote! (2 Petro 2:4) Idadi kubwa ya mapepo yapo huru ulimwenguni, yakisubiri siku ya mwisho ifike yakusanywe yote pamoja na shetani yakatupwe katika lile ziwa la moto.
Haya yaliyopo huru sasa hayatamani kwa namna yoyote kwenda huko kuzimu(au kwa lugha nyingine shimoni), kwasababu yanajua mateso yaliyopo kule, ndio maana yalimsihi sana Bwana wakati ule yasipelekwe shimoni (soma Luka 8:30-32).

Na kitu kingine kisichojulikana na wengi ni kuwa, mtu yeyote ambaye hajampa Kristo Maisha yake, anayo mapepo ndani yake, anaweza akawa anayo machache au mengi, na yanatofautiana ubaya, yapo yaliyo mabaya sana na yapo ya wastani, yapo ambayo madhara yake ni ngumu kuonekana kwa wazi na yapo ambayo madhara yake yanaonekana waziwazi, lakini yote katika yote mtu ambaye hajampa Kristo Maisha yake, mwili wake ni makao ya roho chafu…aidha anajua au hajui..Na wengi wenye mapepo hawajijui kama wanayo, Mpaka siku watakapobadilika ndio watakapojijua kuwa hawakuwa sawa hapo kwanza.

Sasa mtu anayempa Kristo Maisha yake leo na kukusudia kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu mapepo yanamtoka, na kumbuka mapepo yakimtoka mtu sio lazima yalipuke! Hapana! Kufikiri hivyo ni kufikiri kichanga! Mapepo mengi yanawatoka watu pasipo hata kulipuka wala kuonesha mabadiliko yoyote ya mwili, baada ya kipindi Fulani tu mtu ndio atajiona amekuwa tofuati kuliko alivyokuwa hapo kwanza. Kwahiyo baada ya mapepo haya kutoka ndani ya mtu hayaendi kuzimu wala hayaendi jangwani, yanakwenda kutafuta mahali ambapo hapana maji, na huko si kwingine Zaidi ya mtu ambaye hajampa Kristo Maisha yake au kwa Wanyama, kwasababu Wanyama hawana Roho Mtakatifu, kipawa hicho hawajaahidiwa wao…Lakini yanapendelea Zaidi watu kuliko ya Wanyama…Kwahiyo mtu huyo kila siku anakuwa anaongeza mapepo juu ya mapepo ndani yake pasipo kujijua, ndio maana mtu ambaye hajampa Kristo Maisha yake, hali yake ya kiroho kila siku inazidi kuwa mbaya…Kwanini? Kwasababu kila siku anaongoza idadi ya mapepo ndani yake?

Unaweza kutengeneza picha yule mtu Bwana Yesu aliyemwombea alikuwa ana mapepo wangapi? Biblia inasema ni jeshi! Sasa hebu fikiri nguruwe pale walikuwa 2,000 na kila nguruwe tuseme kaingiwa na mapepo mawili tu! Kwa hesabu hizo jumla ya mapepo yaliyokuwa ndani ni wazi kuwa ni Zaidi ya mapepo 4,000 ndani ya mtu mmoja!.. na kila pepo linatabia yake..

Hivyo ndugu ambaye hujampa Kristo Maisha yako au ambaye mguu mmoja leo huko mwingine kule…hayo ndio madhara yatakayokupata endapo hutaamua kufanya maamuzi thabiti sasa…Kama hali yako itazidi kuwa mbaya kila kukicha, shetani yupo na anafanya kazi sasa…Mkabidhi Yesu Kristo Maisha yako ukabatizwe kama hujafanya hivyo, ili akupe na Roho wake Mtakatifu ili vijito vya maji ya uzima vianze kububujika ndani yako. Na ufanikiwe katika roho yako, na mwili wako usiwe makazi ya roho chafu za shetani. Nguvu za shetani sasa zinafanya kazi sana, kuliko kipindi cha nyuma, na hiyo yote biblia inatumbia ni kwasababu anajua kuwa muda wake umebakia mchache, na ndio maana utaona leo hii matendo mengi maovu ya ajabu ajabu yanatokea ulimwenguni, vitu ambavyo huwezi ukadhani kama mwanadamu anaweza kuvifanya..Hivyo fanya bidii uingie katika ulinzi wa Damu ya Yesu Kristo kwa kutubu na kumwamini Yeye.

Bwana akubariki sana.

Tembelea www.wingulamashahidi.org kwa mtiririko mzuri wa masomo kwa masomo Zaidi.
Maran atha!.

1 comment: