"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, August 12, 2019

TUKAZE MWENDO ILI TUUFIKILIE UTIMILIFU.




Mambo ya dunia hii yanatupa picha halisi ya mambo yanayoendelea rohoni, Kwamfano tukiangalia mataifa yaliyoendelea kama ya Ulaya, tukiyalinganisha na mataifa ambayo hayajaendelea kama vile ya Afrika, utagundua kitu kimoja cha tofauti, utaona watu wa huku wanapambana maisha yao yote ili kupata yale mahitaji ya msingi (Basic needs) kama vile Chakula, malazi na mavazi,.Na mtu aliyefanikiwa kuwa na hivyo vitu basi anaonekana tayari ametoka kimaisha ndio maana tunajulikana kama mataifa machanga..Lakini ukitazama yale mataifa yaliyoendelea utagundua kuwa vitu kama hivyo sio kipaumbele chao kwani karibu kila raia anao uhakika wa kupata mahitaji hayo ya msingi wengine tangu wanazaliwa tayari wanayo, kwani serikali tayari ilishaandaa mazingira mazuri kwa raia wao..

Wao kipaumbele chao kikubwa kipo katika mambo ya utafiti, utakuta jopo kubwa la watu limejikita katika mambo ya utafiti maisha yao yote, na matokeo yake ndio tunayoyaona sasa kwa teknolojia wanazozianzisha duniani, uwezo wa kusafiri katika anga za mbali na mambo ya mawasiliano n.k…Na hiyo ndio inayowafanya waonekane kuwa ni mataifa makubwa na watu wake waonekane kama ni watu bora kuliko wengine tukizungumza kibinadamu.

Vivyo hivyo katika mambo ya rohoni, Mtume Paulo aliona baadhi ya makanisa yapo katika hali ya Uchanga, kipindi kirefu kinapita hata wakati mwingine maisha yao yote lakini bado wanahangaika na mambo yale yale ya msingi ya awali, hawaonyeshi dalili ya kuendelea mbele, Watu wanataka kila siku wapigiwe kelele juu ya mafundisho yale yale ya awali,.wanyweshwe maziwa tu na sio vyakula vigumu vya rohoni, Sio kana kwamba Mtume Paulo alikuwa hawezi kuwafundisha mengine, hapana lakini alikuwa anaona kama tu yale ya msingi wanapata shida kuyatii haya mengi watawezaje?..

Na mafundisho yenyewe aliyoyoataja pale ni kama haya: Mafundisho ya TOBA, mafundisho ya kumwamini Mungu, Mafundisho ya Ubatizo, mafundisho ya ufufuo unaokuja, mafundisho ya Hukumu za Mungu zinazokuja, na mafundisho ya ukombozi(kuwekea watu mikono).

Ambayo kimsingi haya yote ni mafundisho ambayo kila siku tunajifunza na tunafundishwa, makanisani, mitandaoni, mikutanoni n.k..

Hapo Je! sisi si, watoto wachanga?, sisi si maskini wa kiroho?.
Waebrania 5:10 “kisha ametajwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki.
11 Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia.
12 Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu.
13 Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga.
14 Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya”.
Waebrania 6 :1 “Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu,
2 na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele.
3 Na hayo tutafanya Mungu akitujalia”.

Hivyo kabla ya kumwomba Mungu atupeleke katika hatua nyingine ya kujifunza siri za ndani za Yesu Kristo, kama hizo ambazo mtume Paulo alizidokeza alipomfananisha na Melkizedeki, kwa jinsi Melkizedeki alivyokuwa hana baba, wala mama, wala mwanzo wa siku wala mwisho, na ndivyo Bwana wetu Yesu alivyokuwa, mfano wa Melkizedeki kuhani wa milele, kuna siri nyingine nyingi sana zimuhusuzo Bwana wetu Yesu Kristo hatuzijui bado , ambazo tukizijua hizo, hatutaishi kama tulivyo..

Kwasababu ni wazi kuwa bado Kristo anajifunua kwetu kila siku, mpaka Yule malaika wa 7 atakapokuwa tayari kupiga baragumu lake, hapo ndipo Siri yote ya Mungu itakapotimizwa.. Na itakapotilimilika SIRI hiyo (Ambayo inamuhusu Yesu Kristo mwenyewe), Mwisho wa kila kitu utakuwa umefika..
Ufunuo 10:5 “Na yule malaika niliyemwona, akisimama juu ya bahari na juu ya nchi, akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni,
6 akaapa kwa yeye aliye hai hata milele na milele, yeye aliyeziumba mbingu na vitu vilivyomo, na nchi na vitu vilivyomo, na bahari na vitu vilivyomo, ya kwamba hapatakuwa na wakati baada ya haya;
7 isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii”.
Hivyo tumwombe Mungu atusaidie tuvute katika hii hatua ya uchanga tuliyopo sasa, Tusifurahie tu wakati wote kuhubiriwa habari za kutubu dhambi, na kubatizwa,..hayo ni maziwa ndugu, bado hatujaanza kula chakula, Tukiweza kuvuka hayo ndipo Mungu atakapotupeleka katika hatua nyingine..Toba na Ubatizo ni mafundisho ya awali ya msingi, lakini jengo lenyewe bado halijasimama…Lengo ni kupandisha jengo sio msingi, ndio maana tunahitaji kukua kila siku…

TUKAZE MWENDO ILI TUUFIKILIE UTIMILIFU.
Shalom.

No comments:

Post a Comment