"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, August 9, 2019

USITAFUTE FAIDA YAKO MWENYEWE BALI YA WENGINE.


1 Wakorintho 10:23 “Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vifaavyo. Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vijengavyo
24 Mtu asitafute faida yake mwenyewe, bali ya mwenzake.
25 Kila kitu kiuzwacho sokoni kuleni, bila kuuliza-uliza, kwa ajili ya dhamiri;
26 maana, Dunia ni mali ya Bwana na vyote viijazavyo.”
Hapo biblia inasema “vitu vyote ni halali” na inasema pia kila kitu kiuzwacho sokoni kuleni, bila kuuliza uliza…

Sasa tunajua sokoni kuna vitu vingi vinauzwa, sio tu chakula, bali hata nguo, viatu, vyombo, vifaa mbali mbali, simu,tv n.k..Hivyo aliposema kila kitu kinachouzwa sokoni tule pasipo kuuliza uliza, tunapaswa tutumie hekima na sio kutafsiri tu mstari kama tunavyousoma…hivyo pale hakumaanisha kuwa kila kitu kinachouzwa sokoni kama kiatu, pombe,mabegi, nguo, sumu za panya, majembe, na mashoka tuyale! Tuyale kwasababu tu yanauzwa masokoni na maandiko yamesema kila kitu kinachouzwa tule bila kuuliza uliza.. Tukitafsiri maandiko kwa namna hiyo, hatutapata chochote!..Ndio maana pia inachanganya wengi sana, pale Mtume Paulo aliposema “nataka ninyi nyote mnene kwa lugha 1 Wakoritho 14:5” na kuutafsiri mstari kama unavyosomeka pale..bila kuelewa kwanini Mtume Paulo alisema vile…

Tunapaswa tuingie ndani ya mstari huo na kujua Maandiko yalikuwa yanamaanisha nini kuwa ‘kila kitu kinachouzwa sokoni tule bila kuuliza uliza’..

Aliposema kila kitu kuizwacho tule, alikuwa anazungumzia katika engo ya vyakula! Sio bidhaa nyingine tofauti na chakula ambazo zinauzwa masokoni, alikuwa anazungumzia tofauti ya aina ya vyakula, kwamfano umeenda China leo kuhubiri wenyeji wakakukaribisha na kukupeleka kwenye masokoni yao ya umma wanaponunuaga vyakula…na huko ukakuta kuna aina ya vyakula tofauti na vile ulivyovizoea kuviona vinauzwa katika jamii yako ya kiafrika..ukakuta pengine samaki wamechanganywa na majani ya mimea Fulani ambayo hujaijua bado, au nyama ya kuku imepikwa na kuchanganywa na vitu usivyovijua bado.. na wakaenda kukuandalia,Hapo ndio unaambiwa usiulize ulize wewe kula! Bila kuuliza uliza kwamba ni nyama ya kiumbe gani imetengenezewa. Wala usiwe na hofu moyoni mwako kwamba unamkosea Mungu wewe kula hivyo vyakula.. kwaajili ya dhamira zao.

Kwasababu wakikuona wewe unakataa kula aina Fulani ya chakula ambacho hata sio kilevi, bali pengine ni mchanganyiko tu wa vitu usivyovifahamu, wataanza moyoni kushtuka na kujiuliza kwanini huyu mtu hali chakula chetu! Ambacho sisi tunaona ni cha heshima, Kwahiyo watakuwa na maswali mengi ambayo hayana msingi wowote wa kuwavuta wao kwa Kristo, kwasababu hata hicho unachokataa wewe kukila Mungu hajasema usikile! Lakini endapo wamekwambia kwamba hichi ni chakula cha miungu yetu! Hapo utakataa ili wao wasije wakaona kwamba na wewe unakubaliana na wanachokifanya, lakini si kwasababu chakula kile ni najisi.

Au fikiria Mchina anakuja huku kwetu unamkaribisha kwako na unampikia mtori asubuhi, unamtengea ghafla! Anakwambia subiri kwanza! Huu mtori umetengenezwa na nini? Anataka umwelezee kila kitu kabla yeye hajaanza kula!!..kwa mtu mwenye roho nyepesi anaweza akakwazika kwa kitendo hicho tu!..Na kuanza kusema moyoni kwani huyu mtu ananifikiriaje?, anadhani mimi ninaweza kumwekea sumu? Au naweza kumwekea kilevi,? Au anakidharau chakula chetu! Au anatuonaje labda! Na mambo kama hayo!..Lakini utakapoona umemwandalia na yeye akakipokea vizuri hata kama hakula kingi, ni wazi kuwa moyoni mwako utafurahi na ni rahisi Zaidi kukipokea kile alichokileta kuliko endapo angekataa au kuanza kukitolea kasoro chakula chako…

Sasa mambo kama hayo ndio Biblia inasema tuyaepuke! Unapofika ugenini ni Dhahiri kuwa wanajua wewe ni mhubiri au mkristo, hivyo hawawezi kukuwekea sumu mezani, wala kilevi kwasababu ulishawahubiria, hivyo ukitengewa kula bila kuuliza uliza. Ili ndani ya dhamiri zao wasije wakajikwaa, na kukikosa hata kile kizuri ulichowapelekea. Hivyo wakati mwingine hata kama umefika mahali wamekutengea vyakula ambavyo huvipendi, kula tu hata kidogo ili mioyoni mwao wasije wakakwazika na kukikataa hata kile kizuri cha rohoni ulichowapelekea. Na sio tu unapokwenda kuhubiri hata unapoalikwa na rafiki yako au mtu yeyote usiwe mtu wa kuuliza uliza.
 
Sasa endapo ukiwa sokoni peke yako una uhuru wa kuchagua upendacho, , lakini kwa watu wenye Imani changa, epuka uchaguzi uchaguzi mbele yao, ni rahisi kuwapoteza…
Fanya vitu kwa faida ya wengine na sio faida yako wewe.
Kadhalika, unapokwenda kumhubiria kahaba, usifike tu na kumhukumu kwa mwonekano wake kwa mara ya kwanza, wala usikatae kumkaribisha kwako akiwa na mavazi yake ya kikahaba, ukimshutumu kwa mara ya kwanza tu kwa mwonekano wake pasipo hata kumhubiria chochote ni rahisi kumpoteza moja kwa moja, ataishia kukuchukia tu! Ndani ya dhamiri yake na kujiepusha na wewe.

Lakini ukaanza kumweleza kwanza mambo ya msingi, habari za Yesu Kristo na tumaini analotoa na hatima ya mambo yote ya ulimwengu huu, ataguswa moyo hata kama sio siku hiyo hiyo lakini baada ya muda Fulani atakwambia nifanyaje au yeye mwenyewe utaona anaanza kubadilika…Bwana Yesu alipokutana na yule mwanamke Msamaria kisimani habari ya kwanza hakuanza na kumwambia wewe ni kahaba, unawaume watano…
hakumwambia hayo mambo, alianza kuzungumza naye habari za ufalme wa mbinguni kwanza, baadaye sana ndipo alipoanza kumwambia habari za Maisha yake kuwa ana waume watano, na huyu aliyenaye sio wake..lakini angeanza tu kwa kumwambia wewe ni kahaba utakwenda motoni! Unadhani ni nini kingetokea? Hapo hakufanya jambo kwa faida yake binafsi, bali kwa faida ya ufalme wa Mbinguni.

Kadhalika unapomhubiria mtu asiye wa Imani yako labda muislamu, asiyejua chochote kuhusu Imani ya kikristo usianze kwa kumwambia unajua kula nguruwe ni ruksa!..sio najisi?..Hivyo kula nguruwe! Huku unamwonyeshea mistari….Ukifanya hivyo ataishia kukuchukia tu na pengine kuanzisha malumbano…Anza kwa kumweleza Habari za Yesu Kristo, na nguvu ya msalaba…hayo mambo mengine yatakuja baadaye sana…kwani asipokula nguruwe Maisha yake yote, siku ile ya hukuma Bwana atamwuliza kwanini ulikuwa huli nguruwe duniani?..unaona! hataulizwa hayo mambo…kwahiyo mambo mengine hayana maana sana kuyakazania kwa watu wachanga!. Hatupaswi kuhubiri ili kutimiza wajibu Fulani au kujionesha tunajua maandiko, bali tunapaswa tuhubiri kwa NIA thabiti kabisa ya kutafuta roho zilizopotea.
1 Wakoritho 8:1“…. Twajua ya kuwa sisi sote tuna ujuzi. Ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga”
Kadhalika ukikutana na Muislamu na kuanza kumwambia YESU NI MUNGU! Hatakuelewa hata kidogo, mambo hayo yanahitaji ufunuo wa Roho, ambao huo ni Mungu mwenyewe anamfunulia mtu taratibu taratibu, sasa kwa mara ya kwanza mtu asiyemjua Mungu jambo hilo haliwezi kumwingia akilini, anahitaji kukaa chini ya madarasa ya Roho kwanza, taratibu taratibu Roho Mtakatifu baadaye sana ataanza kumfunulia SIRI YA YESU KRISTO kuwa ni Mungu sawasawa (1Timotheo 3:16)..

Wanafunzi wa Bwana Yesu wenyewe iliwachukua muda kuelewa jambo hilo, sembuse mtu anayemsikia Kristo leo kwa mara ya kwanza??..Hivyo unapaswa umhubirie kwanza nguvu za msalaba..Nini kilitokea Edeni na ni kwanini kwa kupitia mtu mmoja dhambi iliingia…na ni kwanini kwa kupita mtu mmoja dhambi isifutike!…hapo kidogo kidogo unaanza kumleta kwa YESU, acha amwelewe kuwa Yesu ni nabii tu, kwa kipindi cha mwanzo mwanzo, akishamwelewa kuwa ni nabii, na kumwamini baadaye Roho atampandisha hatua moja Zaidi na kumfunulia kuwa ni mwana wa Mungu, baadaye yeye mwenyewe ndiye atakayekuja kukuthibitishia kwa maandiko kuwa YESU NI MUNGU! Kwahiyo kila kitu ni hatua!

Hata sisi tulipokuwa wadogo hatukuambiwa Watoto wanapatikana wapi, badala yake tulidanganywa tu wanakwenda kununuliwa, lakini tulipokuwa kiufahamu ndipo tulielewa mambo yote kuwa wanazaliwa, na Watoto wa Kiroho ndio hivyo hivyo, hawawezi kujua au kuelewa mambo yote kwa mara ya kwanza.
Ndio maana kwenye huo mstari wa 24 Mtume Paulo anasema “mtu asitafuta faida yake mwenyewe bali ya wengine”

Bwana akubariki sana.

Kama hujaokoka! Kumbuka wokovu unaanzia hapa hapa duniani!...kama vile hukumu inavyoanza hapa hapa duniani, hivyo kama hujampa Bwana maisha yako kwa kutubu na kudhamiria kabisa kuacha dhambi bado unayo nafasi hiyo sasa kabla mlango wa Neema haujafungwa, tubu sasa na ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa Jina la YESU kwa ajili ya ondoleo la dhambi na Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu, kumbuka biblia inasema wote wasio na Roho wa Yesu hao sio wake (Warumi 8:9) Hivyo tafuta Roho Mtakatifu..Huo ndio muhuri wa Mungu.

No comments:

Post a Comment