"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, June 28, 2019

SIKUKUU 7 ZA KIYAHUDI ZINAFUNUA NINI KWETU?


Baada ya wana wa Israeli kutoka Misri na kuingia katika nchi yao ya ahadi Mungu aliwaagiza wazishe zile sikukuu 7 muhimu kama sikukuu za Bwana katika vizazi vyao vyote,.Kwa maelezo marefu juu ya Sikukuu hizi unaweza ukazisoma katika kitabu cha Mambo ya walawi mlango wa 23 wote, Na sikukuu zenyewe ndio hizi:

1) Sikukuu ya Pasaka:
2) Sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu:
3) Sikukuu ya Malimbuko(mzao wa kwanza):
4) Sikukuu ya majuma(Mavuno):
5) Sikukuu ya Baragumu/Tarumbeta:
6) Sikukuu ya upatanisho:
7) Sikukuu ya vibanda:

Sasa embu tuzichambue hizi kwa ufupi na tuone ni jinsi gani zinaweza kuwa na maana katika majira yetu tunayoishi sasa.

SIKUKUU YA PASAKA ni moja ya sikukuu zile tatu za kwanza zilizofuatana.Yaani ilikuwa ikitoka hii inafuata hii, ni sikukuu zilizotimia ndani ya juma moja tu(yaani wiki moja). Mungu aliwaambia wana wa Israeli kila ifikapo tarehe 14 ya mwezi wa kwanza kwa kalenda yao ya kiyahudi ambayo kwetu sisi inaangukia katikati ya mwezi tatu na wa wanne, Siku hiyo waliagizwa na Mungu waishike siku hiyo kama sikukuu ya pasaka, yaani katika siku hiyo wakati wa jioni watamchinja kondoo mume (ambaye ndio pasaka mwenyewe), kisha watamla wote usiku ule ule bila kusaza, wakiwa wamevaa viatu vyao miguuni na mikanda yao viunoni. Na ikitokea wamesaza basi mtu hataruhusiwa kumla siku inayofuata kama kiporo bali atachomwa moto wote ateketee. Mungu aliwaambia wafanye hivyo kila mwaka kama kumbukumbu lao la siku ile Bwana aliyowatoa Misri na kuwaagiza wamchinje yule Pasaka usiku ule kabla Farao kuwaachia waende zao, Siku ile ilikuwa ni ya tarehe 14 ya mwezi wao wa kwanza, ndio siku ambayo damu ya mwanakondoo Yule iliyochukuliwa na kupakwa kwenye vizingiti na miimo ya milango yao, ili malaika Yule wa mauti atakapopita asiwadhuru wazaliwa wa kwanza wa kiyahudi.
Hii inafunua usiku ule wa Bwana Yesu kabla kusulibiwa kwake alipoketi na wanafunzi wake ili kuila pasaka ile, Lakini yeye hakuila bali aliwapa wanafunzi wake divai ile na kuwaambia wanywe kama kumbukumbu la damu yake itakayokwenda kumwagika kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote.

Hivyo ashukuruwe Mungu sisi tuliompokea tumepita kutoka mautini kwenda uzimani, hatuna hati ya hukumu juu yetu, Siku ile Bwana atakapoanza kuangamiza na kuuhukumu ulimwengu wote sisi tutakuwa sehemu salama tumefichwa kwasababu pasaka wetu alishachinjwa kwa ajili yetu..Na kuonyesha jinsi matukio yalivyolandana siku hiyo ambayo Bwana anayasema hayo maneno kwa wanafunzi wake ilikuwa ni siku hiyo hiyo ya tarehe 14 ya mwezi wa Kwanza. Hakuna shaka yeye ndiye Pasaka, Haleluya?

Sikukuu inayofuata ilikuwa ni SIKUKUU YA MIKATE ISIYOTIWA CHACHU, hii ilianza moja kwa moja siku iliyofuata, Wana wa Israeli waliagizwa, wale mikate isiyotiwa chachu kwa muda wa siku 7 yaani kuanzia tarehe 15 ya mwezi ule ule wa kwanza, na mtu yeyote ambaye alionekana akila mikate iliyotiwa chachu (yaani hamira) mtu huyo aliuliwa bila huruma.
Walawi 23:6 “Na siku ya kumi na tano ya mwezi ule ule ni sikukuu kwa Bwana ya mkate usiotiwa chachu; mtaila mikate isiyochachwa muda wa siku saba.
7 Siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu msifanye kazi yo yote ya utumishi.
8 Lakini mtasongeza sadaka kwa Bwana kwa njia ya moto siku saba; siku ya saba ni kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi.”
Hii ikifunua Neno la Mungu lisiloweza kugoshiwa, kumbuka usiku ule ule Bwana Yesu alitwaa mkate na na kusema, huu ndio mwili wangu utolewao kwa ajili yenu uleni..Hata sasa sisi tuliookolewa tunaula mwili wa Kristo kila siku, ili tuwe na uzima ndani yetu. Yeye alisema asiyekula mwili wangu hana uzima ndani yake.(Yohana 6:53) Na mwili wa Kristo ni Neno lake lisiloweza kugoshiwa na mafundisho ya uongo(Chachu), ambao watoto wa Mungu wanakula.. Yesu ndiye mkate wa uzima kweli kweli, mikate mingine yote inayodai kutoa tumaini la baadaye ni mikate iliyotiwa chachu ambayo haiwezi kumpeleka mtu popote.. Mpaka hapo nadhani unaona ni jinsi gani hizi sikukuu zilivyokuwa na maana kwetu sisi wa agano jipya, zinafunua picha halisi ya mambo yatakayokuja kuendelea katika siku za neema.

Sikukuu iliyofuata waliyogizwa waishike ni sikukuu ya (MALIMBUKO)MZAO WA KWANZA: Ni sikukuu ambayo Mungu aliwaagiza waisraeli wote waishike kama kuonyesha shukrani na Heshima kwa Mungu, kwa Baraka Mungu alizowapa za mavuno ya kwanza na hiyo inaambata na kupeleka sehemu ya kwanza katika mavuno yao. Na hii inafanyika siku ya pili baada ya Sabato, yaani jumapili, kumbuka hizi zote zinafanyika ndani ya wiki hiyo hiyo moja.(Walawi 23:9-14). Waisraeli waligizwa hivyo lakini lakini hawakajua mambo hayo yanafunua nini rohoni katika wakati wetu.

Sisi tuliopo sasa ndio tunakuja kujua kuwa baada ya Kristo kukaa siku tatu kaburini, jumapili alfajiri, siku ya kwanza ya juma alifufuka,katika sikukuu hiyo hiyo ya malimbuko ya wayahudi kama mzaliwa wa kwanza katika ya wafu, na vilevile kama mzaliwa wa Kwanza katika ya ndugu wengi.. Kristo ndiye limbuko letu Haleluya..Yeye alikuwa wakwanza kufufuka hivyo na wote waliolala katika Bwana watafufuka na kuwa kama yeye baadaye.

Kisha baada ya sikukuu hiyo kupita Mungu aliwaagiza tena wana wa Israeli wahesabu majuma 7 saba, au sabato 7 kuanzia hiyo siku ya malimbuko ambazo zitakuwa ni siku 49, na itakapofika ile siku ya 50 itakuwa ni Sikukuu ya Mavuno(Au sikukuu ya majuma), Dhumuni kubwa la sikukuu hii ni kumshukuru Mungu kwa ajili ya mavuno ya mwisho. Na Kufunga wakati wa mavuno

Hii inatufunua moja kwa moja, mara baada ya Bwana wetu Yesu Kristo kufufuka siku ile ya jumapili alfajiri aliwaambia wanafunzi wake wasiondoke Yerusalemu mpaka watakapoipokea ile ahadi ya Baba, Na kama tunavyosoma biblia ilipofika siku ile ya Pentokoste, Mungu aliwamwagia kipawa cha Roho Mtakatifu, Sasa hii siku ya Pentekoste ndio kwa jina lingine inaitwa sikukuu ya majuma(Au sikukuu ya mavuno). Ilikuwa ni siku ya 50 baada ya Yesu kufufuka.. Unaona sikukuu hizi zilivyoambatana na matukio muhimu kwa agano letu jipya?. Nne ya hizo zimeshapita..bado tatu mbeleni zinakuja.

Na baada ya hapo tena Mungu aliwaagizwa wana wa Israeli waishike sikukuu ya Baragumu/Tarumbeta, (Hesabu 29:1) Sasa hii inaangukia katika mwezi wao wa 7 tarehe ya kwanza, ambayo kwetu sisi ni katikati ya mwezi wa 9 na wa 10..Utaona hapo ni kipindi kirefu kidogo kinapita mpaka sikukuu nyingine kuanza, Ipo sababu Mungu kuruhusu iwe hivyo,..Sasa siku hii Tarumbeta/Mbiu inapigwa kwa Waisraeli wote kuwaamsha na kuwayafanya wajiweke tayari kwa sikukuu mbili kuu na takatifu zinazokuja mbeleni.

Sasa hii katika Roho inafunua nini? Kumbuka tangu siku ile ya Pentekoste(Yaani kipindi cha Roho Mtakatifu kuachiwa juu ya watu) mpaka sasa tunachosubiria ni Unyakuo ambao huo tunajua utaambatana na parapanda ya Mungu, Ukisoma 1Wakorintho 15:51 utaona inasema “ Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,
52 kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa PARAPANDA YA MWISHO; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.”

Unaona?. Sasa tangu huo wakati mpaka utaona kama ni muda mrefu wa takribani miaka 2000, kufunua kile pindi kirefu tangu ile sikukuu ya majuma, hadi ile sikukuu ya baragumu, baragumu kwa jina lingine ni tarumbeta, au mbiu au paraparanda.

Hivyo ndugu wakati umeshakaribia wa sikukuu hii ya 5 kujifunua kwetu, parapanda italia, na ikilia tu itatimiza makusudi mawili, la kwanza ni kuliondoa Kanisa la Mtaifa duniani kwa ule unyakuo, na la pili itakuwa ni kuwaamasha Wayahudi sasa wajiweke tayari kwa utakaso ambao Mungu anakwenda kuachia juu yao kwa sikukuu inayokwenda kufuata.

6) Sasa sikukuu inayofuata inajulikana kama sikukuuu ya upatanisho: Hii inakuja siku ya 10 ya mwezi huo huo wa saba. Ilikuwa ni siku ambayo Kuhani mkuu anafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi za waisraeli wote, ambayo ndio ile inayofanyika mara moja kwa mwaka, wakati huu kila mwisraeli anapaswa kujitaabisha nafsi yake, kwa kulia kutubia maovu yake, na mtu yeyote atakayeonekana anastarehe katika kipindi hicho mtu huyo atauawa, au yoyote atayeonekana anafanya kazi yoyote ile, vile vile mtu huyo atauawa.
Walawi 23:27 “Lakini siku ya kumi ya mwezi huo wa saba ni siku ya upatanisho; itakuwa kusanyiko takatifu kwenu, nanyi mtazitesa nafsi zenu; nanyi mtasongeza sadaka kwa Bwana kwa njia ya moto”.
Sasa tukirudi katika agano jipya sikukuu hii inafunua nini, kumbuka kanisa wakati huo litakuwa limeshanyakuliwa, siku ile parapanda itakapolia, Na tunafahamu kuwa hadi wakati huu wayahudi wengi bado hawajampokea Kristo kama Masihi wao, sasa mara baada ya unyakuo kupita Mungu atawamwagia tena Roho ya Neema Wayahudi wote, kisha watafunguliwa macho na kugundua kuwa Yule Kristo waliyemchoma wakati ule pale Kalvari ndiye Masihi wao waliokuwa wanamtazamia, siku hiyo ndipo watakapolia na kuomboleza, watatubia maovu yao ndipo Mungu atakapofanya upatanisho wa dhambi zako, na kuwapokea na kuwapigania kama zamani, na wokovu kuanzia huo wakati utakuwa kwa wayahudi sasa wakati huo wale waliobakia katika mataifa ambao hawakwenda katika unyakuo neema itakuwa imeshaondoka kwao, kilichobakia kwao ni kujumuika na mpinga-Kristo kupambana na wayahudi na kikundi kidogo sana ambacho kilikuwa katika mstari lakini kilizembea neema, ndio wale wanawali wapumbavu wanaozungumziwa katika(Ufunuo 25).
Zekaria 12:10 “Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.
11 Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido.
12 Nayo nchi itaomboleza, kila jamaa peke yake; jamaa ya nyumba ya Daudi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Nathani peke yao, na wake zao peke yao;
13 jamaa ya nyumba ya Lawi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Shimei peke yao, na wake zao peke yao.
14 Jamaa zote zilizosalia, kila jamaa peke yake, na wake zao peke yao.”
Wakati huu ndipo Mungu ataanza kuyahukumu mataifa yote duniani kwa kupitia Taifa la Israeli watu wake. Unaweza kuona ni wakati gani huu tunaishi, Israeli sasa imeshakuwa taifa lililosimama, kinachongojewa ni unyakuo tu, Mungu aanze kutenda nao kazi..

Sikukuu ya 7 na ya Mwisho ni sikukuu ya VIBANDA: Sikukuu inaanza tarehe 15 ya mwezi huo huo wa 7, Ukiangalia utaona nazo hizi tatu za zinaongozana, kutoka tarehe 1, mpaka 10, na sasa 15, kama tu vile zile sikukuu tatu za kwanza zilivyoongozana..Ni kufunua kuwa tangu kipindi kile cha Unyakuo hadi mambo yote kuisha kitakuwa ni kipindi kifupi sana, yaani kulingana na biblia ndani ya miaka 7 mambo yote yatakuwa yameisha.

Sasa katika sikukuu hii Mungu aliwaagiza wana wa Israeli watengeze vibanda, nje ya nyumba zao kwa miti mbalimbali au majani ya mitende, na ni amri kwa kila mwisraeli ndani ya siku hizo yaani saba anapaswa alale nje kwenye vibanda hivyo walivyovitengeneza huku wakimfurahia Bwana wakikumbuka jinsi alivyowatoa katika nchi ya Misri na kukaa katika vibanda wakati ule walipokuwa jangwani. Wakati ambapo maskani ya Mungu ilikuwa na Watoto wake jangwani…Hizo ndizo sikukuu kuu 7 za Bwana ambazo aliwaagiza wana wa Israeli wazishike kila Mwaka milele na milele.

Sasa sikukuu hii ya saba katika Roho: Inafunua ule utawala wa miaka 1000 ambao Bwana Yesu atakuja kutawala hapa duniani kama mfalme wa wafalme na Bwana wa Mabwana, pamoja na watakatifu wake na wayahudi wake..Biblia inasema wakati huo. Mataifa yote yatapaswa yatii amri ya Mfalme Yesu, na kuishika sikukuu ya vibanda.

Zekaria 14: 9 “Naye Bwana atakuwa Mfalme juu ya nchi yote; siku hiyo Bwana atakuwa mmoja, na jina lake moja.
10 Nchi yote itageuzwa kuwa kama Araba, toka Geba mpaka Rimoni upande wa kusini wa Yerusalemu; naye atainuliwa juu, atakaa mahali pake mwenyewe, toka lango la Benyamini mpaka mahali pa lango la kwanza, mpaka lango la pembeni; tena toka mnara wa Hananeli mpaka mashinikizo ya mfalme.
11 Na watu watakaa ndani yake, wala hakutakuwako laana tena; lakini Yerusalemu utakaa salama……………………….
16 Hata itakuwa, ya kwamba kila mtu aliyesalia wa mataifa yote, waliokuja kupigana na Yerusalemu, atakwea mwaka baada ya mwaka ili kumwabudu Mfalme, Bwana wa majeshi, na kuishika SIKUKUU YA VIBANDA.
17 Tena itakuwa, ya kwamba mtu awaye yote wa jamaa zote zilizomo duniani, asiyekwea kwenda Yerusalemu ili kumwabudu Mfalme, Bwana wa majeshi, mvua haitanyesha kwao.
18 Na kama jamaa ya Misri hawakwei, wala hawaji, pia haitanyesha kwao; itakuwako tauni, ambayo Bwana atawapiga mataifa, wasiokwea ili kushika sikukuu ya Vibanda.

(Kwa maelezo ya ziada kuhusu sikukuu ya vibanda⏩ bofya hapa

Hii ni kuonyesha kuwa wakati huo, Bwana pamoja na watakatifu na wayahudi, watasterehe na Kutawala dunia nzima, ambapo Maskani ya Mungu itakuwa pamoja na wanadamu duniani.. na ndio biblia inasema Fimbo ya chuma itatumika kwa yale mataifa ambayo yataonekana hayatii Amri za Mfalme YESU na watakatifu wake.

Unaona jinsi siku zilivyoisha?, wakati wowote parapanda italia na bibi-arusi atakwenda kumlaki Bwana mawinguni, je! Na wewe utakuwa mmojawapo?. Kama huna uhakika basi muda unaosasa mchache wa wewe kutubu, geuka mfuate Kristo kwa nia moja, ulimwengu usikusonge ukasahau kuyaangalia na mambo yanayokuja. Dunia inapita ndugu, Je! Katika maisha unayoishi Kristo yupo ndani yako?. Uamuzi ni wako. Ombi langu ni utubu sasa.

Bwana akubariki.
www.wingulamashahidi.org

No comments:

Post a Comment