"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, June 28, 2019

NAMNA GANI NITAPOKEA NGUVU ZA BWANA YESU?.


Shalom. Jina la Bwana wa Utukufu Yesu Kristo, libarikiwe.Biblia inasema katika kitabu cha Marko..
Marko 5:21 ‘Hata Yesu alipokwisha kuvuka kurudia ng'ambo katika kile chombo, wakamkusanyikia mkutano mkuu; naye alikuwa kando ya bahari.
22 Akaja mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo; hata alipomwona, akaanguka miguuni pake,
23 akimsihi sana, akisema, Binti yangu mdogo yu katika kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako juu yake, apate kupona, na kuishiAkaenda pamoja naye; mkutano mkuu wakamfuata, wakimsonga-songa.
24 Akaenda pamoja naye; mkutano mkuu wakamfuata, wakimsonga-songa.
25 Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili,
26 na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya
27 aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake;
28 maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona
29 Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule.
30 Mara Yesu, hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano, akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi yangu?
31 Wanafunzi wake wakamwambia, Je! Wawaona makutano wanavyokusonga-songa, nawe wasema, Ni nani aliyenigusa?
32 Akatazama pande zote ili amwone yule aliyelitenda neno hilo.
33 Na yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka, akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza kweli yote.
34 Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena.
Katika mfano huu, tunaona Bwana Yesu akitokwa na Nguvu, lakini wengi wanafahamu kuwa nguvu hizo zilikuwa ni za mwili…na hata mimi nilikuwa nafahamu hivyo mwanzoni…kwamba yule mwanamke alipomgusa tu Bwana, Basi Bwana alihisi kuna udhaifu Fulani umeingia mwilini mwake..mfano wa mtu aliyekuwa amelima hekari 10 za shamba na nguvu kumpungukia na kukaa chini...Lakini tafsiri hiyo si kweli..Nguvu zilizomtoka Bwana ni nguvu za Rohoni ..Yaani nguvu za uponyaji. Na hazikutoka na kumwendea tu yule mwanamke aliyekuwa anatokwa na damu..bali zilikuwa zinatoka na kuwaendea watu wote waliokuwa wanamwendea waponywe.

Sasa hizo nguvu kwa ufupi kama tulivyosema ni nguvu za uponyaji…Na kama umegundua nguvu hizo, mtu anaweza kuzitwaa kutoka kwake Bwana pasipo hata idhini ya Bwana mwenyewe, kama huyu mwanamke alivyofanya…hakumwambia wala kumwomba Bwana amponye, wala hakuwa mfuasi wa Bwana Yesu…lakini aliutwaa uponyaji wake pasipo hata kumshirikisha Bwana…na pia Bwana mwenyewe anaweza kumpa mtu kwa idhini yake mwenyewe kama huyo mkuu wa Sinagogi alivyomtaka Bwana akamwekee mkono binti yake..Ni nguvu zile zile zilizomtoka Bwana na kumponya yule mwanamke ndio hizo hizo ambazo zilikwenda kumfufua yule binti wa Mkuu wa sinagogi…zote ni nguvu zilizotoka ndani ya Bwana.

Tukiendelea na mstari wa 35, tunaweza tukaona jambo hilo..
Marko 5:35 ‘’Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu?
36 Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu.
37 Wala hakumruhusu mtu afuatane naye, ila Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye Yakobo.
38 Wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo makuu.
39 Alipokwisha kuingia, akawaambia, Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu.
40 Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana.
41 Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka.
42 Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu.
43 Akawaonya sana, mtu asijue habari ile; akaamuru apewe chakula’’.
Hata sasa Bwana hajaishiwa nguvu…bado zinaendelea kutoka, na tunaweza kuzitwaa kwake pasipo hata idhini yake, na hapo kinachohitajika ni Imani tu!. Wengi wanajua mpaka upokee uponyaji Fulani inahitaji umjue sana Mungu, uwe kwenye maombi ya muda mrefu ya kufunga na kuomba..hapana Mungu hayupo hivyo kabisa….

Wakati mwingine ndio maana hata watu wasio waKristo, ambao hata hawaielewi Imani ya Kikristo, ni rahisi kupokea uponyaji kwa Yesu kuliko hata wakristo, Unajua ni kwanini?...Ni kwasababu hiyo hiyo, kupokea nguvu kutoka kwa Bwana haihitaji wewe umjue sana, formula yake ni ndogo sana! Kugusa pindo lake kwa Imani tu!..Na watu wengi wasio wa Kristo ndio wanapokeaga uponyaji wao kwa njia hiyo..wanamgusa upindo tu na wanavuta nguvu za Mungu ndani yao..Sasa sio kwamba ukiponywa na Mungu ndio upo sawa na Mungu, hapana! Hivyo ni vitu vingine, hapa tunazungumzia habari ya uponyaji.
Kadhalika na sasa, usingoje Umjue Bwana Zaidi ndio unufaike kutoka kwake,! Hapana bali hata katika hiyo hali yako ya kikristo, Mguse Bwana katika pindo lake upokee Neema za kumjua yeye Zaidi, mguse upindo wa vazi lake Upokee Roho Mtakatifu Zaidi, Mguse Upindo wa vazi lake upokee nguvu za kumwabudu yeye Zaidi na za kumwimbia, na za kuwahubiria wengine habari njema, mguse pindo lake akuongezee hekima…Hizo nguvu zipo, haihitaji umfahamu sana..ni Kuamini tu kwamba ukimwomba atakupa!!..na atakapokupa ndio itakuwa mwanzo wa wewe kumjua Zaidi…Na hivyo unamwendea kwa imani na kumwambia Bwana, leo hii nataka niwe chombo chako kiteule, nifinyange na kunitengeneza.

Baada ya kuomba hivyo hapo hapo anza kuishi Maisha yanayolingana na ulichomwomba, baada ya muda mfupi utaona mabadiliko makubwa kwenye Maisha yako, yote uliyomwomba utakuwa umeyapata.

Bwana akubariki.

No comments:

Post a Comment