"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, June 28, 2019

IMANI NI KAMA MOTO.


Habari ya uzima wako mtu wa Mungu, Nakukaribisha tuzitafute kwa pamoja Tunu za rohoni (Neno la Mungu) Sabuni ya kweli ya roho zetu..

Leo tutaangazia siri mojawapo ya Imani ambayo tukiijua basi hatutaogopa jambo lolote liwe kubwa au dogo mbele yetu. Kama kichwa cha somo kinavyosema “Imani ni kama Moto”, Hii Ikiwa na maana tukiujua ufunuo ulio katika moto basi hatutaogopa ukubwa wa kichaka au msitu ulio mbele yetu, Embu jaribu kufikiria Leo unapokwenda katika mbuga za wanyama marufuku ya kwanza unayopewa kule ni “hakuna kuvuta sigara mbugani”, ni kwasababu gani, ni kwasababu wanajua ule moto kidogo, uliopo juu ya kile kipande cha sigara kinaweza kuleta madhara makubwa sana. Hata wewe leo hii hii ukapewa kiberiti na mbele yako zikapangwa kuni kama mlima, ni wazi kuwa huwezi kuugopa wingi ule wa Kuni kwasababu unajua ufunuo ulio katika moto.
Kwamba Moto kidogo tu unatosha kumaliza kila kitu, una tabia ya kukua na kuongezeka kulingana na ukubwa wa shuhuli yenyewe, kama ni kuunguza karatasi, utakuwa ukubwa wa kulingana na karatasi, kama ni kuunguza mbuyu utakuwa kulingana na saizi ya mbuyu kama ni kuunguza msitu vile vile utakuwa mkubwa sana kulingana na saizi ya msitu wenyewe..Lakini chanzo chake kilikuwa ni kitu kidogo sana yaani njiti moja tu ya kiberiti.

Na ndivyo ilivyo Imani, Imani inatabia ya kukua kulingana na ukubwa wa jambo, lakini inaanza kama chembe ya haradali, Usitazamie mpaka uwe na imani kubwa kama bomu la atomiki ndio utaweza kutatua tatizo Fulani kubwa, ukiwa na mtazamao huo basi uwe na uhakika kuwa utakwama tu, hicho kiwango hutakaa ukifikie, ni sawa na mtu ambaye anajaribu kupakia moto mwingi kwenye mashehena ili aende kuumwaga kwenye msitu ili uwake?, tengeneza picha mtu huyu kwanza atawezaje wezaje kuukusanya moto pamoja, kwasababu moto ni kitu kisichoweza kushikika, wala kukusanyika. Ndivyo ilivyo Imani usijaribu kuichanga imani iwe nyingi ili siku moja ujaribu kufanya jambo Fulani utakwama tu.

Sasa embu tutazame kisa kimoja katika Biblia ambacho na sisi tunaweza kujifunza Jambo ndani yake kuhusu somo hili. Zamani za waamuzi, wana wa Israeli wapomlilia Mungu awepe mfalme kama watu wa Mataifa mengine walivyo na wafalme..Mungu alisikia kilio chao na kuwapa mfalme mmoja aliyeitwa Sauli. Sasa huyu Sauli biblia inasema alikuwa ni mtu shujaa sana, mtu ambaye Mungu alimvika ujasiri mwingi katika vita..Na yeye alikuwa na mtoto wake kipenzi aliyeitwa Yonathani, wote hawa walikuwa mashujaa kweli walipigana kita vingi sana na Mungu kuwapa ushindi mkuu lakini ilifika wakati wafilisti waliwazingira, mambo yalikuwa magumu kweli kwa Israeli.

Wafilisti waliwapandia na jeshi lao lote, pamoja magari mengi sana ya vita, na watu wasioweza kuhesabika kama mchanga wa baharini ili kupigana nao. Hivyo Israeli walipoona vile, walivunjika moyo sana, biblia inasema ndipo watu wakaanza kwenda kujificha katika mapango, na katika vichaka, na katika miamba, na katika mashimo, na katika mabirika. (1Samweli 13:6). Na wengine wakawa wakimbizi katika nchi jirani, Ndipo watu wengi wakamfuata Sauli kwa kutetemeka waone atachukua uamuzi gani, Sauli kuona vile akautafuta Uso wa Mungu kwa Samweli lakini Samweli hakuja kwa wakati alioutarajia, ndipo watu wengi wakamkimbia kwenda mbali kabisa na Israeli.. Maana jeshi lile lilivyokuwa kubwa walijua kabisa kulikuwa hakuna kupona mtu..si mfalme wala mtumwa.

Na kibaya zaidi hakukuwa na mtu hata mmoja aliyekuwa na Panga wala mkuki isipokuwa Sauli tu na Yonathani mtoto wake, kwani kipindi kile walikuwa wanawategemea sana wafilisti kama wahunzi wao wa kuwatengenezea silaha sasa, wahunzi wao ndio wamekuwa maadui zao, unaona hiyo ni shida mara dufu.. Jaribu kutengeneza picha labda Nigeria inakuja kupigana na Tanzania, na hakuna mwanajeshi hata mmoja mwenye silaha,isipokuwa raisi tu na mtoto wake, na unaambiwa wameshavuka Kagera wanashuka, hata kama ni wewe lazima hofu itakuingia na kikubwa utakachofanya ni kuondoka kukimbilia Kenya au nchi jirani unusuru roho yako na familia yako au kujificha. Ndivyo ilivyokuwa kwa Israeli kipindi hicho.
Lakini ilifikia sikumoja Yonathani akasema moyoni mwake ninachoogopea ni nini, akamwamini Mungu, akakusudia kuondoka kuwafuata mamilioni ya wafilisti akiwa yeye peke yake pamoja na mtumwa wake bila kumwambia mtu yoyote, hata baba yake hakumweleza..hapo ndipo Imani kama njiti ilipoanza kutenda kazi, kwenda kuchoma msitu…wakati mwingine ukikusudia kufanya kitendo cha Imani, usimshirikishe kila mtu, utakutana na vipingamizi visivyokuwa na sababu..

Tunasoma hayo katika:
1Samweli 14:6 “Basi, Yonathani akamwambia yule kijana aliyemchukulia silaha zake, Haya! Na twende tukawavukie ngomeni hao wasiotahiriwa; yamkini Bwana atatutendea kazi; kwa maana hakuna la kumzuia Bwana asiokoe, kwamba ni kwa wengi au kwamba ni kwa wachache.”
Yonathani hakusubiri Maono kutoka kwa Samweli ndio atende jambo, hakusubiri aote ndoto ndipo afanye jambo, hakungojea wapate msaada wa kijeshi kutoka nchi za jirani wapate jeshi la kutosha ndio Imani ya kupambana nao ije, hapana yeye aliifahamu siri ya Imani.

Na alipofika mbeleni alikutana kweli na jeshi la wafilisti, Yonathani na mwenzake wakasema tusimame hapa ikiwa watatuita tuwafuate kule walipo basi hiyo ni ishara tosha ya kuwa Mungu yupo upande wetu tuwamalize, na kweli walipowafikia pale wakawaambia pandeni huku, ndipo walipojua kuwa hawa ndio nyama yetu, walipanda kule juu sio kwa uowoga woga, bali walipanda kwa ujasiri na kwa kasi kama wanyama, kwa mikono yao na miguu yao..na walipofika pale ndani ya eneo dogo sana Yonathani aliwaua mashujaa 20 kwa mpigo,huku Yule kijakazi wake akiwamalizia, na pale pale kukatokea tetemeko kubwa lisilo la kawaida, wale wafilisti waliokuwa kwenye makambi, na wale waliokuwa wanaendelea kuteka nyara wakaogopa sana, mpaka nchi nayo ikatetemeka kwa Imani ile.. watu wakaanza kukimbia ovyo ovyo kama vichaa,..

Hadi huku nyuma Sauli alipokuwa amejificha na mashujaa wake, wakashangaa kilele zile zinatokea wapi, kuona vile wakanyanyuka na wao kushuka vitani, na kule vitani sasa cha ajabu ni kuwa upanga wa kila mmoja ukawa juu ya mwenzake, wakauana wafilisti wengi sana…na kulikuwa na baadhi ya wayahudi ambao Wafilisti waliwateka nyara na siku ile ya vita walishuka nao wawasaidie vitani, lakini walipoona wokovu unarudi kwao nao pia wakawageuka wakaanza kuwaua…Unaona jinsi imani kama moto inavyokuwa kulingana na ukubwa wa tatizo..

Hivyo nguvu ikazidi kuongezeka sana, hata na wale waisraeli wengine waliokuwa wamejificha mashimoni, na vichakani nao pia wakapata nguvu wakajitokezeka kuendeleza mapigo..Hiyo yote ni matunda ya imani ya mtu mmoja tu Yonathani. Siku hiyo wakapata ushindi mnono sana, kutoka kwa Mungu..(hapo nimeeleza kwa ufupi tu Kwa muda wako binafsi unaweza ukasoma habari yote 1Samweli 13&14,.)

Lakini nataka uone ni jinsi gani Imani inavyotenda kazi, Leo hii unapofikiria kumtumikia Mungu, usiangalie kanisa liko wapi,?, usiangalie ni watu wangapi wananisapoti, nina fedha kiasi gani za kuhubiri, ukifikiria hivyo ndugu hutafika popote, hapo ulipo anza, kitaonekana ni kidogo, lakini fahamu kuwa imani umbo lake sikuzote ni kama chembe ya haradali, lakini matokeo yake ni milima mikubwa..Na hiyo imani ipo ndani ya kila mmoja..

Vile vile na katika mambo yako mwenyewe binafsi, usifirie labda ugonjwa huu hautikibiki, au jeraha hili haliponyeki, mimi nimezaliwa katika ulemavu tangu utotoni siwezi kurudia katika hali yangu ya kawaida, nataka nikuambie Amini, tu kama unavyouamini moto..Tatizo lote litayeyuka kama utaendelea kudumu kutika kumwamini YESU Mponyaji wetu.

Na pia katika kazi zako na shuhuli zako binafsi, usiogope kidogo unachoanza nacho, ukiwa na imani huku ukiwa mwaminifu kwa hicho unachokifanya unatenda haki, hayo ni matendo ya imani, Mungu atakikuza na kuwa kikubwa..na kufunika vya wengine wote, ikiwa tu utafanya kwa uaminifu huku unamcha Mungu.

Bwana akubariki sana.
www.wingulamashahidi.org

No comments:

Post a Comment