Shalom…Karibu katika mwendelezo wa
Kitabu cha Ufunuo..ambapo leo kwa Neema za Bwana tutaendelea na ile sura la
10..Kama hujapitia sura zilizotangulia, ni vizuri ungezipitia kwanza ili tuweze
kwenda pamoja katika hizi sura zinazofuata.
Katika sura iliyopita tumeona
malaika sita wakipita baragumu zao, na tuliona matukio yaliyoambatana na
baragumu hizo, lakini katika sura hiyo hatukuona malaika wa saba akipiga
baragumu lake, ikifunua kuwa kuna vitu Fulani vinapaswa viendelee kabla malaika
wa mwisho kupiga baragumu…Na ndio tunaona katika sura hii ya 10, Yohana
anakatishwa maono ya baragumu la mwisho la saba na kuonyweshwa ono lingine la
Ajabu, ambalo ufunuo wake utatimia kabla ya baragumu la mwisho la saba
kupigwa..Tusome.
Ufunuo 10: 1 “Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto”.
Sasa huyu malaika si mwingine Zaidi
ya Bwana Yesu Kristo, kumbuka Bwana Yesu sio malaika viumbe wa rohoni
wanaotumika mbinguni, hapana! Bali ni “MALAIKA WA AGANO” au kwa lugha nyingine
“MJUMBE WA AGANO” (Malaki 3:1 Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye
ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake
ghafula; naam, yule MJUMBE WA AGANO mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema
Bwana wa majeshi.
…Kwa lugha ya kiingereza “ANGEL OF
THE COVENANT or MESSENGER OF THE COVENANT”…Neno malaika ni neno la kigiriki
lenye tafsiri ya MJUMBE…kwahiyo kuna aina mbili za wajumbe,1) Wajumbe wa
kimbinguni ambao ndio malaika wa rohoni, 2) na pia wapo wajumbe wa kidunia,
ambao hao ni wanadamu…Yohana Mbatizaji alikuwa ni Mjumbe wa Mungu wa kidunia,
Gabrieli ni mjumbe wa Mungu wa kimbinguni…wote hawa ni Malaika, kwa kigiriki ‘Angelos’
kwa kiebrania ‘Malokh’ kwa Kiswahili ‘Malaika’. Kadhalika wale malaika saba wa
makanisa saba ya Asia tuliowaona katika Ufunuo Mlango wa 2 na wa 3 wale ni
wanadamu.
Hivyo katika Ono hili Yohana
anaonyeshwa Malaika mwenye nguvu akitoka mbinguni, kirahisi Zaidi tunaweza
kusema Yohana alimwona Mjumbe mwenye nguvu akitoka mbinguni…Sasa Mjumbe huyu si
mwingine Zaidi ya BWANA YESU KRISTO, Akiwa katika mfumo wa ‘KIMALAIKA WA
MBINGUNI’..Ni Yesu Kristo mwenyewe akijidhihirisha kama Malaika katika ono… lakini
utasema Bwana anaweza akajidhihirisha
kama Malaika?...Jibu ni ndio! Anaweza…
Mwanzoni kabisa wa kitabu hichi
tunamwona akijifunua kwa sifa kama za viumbe vya rohoni, malaika walizo nazo,
utaona katika Ono Yohana alimwona ana macho kama miali ya moto…na miguu yake
kama shaba iliyosuguliwa sana. (Ufu.1:13-15), hakuna mwanadamu wa namna
hiyo…Lakini alikuwa ni Bwana akijifunua kwa sifa za malaika..Na hapa hivyo
hivyo ni Bwana Yesu yule yule akishuka kutoka Mbinguni kwa mfano wa Malaika…Uso
wake uking’aa kama jua, na miguu yake kama nguzo ya moto…Uso wake kung’aa kama
jua unadhihirisha utukufu wake… ukuu wake, kama vile jua linavyong’aa na
kuangaza sana na kuwa Nuru ya Ulimwengu mzima..Kadhalika Kristo naye ni Nuru ya
ulimwengu, maandiko yanasema hivyo katika Yohana 8:12..Na ni Kristo pekee
ambaye uso wake unang’aa kama jua, hakuna mjumbe wowote wa duniani wala
mbinguni ambaye uso wake unang’aa kama jua..Ndio maana utaona tena
alijidhihirisha kwa namna hiyo mbele ya wanafunzi wake katika..
Mathayo 17: 1 “Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani; 2 akageuka sura yake mbele yao; USO WAKE UKANG'AA KAMA JUA, mavazi yake yakawa meupe kama nuru”.
Na pia katika Ono alilooneshwa
Yohana alimwona, akiwa amevikwa wingu kama vazi, wingu linaashiria utukufu wa
Mungu, ndio maana tunasoma mahali Fulani kwamba Kristo atakuja na Mawingu, kama
alivyoondoka na mawingu, na sisi tutamlaki mawinguni (Utukufuni). Na pia
tunaona juu ya kichwa chake kulikuwa na upinde wa Mvua, Upinde wa Mvua
unaashiria Agano la Mungu analofanya na wanadamu, Kwamba Kristo ni Bwana wa
maagano, kama vile alivyoweka Agano lake na nchi kuwa hataiangamiza dunia tena
kwa gharika ya maji, na mpaka leo hilo Neno lake hajalitangua, vivyo hivyo,
maneno yake mengine yote yaliyosalia hawezi kuyatangua, yeye ni Mungu wa
kushika maagano, ndio maana unaona juu ya kichwa kuna moja ya ishara ya Maagano
yake aliyoyafanya juu ya nchi kuashiria kuwa mwenye mamlaka ya kuangia maagano
amesimama naye ni mmoja tu Yesu kristo.
Tukiendelea na mstari wa pili biblia
inasema..
Ufunuo 10:2 “Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, nao wa kushoto juu ya nchi”
Katika mkono wake wa alikuwa na
kitabu kilichofunguliwa..Kitabu hichi ni kitabu cha Ukombozi, ambacho ndio kile
tulichokiona katika mlango wa 5 wa kitabu hichi cha Ufunuo..kitabu hichi ndio
kimebeba siri zote za URITHI WA MWANADAMU, yaani mwongozo wote wa namna ya
kuishi katika hii dunia milele kama Mungu alivyomkusudia mwanadamu aishi, na
kilikuwa ndani na nje na kimefungwa na mihuri saba…Na kama tulivyosoma katika
Ufunuo Mlango wa 5 hakuonekana mtu yoyote mbinguni au duniani aliyestahili
kukifungua wala kukitazama kitabu hicho isipokuwa Mwana-Kondoo pekee tu peke
yake, Na hivyo mwanakondoo ndiye akakipokea na akazivunja mihuri zake..Na hapa
anaonekana akikishika kikiwa kimefunguliwa.
Ndugu, Siri zote za ukombozi
zimuhusuzo mwanadamu, kuanzia kuumbwa kwake mpaka sasa, na urithi wote wa namna
ya kuitawala hii dunia na siri zote, mpaka milele anazo sasa Bwana wetu Yesu
Kristo, yeye ndiye aliyeketi sasa katika Kiti cha Enzi, alipokuwa hapa duniani
alikuwa hajapokea bado mamlaka,hivyo hata siku ya kurudi kwake ilikuwa
haijafunuliwa ndio maana akasema…siku hiyo hakuna aijuaye isipokuwa Baba
tu!..Lakini sasa ameshakipokea hicho kitabu cha Ukombozi, hivyo siri zote
zikiwemo tarehe na muda, na saa ya kuuhukumu ulimwengu anazijua, hakuna
kilichojificha tena kwake. Mwanzo wa kuumbwa kwa ulimwengu, na vizazi vyote na
kila kitu kimewekwa Dhahiri mbele zake.
Na hapa anaonekana amekishika hicho
kitabu kikiwa kimefunguliwa, hakina tena mihuri kwasababu mihuri yote
imeshavunjwa, na akashuka na kuweka mguu wake wa kuume juu ya bahari na wa
kushoto juu ya nchi.
Kwanini ameweka hivyo miguu yake
mmoja habarini mwingine nchi kavu…Tutakuja kuona hapo mbeleni kidogo sababu ya
yeye kufanya hivyo.
Tukiendelea na mstari unaofuata
Yohana anaendelea kuona na kusikia mambo mapya..
Ufunuo 10: 3 “Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao.4 Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike."
Sasa tunaona pindi huyu Malaika
aliposhuka tuu, alilia kwa sauti kuu…kama vile simba angurumaye…Naam Kristo ni
Simba wa Yuda akinguruma, mbingu na nchi ni lazima zitetemeke…Yohana alimwona
katika maono mengine mwanzoni kabisa wa kitabu hichi, akasema sauti yake ikiwa
kama sauti ya maji mengi, lakini hapa anatoa sauti kama ya Simba. Na cha ajabu
Zaidi, alipotoa hiyo sauti, ikaambatana na ngurumo..Ni kawaida mahali pakitokea
sauti kubwa ni lazima hiyo sauti itikise vitu Fulani mahali Fulani ambavyo hivyo
vitu kwa mtikisiko huo vitatoa sauti fulani…Hata ukiangalia spika kubwa
zinazotumika kwenye mikutano..utaona zinapotoa yale mawimbi yake makubwa ya
sauti, kuna kitu mfano wa kitambaa kigumu kimewekwa kwa mbele..na utaona na
chenyewe sauti inapotoka kinakuwa kinatikisika na kama sio imara kinaweza hata
kuchanika..kwaajili ya nguvu ya Sauti..Na pia utaweza kusikia mwangwi wake mahali
Fulani kwa mbali…hata mara nne au tano…lakini ni sauti hiyo hiyo moja, imezaa
nyingine nyingi…..Na ndivyo hapa, Sauti moja ya Kama mngurumo wa Simba
imetengeneza ngurumo nyingine saba mahali Fulani.
Na Yohana aliposikia hizo sauti za
Ngurumo saba…alikuwa tayari kuandika…kwasababu aliambiwa aandike kila
alichokiona na kukisikia…Lakini alipokuwa katika kuandika sasa sauti ya hizi
ngurumo saba, akasikia sauti ikimwambia “USIANDIKE! Hayo maneno uliyoyasikia
yaliyonenwa na hizo ngurumo saba.”
Sasa hizi ngurumo saba ni sauti
saba, ambazo zote zimeakisi kutoka kwenye ili sauti moja kuu ya KRISTO YESU..Ni
kama mwangwi…Kwahiyo ni wazi kuwa zitakuwa zinazungumzia kitu kimoja…zitakuwa
hazipingani…isipokuwa zitakuwa zinatofautiana kidogo sana katika kutoa ujumbe
kwasababu hata mwangwi ulioakisiwa kwenye jiwe ni tofauti na uliokisiwa kwenye
mwamba…ingawa maneno ni yale yale, isipokuwa yameakisiwa katika sehemu mbili
tofauti..Na ngurumo saba zitakuwa ni sauti saba, zenye ujumbe unaokaribiana
sana, usiopingana na mwingine…ambazo zitakuja kufunuliwa kipindi kifupi sana
kabla ya unyakuo kufika. Katika hizo Bibi arusi atapata Imani ya kwenda kwenye
unyakuo…Zitakuwa ni Siri Fulani baadhi ambazo zipo katika kile kitabu Bwana
Yesu alichokishika katika mkono wake kilichofunguliwa…Na Siri hizo Bwana
atazifunua kwenye Kanisa lake kupitia huduma 7/watu 7 ambao atawanyanyua kwa
kipindi kimoja. Kumbuka mambo hayo hayajaandikwa kwenye biblia, yatakuwa ni
mambo mapya kabisa, Kutakuwa na vitu vya kipekee kwa Bibi-arusi, na hiyo ndiyo
itamletea Imani ya kwenda kwenye unyakuo…Kwa maelezo marefu kuhusu “ngurumo
saba” bofya hapa⏩ ngurumo saba
Tukiendelea mbele Zaidi tunasoma..
Ufunuo 10:5 “Na yule malaika niliyemwona, akisimama juu ya bahari na juu ya nchi, akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni,6 akaapa kwa yeye aliye hai hata milele na milele, yeye aliyeziumba mbingu na vitu vilivyomo, na nchi na vitu vilivyomo, na bahari na vitu vilivyomo, ya kwamba hapatakuwa na wakati baada ya haya;7 isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii”.
Sasa tukirudi pale, kwanini Mguu
mmoja Bwana aliuweka juu ya nchi na mwingine juu ya Bahari…Ni kwasababu ya
KIAPO kinachokwenda kufuata..
Katika hali za kawaida za desturi za
kiulimwengu, watu wakienda mahakamani, wakitaka kutoa ushahidi au kuzungumza
ukweli, sharti wasimame wima, hauwezi kuapa huku umekaa… na baada ya hapo,
unanyoosha mkono wako mmoja wa kuume juu! Na kisha anaapa kusema ukweli…Kama ni
kiongozi anaapishwa anakamata kile kitabu anachoapia na kukinyanyua juu na
kuapa kupitia hicho.
Na hapa Bwana anakwenda kuapa! Na
kuna vitu vitatu ambavyo wanadamu waliambiwa wasiape kabisa cha kwanza.1)
MBINGU: kwasababu ndipo kiti cha Enzi cha Mungu kilipo 2) NCHI: kwasababu ndipo
pa kuwekea miguu pa Mungu 3) KICHWA: kwasababu hatuwezi kuufanya unywele wetu
kuwa mweupe au mweusi.
Mathayo 5:33 “Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiape uongo, ila mtimizie Bwana nyapo zako;34 lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu;35 wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu.36 Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi”
Lakini huyu Malaika Mkuu unaona
anakiuka vyote hivyo…Kwanini? ni KWASABABU Kilichopo Mbinguni ndio kiti chake
cha Enzi, hakuna aliye zaidi yake…Na pia anaapa kwa nchi kwasababu ndipo ilipo
Miguu yake…Ndio maana unaona mguu mmoja upo juu ya Bahari na mwingine juu ya
nchi. Na vilevile kuonyesha kuwa anamiliki vyote vilivyo chini ya nchi kuzimu(ambapo
ni baharini) na juu ya nchi (ambapo ni duniani). Kwahiyo ni uthibitisho tosha
kuwa huyo si mwingine Zaidi Ya MKUU WA UZIMA MWENYEWE YESU KRISTO, MUNGU
MKUU.Haleluya!!...Na hapa anaapa kwa kusema kuwa…
“hapatakuwa na wakati baada ya haya; 7 isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii”
Hapatakuwa na wakati baada ya
haya…anamaanisha kuwa, Dunia haitaendelea kuwepo tena baada ya hayo..isipokuwa
katika siku za malaika wa saba atakapokuwa tayari kupita baragumu. Sasa kumbuka
mpaka kufikia hapa Malaika wa saba alikuwa bado hajapiga baragumu
lake..baragumu sita zimeshapita…Tutakuja kuona baragumu ya saba itapolia ni nini
kitatokea…lakini kwa ufupi Baragumu la saba linahusiana na siku ya BWANA
yenyewe. Ambapo hakuna tena muda.Mambo yote yatakuwa yamekwisha hakuna tena
nyakati wala vipindi vya wanadamu…Utakuwa ni wakati wa kuanza majira mapya…
Kwahiyo huyu Malaika Mkuu anaapa
ikimaanisha ni “hakika na ndivyo itakavyokuwa” kuwa hakutakuwa tena na muda wa
nyongeza…Isipokuwa katika siku za malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga
baragumu…Katika siku za Malaika wa saba kupiga baragumu hizo ndio siku za
mwisho..hakutakuwa na baragumu la nane wala muhuri wa 8.
Lakini ukiendelea mbele kidogo
inasema “7 isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari
kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri
watumishi wake hao manabii.”
Mwisho Malaika wa saba atakapopiga
baragumu ndipo SIRI YA MUNGU itakapotimizwa. Ikiwa na maana kuwa hii siri ya
Mungu bado haijatizizwa mpaka sasa…Maana yake bado yote haijafunuliwa…kuna
sehemu haijatimizwa, na hiyo itatimizwa katika siku za Baragumu la malaika wa saba..
Sasa hapa biblia inasema ni SIRI itatimizwa…yaani ipo MOJA sio siri zitatimizwa
kana kwamba zipo nyingi hapana.
Sasa hiyo SIRI ni IPI? Kwa ufupi
SIRI HII ni YESU KRISTO..Yeye ndiye SIRI YA MUNGU
Wakolosai 1:26 “siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake;27 ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu”.
Sehemu ya kwanza ya siri hii
ilifunuliwa ilifunuliwa kwetu sisi mataifa kwamba KRISTO YESU, yule Masihi
aliyekuja hakuwa zawadi kwa wayahudi tu peke yao..bali hata kwetu sisi watu wa
mataifa, kwasababu hiyo tukapata baraka kubwa sisi tuliokuwa hatustahili, hiyo
ilikuwa ni SIRI iliyofichwa ndani ya YESU KRISTO, tunapokea uponyaji kwa
Kupitia YESU Kristo, wafu wanafufuliwa, tunazungumza lugha mpya, tunawekea watu
mikono wanapata afya nk. Tunahesabiwa kuwa uzao wa Ibrahimu. Mambo hayo ambayo
zamani za agano la kale, yasingeingia akilini kwamba siku moja Masihi wanayemtarajia
eti atawapa Uwezo wa kipekee namna hiyo watu wa mataifa, wasio hata wa uzao wa
Ibrahimu kwahiyo hiyo ilikuwa ni siri na ilipokuja kufunuliwa iliwashangaza
wengi sana.
Mtume Paulo aliiandika siri hiyo katika
Waefeso 3:4 “Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo.5 Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho;6 ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili;7 Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa.
Pia sehemu nyingine ya siri hiyo
ambayo imefunuliwa kwetu ni kuwa YESU NDIO YEHOVA mwenyewe. Alipokuwepo duniani
siri hiyo ilikuwa bado imefichwa miongoni wa wanadamu wote, wanamjua tu kama
mwana wa Mungu mteule wa Mungu, lakini siku alipopaa na Roho Mtakatifu
afumbuaye mafumbo aliposhuka juu ya mitume ndipo siri hiyo ikafichuka kumbe
tulikuwa tunatembea na Mungu duniani pasipo sisi kujua. Mtume Paulo aliliweka
wazi hilo na kusema..
1Timotheo 3:16 “Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu.”
Unaona?…Kadhalika ipo sehemu nyingine ya
Siri hii hii ya huyu mmoja ambayo bado haijatimia, mwishoni kabisa mwa wakati
wa baragumu la saba ndio itakuwa imemalizika yote..Somo linalohusu SIRI YA
MUNGU ni pana kidogo..unaweza ukalipata kwa kubofya hapa ⏩ Siri ya Mungu.
Tukizidi kuendelea mbele tunasoma…
Ufunuo 10:8 “Na sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi.9 Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali.10 Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu.11 Wakaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi”.
Baada ya Malaika huyu Mkuu kuapa kwa
sauti kuu, Yohana anaisikia tena ile sauti iliyomwambia asiandike zile ngurumo
saba, ikimwambia akakitwae kile kitabu mkononi mwa yule malaika na akile, nacho
kitakuwa kitabu kama asali kinywani bali tumboni kitakuwa kichungu.
Hapa Yohana anaambiwa akitwae akile,
kwa namna ya kawaida huwezi kula kitabu, kwahiyo hilo ni ono, na kitabu hicho
hakuambiwa akisome, hapana bali akile…kusoma ni tofauti na kula, mtu asomaye
anaingiza taarifa katika Akili yake…lakini mtu alaye anaingiza taarifa au uzima
ndani ya mwili wake…Kwasababu kile alichokila kinaingia katika tumbo lake kisha
kinameng’enywa na kuingia katika damu na mfumo wa mwili mzima…baadaye kile
alichokila kinageuka sehemu ya yeye kinageuka na kuwa nyama yake, misuli yake,
Ngozi yake n.k…
Na sisi Neno la Mungu hatujapewa kulisoma
tu au kulikariri hapana! bali tumepewa
tulile katika roho, ndio Maana Bwana anasema yeye ni “chakula cha uzima” ili
kitakapoingia katika miili yetu ya roho kiwe ni sehemu yetu!..
Sasa hapa Yohana anaambiwa atwae akile, mfano ule ule wa Nabii Ezekieli alioambiwa atwae GOMBO lile na kulila…
Ezekieli 2:8 Bali wewe, mwanadamu, sikia neno hili ninalokuambia; usiwe wewe mwenye kuasi kama nyumba ile yenye kuasi; funua kinywa chako, ule nikupacho. 9 Nami nilipotazama, mkono ulinyoshwa kunielekea; na tazama, gombo la chuo lilikuwa ndani yake.
10 Akalikunjua mbele yangu; nalo lilikuwa limeandikwa ndani na nje; ndani yake yalikuwa yameandikwa maombolezo, na vilio, na ole!Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli.
Ezekieli 3: 1 “Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli.2 Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo.3 Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali.4 Akaniambia, Mwanadamu, haya! Waendee wana wa Israeli ukawaambie maneno yangu.”
Nabii Ezekieli alipewa alile lile
gombo kabla ya kwenda kusema na Wana wa Israeli, gombo tafsiri yake ni KITABU.
Kwahiyo Bwana alimpa Neema ya ufunuo wa kipekee juu ya maneno yake ili
atakapokwenda kusema na wana wa Israeli na kuwaonya! Azungumze kitu
anachokielewa na kinachotoka ndani yake..Na baada ya hapo tunamwona Ezekieli
akipata nguvu ya ajabu katika kwenda kuwapa unabii wana wa Israeli
waliohamishwa, utaona alikuwa ananguvu nyingi kiasi cha kuweza hata kustahimili
ishara Mungu alizokuwa anampa, wakati mwingine alikuwa anaambia alale ubavu
mmoja kwa siku 430 na ubavu wa pili kwa siku 40, sehemu nyingina anaambiwa ale
kinyesi ili kuwa ishara kwa wana wa Israeli,sehemu nyingine Mungu anamuua mke
wake aliyempenda, halafu anaambiwa asiomboleze bali avae nguo nzuri, awe kama
mtu ambaye hana msiba wowote n.k .mambo hayo yote aliweza kuyafanya baada ya
kulishwa hilo gombo..vinginevyo kwa hali ya kawaida asingeweza.
Kadhalika na Yohana hapa anapewa
kile kitabu akile. Sasa Katika siku za Mwisho kutakuja uamsho wa mwisho, ambapo
Roho Atamwagwa tena kama siku ile ya Pentekoste na kama ilivyotokea kule Mtaa
wa Azusa, Marekani…Bibiarusi atapokea nguvu ya kwenda kutoa unabii kwa mataifa,
lugha na jamaa wa dunia nzima..nguvu ya Roho Mtakatifu itamwezesha bibiarusi
kufanyika ishara kwa dunia nzima kipindi kifupi kabla ya unyakuo, lakini
ijapokuwa wengi wataona ishara za namna hizo lakini hawataamini. Kwahiyo Yohana
katika hilo ono anamwakilisha bibiarusi wa Kristo atakavyokuja kupokea ufunuo
katika siku za mwisho…Ingawa pia baada ya Yohana kutoka Patmo, alizunguka
sehemu nyingi kutoa unabii kutimiza sehemu hii ya maandiko..lakini ufunuo
halisi utakuja kutimia katika siku za mwisho ..
Je! Umempa Bwana Maisha yako?..Unaona
ni kwa jinsi gani tunaishi katika muda wa kumalizia, Kristo yupo mlangoni, na
hata kama huamini atakuja, basi fahamu kuwa hujui siku yako ya kufa, inaweza
ikawa ni leo..Sasa huko utakapokwenda utakuwa mgeni wa nani ?..hukukaa kikao na
yeyote cha kuamua wewe kuja duniani kadhalika hutakaa kikao na yeyote cha kuamua ni lini utaondoka! Hukuja na kitu
utaondoka bila kitu! Hivyo jitafakari Maisha yako yatakapoishia..Na kama umempa
Bwana Maisha yako kumbuka maandiko yanasema “pasipo utakatifu hakuna mtu
atakayemwona Mungu (Waebrania 12:14)” je! Maisha yako yanastahili wokovu?.
Kama hujajiweka sana, na kujiandaa
huu ndio muda wa kufanya hivyo haraka bila kuchelewa, tubu dhambi zako zote kwa
kumaanisha kutokuzifanya tena, na kisha katafute ubatizo sahihi wa maji mengi
na kwa Jina la Yesu Kristo kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako kulingana na
Matendo 2:38, na kisha Bwana atakuzawadia nguvu ya kushinda dhambi (Roho wake
Mtakatifu). Na yeye ndiye atakayekutia MUHURI mpaka siku ya ukombozi wako
Katika huyo utakuwa na uhakika wa kwenda mbinguni.
Usikose mwendelezo huu w asura
zinazofuata.
Shalom! Maran atha!
No comments:
Post a Comment