"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, August 26, 2019

MANENO YA MUNGU YANAPINDULIWAJE?


Siku moja nilikuwa ninamsikiliza Mh.Raisi akizungumza na wafanyabiashara Ikulu, nikapata kitu ambacho kiuhalisi ndio kinachoendelea katika Ukristo isipokuwa tu ni katika upande mwingine wa shilingi. Kwa kawaida mimi sio mfuatiliaji wa mambo ya siasa, lakini siku hiyo nilijikuta ninasikiliza mahojiano kati ya Raisi na wafanyabiashara ikulu ni hotuba wakipeleka changamoto zao na malalamiko yao wanayokumbana nayo katika taasisi cha kiserikali hususani TRA….Wengi wao walipewa nafasi ya kutoa kilicho moyoni mwao..Na baadaye Raisi akasema hawa watu wa taasisi za umma, wanatumia kauli mbiu yake ya kuchapa kazi, ili kuwakandamiza wafanyabiashara na wananchi kwa kuwapa makadirio makubwa kushinda uwezo wao wa kulipa..Na wakishamaliza kuwakandamiza wanatumia kauli ya HAPA KAZI TU!, yaani kwa lugha nyepesi tunaweza kusema wanaongezea makali kile Raisi anachokiamini kwa kutimiza matakwa yao binafsi, ambayo hayalengi kujenga bali kubomoa ..Hilo ni jambo ambalo lilimuhuzunisha sana Mh Raisi.
 
Sasa ukiangalia, ni kweli kauli mbiu ya Raisi ni kuwa kila mtu achape kazi, lakini hakuwa na lengo la kumaanisha kuzidi mipaka hadi kuwakandamiza watu wenye nia njema ya kulijenga Taifa..Bali kanuni hiyo ilikuwa inalengo la kuwahamasisha wananchi wafanya kazi kwa bidii..

Leo hii ukirudi katika ukristo utakutana pia na hili neno maarufu, “Hatuishi chini ya Sheria, bali tupo chini ya neema”(Warumi 6:14)..Na hivyo Mungu haangalii matendo yetu bali Roho zetu…Ukiangalia ni kweli kabisa biblia inatuambia hivyo, lakini tunashindwa kufahamu Neno hilo lilikuwa linawahusu watu wa namna gani..

Neno hilo lilikuwa linawahusu watu waliokuwa ndani ya Kristo na wala sio walio nje ya Kristo, ikiwa na maana kuwa katika bidii yako ya kuishi maisha ya kumpendeza Mungu ndani ya Kristo, Usihesabu kuwa hicho ndicho kinachokupa uhalali kwa kukubaliwa na Mungu au kwenda mbinguni..,Hapana, mbinguni ni mahali patakatifu sana, hakuna kinyonge kitakawezakuingia na kama hivyo hakuna mtakatifu yoyote ambaye angestahili kwenda mbinguni isipokuwa YESU KRISTO tu peke yake kwasababu yeye ndiye hakuwahi kutenda dhambi yoyote tangu kuzaliwa kwake hadi kufa kwake..

Hivyo ili na sisi tuhesabiwe kama watakatifu basi neema lazima ichukue nafasi yake, lakini huku tukiwa bado ndani ya Kristo, na tukijitahidi kuishi maisha makamilifu na matakatifu kwa kadiri tuwezavyo..Lakini leo hii utakuta, mtu anatembea uchi barabarani, anavaa vimini na suruali kama soksi, na bado anajiita mkristo, ukimuuliza kwanini unafanya hivi . Anakwambia Biblia inatuambia hatuishi chini ya sheria bali chini ya neema, Mungu haangalii vya nje bali vya ndani.

Hata mtu aliye nje ya wokovu utamsikia akizungumza maneno hayo hayo, hatupo chini ya sheria bali chini ya neema. Nataka nikuambie, biblia inasema katika siku za mwisho maneno haya ..“lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika. (2Timotheo 3:13)..

Usikubali kudanganyika, Maovu yanavyozidi kuongezeka shetani ndivyo anavyotumia silaha ile ile ya maandiko kudanganya watu wengi. Kama vile tu alivyojaribu kutumia silaha hiyo kumdanganya Bwana Yesu kule jangwani…Ukiendelea na mtazamo huo kuwa tunaokolewa kwa neema na sio kwa matendo na huku unafanya mambo maovu kwa makusudi, unawasababishia wengine watende dhambi ya kutamani kwa ajili yako, kuwa na uhakika tu siku ile utahukumiwa na Mungu kwa kushindwa kulipambanua Neno la Mungu ipasavyo.
Warumi 6:15 “Ni nini basi? Tufanye dhambi kwa sababu hatuwi chini ya sheria bali chini ya neema? Hasha!
16 Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki.”
Na Neno lingine lililo maarufu leo hii, utalisikia kila mahali ni hili ‘Usihukumu usije ukahukumiwa’..Na kwamba ikitokea mtu anahubiri kuwa walevi wote na waasherati wataenda motoni, kama biblia inavyosema anaambiwa kuwa anahukumu…Lakini mtu huyo huyo yupo tayari kumweleza kwa uwazi wote mtoto wake ikiwa anapotea mwisho wake utakavyokuwa, utasikia anamwambia usiposoma mwanangu, utaishia kuwa teja, au kuwa kibaka, au kuwa maskini…hilo kwake haoni kama ni hukumu, lakini yeye akihubiriwa kwamba endepo akiendelea kuwa mlevi ataishia jehanamu ya moto utasikia anakumbia unahukumu, mwenye uwezo wa kuhukumu ni Mungu tu!…Hiyo yote ni kutokana na kushindwa kulichambua vizuri neno la Mungu. Utakapokwenda mahali popote ukaanza kuwafundisha tu watu wadhara ya dhambi na mwisho wake ni upi, utasikia wakisema unawahukumu..

Na mambo mengine mengi tu, ya namna hiyo. Hivyo tunapaswa tukae mbali na misemo hiyo, ambayo inatumia kivuli cha maandiko kusitiri maovu na mabaya. Kwasababu siku ile Mungu hatakuwa radhi na sisi.

Kama bado haujafahamu thamani ya kuwa ndani ya Kristo, ni vema ufanya hivyo sasa kabla ya mlango wa neema haujafungwa..Unachopaswa kufanya ni kutubu kwa kumaanisha kabisa kuacha kufanya dhambi, kisha tafuta mahali wanapobatiza ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi, na kwa Jina la BWANA YESU KRISTO, upate ondoleo la dhambi zako kama bado hujafanya hivyo..kisha Uukulie wokovu mpaka siku ya kunyakuliwa..

Ubarikiwe sana. Tafadhali “Share” Ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki.
 

No comments:

Post a Comment