"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Sunday, October 9, 2016

JINSI SHETANI ALIVYOINGIA KATIKA UJUMBE WA MALAKI 4:5-6

Watu wengi, sana sana waamini wa ujumbe wa ndugu William Branham wameshindwa kuulewa ujumbe huu wa thamani Mungu aliotupa una maana gani. Kwa uelewa wao wa kawaida umewafanya hata wale wasio waamini wa ujumbe huu kuona kama ni kikundi fulani cha occult au kikundi kinachomwabudu mtu. Shetani amenyanyua watu wasiokuwa na Roho Mtakatifu ili kuuchafua ujumbe na uonekane kama haufai. Lakini hila za yule mwovu hazitadumu.Lakini Bwana anaurejesha upya.

Roho hii ya shetani imeingia kwa wanaojiita waumini wengi na kumtukuza Nabii zaidi ya BWANA WETU YESU KRISTO aliyetufia msalabani. Nabii alikuwa mtu wa Mungu mnyenyekevu, aliyewarudisha watu kwa Kristo wala hakumwambia mtu yeyote, amwabudu au amkuze kushinda YESU KRISTO.Lakini baadhi ya watu shetani aliowanyanyua wameiingia katika ujumbe huu wa saa na kumwabudu Mtu, zaidi ya BWANA WETU YESU KRISTO.kiasi cha kwamba hata watu wasioamini wanashindwa kuvutiwa na ujumbe. Kumbuka wakatoliki wana picha ya Bikira Mariam wakidhani wanamuheshimu Mariam, Hawakujua kuwa Mariam alimtumikia Yesu, kwa kuwa hawakuitambua huduma ya Mariam. leo hii wanamwabudu Mariam ambazo ni ibada za sanamu. Vivyo hivyo baadhi ya waamini wa ujumbe huu, wanafahamu zaidi juu ya nabii na familia yake na picha zake kuliko wanavyomjua BWANA YESU KRISTO wakidhani ndio wanamheshimu nabii wamesahau kuwa wameiga hayo kutoka kwa mama yao Katoliki. kuwa na picha sio vibaya lakini tunaposahau ujumbe aliouleta nabii zinageuka kuwa ibada za sanamu. Mkristo yeyote anapaswa kulielewa hilo.

William Branham alikuja kuturejesha sisi kwa KRISTO YESU,( ndio kiini cha ujumbe wake) lakini watu wamemwacha Bwana aliye mwokozi wetu na kumhubiri nabii,

Biblia imeachwa kusomwa na kuhubiriwa, badala yake ni vitabu tu vya ujumbe vinavyohubiriwa makanisani. kitu ambacho nabii hakukiagiza wala kukifundisha, ndugu William Branham alisema " Hata mimi mwenyewe nikifundisha jambo lolote kinyume na biblia, usilichukue hilo"

Na shetani pia ameingia katika ujumbe hata kufikia hatua ya watu kumuabudu Nabii kama Mungu, wengine wanabatiza kwa jina la William Marrion Branham na sio kwa jina la BWANA YESU KRISTO tena.Hii ni roho ya mpinga kristo ikitenda kazi ndani ya ujumbe.Kumbuka sio mambo yote ndugu William Branham aliyoyasema ni 'HIVI ASEMA BWANA"..Lakini kuna baadhi ya watu wanahubiri kwamba kila neno ndugu Branham alilosema ni HIVI ASEMA BWANA. na kuwafundisha watu washikilie tu masomo ya kwenye vitabu, wakisema hayo tu yanatosha siri za Mungu zote zimeshafichuliwa ndani yake. Pia Utakatifu, karama za rohoni na ubatizo wa ROHO MTAKATIFU hazihubiriwi tena. Na wengine wao hawaamini tena katika kusambaza injili.

Biblia ndio kitabu pekee cha ukombozi wa mwanadamu, chenye pumzi ya Bwana na BWANA YESU KRISTO ndiye mtunzi wa hicho kitabu. hatujaokolewa kwa damu ya mwanadamu yeyote, wala mtume yeyote, wala nabii yeyote wala malaika yeyote. Hawa wote ni watumishi wanaoturudisha kwa Bwana, na sio sisi tuwageuze wao waichukue nafasi ya BWANA YESU KRISTO. hizo ni ibada za sanamu, na za wafu ambazo zinafanywa pia na kanisa Katoliki. Kuwaabudu watakatifu na Jeshi la mbinguni. wakidhani wanawatii manabii wa Mungu. Kumbe wanamwabudu shetani mwenyewe bila wao kujijua.

Hivyo ndugu ikiwa wewe ni mwamini wa ujumbe huu wa malaki 4. Ni vizuri kutambua kuwa ujumbe huu unamaana gani, na unakuelekeza wewe wapi? ukishakwisha kuuelewa utaona sababu ya wewe kumpenda BWANA YESU KRISTO na kumwabudu YEYE PEKE YAKE , na kuifanya biblia kuwa ni mwongozo wako,sio vitabu vya ujumbe, vile viwe kukurudisha wewe katika neno lakini sio viwe litrujia yako. na pia kuona sababu ya wewe kutokupingana na KWELI, Kama hautaweza kufanya hivyo basi ujue kabisa haujauelewa wala haupo kwenye ujumbe. Haijalishi una picha ngapi za nabii, au umesoma vitabu vingapi vya nabii, au unamuheshimu nabii kiasi gani au unahudhuria kanisani mara ngapi.

Naamini Mungu atakubadilisha na kukupa uelewa zaidi juu ya ujumbe wa ndugu. William Branham unamaana gani.


Mungu akubariki.

No comments:

Post a Comment