"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, October 7, 2016

UNYAKUO

Imekuwa ikijulikana na wengi kuwa unyakuo utakuwa ni tendo la ghafla. kufumba na kufumbua mamilioni ya watu watatoweka, watu watakuwa wakikimbia mabarabarani, ulimwengu mzima utataharuki, ndege zitaanguka, ajali nyingi zitatokea duniani, amani itapotea ghafla na watu watakuwa wakilia na kuomboleza, wakimwona mpinga-kristo akipanda kutoka kuzimu kuleta uharibifu duniani kote. Lakini Je! ni kweli unyakuo utakuwa kwa namna hiyo kulingana na maandiko?. Tukisoma;

1wathesalonike 4:16-17 "Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na MWALIKO, na SAUTI YA MALAIKA MKUU, na PARAPANDA YA MUNGU; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele".

Tukiyachunguza haya maandiko hapa juu tunaona kuwa kuna hatua tofauti tatu zitakazoambata na kuja kwa Bwana Yesu kulichukua kanisa lake: Hatua ya kwanza: Bwana atashuka kutoka mbinguni na 'MWALIKO'.na hatua Ya pili: Bwana atashuka na 'SAUTI YA MALAIKA MKUU'..na hatua Ya tatu: Bwana atashuka na 'PARAPANDA YA MUNGU'. Hii inaashiria kwamba kuja kwa Bwana kutakuwa ni kwa hatua za kufuatwa.na sio ghafla tu kama inavyodhaniwa. Tunapaswa tuzitambue tambue ili tusiwe gizani kwa jinsi siku zinavyokaribia, Hebu tuzitazame hizi hatua tatu kwa undani zaidi.

HATUA YA KWANZA:

Biblia inasema 1wathesalonike 4:16 "Bwana atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko" sasa hili neno “mwaliko” kama linavyozungumziwa hapo halimaanishi ule mwaliko wa kama mtu anaalikwa kwenye sherehe fulani hapana! Bali inamaanisha Kilele za nguvu zinazoambatana na nderemo na vifijo kuashiria kuwa mtu fulani wa kipekee anakaribia kuwasili mfano,Raisi, Bwana arusi n.k,... Hii ni kwa kusudi la kumfanya mtu anayemngojea kujiweka tayari kumlaki atakapofika langoni mwake, ili isiwe ghafla ghafla.

Hivyo Tukisoma kwenye tafsiri nyingine za biblia, mfano ile biblia ya kiingereza KJV inatuambia..
''For the Lord himself shall descend from heaven with a SHOUT, with the voice of the archangel, and with the trump of God: and the dead in Christ shall rise first:"

Sasa Hapo neon 'Shout' linamaanisha ni kupaza sauti kuu za kelele kwa nguvu, ili kumfanya mlengwa aamke au awe makini kujianda na tukio linalokwenda kutokea mbele.

Ili tuelewe vizuri juu ya maneno haya na jinsi mwaliko ulivyo, tupitie baadhi ya vipengele vya maandiko, kama tunavyosoma mfano wa wale wanawali kumi. Katika Mathayo 25, tunasoma…

Mathayo 25:1-13" 1 Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi. 2 Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara.
3 Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao;
4 bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao.
5 Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi.
6 Lakini usiku wa manane, PAKAWA NA KELELE, Haya, bwana arusi; TOKENI MWENDE MKUMLAKI.
7 Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao.
8 Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika.
9 Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.
10 Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa.
11 Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie.
12 Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi.
13 Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa. "

Hivyo turudi katika kizazi hichi tuishicho, sote tunajua kuwa kuja kwa Bwana wetu YESU KRISTO kumefananishwa na wale wanawali kumi waliokuwa wakingoja kumlaki Bwana wao atakapokuja waende naye arusini, Na tunaona ilipofika usiku wa manane wote waliishiwa nguvu, na kusinzia kwa kuona Bwana wao anakawia kwa kungojea sana, Lakini ghafla usiku ule ule pakawa na ''KELELE kubwa ikisema Tazama! Bwana arusi anakuja''.

Kwahiyo kitendo kile cha zile kelele kuwaamsha hawa wanawali 10 kutoka usingizini huo ndio ule 'Mwaliko' unaozungumziwa pale kwenye ( 1wathesalonike 4:16-17). ambapo biblia inasema, Bwana atashuka pamoja na mwaliko… ni kwa dhumuni la kumwamsha bibi arusi ili ajiweke tayari kwa kwenda kumlaki Bwana wake. Na kama huo mwaliko usingepita kwanza hakuna mwanawali yoyote angeweza kutambua kuja kwa Bwana wake, wote ingewajia kama mwivi, Hivyo jambo hili kutangulia ni mahususi ili kumfanya aamke usingizini na kuaacha mambo yake anayoyafanya yote aanze kuiweka taa yake sawa, kwasababu muda waliokuwa wanauongojea umewasili.

Lakini Hatua hii ilianzia wapi katika kanisa?

Kanisa lilipokuwa limelala katika vipindi vyote vya nyuma baada ya roho ya mpinga Kristo kuliharibu, na kulipindua kama tunavyosoma katika historia ya ukristo jinsi kanisa lilivyopitia katika kipindi kirefu cha giza, na jinsi lilivyoingia katika mafundisho ya upotofu pale ukristo ulipooana na upagani na kuendelea hivyo kwa muda mrefu sana wa mamia ya miaka..Sasa muda wote huo ulikuwa ni muda kanisa lilikuwa limelala, Lakini ulipofika wakati wa Bwana kushuka kulijilia kanisa lake tena, hakuja ghafla, kwasababu hakuna ambaye angestahili kwenda naye, alianza kwanza na kutanguliza Mwaliko wake, ni ujumbe wa kumwamsha kwanza bibi arusi kutoka usingizini yaani (mwaliko) na kumfanya aiweke tayari taa yake na ahakikishe pia inayo mafuta ya ziada (mafuta ni Roho Mtakatifu na mafuta ya ziada ni ufunuo wa Roho wa Mungu).

kwahiyo huu MWALIKO ni UAMSHO wa Roho ambao unatangaza ujio wa Bwana Yesu kulichukua kanisa lake na watu wajiweke tayari kumpokea Bwana wao. Kama tulivyoona katika

(Mathayo 25:6..na ilipofika usiku wa manane pakawa na ''KELELE Bwana arusi anakuja''). Sasa huu mwaliko ulianza na Martin Luther mjumbe wa kanisa la tano, ukaendelea hivyo hivyo na John Wesley mjumbe wa kanisa la sita, Na mwisho Bwana aliutoa tena kwa kupitia mjumbe wa kanisa la saba William Branham,.. Kumbuka sauti hiyo ya mwaliko ilianza kusikika kutoka mbali, na ilivyokuwa inazidi kukaribia ndivyo ilivyozidi kuwa kubwa zaidi, Hivyo sauti ya mwaliko wa kanisa hili la mwisho la Laodikia ni kali, kuliko ilivyokuwa kwa kanisa la tano au la sita. Kwasababu Bwana yupo mlango kufika amtwae Yule mwanawali mwerevu aliyeitii sauti ya mwaliko. Kumbuka ndugu Ujumbe tulionao sasahivi ni KUTOKA kabisa katika mifumo ya dini na madhehebu na kuishi maisha ya utakatifu, Ni kuishi kama mtu anayemngojea Bwana wake, Huko ndiko kuzitengeneza Taa zetu.

Luka 12: 35 “Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na TAA ZENU ZIWE ZINAWAKA;
36 nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, ATAKAPORUDI KUTOKA ARUSINI, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara.
37 Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia.
38 Na akija zamu ya pili, au akija zamu ya tatu, na kuwakuta hivi, heri watumwa hao”.

Unaona hapo?..MWALIKO wa kuja kwa Bwana ulishaanza tangu wakati wa kanisa la tano, na la sita, na unaendelea na la saba. Ulianza na Martin Luther, kwa ujumbe wa kuwahubiria watu watoke, kutoka katika ile dini ya uongo(Katoliki). Ndipo kuanzia huo wakati bibi-arusi wa kweli wakaanza kuzitengeneza TAA zao, lakini cha kusikitisha ni baadhi yao hawakuwa na mafuta ya kuwatosha ya ziada (Ufunuo wa Roho),kuwawezesha kudumu katika hayo mpaka Bwana wao atakapokuja, hivyo kilichowatokea ni wao kudumu katika dhehebu linaloitwa Lutherani, hawamruhusu tena Roho wa Mungu kufanya kazi ndani yao, wakawa wametosheka na mapokeo yao tu, hawakujua kuwa inawapasa wapige hatua nyingine katika kumjua Mungu,..[Wanadamu tumeumbiwa kukua kila siku, katika mambo yote, kadhalika na mambo ya rohoni ukiona hukui jua tu kuna tatizo mahali Fulani.]

Kadhalika John Wesley mjumbe wa kanisa la sita naye pia aliutangaza ule mwaliko kwa nguvu zaidi kuliko Luther wengi walitengeneza taa zao lakini ulipofika wakajitengenezea dini na kusababisha taa zao nao kuzima, na katika kanisa la mwisho la Laodikia Bwana alimnyanyua mjumbe wake tena Ndugu. William Branham na sauti kubwa na ya mwisho ya mwaliko kuwaambia watu watoke wakamlaki Bwana wao maana ameshafika na muda umekwisha, sasa bibi-arusi wa kweli atatoka katika hili kanisa la mwisho kwa kutii sauti ya mtumishi wake na kwenda katika hatua inayofuata yaani ya “sauti ya Malaika Mkuu”, lakini pia kama makanisa mengine ya nyuma yalivyomzimisha Roho kwa kujiundia madhehebu kadhalika na katika kanisa hii la Mwisho wapo waliojiundia dhehebu, na kujiita wa-Branhamu, kama tu wafuasi wa Luther walivyojiita wa-luther, kadhalika na kundi hili pia halitafika katika hatua inayofuata ya sauti ya malaika mkuu, kundi hili litaishia njiani, kwasababu limemzimisha Roho, kumbuka Bwana hajawahi kuleta dhehebu lolote, Bwana huwa analeta UAMSHO kama ilivyotokea siku ya Pentekoste, madhehebu yote ni mifumo ya wanadamu inayodai kumtafuta Mungu lakini ndani yake imejaa mapokeo ya wanadamu na dogma zinazochukua nafasi ya Roho Mtakatifu, na kumzimisha kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba anaonekana mwanadamu au mapokeo zaidi ya YESU KRISTO Mungu wetu,na ndio maana Bwana kayakataa.

Hizi ni nyakati za mwisho, utafika wakati utatamani sekundi moja ya kuwa mtakatifu utakosa, siku hiyo utakapogundua kuwa umeachwa, leo unahubiriwa tunaishi katika siku za mwisho unadhihaki unasema Bwana Yesu hawezi kurudi kizazi hiki,bado sana, ni kweli hatujui siku wala saa lakini alitupa majira ya kuja kwake na dalili zote zinaonyesha kuwa tunaishi katika kizazi ambacho tukashuhudia kuja kwa pili kwa Yesu Kristo. Kwahiyo kama hautaweza kuitikia hii sauti ya MWALIKO kwa kujiweka tayari kumpokea Bwana sasa kama mwokozi wako, na kwa kupokea Roho Mtakatifu na kuishi maisha yampendezayo Mungu ya utakatifu sawa sawa na NENO na sio sawasawa na dhehebu lako au dini yako, hautawezi kuendelea hatua inayofuata, na wala hautaijua, utafanana na wale wanawali wapumbavu waliokosa mafuta katika taa zao. Tunaishi katika wakati wa matenganisho, Bwana anawatenga wanawali werevu kutoka katika wanawali wapumbavu, anatenga magugu na ngano, magugu atawatuma watu (manabii wa uongo) wayafunge matita matita (madhehebu) na ngano atawatuma watumishi wake wayakusanye(kwa ajili ya unyakuo) ghalani mwake. Je! Wewe upo kundi gani?

HATUA YA PILI:

1 wathesalonike 4:16 "BWANA ATASHUKA NA SAUTI YA MALAIKA MKUU"
Hii ni hatua ya pili na itawahusu tu wale waliokwisha kuisikia sauti ya mwaliko(yaani wanawali werevu), wale ambao wamekwisha weka taa zao tayari wakiwa na mafuta ya ziada ambayo ni Roho Mtakatifu na Roho ya ufunuo (ya kutaka kumjua Mungu zaidi na zaidi pasipo kumzimisha ndani yao) hawa ndio wale wanawali wenye busara. 
 
Tunapaswa tujiulize hii sauti ya Malaika Mkuu ni ipi??
Tukisoma Katika kitabu cha..
 
ufunuo 10:1-7 " Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto. 2 Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, nao wa kushoto juu ya nchi.
3 Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao.
4 Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike.
5 Na yule malaika niliyemwona, akisimama juu ya bahari na juu ya nchi, akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni,
6 akaapa kwa yeye aliye hai hata milele na milele, yeye aliyeziumba mbingu na vitu vilivyomo, na nchi na vitu vilivyomo, na bahari na vitu vilivyomo, ya kwamba hapatakuwa na wakati baada ya haya;
7 isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii."

Huyu Malaika mwenye nguvu anayezungumziwa hapa akishuka kutoka mbinguni ni BWANA YESU KRISTO, kumbuka neno malaika maana yake ni “mjumbe” na Bwana Yesu anajulikana kama “mjumbe wa Agano” Malaki 3: 1 “Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule MJUMBE WA AGANO mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi”.
 
Na hapa kwenye ufunuo anaonekana akiwa ameshika kitabu kidogo, na hichi kitabu si kingine zaidi ya kitabu cha ukombozi wa mwanadamu, ndio kile kilichokuwa kimetiwa mihuri saba, Ufunuo 6 na tunasoma pia aliapa “hakutakuwa na wakati baada ya hapa” kuashiria kuwa muda utakuwa umeisha wakati atakapokuwa anazungumza, tunaona pia alipolia kwa sauti kuu kama simba angurumavyo zile NGURUMO SABA zikatoa sauti zao ambazo Yohana aliambiwa asiziandike, hizo ni siri ambazo hazijarekodiwa mahali popote katika biblia ni siri zitakazokuja kufichuliwa katika hatua hii ya pili, na ni kwa ajili tu ya kumpa bibi arusi imani ya kwenda katika unyakuo.

Kwahiyo hii ya SAUTI YA MALAIKA MKUU ni siri ya zile ngurumo saba, ambazo zitakuja kuhubiriwa kwa bibi-arusi aliyeko ulimwenguni kote,Hizi ngurumo saba zitakapotoa sauti zao ndipo bibi arusi atapata imani kamili ya kwenda kwenye unyakuo, katika uamsho huu yatahubiriwa mambo ambayo hayajaandikwa katika biblia, haimaanishi kwamba yatapingana na biblia hapana bali ni mambo ambayo hayajarekodiwa katika biblia yatakuwa ni ufunuo wa mambo mapya mahususi tu kwa wale wakristo ambao wameitikia wito wa sauti ya mwaliko.Uamsho huo hautakuwa wa watu wote wa dunia nzima, hapana bali utakuwa ni wa kikundi kidogo sana Bwana alichokipa neema kuvuka hatua ya kwanza ya mwaliko.
 
Mungu alikuwa na makusudi kwanini alimwambia Yohana asiziandike zile ngurumo saba kwa wakati ule, ni kwa sababu maalumu zije zifunuliwe kipindi cha siku za mwisho katika hatua hii ya pili,kwa bibi arusi wa Kristo aliyewekwa tayari, ni siri zilizoandikwa katika kile kitabu kidogo kilichokuwa kimeshikwa na yule malaika mkuu(Yesu Kristo). Wakati huo hizo ngurumo zitakapokuwa zinatoa sauti zao, hawa wengine hawatafahamu chochote, kwao wataona kama ni imani mpya imezuka duniani..Lakini walio na Roho Mtakatifu kweli kweli watafahamu kwa uweza wake, kutaambatana na maagizo ya kufuata mahususi kwa bibi-arusi wa Kweli.

kwahiyo hiyo Huyu MALAIKA MKUU tuliyemsoma kwenye 1Thesalonike 4:16 , ndiye huyo tunayemwona katika kitabu cha ufunuo sura ya kumi aliyetoa zile ngurumo saba. Na si mwingine zaidi ya Bwana Yesu Kristo.
 
HATUA YA TATU:
Hatua hii ni ya mwisho na inahusu PARAPANDA YA MUNGU .Tukisoma 1wathesalonike 4:16" Inasema..Bwana atashuka na parapanda ya Mungu. nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele"

Hii ni sauti ya parapanda ya YESU kwa wafu kwa ajili ya ufufuo, hapa ndipo wafu watakapoisikia sauti ya Mungu ikiwaita huko waliko nao watafufuka na kuivaa miili ya utukufu na kuungana pamoja na wale walio hai na kwenda kumlaki Bwana mawinguni, kama vile Lazaro alivyoisikia sauti ya Bwana ilipomwambia njoo huku nje Yohana 11:43 naye akafufuka. ndivyo itakavyokuwa kwa wafu waliokufa katika Kristo siku ile watakapoisikia sauti ya parapanda ya mwisho.

Yohana 5:25 Inasema.. "Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai." 
 
Hii ndio hatua ya mwisho na sisi tulio hai miili yetu itabadilika kufumba na kufumbua na kuungana na waliofufuliwa kwenda mbinguni kwa BWANA WETU YESU KRISTO.
 
Na sio wakristo wote watanyakuliwa bali wale tu walioitikia mwaliko, na sauti ya malaika Mkuu, na hatua hii inafananishwa na “check-in procedures” katika safari za ndege.
 
Na kumbuka sio watu wote watafahamu kama unyakuo umepita watu wasiofahamu wataendelea na shughuli zao kama kawaida, itakuwa ni siri hakutatokea vurugu wala ajali mabarabarani, kama kukitokea vurugu mpinga-kristo atafanyaje kazi sasa hapo? Na nani atashawishika kupokea chapa ya mnyama? Ni dhahiri kuwa hakuna atakayeshawishika kwasababu watu wote watamjua mpinga-kristo amefika, na unyakuo hapo utakuwaje wa siri tena?? lakini siku hiyo wengi hawatamjua mpinga-kristo wala chapa yake kwasababu hatakuja akiwa na mapembe, atakuwa ni mtu anayeheshimika,na kukubalika na dunia, atakuja na kivuli cha amani, na atapendwa na wengi, na atakuwa ni mtu wa kidini, na anashika biblia, lakini ndani yake ni utendaji kazi wa shetani wenyewe, atawadanganya wengi waipokee ile chapa, na ni muhimu pia kufahamu namba 666 sio chapa ya mnyama, hilo ni jina la mnyama na sio chapa yake, chapa yake ni kitu kingine kabisa. Ikiwa namba 666 ndio chapa yake, watu wengi pia siku hiyo wataikataa, lakini siku hiyo mamilioni ya watu wataipokea kwasababu hawataijua, Hivyo ni kuwa makini sana na hizi nyakati.

Ndugu mpendwa ujue mpaka wakati huu tuliopo unyakuo umeshakwisha kuanza,na hatua ya kwanza ya mwaliko ndiyo tuliyopo sasa ni wakati wa kutengeneza taa zetu tuhakikishe tumepokea Roho Mtakatifu na tumeitikia vizuri UJUMBE WA SAA HII ambao ni KURUDI KATIKA UKRISTO WA BIBLIA na kutoka katika mifumo ya madhehebu ambayo yamewapofusha wengi macho na yamewasababishia wafanye uasherati na yule mama wa makahaba( ufunuo 17) ambalo ni kanisa la roman katholiki. Hivyo basi kwa kuitikia hivyo inatufanya sisi kuwa bikira safi waliotayari kumlaki Bwana.

Hatua inayofuata itakuwa ni zile Ngurumo saba na watakaoweza kuzipokea ni wale bikira safi tu na ndiyo hatua tunayoisubiria sasa na iko mbioni kutokea, uamsho mkubwa unakuja mbeleni, siri hizo hazitaweza kueleweka na mtu wa kawaida asiyekuwa na Roho wa Kristo.Kisha baada ya hapo ni parapanda ya mwisho ya kwenda kumlaki Bwana mawinguni wafu watafufuliwa na sisi tutaungana nao kwenda mbinguni ndio siku hiyo mmoja atatwaliwa na mmoja ataachwa, kama Elisha alivyotwaliwa na Eliya kuachwa kama Henoko alivyotwaliwa na Nuhu kuachwa. Ni kwasababu gani? Ni kwasababu Eliya alikuwa na ufunuo wa ziada zaidi ya Elisha, na kadhalika Henoko alimpendeza Mungu na alikuwa ana ufunuo wa ziada zaidi ya Nuhu, hivyo wakashuhudiwa kwamba hawataonja mauti ni bibi-arusi wa siku za mwisho aliyepita hatua ya kwanza, atashuhudiwa kuwa hatakufa hata atakapomwona Bwana akija mawinguni, kuja kwa Bwana kwake hakutakuwa siri, atajua siku atakapoondoka,

1 Wathesalonike 5: 1 “Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.
2 Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.
3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.
4 Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi.
5 Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza.
6 Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.
7 Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku.
8 Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu”.
 
je! bado unafanya mzaha na haya maisha katika hichi kipindi cha hatari tunachoishi sasa cha kuja kwa BWANA YESU KRISTO kwa mara ya pili,? bado unaupenda ulimwengu unaokwenda kuisha, unaendelea kuwa mwasherati, mlevi,mwongo,mwizi, una majivuno,mlafi,kusengenya, kuvaa vimini, mawigi na mahereni, na kupaka wanja, lipstick, na fashion?? Bado unaendelea kuwa mlevi,na mtazamaji pornography, bado unaendelea kuwa msagaji, mlawiti na mfanyaji masturbation? Bado unaendelea kuwa mtukanaji, Kuzimu! Ipo usidanganyike!Tafuta Roho Mtakatifu Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, Muda umeenda sana. Leo hii tubu kisha ukabatizwe katika ubatizo sahihi kwa jina la Yesu Kristo, kisha Bwana mwenyewe atakupa ahadi ya Roho Mtakatifu aliyowaahidia waitakayo.
 
Mungu akubariki sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine ili wapone na Mungu atakubariki.

Kwa mafundisho mengine mengi unaweza

No comments:

Post a Comment