"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, December 28, 2016

MASWALI YALIYOULIZWA NA MAJIBU YAKE: SEHEMU YA 8

SWALI 1; Wale manabii 400 waliomtabiria mfalme Ahabu wakati wa Mikaya walikuwa ni manabii wa Mungu au?
JIBU:ndio wale manabii 400 waliomtabiria Ahabu (1wafalme 22 )walikuwa ni manabii wa Mungu, na hapo kabla walikuwa wanapokea unabii sahihi kutoka kwa Mungu kwasababu manabii zamani walikuwa wanajaribiwa kabla ya kuitwa mbele za wafalme, kwahiyo ni dhahiri walikuwa wanatoa unabii na unatimia, japo mioyo yao haikuwa mikamilifu mbele za Mungu kama ilivyokuwa kwa nabii Mikaya...walikuwa wanapenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu na ndio maana walikuwa wanakaa katika majumba ya kifalme, wakisifiwa na wafalme mfano wa manabii wengine kama hawa tunamwona nabii Balaamu(hesabu 22)..huu ni mfano pia wa manabii wengi tulionao sasa wanapenda pesa,umaarufu,ukubwa, wanawatolea watu unabii ili wapate pesa, watu kama hao ni rahisi kuingiwa na roho zidanganyazo, na kuwafanya leo wasikie kutoka kwa Mungu kesho wasikie kutoka kwa shetani..lakini manabii kama Mikaya ambao ni wachache sana wao  husimama katika Neno, huishi maisha matakatifu na kusema kile Mungu anachotaka tu waseme  pasipo kujali cheo cha mtu, hivyo Mungu anawaepusha na roho zidanganyazo na unabii wao unakuwa thabiti na hakika, lakini kwa hao wengine wanafungua milango kwa roho zidanganyazo kama ilivyowatokea wale manabii 400.

SWALI 2; Isaya 4:1 na siku hiyo wanawake saba watamshika mtu mume mmoja wakisema, tutakula chakula chetu na kuvaa nguo zetu wenyewe lakini tuitwe  tu kwa jina lako; utuondolee aibu yetu. Je; andiko hili linamaanisha nini? Kwanini wanawake? Kwanini wawe saba? Kwanini chakula chao na nguo zao na sio za mume wao? maanake mume akioa moja ya majukumu ya kwake kufanya kwa mkewe ni kumlisha na kumvika sasa hawa wanakula na kuvaa vya kwao ni kitu gani hawa wanawake?

JIBU:ufunuo wa mstari huo ni huu..wanawake saba ni makanisa saba (katika vipindi saba vya kanisa kama inavyooneka katika ufunuo 2 & 3)..mtu mume mmoja ni Yesu Kristo,.Lakini hao wanawake wote 7 wanasema watakula chakula chao wenyewe na kuvaa nguo zao wenyewe bali waitwe tu kwa jina la yule mtu mume mmoja ambaye ni Yesu Kristo.Jambo hili la kusema tutakula chakula chetu na kuvaa nguo zetu wenyewe ni tabia za hayo makanisa yote 7 yalivyokuwa, kila kanisa lilikuwa na tabia yake pekee, na yote yanatafuta kumpendeza Yesu Kristo lakini kwa njia zao wenyewe, kwahiyo hicho "chakula" kinachozungumziwa hapo ni mapenzi yao wenyewe, na mienendo yao wenyewe hawataki chakula cha Bwana wao,(ambalo ni neno la Kristo lisiloghoshiwa), wala hawataki "mavazi" ya Bwana wao(Ambao ni utakatifu na matendo mema soma ufunuo 19:8,) bali waitwe tu kwa Jina la Bwana Yesu aibu yao iwaondoke hii aibu ina maana waiepuke hukumu itakayokuja na ndio maana yale makanisa yote hayakuweza kuoana na Kristo kikamilifu yalikuwa na mapungufu yake, na sisi pia tupo katika kanisa la mwisho la saba la LAODIKIA ni kanisa vuguvugu,na ndilo lililomkinai Bwana wake kuliko mengine yote yaliyotangulia soma..

ufunuo 3:14-22,"14 Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.
19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.
22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa."


lakini tunapaswa wote tushinde ili tuvuke kutoka kuwa masuria na kuwa bibi-arusi safi wa Yesu Kristo waliokubaliwa tayari kwenda kwenye arusi ya mwanakondoo itakayofanyika mbinguni kwa Baba.Kumbuka bibi-arusi sio sawa na suria.Kwahiyo ndugu watakaoshiri karamu ya mwanakondoo ni bibi-arusi tu, je! wewe ni bibiarusi? umepokea Roho Mtakatifu? umejiweka tayari kumpokea Bwana wako atakaporudi? matendo yako yanastahili wokovu? jibu lipo moyoni mwako. Tubu sasa umgeukie Bwana kumbuka tunaishi kizazi ambacho kitashuhudia kuja kwa pili kwa Kristo.

ufunuo 19: 7 Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari.
8 Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing'arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu.

SWALI 3: je ni lini Yesu atajitambulisha kwa ndugu zake, ni wakati wa dhiki kuu au baada ya ile dhiki kuu kuisha?

JIBU: Yesu Kristo atajitambulisha kwa ndugu zake, kwa kupitia injili ya wale manabii wawili(ufunuo 11)...hao manabii watawahubiria kuwa Yesu kristo waliyemsulubisha miaka 2000 iliyopita ndiye masihi wao. watawaamini kutokana na ishara kuu na miujiza watakayoitenda hao mashahidi wawili, kama manabii wao wa kale mfano wa Musa na Eliya. kwahiyo wale wayahudi 144,000 wataamini na kutubu kwa kumuombolezea waliyemchoma mkuki pale kalvari..zakaria 12:10"  Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza. ". Kwahiyo wakati wa hao manabii wawili ambao watahubiri siku 1260 ambayo ndiyo ile miaka mitatu na nusu ya kwanza ya lile juma la 70 la danieli, kipindi hicho ndicho wayahudi watamwamini YESU KRISTO, wakati kanisa la mataifa(bibi arusi wa Kristo) litakuwa limeshakwenda kwenye unyakuo.

SWALI 4: mwanzo 4:15 "Bwana akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. Bwana akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga. " je! hiyo alama ni ipi Bwana aliyomtia Kaini mpaka mtu akimwona asimuue?.

JIBU: Baada ya Hawa kuzini na yule nyoka kwenye bustani ya edeni(kumbuka nyoka hakuwa reptilia/ au kiumbe fulani kinachotambaa kwa tumbo kama huyu nyoka tunayemwona sasa hivi, bali alikuwa anakaribia kufanana na mtu, akitoka nyani, alikuwa anafuata nyoka kisha mwanadamu, alikuwa anatembea kama mtu, anazungumza, anafikiri n.k lakini baada ya kuasi Mungu akamlaani ndipo akawa nyoka kama tunavyomwona leo, anatembea kwa tumbo, kwa ufupi ni mnyama aliyelaaniwa kuliko wanyama wote kama biblia inavyomwelezea.). Hivyo basi kitendo kilichofanyika pale bustani ya Edeni ni uasherati, Hawa alizini na nyoka, kisha Hawa akaenda kuzini tena na mumewe(Adam) ikapelekea Hawa kubeba mimba ya mapacha wasiofanana, kila mmoja akiwa amebeba asili ya baba yake(jambo hili limehakikiwa na wanasayansi kwamba inaweza ikatokea mama mmoja kubeba mimba ya mapacha wenye baba wawili tofauti,) tazama picha hapa chini, ni matukio ya kawaida na yanatokea kila siku duniani;
        
              (mapacha wenye baba wawili tofauti, kila mmoja na baba yake lakini mama mmoja)
Kwahiyo Kaini baba yake alikuwa ni nyoka, na Habili baba yake alikuwa ni Adamu. Hivyo baada ya kuzaliwa Habili kama mzao wa Mungu alimtolea Mungu dhabihu bora kuliko mwenzake, na ndipo Kaini akamwonea wivu akamuua ndugu yake. Mungu akamlaani Kaini kwa kosa la kumuua ndugu yake. Kaini baada ya kuona adhabu aliyopewa na Mungu ni kubwa  kama tunavyosoma mwanzo 4:8-15 "8 Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]Ikawa walipokuwapo uwandani,Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua.
9 Bwana akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?
10 Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.
11 Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;
12 utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani.
13 Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki.
14 Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua.
15 Bwana akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. Bwana akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga. "

    Kwahiyo hii alama Bwana aliyomtia Kaini sio alama kama chapa fulani kwenye mwili(tatoo) wake, Bali tukichunguza maandiko tunaona kuwa Mungu alimwongezea ukubwa wa mwili wake na akili nyingi(inteligency), tunaona katika kipindi cha Nuhu ule uzao wa Kaini ulikuwa ni wa watu wakubwa walioitwa "majitu (wanefili)" kwahiyo kwa ukubwa huu mtu yeyote asingeweza kupigana nao au kuwatishia, na kwenye upande wa akili tunaona katika mwanzo 4 wana wa kaini walianza kuwa na ustaarabu kwa haraka kama ugunduzi wa vyuma, shaba, ustadi wa vyombo vya miziki n.k.waliitwa watu hodari na wenye sifa wakati ule(mwanzo 6:4) inaelezea..wao ndio waliotengeneza mapiramidi ambayo yamesimama mpaka sasa  kwahiyo tunajua hata leo taifa lenye ujuzi mwingi kama teknolojia kubwa ni dhahiri kuwa taifa hilo litaogopeka na hakuna mtu atayakayedhubutu kwenda kulidhuru ndivyo ilivyokuwa kwa Kaini, Mungu alimpa ukubwa na ujuzi mwingi ambao ulikuwa kama ulinzi kwake. Lakini ule uzao mwingine wa Adamu ambao ni uzao wa Mungu wao walikuwa ni wafugaji tu na wakulima, na walikuwa ni wanadamu wenye miili ya kawaida.

No comments:

Post a Comment