"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, July 19, 2017

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 16

SWALI 1: Bwana aliposema kuwa yeye ni "Mungu wa miungu" alikuwa na maana gani?..je! yeye ni Mungu wa sanamu?

JIBU: Tukisoma kumbukumbu 10:17 "Kwa maana Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, asiyependelea nyuso za watu, wala hakubali rushwa. ". Hapa  tunaona Mungu anajitambulisha yeye kama Mungu wa miungu sasa swali hawa miungu ni wakina nani?.
Bwana Yesu alisema

 Yohana 10:33 "Wayahudi wakamjibu, Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe; bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu.
34 Yesu akawajibu, Je! Haikuandikwa katika torati yenu ya kwamba, Mimi nimesema, Ndinyi miungu?
35 Ikiwa aliwaita miungu wale waliojiliwa na neno la Mungu; (na maandiko hayawezi kutanguka); " .
36 je! Yeye ambaye Baba alimtakasa, akamtuma ulimwenguni, ninyi mnamwambia, Unakufuru; kwa sababu nalisema, Mimi ni Mwana wa Mungu? "

 Kwahiyo unaona hapo miungu inayozungumziwa hapo ni WATOTO WA MUNGU. wengi wanadhani kuwa miungu iliyozungumziwa pale ni "SANAMU" LA! sivyo. Mungu hawezi akawa ni Mungu wa sanamu. Na tunajua tabia za miungu ni lazima zifanane na Mungu, Hivyo basi kazi zile zile Mungu anazozifanya lazima na miungu izifanye, kwa mfano Mungu alitumia NENO lake kuumba na kufanya kila kitu na sisi vivyo hivyo kwa NENO lake tunaweza tukafanya kazi za Mungu vile vile kama yeye. Lakini tusipoweza kufanya hivyo inamaana sisi sio miungu kwasababu hatufanani na yeye. Kwahiyo ili sisi tuwe miungu lazima tuwe ni WATOTO WA MUNGU wenye tabia hizi: Upendo, Imani, Haki, Utakatifu,  n.k.


Swali 2:
Naomba kufahamu maana ya huu mstari...Mathayo 5:39 "Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. "


JIBU:  Bwana Yesu aliposema mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili na sawasawa na alivyosema pia “mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia.” Hii ikiwa na maana kuwa kwa kufanya hivyo utakuwa umeushinda uovu na utafanikiwa kuiokoa roho ya mtu kuliko kuingamiza. kwasababu kwa kufanya vile Biblia inasema utakuwa umempalia makaa ya moto kichwani pake, akijiuliza ni kwanini sikutendewa kama mimi nilivyomtendea hivyo baadaye atajiona yeye ndiye mwenye makosa na kugeuka na kutubu. Lakini atakapokupiga na wewe ukamrudishia, au atakapochukua mali yako nawe  ukaenda kuchukua ya kwake atachomwaje dhamira na kujiona yeye ni mwenye dhambi? hivyo atabakia kuwa vilevile tu na kukuona wewe ni mtu wa kawaida tu kama watu wengine. 

Na ndio maana Bwana Yesu alisema tuushinde ubaya kwa wema, ili tuwe wakamilifu kama Baba yetu alivyomkamilifu. Aliendelea kusema...
Mathayo 5:41 “Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili.
42 Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo.
43 Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;
44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,
45 ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.
46 Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?
47 Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?
48 Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu. “


SWALI 3:
Je! Kuna malaika wanaotembea na watu?


JIBU: Ndio wapo malaika wanaotembea na watu lakini sio watu wote ila wale tu wanaotembea katika NENO la Mungu, Tukisoma waebrania 1:13 “Je! Yuko malaika aliyemwambia wakati wo wote, Uketi mkono wangu wa kuume Hata nitakapoweka adui zako chini ya nyayo zako? JE! HAO WOTE SI ROHO WATUMIKAO?, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu? “.
Kwahiyo tunaona hapo malaika wanatembea na wale tu “watakaourithi wokovu”,  ambao ni wale wanaolishika NENO la Mungu ndio hao tu “watakaowahudumia”. Tunaweza tukaona mfano wa watu hawa kwenye biblia kama Petro (matendo12:15) na Mtume Paulo tukisoma
 matendo 27:23 Kwa maana usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama karibu nami,
24 akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe. “ .Hii inathibitisha kuwa Paulo alikuwa na malaika anayetembea naye.
Pia wana wa israeli jangwani Mungu aliwatumia malaika awaongoze katika safari yao ya kwenda kaanani ndio yule aliyekuwa akisimama katika “nguzo ya moto” usiku na  “nguzo ya wingu” mchana...kutoka 23:20 Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea. “...kutoka 23:23 “Kwa kuwa malaika wangu atatangulia mbele yako, na kukufikisha kwenye Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhivi, na Myebusi; nami nitawakatilia mbali. “.

Hivyo basi kazi ya malaika wa Mungu ni kuhakikisha NENO la Mungu unalolishikilia linatimia juu yako kwa mfano NENO la Mungu linaposema “KWA KUPIGWA KWAKE SISI TUMEPONA”. Mtu yeyote anayeliamini hili NENO na kulishikilia Bwana anamtuma malaika wake kuhakikisha kwamba hilo NENO linatimia juu yake na hatimaye anapokea uponyaji wake haijalishi itachukua muda gani ni lazima lije kutimia. Lakini kama hauliamini na kulishika NENO la Mungu ni dhahiri kuwa malaika wa Mungu hatakuwa na kazi juu yako hivyo utabakia tu kuwa kama mtu asiyekuwa na msaada.


Mfano mwingine NENO la Mungu linaposema “ Luka 6:38 ..Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa. “..Sasa kitendo cha wewe kuliamini hili NENO na kuwapa watu vitu,(mfano kuwasaidia maskini, na wahitaji) Malaika wa Bwana anakuja kuhakikisha kuwa hilo NENO linakuja kutimia la wewe kulipwa kwa kipimo kile kile ulichompimia mwenzako ili NENO la Mungu liwe dhahiri na kweli. Lakini kama usipolishika hilo NENO yule malaika hawezi kuja kutembea na wewe kwasababu haoni jambo la kufanyia kazi ndani yako.


Vivyo hivyo na maneno mengine yote ya Mungu, kwa jinsi unavyoyashika na kuyaishi maneno ya Mungu ndivyo unavyofungua milango ya malaika wa Mungu kutembea na wewe lakini usipoliamini NENO la Mungu na kuliishi utabakia kuwa mtu usiyeona uweza wa Mungu juu ya maisha yako. Pasipo IMANI haiwezekani kumpendeza Mungu.
 Mungu akubariki!

No comments:

Post a Comment