"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, March 13, 2018

DANIELI: Mlango wa 10

Jina la Bwana wetu YESU KRISTO libarikiwe.
 
Karibu katika mwendelezo wa kitabu cha Danieli, leo tukitazama ile sura ya 10, Kama tukiangalia kwa undani kitabu hichi tutaona kuwa sehemu kubwa ya Unabii Danieli aliopewa ulikuwa unahusu zile FALME 4 zitakazotawala mpaka mwisho wa dunia, ambazo ni 1) BABELI 2) UMEDI & UAJEMI 3) UYUNANI na 4) RUMI.


Lakini kama ukichunguza ile sura ya pili, utaona Danieli alifunuliwa kwa juu juu picha inayohusu falme hizo, kwa kupitia ndoto ya mfalme Nebukadneza aliyoiota juu ya ile sanamu, tunaona pale hakupewa maelezo yoyote marefu kuhusu hizo falme, alionyeshwa tu utaanza ufalme wa kwanza ambao ni wa dhahabu, kisha fedha, halafu shaba na mwisho chuma, hakupewa hata majina ya falme hizo zitakazokuja kutawala baadaye isipokuwa Babeli tu.

Lakini pamoja na hayo Danieli hakuridhika aliendelea kumsihi Mungu amfunulie undani wa mambo hayo na ndio maana tunaweza kuona katika sura ya 7, akionyeshwa maono yanayohusu jambo lilelile isipokuwa hapa yameingia kwa undani zaidi tofauti na alivyoonyeshwa kule kwanza.

Tunasoma aliona wanyama 4 wakitoka baharini ambao ndio zile zile falme 4 zenyewe. Mnyama wa kwanza ndio yule kama simba(Babeli), wa pili alikuwa kama dubu na mifupa mitatu ya mbavu mdomoni mwake ambayo tulishaona tafsiri yake ni nini, wa nne alikuwa mfano wa chui mwenye vichwa vinne, na tunaona Danieli alipewa tafsiri juu ya vichwa vile akaelezwa kuwa watakuwa ni wafalme 4 watakaonyanyuka katika huo utawala wa tatu ambao ni wa uyunani, pia akaonyeshwa mnyama mwingine wa mwisho wa 4 ambaye alikuwa mbali sana na wale wengine kimaumbile.


Pamoja na hayo Danieli katika maono haya alitajiwa na majina ya falme hizi 2 zitakazofuata, tofauti na maono yale ya kwanza hapa alifunuliwa kuwa ufalme wa pili utakuwa ni UMEDI & UAJEMI, na watatu utakuwa ni ufalme wa UYUNANI. Kwa undani wa maelezo haya unaweza ukasoma mlango wa 7 tuliokwisha kuupitia.

Lakini bado tunaona Danieli baada ya kuona hayo picha bado haikuwa dhahiri kwake hivyo alikuwa na shauku ya kuzidi kufahamu juu ya mambo hayo yataishiaje, na ndio tunaona katika ile sura ya 8 Mungu aliendelea kumfunulia juu matukio yatakayokuwa yanatendeka ndani ya hizo falme, hapa tunaona akionyeshwa yule kondoo mwenye pembe mbili na Beberu, ambapo yule Beberu alikuja kumshambulia yule kondoo na kumuua kwa ile pembe moja aliyokuwa nayo, ambayo baadaye ilikuja ikavunjika na kuzuka pembe nyingine nne.


Sasa Danieli alizidi kuonyeshwa kwa ufafanuzi zaidi mambo yatakayokuja kutokea katikati ya hizi falme, kwamba yule kondoo mwenye pembe mbili ni ufalme wa Umedi & Uajemi, na yule beberu ni ufalme wa uyunani, na ile pembe moja ni mfalme wa kwanza wa uyunani ambaye atanyanyuka na kuuvunja ufalme wa Uajemi, kumbuka mambo hayo yote Danieli hakuonyeshwa katika maono mengine yaliyotangulia, hivyo unaweza ukaona ni mambo yale yale isipokuwa Danieli anafunuliwa kwa undani zaidi, ukiendelea kusoma utaona alionyeshwa pia kutakuwa na pembe nyingine ndogo itakayozuka katikati ya zile pembe 4, itakayojitukuza mbele za Mungu na huyu si mwingine zaidi ya ANTIOKIA EPIFANE 1V. wa uyunani kama historia inavyoonyesha.


Kumbuka Danieli wakati anaonyeshwa juu ya Falme hizi ukisoma katika ile sura ya 7 aliona pembe ndogo(mpinga-kristo) ikizuka katika ufalme wa mwisho wa 4 ambao tunafahamu ni Rumi, lakini hakuonyeshwa pembe nyingine ndogo itakayozuka katika Ufalme wa 3 wa uyunani, lakini hapa tunaona ameonyeshwa pembe hii katika sura hii ya 8. Hivyo tunaona ni mwendelezo wa maono yale yale isipokuwa kwa undani zaidi.


Vivyo hivyo ukiendelea sura ya 10, 11 na ya 12, utaona jinsi Danieli akifunuliwa maono yale yale kwa uchambuzi zaidi, tukio baada ya tukio, mpaka maono yale yakawa dhahiri kwake.
Kwenye Sura hii ya 10 tunaona Danieli akijisogeza mbele za Mungu kwa unyenyekevu akimsihi Mungu ampe ufahamu zaidi juu maono hayo aliyokuwa anafunuliwa na ndio maana utaona baada ya kufunuliwa biblia inasema "alifahamu na kuelewa maono yale", ikiwa na maana hapo mwanzo mambo yale hayakuelewa vizuri kwake.


Tukisoma..
Mlango 10:1-21”

1 Katika mwaka wa tatu wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, Danieli, ambaye jina lake aliitwa Belteshaza, alifunuliwa neno; na neno lile lilikuwa kweli; maana ni VITA VIKUBWA; naye akalifahamu neno lile, akaelewa na maono hayo.
2 Katika siku zile mimi, Danieli, nalikuwa nikiomboleza muda wa majuma matatu kamili.
3 Sikula chakula kitamu, wala nyama wala divai haikuingia kinywani mwangu, wala sikujipaka mafuta kabisa, hata majuma matatu kamili yalipotimia.
4 Na siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilipokuwa kando ya ule mto mkubwa, Hidekeli;
5 naliinua macho yangu, nikatazama, na kumbe, mtu aliyevikwa nguo za kitani, viuno vyake vimefungwa dhahabu safi ya Ufazi;
6 mwili wake pia ulikuwa kama zabarajadi safi, na uso wake mfano wa umeme, na macho yake kama taa za moto, na mikono yake na miguu yake rangi yake kama shaba iliyosuguliwa sana, na sauti ya maneno yake kama sauti ya umati wa watu.
7 Nami, Danielii, nikaona maono haya peke yangu; maana wale watu waliokuwa pamoja nami hawakuyaona maono haya; lakini tetemeko kuu liliwashika, hata wakakimbia ili kujificha.
8 Basi nikaachwa peke yangu, nikaona maono haya makubwa, wala hazikubaki nguvu ndani yangu; maana uzuri wangu uligeuzwa ndani yangu kuwa uharibifu, wala sikusaziwa nguvu.
9 Walakini naliisikia sauti ya maneno yake; nami niliposikia sauti ya maneno yake, ndipo nikashikwa na usingizi mzito, na uso wangu umeielekea nchi.
10 Na tazama, mkono ukanigusa, ukaniweka juu ya magoti yangu, na vitanga vya mikono yangu.
11 Akaniambia, Ee Danieli, mtu upendwaye sana, yafahamu maneno nikuambiayo, ukasimame kiwima-wima; maana kwako nimetumwa sasa. Na aliponiambia neno hili, nalisimama nikitetemeka.
12 Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako.
13 Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi.
14 Sasa nimekuja kukufahamisha mambo yatakayowapata watu wako katika siku za mwisho; maana maono hayo ni ya siku nyingi bado.
15 Na alipokwisha kusema nami maneno hayo, nikauelekeza uso wangu chini, nikawa bubu.
16 Na kumbe, mmoja mfano wa wanadamu akanigusa midomo yangu; ndipo nikafumbua kinywa changu, nikanena, nikamwambia yeye aliyesimama karibu nami, Ee Bwana wangu, kwa sababu ya maono haya huzuni zangu zimenipata tena; hata asikusaziwa nguvu.
17 Maana, mtumishi wa Bwana wangu huyu atawezaje kusema na Bwana wangu huyu? Kwa maana kwangu mimi, mara hazikusalia nguvu ndani yangu, wala pumzi haikusalia ndani yangu.
18 Kisha mmoja mfano wa mwanadamu akanigusa tena, akanitia nguvu.
19 Akasema, Ee mtu upendwaye sana, usiogope; amani na iwe kwako, uwe na nguvu, naam, uwe na nguvu. Aliposema nami nikapata nguvu, nikasema, Ee Bwana wangu, na aseme Bwana wangu; kwa maana umenitia nguvu.
20 Ndipo akasema, Je! Unajua sababu hata nikakujia? Na sasa nitarudi ili nipigane na mkuu wa Uajemi; nami nitakapotoka huku, tazama, mkuu wa Uyunani atakuja.
21 Lakini nitakuambia yaliyoandikwa katika maandiko ya kweli; wala hapana anisaidiaye juu ya hao ila huyo Mikaeli, mkuu wenu.

Kumbuka sura hii inaeleza jinsi Gabrieli alivyomtembelea Danieli, akimweleza sababu ya kukawia kwake, kwamaana hata baada ya Danieli kumaliza kufunga na kuomboleza majibu yalikuwa hayajafika bado, Lakini ujumbe kamili Gabrieli aliomletea ulikuwa unahusu maelezo ya ndani kabisa yahusuyo zile falme na sio kitu kingine, ambayo tutakuja kuona katika sura ya 11 na 12.

Lakini katika sura hii tutaona SIRI zilizopelekea Danieli kupokea mafunuo makubwa kama yale, Awali ya yote Danieli alisema NI VITA VIKUBWA, ikiwa na maana kuwa kuna upinzani mkubwa katika kuyapata mambo hayo, Tunaweza kusoma pale Gabrieli alimwambia "Tangu siku ile ya kwanza alipoutia moyo wake ufahamu maombi yake yalisikiwa Lakini mkuu wa ufalme wa uajemi alimpinga siku 21..."

Tunajifunza nini hapo? Mungu huwa hamjibu mtu maombi yake baada ya kufunga na kuomba, hapana bali huwa anamjibu mtu maombi yake pale tu anapotia moyo wake ufahamu, na ndipo maagizo yanatolewa papo hapo na ndio maana Bwana Yesu alisema (Mathayo 6:8) "Baba yetu anajua tunachohitaji kabla hata hatujamwomba" unaona?.. Lakini sasa adui yupo huyo ndiye anayehakikisha majibu hayafiki kwa muhusika, hivyo inahitaji kupigana vita kumshinda.


VITA KATIKA ANGA.

Kama ukisoma hapo juu utaona kuwa mkuu wa ufalme wa uajemi alimpinga Gabrieli, pia ukiendelea kusoma utaona alisema "atakapotoka huko kupigana na mkuu wa uajemi, mkuu mwingine w a Uyunani atakuja". Sasa kumbuka hawa wakuu wa uajemi na uyunani sio wafalme wa dunia, bali ni roho za mashetani zilizokuwa zinaendesha hizo falme 4 za dunia, kumbuka wakati Danieli anafunuliwa maono haya alikuwa katika Ufalme wa Uajemi, Babeli ilikuwa imeshaanguka, Hivyo mkuu wa ufalme wa Babeli (PEPO) alikuwa ameshaondoka, lililopo hapo ni la uajemi, kisha litakuja PEPO la Uyunani na mwisho litakuja la RUMI, ambalo ndio lipo sasahivi likitenda kazi.


Lakini kumbuka kama biblia inavyosema Waefeso 6:12 "Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya FALME na mamlaka, juu ya WAKUU WA GIZA HILI, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. "
Neno hilo likiwa na maana kuwa hatutumia njia za kibinadamu kushinda na hizi FALME za giza, Kushindana kwetu sio kusema ninatuma kombora, au moto, kuzimu, au maombi ya kuteketeza anga na wakuu wa anga, hapana Danieli hakufanya hivyo, njia hiyo ni kwa namna ya damu na nyama na haiwezi kumshinda shetani hata kidogo, bali biblia inaendelea kusema..

Waefeso 6: 13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.
14 Basi simameni, hali mmejifunga KWELI viunoni, na kuvaa dirii ya HAKI kifuani,
15 na kufungiwa miguu UTAYARI tupatao kwa Injili ya amani;
16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya IMANI, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.
17 Tena ipokeeni chapeo ya WOKOVU, na upanga wa ROHO ambao ni NENO LA MUNGU;

Hivyo malaika kabla ya kuwasilisha maombi ya mtu kwanza huwa anakutana na MSHITAKI HAPO JUU (mkuu wa giza na mapepo yake), ambaye anatushitaki sisi mbele za Mungu (Ufunuo 12:10)kwa kuonyesha kwamba hatustahili kukipokea kitu tunachokiomba, na hoja yake ikiwa na nguvu, majibu hayatufikii anayazuia kwa kuwa ana hati miliki yako, (kwamfano, mtu anaomba jambo fulani kwa Mungu halafu bado anamashaka mashaka kama kweli atajibiwa maombi yake au la!. biblia inasema lolote muombalo aminini ya kwamba mmepokea nalo litakuwa lenu. Sasa mwovu, akikuangalia na kuona kuwa hauna Imani ya kupokea jambo hilo mitikisiko fulani inakutokea unakataa tamaa, yeye anatumia hiyo nafasi kukushitaki mbele za Mungu kuwa huyu mtu hana uhakika na anayemwomba hivyo hastahili kupokea hicho kitu, hapo shetani anakuwa ameshinda vita, hivi ndio vita vinavyopiganwa. Na ndio maana biblia inasema Imani ni ngao itakayoweza kuzima mishale yote ya moto ya yule mwovu.

Yakobo 1:5-8" Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.
6 Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku.
7 Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.
8 Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote. "

Mfano mwingine mtu anaomba Neno fulani kwa Mungu, halafu hajakoloewa, tatizo sio kwamba maombi yake hayajasikiwa, hapana bali MKUU WA GIZA yupo hapo juu akipeleka hoja juu ya maisha yako mbele za Mungu, kwamba Neno linasema " Mtu yeyote asiye na Roho wa Kristo huyo sio wake (Warumi 8:9)" Hivyo yule malaika aliyetumwa kukuletea majibu akikutana na hoja zenye nguvu kama hizo atakwama, maana yule mshitaki atamwambia, Mtu huyu ni mali yangu kwasababu hana Roho wa Mungu, hivyo haya majibu hayamuhusu. Sasa mtu wa namna hii kakosa CHEPEO YA WOKOVU na UPANGA WA ROHO. hivyo lazima vita hivi vimshinde tu na akose anachokitafuta.

Mfano mwingine mtu anayeabudu sanamu (sanamu za bikira Maria, na watakatifu, pamoja na kusali rozari), halafu bado unakwenda kumwomba Mungu, mkuu wa giza atapeleka hoja, za kimaandiko "Kutoka 20:4 inasema Mungu atawapatiliza maovu yao hao wote wanaoabudu sanamu kwa wivu wake", Hivyo badala ya kupokea baraka, yanageuka kuwa laana kwa mtu huyo..

Neno la Bwana linasema..
 
Ezekieli 14: 3,& 7-8 "Mwanadamu, watu hawa wametwaa VINYAGO vyao na kuvitia mioyoni mwao, nao wameweka kwazo la uovu wao mbele ya nyuso zao. Je! Ni laiki yangu NIULIZWE na wao katika neno lo lote?
.......7 Kwa maana kila mtu wa nyumba ya Israeli, au wa wageni wakaao katika Israeli, ajitengaye nami, na kuvitwaa vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na KULIWEKA KWAZO LA UOVU MBELE YA USO WAKE, kisha kumwendea nabii, na kuniuliza neno kwa ajili ya nafsi yake; mimi, Bwana, nitamjibu, mimi mwenyewe;
8 nami nitaukaza uso wangu juu ya mtu yule, na kumfanya kuwa ajabu, awe ishara na mithali, nami nitamkatilia mbali, asiwe kati ya watu wangu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. "

Kwahiyo kwa Danieli mpaka majibu kama hayo kumfikia, aliweza kumshinda (mkuu wa uajemi) katika nyanja zote katika ulimwengu wa roho, hivyo shetani alishindwa kwasababu hakuwa na hoja yoyote ya kumshitaki mbele za Mungu yamfanye asipokee majibu yake.

Na faida aliyoipata Danieli baada ya kushinda tunaweza kuiona katika sura zinazofuata, Mungu aliweza kumfunulia agenda na mpango mzima wa mambo yanayokuja mbeleni juu ya ufalme aliokuwepo na unaokuja wa Uyunani pamoja na ule wa mwisho. hatua kwa hatua tofauti na maono aliyokuwa anayaona mwanzo, mambo hayo utayaona katika sura ya 11 na 12.

Kwahiyo kwa ujumla tunaweza kujifunza katika sura hii Danieli ni mtu aliyekuwa anahama kutoka utukutu hata utuktufu, ono moja halikumfanya aridhike na hali aliyopo aliendelea kutafuta kwa kusoma vitabu na kuomba mpaka mambo yote ya mbeleni yakawa wazi kwake, na sisi vivyo hivyo tunahitaji kusoma sana maandiko na kuomba, mpaka mambo yatakayotukabili huko mbeleni yawe wazi kwetu, hatupaswi kuridhika tu katika hali tulizopo angali tukijua hatufahamu yanayokuja mbeleni.


Biblia inasema Bwana Yesu alikuwa akiongezeka KIMO na HEKIMA, kumbuka sio KIMO cha urefu bali Kimo cha kumjua Mungu, na aliongezeka hekima pia ya kuyajua mapenzi ya Mungu, ikiwa na maana kuwa alipozaliwa sio kwamba alikuwa anajua kila kitu kama ndio hivyo alipokuwa na miaka 12 asingekuwa anawasikiliza na kuwauliza maswali marabi, Hii inaonyesha kuwa alikuwa anakua kwa hekima. Sasa kama yeye ambaye ni Bwana wetu alifanya hivyo inatupasaje sisi?. Tunapaswa tukue tufikie cheo cha kimo cha utimilifu wake (Waefeso 4:13).

Kumbuka pia mkuu wa giza tulilopo sio tena wa uyunani au uajemi bali ni RUMI, na ni roho inayowapofusha watu wasione mbele, wala wasitake kufahamu mambo ya mbele kama wale wengine walivyomzuia Danieli asione mambo ya mbeleni, kwahiyo fahamu kuwa vita vilivyopo sasahivi ni vikubwa kuliko vile vya Danieli. Si ajabu watu wamepoteza hamu ya kufahamu mambo ya mbeleni na mbinguni, injili wanazopenda kuzisikia ni za mafanikio tu, na mambo ya ulimwengu huu yanayopita, ni dhahiri kabisa mkuu wa giza hili amewapofusha macho.

Hivyo ndugu kama unaabudu sanamu, kama hujaokolewa, kama unaishi katika dhambi, kama Huliamini Neno la Mungu, una mashaka upo vuguvugu, fahamu upo chini ya mamlaka ya mkuu wa anga hili, na yeye ndiye mshitaki wako mbele za Mungu usiku na mchana ili usione mambo ya mbeleni au usipokee baraka za Mungu na mwisho kabisa usiione mbingu.
 
Bwana akubariki.

No comments:

Post a Comment