Jina la Bwana wetu na mwokozi wetu YESU KRISTO libarikiwe;
Katika sura hii tunaona Danieli kwa shauku ya kutaka kujua hatma ya Taifa lake Israeli na watu wake,hata lini wataendelea kukaa katika nchi ya ugenini,aliazimu kutafuta kwa bidii, kwa njia nyingi ikiwemo kwa kusoma VITABU, na kufunga na kuomba juu ya jambo hilo mpaka akasikiwa. Kama tunavyosoma;
Danieli 9:1-2 " Katika mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya milki ya Wakaldayo;2 katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii, KWA KUVISOMA VITABU, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, MIAKA SABINI.
Tukisoma habari hii tunaona Danieli alikwenda kusoma VITABU, na sio KITABU, ikiwa na maana kuwa alisoma kitabu zaidi ya kimoja, na moja ya hicho kilikuwa ni kitabu cha Yeremia Nabii. Na katika kuchunguza kwake alikutana na maandiko yanayosema hivi.
Yeremia 29:1-10" Maneno haya ndiyo maneno ya waraka, ambao nabii Yeremia aliupeleka toka Yerusalemu, kwa hao waliobaki wa wakuu waliochukuliwa mateka, na kwa makuhani, na kwa manabii, na kwa watu wote, ambao Nebukadreza aliwachukua mateka toka Yerusalemu hata Babeli.2 (hapo walipokwisha kutoka Yerusalemu Yekonia mfalme, na mama yake mfalme, na matowashi, na wakuu wa Yuda na Yerusalemu, na mafundi, na wahunzi;)3 kwa mkono wa Elasa, mwana wa Shafani, na Gemaria, mwana wa Hilkia, (ambao Sedekia, mfalme wa Yuda, aliwatuma hata Babeli, kwa Nebukadreza, mfalme wa Babeli), kusema,4 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, AWAAMBIA HIVI WATU WOTE WALIOCHUKULIWA MATEKA, NILIOWAFANYA WACHUKULIWE TOKA YERUSALEMU MPAKA BABELI;5 Jengeni nyumba, mkakae ndani yake, kapandeni bustani, mkale matunda yake;6 oeni wake, mkazae wana na binti; kawaozeni wake wana wenu, mkawaoze waume binti zenu, wazae wana na binti; mkaongezeke huko wala msipungue.7 Kautakieni amani mji ule, ambao nimewafanya mchukuliwe mateka, mkauombee kwa Bwana; kwa maana katika amani yake mji huo ninyi mtapata amani.8 Maana Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Manabii walio kati yenu, na wabashiri wenu, wasiwadanganye ninyi, wala msisikilize ndoto zenu, mnazootesha.9 Kwa maana kwa jina langu hutabiri maneno ya uongo kwenu; mimi sikuwatuma, asema Bwana.10 Maana Bwana asema hivi, BABELI UTAKAPOTIMIZIWA MIAKA SABINI, NITAWAJILIA NINYI, NA KULITIMIZA NENO LANGU JEMA KWENU, KWA KUWARUDISHA MAHALI HAPA."
Unabii huu Bwana aliwaambia watu wa Yuda kwa kinywa cha Yeremia kutokana na maasi yao na uovu wao kwamba watachukuliwa mateka na watu wa Babeli nao watakaa huko kwa muda wa miaka 70 kisha Bwana atawajilia tena na kuwarudisha katika nchi yao. Kumbuka wakati wayahudi wote wakiwa wamelala licha ya kuwa katika hali yao ya utumwa Danieli aliazimu binafsi kutafuta kufahamu majira na nyakati anazoishi, kwa maana Bwana Yesu alisema katika Mathayo 7, tafuteni nanyi mtaona, kwa maana kila atafutaye huona. Hivyo Danieli kwa kufanya hivyo kutafuta kwa bidii, Mungu alimjalia kuona kuwa imebakia miaka miwili tu, mpaka wao kutoka Babeli yaani walikuwa wameshamaliza miaka 68 kati ya ile 70 ya wao kukaa utumwani. Na ndio maana Biblia imemwita Danieli kama mtu mwenye Hekima, na mtu apendwaye sana.kwasababu ni mtu aliyependa kutafuta kujua majira na saa anayoishi.
Vivyo hivyo na kizazi chetu cha mwisho tulichopo, Mungu ameshaweka majira ya watoto wake kwenda kwenye unyakuo na siku ambayo hii Babeli ya rohoni itakapo hukumiwa, Kumbuka Mungu hana desturi ya kumlazimisha mtu kufahamu agenda yake ya ukombozi bali wale waliotayari na wanaotafuta kujifunza na kutuka kujua ndio watakaofahamu, na Mungu atawaongoza katika Kusoma, na ndio maana kuna umuhimu sana wa KUJIFUNZA na KUYACHUNGUZA MAANDIKO kila Siku, kwasababu SIRI nyingine hazitafahamika isipokuwa kwa kujifunza sana NENO LA MUNGU kwa mfano wa Danieli.
Hauoni hata katika majira tunayoishi, ile roho ya mpinga-kristo inatenda kazi, na inatenda kazi ndani ya kanisa lakini ni wachache tu ndio wanaweza kuliona ni kwasababu Biblia inasema ni wenye hekima tu, ndio watakaojua, na Hekima hii huja kwa kusoma, na kujifunza chini ya uongozo wa Roho Mtakatifu, Kumbuka hata jina la yule mnyama, inahitaji hekima kulijua, kwamba ukihesabu jina lake ndio ilete jumla ya 666. (VICARIVS FILII DEI).
Ufunuo 13:17 tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile, yaani, jina la mnyama yule, au hesabu ya jina lake. 18 Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na akili, na AIHESABU HESABU YA MNYAMA HUYO; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita.
Vivyo hivyo Bwana Yesu alisema katika Luka 12:54 Akawaambia makutano pia, Kila mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara husema, Mvua inakuja; ikawa hivyo.
55 Na kila ivumapo kaskazi, husema, Kutakuwa na joto; na ndivyo ilivyo.
56 Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya?"
Hivyo ni vema kufahamu MAJIRA unayoishi, kwamba dalili zote zinaonyesha unyakuo umekaribia, kwamfano kulingana na biblia, yale makanisa 7 yanayozungumziwa katika ufunuo 2&3, sita kati ya hayo yameshapita na wajumbe wake wameshapita na sasa ndio tupo katika kanisa la saba na la mwisho liitwalo LAODIKIA na mjumbe wake alishapita, hili ndio kanisa la mwisho litakaloshuhudia kuja kwa pili kwa Kristo, lakini cha kusikitisha watu wengi hawalijui hilo kwasababu hawataki kusoma na kujifunza NENO la Mungu kwa undani.
Ishara nyingine inayoonyesha kuwa tunaishi katika kizazi ambacho kinaweza kushuhudia kuja kwa pili kwa Kristo ni kunyanyuka kwa taifa la Israeli, kumbuka kwa muda wa miaka zaidi ya 2000 taifa la Israeli lilikuwa limetawanyika kwenye mataifa mbalimbali duniani, lakini mwaka 1948 Mungu alilirejesha tena na kuwa taifa huru, na sasa hivi limetimiza miaka 70, na Bwana alisema kwa MTINI jifunzeni mfano mtakapoanza kuona unachipua tena, basi mjue wakati wa mavuno umekaribia," Kumbuka Mtini unafananishwa na Taifa la Israeli (Yeremia 24)
Hivyo tukiona Israeli inachipuka tena basi tujue wakati wa Bwana Kurudi umekaribia..Lakini Bwana alizidi kusema ..Amin! Amin! nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia". Kwahiyo kizazi kinachozungumziwa hapo ni kizazi kilichoshuhudia Taifa la Israeli kuchipuka tena, na ndio hichi kizazi tunachoishi mimi na wewe. Hizi ni baadhi tu ya ishara nyeti ambazo zinatuonyesha kuwa hatuna muda mwingi tena hapa duniani. Ukombozi wetu upo karibu.
Tukirejea katika kitabu cha Danieli tunafahamu hakuishia tu kusoma kitabu cha Yeremia bali hata vingine kwamfano kitabu cha Isaya, kilishatabiri mambo kama hayo hayo (Soma Isaya 13 & 14).
Hivyo baada ya kuyajua hayo ndipo Danieli akamgeukia Mungu wake kumwomba dua na kumsihi sana juu ya dhambi zake na za watu wake Israeli.
MAOMBI YA DANIELI:
Tunasoma..
Danieli 9:2-23 "Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu.4 Nikamwomba Bwana, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake;5 tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako;6 wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi.7 Ee Bwana, haki ina wewe, lakini kwetu sisi kuna haya ya uso, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa.8 Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi.9 Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi;10 wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii.11 Naam, Israeli wote wameihalifu sheria yako, kwa kugeuka upande, wasiisikilize sauti yako; basi kwa hiyo laana imemwagwa juu yetu, na uapo ule ulioandikwa katika sheria ya Musa, mtumishi wa Mungu; kwa sababu tumemtenda dhambi.12 Naye ameyathibitisha maneno yake, aliyoyanena juu yetu, na juu ya waamuzi wetu waliotuamua, kwa kumletea mambo maovu makuu; maana chini ya mbingu zote halikutendeka jambo kama hili, lilivyotendeka juu ya Yerusalemu.13 Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Musa, mabaya haya yote yametupata lakini hata hivyo hatukumwomba Bwana, Mungu wetu, atupe fadhili zake, ili tugeuke na kuyaacha maovu yetu, na kuitambua kweli yake.14 Basi Bwana ameyavizia mabaya hayo, akatuletea; maana Bwana, Mungu wetu ni mwenye haki katika kazi zake zote azitendazo; na sisi hatukuitii sauti yake.15 Na sasa, Ee Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako hawa katika nchi ya Misri kwa mkono hodari, ukajipatia sifa, kama ilivyo leo; tumefanya dhambi, tumetenda maovu.16 Ee Bwana sawasawa na haki yako yote, nakusihi, hasira yako na ghadhabu yako zigeuzwe na kuuacha mji wako Yerusalemu, mlima wako mtakatifu; maana kwa sababu ya dhambi zetu, na maovu ya baba zetu, Yerusalemu na watu wako wamepata kulaumiwa na watu wote wanaotuzunguka.17 Basi sasa, Ee Mungu wetu, yasikilize maombi ya mtumishi wako, na dua zake, ukaangazishe uso wako juu ya patakatifu pako palipo ukiwa, kwa ajili ya Bwana.18 Ee Mungu wangu, tega sikio lako, ukasikie; fumbua macho yako ukautazame ukiwa wetu, na mji ule ulioitwa kwa jina lako; maana hatukutolei maombi yetu kwa sababu ya haki yetu, lakini kwa sababu ya rehema zako nyingi.19 Ee Bwana, usikie; Ee Bwana, usamehe; Ee Bwana, usikilize, ukatende, usikawie; kwa ajili yako wewe, Ee Mungu wangu; kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa jina lako.20 Basi hapo nilipokuwa nikisema, na kuomba, na kuiungama dhambi yangu, na dhambi ya watu wangu Israeli, na kuomba dua yangu mbele za Bwana, Mungu wangu, kwa ajili ya mlima mtakatifu wa Mungu wangu;21 naam, nilipokuwa nikinena katika kuomba, mtu yule, Gabrieli, niliyemwona katika njozi hapo kwanza, akirushwa upesi, alinigusa panapo wakati wa dhabihu ya jioni.22 Akaniagiza, akaongea nami, akasema, Ee Danielii, nimetokea sasa, ili nikupe akili upate kufahamu.23 Mwanzo wa maombi yako ilitolewa amri, nami nimekuja kukupasha habari; maana wewe unapendwa sana; basi itafakari habari hii, na kuyafahamu maono haya. "
Jambo la kujifunza hapo tunaweza kuuona unyenyekevu wa Danieli mbele za Mungu, ijapokuwa alikuwa ni mtu mkamilifu aliyependwa na Mungu lakini alijihesabia kuwa ni mwenye makosa pamoja na watu wake, alitubu kwa kufunga na kuugua, Vivyo hivyo na Bwana wetu YESU KRISTO, ingawa alikuwa ni mkamilifu hakutenda dhambi hata moja, lakini alitubu kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili yetu kwa kufunga na kuomba kwa dua nyingi pamoja na machozi.
Waebrania 5:7-10" Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu;
8 na, ingawa ni MWANA, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata;
9 naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii;
10 kisha ametajwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki. "
Lakini wengi wetu inapotokea Bwana ametupa kibali fulani mbele zake, ndio wakati wa kujiinua na kujiona bora kuliko wengine wote, pengine kwasababu Mungu amekupa karama fulani aidha ya uchungaji, au unabii, au uponyaji, au lugha, au maono, au miujiza ukaanza kujiona bora mbele za Mungu kuliko wengine, lakini kwa Danieli haikuwa hivyo, licha ya kwamba alikuwa na vipawa vyote hivyo, lakini alijinyenyekeza.
Vivyo hivyo tunamwona na Bwana wetu YESU KRISTO pamoja na kwamba alikuwa ni Mungu mwenyewe katika mwili lakini alijishusha kiasi cha kufikia kuosha miguu ya wavuvi(mitume). Kama wao walifanya hivyo inatupasaje sisi tunaojiita watu wa Mungu, .??
Tukiendelea kusoma tunaona Malaika Gabrieli alimjia Danieli kumtia moyo na kumpa vitu vingine vya ziada kuliko hata vile alivyokuwa anavitazamia, licha tu ya kuonyeshwa mambo yahusuyo kutoka Babeli alioonyeshwa pia mambo yatakayokuja kutokea mpaka mwisho wa Dunia kwa watu wake.
MAJUMA 70:
Tukisoma..
Danieli 9:23-27" Mwanzo wa maombi yako ilitolewa amri, nami nimekuja kukupasha habari; maana wewe unapendwa sana; basi itafakari habari hii, na kuyafahamu maono haya.24 Muda wa majuma sabini umeamriwa juu ya watu wako, na juu ya mji wako mtakatifu, ili KUKOMESHA MAKOSA, na KUISHILIZA DHAMBI, na KUFANYA UPATANISHO KWA AJILI YA UOVU, na KULETA HAKI YA MILELE, na KUTIA MUHURI MAONO NA UNABII, na KUMTIA MAFUTA YEYE ALIYE MTAKATIFU.25 Basi ujue na kufahamu, ya kuwa tangu kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hata zamani zake masihi aliye mkuu; kutakuwa na majuma saba; na katika majuma sitini na mawili utajengwa tena pamoja na njia kuu zake na handaki, naam, katika nyakati za taabu.26 Na baada ya yale majuma sitini na mawili, masihi atakatiliwa mbali, naye atakuwa hana kitu; na watu wa mkuu atakayekuja watauangamiza mji, na patakatifu; na mwisho wake utakuwa pamoja na gharika, na hata mwisho ule vita vitakuwapo; ukiwa umekwisha kukusudiwa.27 Naye atafanya agano thabiti na watu wengi kwa muda wa juma moja; na kwa nusu ya juma hiyo ataikomesha sadaka na dhabihu; na mahali pake litasimama chukizo la uharibifu; na hivyo, hata ukomo, na ghadhabu iliyokusudiwa imemwagwa juu yake mwenye kuharibu. "
Kama tunavyosoma hapo kutakuwa na majuma 70 yaliyoamuriwa juu ya watu wake Danieli (Yaani wayahudi pekee). Kibiblia juma moja, linasimama kama miaka 7, hivyo majuma 70, ni sawasawa na miaka (7x70 = 490), Hivyo kutakuwa na miaka 490 kwa wayahudi mpaka mwisho wa mambo yote utakapofika(yaani mwisho wa dunia).
Tukisoma pia tunaona "tangu kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hata zamani zake masihi aliye mkuu". kutakuwa na majuma 7 na 62 ambayo ni sawasawa na majuma 69, Kumbuka miaka hii ilianza kuhesabiwa pale tu amri ya kuujenga upya Yerusalemu ilipotolewa, na jambo hili lilitimizwa na Mfalme Koreshi wa Uajemi, aliyetabiriwa na Bwana tangu zamani za nabii Isaya kwamba ataujenga upya Yerusalemu.
Tukisoma Isaya 44:26-28 " nilithibitishaye neno la mtumishi wangu, na kuyafikiliza mashauri ya wajumbe wangu; niuambiaye Yerusalemu, UTAKALIWA NA WATU, nayo miji ya YUDA, ITAJENGWA, nami nitapainua mahali pake palipobomoka;
27 niviambiaye vilindi, Kauka, nami nitaikausha mito yako;
28 nimwambiaye KORESHI, MCHUNGAJI WANGU, naye atayatenda mapenzi yangu; hata ataunena Yerusalemu, Utajengwa; na hilo hekalu, Msingi wako utawekwa. "
Pia ukisoma Isaya 45:1, 45:13, utaona jambo hilo, Kuwa Mungu alishamtabiri Koreshi amjengee nyumba kule Yerusalemu. Na amri ya kujenga tena Yerusalemu ilikuja kutoka mwaka 454 KK.
Hivyo ndani ya haya majuma 69 ya kwanza, yaani miaka 483 Jerusalemu ulijengwa tena na njia kuu zake na handaki zake katika nyakati za taabu kama biblia inavyosema.
Tukiendelea mstari wa 26 unasema "Na baada ya yale majuma sitini na mawili, masihi atakatiliwa mbali, naye atakuwa hana kitu". Kwahiyo tunaona hapo mara baada ya yale majuma 69 kuisha(yaani 62+7) MASIHI atakatiliwa mbali. Jambo hili lilitimia mwaka 30WK, wakati Bwana YESU aliposulibiwa, hivyo kukamilisha miaka 483 tangu agizo kutolewa na Mfalme Koreshi kuujenga upya Yerusalemu.
Na kama tunavyoendelea kusoma "watu wa mkuu atakayekuja wataungamiza mji". Huyu mkuu anayezungumziwa hapa ni Mpinga-kristo ambaye atakuja siku za mwisho, naye atatokea RUMI, kwasababu biblia inasema watu wake ndio watakaouteketeza mji, na hii ilitimia mwaka 70WK pale jeshi la Rumi lilipouzunguka mji wa Yerusalemu na kuuteketeza kwa moto ili kutimiza ule unabii wa Bwana Yesu aliousema juu ya mji wa Yerusalemu (ukisoma katika Luka 19:41-44).
Kwahiyo mpaka hapo litakuwa limesalia Juma moja yaani miaka 7 kutimiza yale majuma 70. Lakini ukitazama utaona wayahudi baada ya kumkataa MASIHI wao muda wao ulisimamishwa (Luka 13:34-35) na Mungu akaacha kushughulika nao, hivyo neema ikahamia kwa mataifa, na ndiyo iliyopo mpaka sasa hivi, takribani miaka zaidi ya 2000, lakini haitadumu huku siku zote, wakati utafika nao umeshakaribia na neema itarudi tena Isreali kwa muda mfupi kumalizia juma lao moja la mwisho yaani miaka 7, na kumbuka wakati wa mataifa utaisha pale tu kanisa litakaponyakuliwa.
(Warumi 11:25" Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, MPAKA UTIMILIFU WA MATAIFA UWASILI.
26 Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake.
27 Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao. )
Tukiendelea mstari wa 27 tunasoma.." Naye atafanya agano thabiti na watu wengi kwa muda wa juma moja; na kwa nusu ya juma hiyo ataikomesha sadaka na dhabihu; na mahali pake litasimama chukizo la uharibifu; na hivyo, hata ukomo, na ghadhabu iliyokusudiwa imemwagwa juu yake mwenye kuharibu."
Sasa kumbuka huyu anayezungumziwa hapa ni mpinga-kristo (ambaye ndie yule mkuu wa watu atakayekuja), atafanya agano thabiti na watu wengi kwa juma moja, na katika nusu ya juma, yaani miaka mitatu na nusu ya kwanza atalivunja,
Hii itatokea baada ya unyakuo kupita pale mpinga-kristo (PAPA) atakapoingia agano la amani na wayahudi kwa muda wa juma moja wakati huo Hekalu la tatu YERUSALEMU litakuwa limeshajengwa na sadaka za kuteketezwa za daima zitakuwa zinaendelea, lakini katikati ya Juma hilo moja atalivunja hilo Agano, na kuzuia sadaka zote na dhabihu zisitolewe katika nyumba ya Mungu. Zaidi ya yote atataka yeye aabudiwe kama Mungu (2Wathesalonike 2:2), hilo ndilo chukizo la uharibifu. Na katika hiyo miaka mitatu na nusu ya mwisho atawaua watu wote watakaokataa kumsujudia yule mnyama au kupokea chapa yake katika kipindi kinachojulikana kama kipindi cha DHIKI KUU.
Kumbuka dhiki hii ilikusudiwa kwa wayahudi tu lakini na kwa watakaobaki (watu wa mataifa ) wasiokwenda kwenye unyakuo nao pia wataipitia. Lakini mwisho wake(mpinga-kristo) utafika ghafla, na makao yake yataharibiwa na kuangamizwa kabisa.
Kisha baada ya hapo utakuja utawala mpya wa miaka 1000 usio na uharibifu wa BWANA wetu YESU KRISTO, naye atatawala na watakatifu wake MILELE na MILELE.
Tukiyajua haya kuwa wakati tulionao ni mfupi tunapaswa kila siku tuufanye imara WITO WETU, NA UTEULE WETU(2Petro 1:10). Kwa maana ..1Wakoritho 6:9-10" Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi. "
Mungu akubariki.
No comments:
Post a Comment