"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, May 22, 2018

JE! WEWE NI MWANA WA IBRAHIMU?.


Utaketi pamoja na Ibrahimu katika ufalme wa Mungu katika siku ile?. Ni vigezo gani vitakufanya ukidhi viwango vya kufanana na Ibrahimu. Jibu lipo dhahiri ni IMANI. Unapaswa uwe na imani kama ya Ibrahimu, Ikiwa na maana kuwa uyachunguze maisha yake, Jinsi alivyoenenda mbele za Mungu kwa IMANI na uyaige. Sio kuiga alichokifanya, bali ni kuiga mwenendo wake.

Ibrahimu alimchukulia Mungu, au ALIMUHESABIA Mungu kuwa anauwezo wa kufanya mambo yote. Aliweza kuamini vitu visivyowezekanika, na ndio maana aliweza kutembea na Mungu kwa muda wote ule pasipo kujikwa kwaa, aliamini Mungu angeweza kumpa mtoto hata kama akiwa na miaka 100 au 1000, kwasababu aliufahamu ukuu wake, hivyo hakudhubutu kumwekea Mungu mipaka, kwamba hapa anaweza, na hapa hawezi. Na alipopewa mtoto Bwana akamuhitaji kwa ajili ya dhabihu,.Lakini Ibrahimu hakusua sua kuuliza mara mbili, kwasababu alijua Mungu anaweza hata kumfufua tena mtoto wake na kumrudisha kutoka katika wafu.
Waebrania 11: 17 " Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee;
18 naam, yeye aliyeambiwa, Katika Isaka uzao wako utaitwa,
19 AKIHESABU YA KUWA MUNGU AWEZA KUMFUFUA HATA KUTOKA KUZIMU; akampata tena toka huko kwa mfano. "
Ibrahimu alizingatia vitu kama hivyo AKIMUHESABIA Mungu anaweza mambo yote, na ndio maana hadi leo hii anaitwa Baba wa Imani. Na wote wenye Imani zinazofanana na hiyo yake wataitwa WANA WA IBRAHIMU, na watarithi ahadi zile zile Ibrahimu alizoahidiwa na Mungu.

Hivyo Mungu anapendezwa na watu wenye kumwamini kwa asilimia zote, Kuna mahali Bwana Yesu alipokuwa anafuatwa na makutano makubwa ya watu, alikutana na akida mmoja, aliyemshangaza sana..tusome.

Mathayo 8:5-13

"5 Hata alipoingia Kapernaumu, akida mmoja alimjia,
6 akamsihi, akisema, Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza, anaumwa sana.
7 Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye.
8 Yule akida akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; LAKINI SEMA NENO TU!, na mtumishi wangu atapona.
9 Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya.
10 Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, SIJAONA IMANI KUBWA NAMNA HII, KWA YE YOTE KATIKA ISREALI.
11 Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao WATAKETI PAMOJA NA IBRAHIMU, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni;
12 bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
13 Naye Yesu akamwambia yule akida, Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini. Mtumishi wake akapona saa ile ile".
Kumbuka akida huyu hakuwa myahudi (mwisraeli), au mtu aliyeijua torati ya Musa, hapana bali alikuwa ni mtu wa mataifa, tena Mrumi, jamii ya watu wa Pontio Pilato isipokuwa yeye alikuwa na hofu ya Mungu tofauti na wale wengine. Wakati huo aliposikia kidogo tu ya Kwamba Bwana YESU anaponya wagonjwa na kufufua wafu na kutenda miujiza... moja kwa moja akafahamu ule ni uweza mkubwa wa Mungu. Hivyo akamwamini kwa KUMUHESABIA, kuwa ataweza kufanya pia na mambo ambayo yanaonekana hayawezekani machoni pa watu.

Tofauti na desturi za watu wengine, ambao walitaka mpaka waende kuwekewa mikono na Bwana Yesu, ndio waamini kwamba wataponywa, wengine mpaka watembelewe manyumbani kwao ndipo waamini, wengine mpaka waone kwanza ishara ndipo waamini. Lakini huyu moja kwa moja alisema "sema Neno tu na mtumishi wangu atapona"..Na jibu la Bwana lilikuwa ni " Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli. "...Imani hii iliwavuka wayahudi wote wa Israeli, iliwapita makuhani wote ambao kwa wakati huo walikuwa wanavukiza uvumba katika nyumba ya Mungu..Iliwapita mitume wa Yesu ambao kila siku walikuwa wanatembea naye..Iliwapita mafarisayo na waandishi na wazee wote wa Israeli wenye hekima na ujuzi wa torati, iliwapita hata yale makutano makubwa yaliyokuwa yanamfuata Yesu pale.

Na haikuishia hapo tu, Bwana alisema pia. " 11 Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni;
12 bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno "

Umeona hapo, watatoka wengine wengi kutoka pembe 4 za dunia, ikiwa na maana kuwa watatoka watu sehemu zisizojulikana zilizodharauliwa, sehemu ya watu wasiokuwa na maana, pengine wasiojulikana na kanisa, watu wasio na umaarufu n.k. hao wote watakuja kuketi na Ibrahimu yaani watashiriki pamoja baraka Mungu alizomuahidia Ibrahimu. kwasababu wameonekana kuwa na Imani kama ya Ibrahimu mfano wa yule akida.

Ukichunguza kwa karibu utaona kuwa Bwana alikuwa katika utaratibu wa kuwaponya watu wote waliokuwa wanamfuata lakini hakuwa anazungumza chochote baada ya kuwaponya, kwasababu hakuona kitu kingine cha ziada ndani yao. Lakini kwa akida aliona kitu cha ziada, vivyo hivyo na kwa yule mwanamke aliyekuwa anatokwa na damu kwa muda wa miaka 12 (Luka 8:43), aliona makutano wote wanataka njia zile zile za kuponywa tu, kuwekewa mikono, kutembelewa nyumbani, kuombewa, wengine walishatuma maombi ya kumwona Bwana pengine mwezi mmoja kabla, wengine walikuwa wameshamaliza ngazi za chini, wameshatoka kuwaona mitume, sasa wanakaribia ngazi ya juu ya kumfikia YESU, n.k. Lakini yeye alisema kwanini nipitie shida zote hizo,pengine angetaka kusubiria mpaka zamu yake ifike ingemchukua mwaka mzima, isitoshe kulikuwa na watu wenye matatizo makubwa hata kuliko yeye, lakini yeye alisema "nikishika pindo la vazi lake tu nitapona saa hiyo hiyo", ALIMUHESABIA kuwa kama mikono yake inaponya kwanini na vazi lake lisiponye pia?. Kadhalika na yule mwanamke wa Tiro (Mathayo 15:21), Kadhalika na Zakayo naye. n.k.

Lakini leo hii wengi, tunataka tumfikie BWANA kwa njia zile zile za makutano, kumbuka hata leo jambo lile lile linajirudia Bwana Yesu kazungukwa na makutano mengi,(Mabilioni ya watu duniani) kila mtu anataka kumwona Bwana, kila mtu anataka kuponywa, kila mtu anataka kupewa hitaji la moyo wake. n.k. Fahamu tu, mpo wengi wenye shida za kukutana na BWANA. Na wote amewaahidia kuwaponya kwa majira yake, lakini je! ni wangapi kati ya hao wanaugusa moyo wa BWANA, kwa mfano wa yule AKIDA, au yule mwanamke aliyekuwa anatokwa damu? Kiasi cha kufikia kuahidiwa kuketi pamoja na Ibrahimu katika ufalme wa mbinguni?.

Unapopata shida, au unapokuwa na mahitaji fulani kwanini jambo la kwanza unakimbilia kwa watumishi au wachungaji wakuombee?, Wewe kwani Mungu wako hayupo?, kwanini unakimbilia mataifa mengine au Israeli kutafuta suluhisho la matatizo yako, angali Bwana wako yupo karibu na wewe hapo ulipo? Fanya tu kitu cha ziada ndugu, MUHESABIE BWANA, kama anauwezo wa kumtumia mtumishi fulani kuniponya, vivyo hivyo anaweza akanitumia mimi mwenyewe kwa kinywa changu kunitimizia mahitaji yangu. Mungu hana ngazi, kwamba ukitaka umfikie yeye sharti uanze kwanza kwa shemasi kisha mchungaji halafu Mungu. hapana. Akitoka Mungu ni wewe. Sio Padri, wala kasisi wala Nabii anapaswa kuwa kiunganishi chako wewe na Mungu. Yesu pekee ndiye anayesimama hapo katikati.

Pengine watu walimdhihaki yule akida, anachezea nafasi ya kipekee ya kutembelewa na Bwana nyumbani kwake, lakini badala yake Mungu ndiye aliyependezwa na yeye kuliko watu wote. Vivyo hivyo wengine wanatamani mpaka watokewe na YESU au Malaika,au watembelewe na mchungaji ndipo waamini, na kuanza kumtumikia Mungu, wakidhani kuwa hayo ndio mapenzi ya Mungu. Lakini wapo ambao hawatayaona hayo wala hawatayahitaji hayo yote, na watakumpendeza Bwana na kuketi pamoja na Ibrahimu siku ile. Na wana wa Ufalme (ambao wangepaswa wenyewe ndio wawe vielelezo) watatupwa nje.

Hivyo ndugu yangu, tujitahidi sote, tupige mbio tufikie vile viwango vya IMANI ya kumpendeza Mungu kwa kufanya kitu cha ziada kwake, njia ambazo hazijazoeleka na wengi na hii haiji isipokuwa kwa KUMUHESABIA Mungu kuwa anaweza yote, anaweza kufanya mambo yasiyowezekanika.

Mungu akubariki.

Tafadhali share kwa wengine ujumbe huu na Mungu wetu atakubariki.

No comments:

Post a Comment