"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, May 8, 2018

UMUHIMU WA KUISHI MAISHA YAMPENDEZAYO MUNGU SASA.

Jina kuu la Bwana wetu YESU KRISTO libarikiwe daima.

Ni rahisi kudhania kuwa pindi unapoonza kufanya kazi ya utumishi wa Mungu hapo ndipo Mungu anaanza kupendezwa na wewe. Mfano pale mtu anapoanza kuhubiri, au kuwaleta watu kwa Kristo, au kufanya maombezi au huduma ya namna yoyote ile n.k. kwamba kuanzia huo wakati na kuendelea ndio wakati Mungu anapendezwa na mtu huyo?!. Lakini je! hilo ni kweli kwa wakati wote?.

Tujifunze kwa kiongozi wetu Bwana Yesu kwa maana yeye mwenyewe alituambia.."..TUJIFUNZE KWAKE (Mathayo 11:29)". Je! ni wakati upi Bwana Yesu alishuhudiwa kwamba kampendeza Mungu?. Tunasoma katika Marko 1:11 "na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; NIMEPENDEZWA NAWE ". Sauti hii ilisikika wakati Bwana Yesu alipokuwa anabatizwa na Yohana katika ule mto Yordani, kabla hata hajaanza huduma yake.Unaona hapo alikuwa ameshashuhudiwa kwamba amempendeza Mungu Na alikuwa ameshapewa vitu vyote na baba yake kabla hata hajaanza kuhubiri wala kufanya muujiza wowote.

Kumbuka kumpendeza huko au kupewa vyote na Baba, hakukuja kwasababu tu yeye alikuwa ni Mungu, hapana, Bali kuna vitu vingine vilivyomfanya afikie kiwango hicho kikubwa sana cha kumpendeza Mungu. Nacho hatukipati pengine zaidi ya ndani ya ile miaka 30 BWANA YESU aliyoishi kabla ya kuanza huduma yake.

Injili hazijarekodi kwa urefu maisha hayo aliyoishi miaka 30, isipokuwa matukio machache sana, ambayo ni yale alipokuwa anazaliwa, na lile tukio alipokuwa na miaka 12, na sehemu nyingine alipokuwa anamsaidia baba yake kazi za useremala. Lakini sehemu kubwa ya maisha yaliyobakia Mungu aliyaficha kwa makusudi maalumu ili sisi tutafute kufahamu ni nini hasa kilichomfanya Mungu apendezwe naye kabla hata ya kuanza huduma yake. Wengi tunadhani Bwana alipokuwa anafufua wafu,anatenda miujiza,anaponya wagonjwa, anahubiri n.k. ndio kipindi hicho ambacho Mungu alianza kupendezwa na yeye sana. Hapana alipendezwa kwanza kwa maisha aliyoishi ambayo hayajarekodiwa kwenye Injili zile nne lakini yapo kwenye biblia.

Sasa tutapataje kuyajua maisha yake.?

Kama tunavyofahamu ili kufahamu tabia ya mtu, ni vizuri kuangalia historia ya familia yake, au jamii ya watu aliyotokea, ndio maana watu sana sana wanapenda kuangalia tabia za baba, babu, n.k.ili kulinganisha na tabia ya mtoto. kwasababu wanajua kwa namna moja au nyingine kuna aina fulani ya mwenendo au tabia itakuwa imerithiwa kutoka kwao. Hivyo tukirudi kwenye biblia tunaousoma pia ukoo wa Bwana Yesu . Ukoo ule haukuandikwa kutufurahisha tu, bali ulikuwa unamaana kubwa ili kutusaidia sisi kuyajua maisha ya YESU mwokozi wetu yalivyokuwa kabla hajaanza huduma na yanatufundisha nini.. Hivyo ni vizuri kusoma biblia kwa kujifunza, kuliko kusoma kama hadithi tu.. Embu tuusome huu ukoo kidogo..
Mathayo 1

1 Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu.
2 Ibrahimu alimzaa Isaka; Isaka akamzaa Yakobo; Yakobo akamzaa Yuda na ndugu zake;
3 Yuda akamzaa Peresi na Zera kwa Tamari; Peresi akamzaa Esromu; Esromu akamzaa Aramu;
4 Aramu akamzaa Aminadabu; Aminadabu akamzaa Nashoni; Nashoni akamzaa Salmoni;
5 Salmoni akamzaa Boazi kwa Rahabu; Boazi akamzaa Obedi kwa Ruthu; Obedi akamzaa Yese;
6 Yese akamzaa mfalme Daudi; Daudi akamzaa Suleimani kwa yule mke wa uria;
7 Sulemani akamzaa Rehoboamu; Rehoboamu akamzaa Abiya; Abiya akamzaa Asa;
8 Asa akamzaa Yehoshafati; Yehoshafati akamzaa Yoramu; Yoramu akamzaa Uzia;
9 Uzia akamzaa Yothamu; Yothamu akamzaa Ahazi; Ahazi akamzaa Hezekia;
10 Hezekia akamzaa Manase; Manase akamzaa Amoni; Amoni akamzaa Yosia;
11 Yosia akamzaa Yekonia na ndugu zake, wakati wa ule uhamisho wa Babeli.
12 Na baada ya ule uhamisho wa Babeli, Yekonia akamzaa Shealtieli; Shealtieli akamzaa Zerubabeli;
13 Zerubabeli akamzaa Abihudi; Abihudi akamzaa Eliakimu; Eliakimu akamzaa Azori;
14 Azori akamzaa Sadoki; Sadoki akamzaa Akimu; Akimu akamzaa Eliudi;
15 Eliudi akamzaa Eleazari; Eleazari akamzaa Matani; Matani akamzaa Yakobo;
16 Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa YESU aitwaye Kristo.
17 Basi vizazi vyote tangu Ibrahimu hata Daudi ni vizazi kumi na vinne; na tangu Daudi hata ule uhamisho wa Babeli ni vizazi kumi na vinne; na tangu ule uhamisho wa Babeli hata Kristo ni vizazi kumi na vinne.
Laiti Kama mafarisayo na masadukayo wangefuatilia kwanza historia ya Yesu katika ukoo wake kabla ya kuzaliwa wasingepata shida kumtambua au kumwamini YESU kama yeye ndio Mwokozi. Mfano tukisoma habari ya Ibrahimu na Isaka, mwanzo kabisa wa ukoo, tunaona Ibrahimu alimtoa mwanawe pekee, kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Mungu, ikifunua kuwa masiya atakayekuja atabeba tabia zinazofanana na hizo kwamba Isaka ni mfano wa Bwana Yesu na Ibrahimu kama Mungu, kwahiyo wasingepaswa washangae wamwonapo Bwana kujitoa nafsi yake kama mwanakondoo kwa wengine.

Kadhalika na maisha ya wale wote walioandikwa katika ule uzao, walibeba tabia fulani zinazomtabiri Bwana, hatuna muda wa kupitia mmoja mmoja lakini tumwangalie mmoja wa mwisho Daudi, yeye alikuwa ni Mfalme, lakini ufalme wake ulipatikana kwa taabu na shida nyingi maadui zake walimzunguka kila pande, ikampelekea kuandika zile zaburi alipokuwa katika shida, Kama vile Daudi alivyopitia shida kutoka kwa maadui zake, vivyo hivyo Bwana Yesu kabla ya kuupokea ufalme ilimpasa apitie taabu nyingi na kukataliwa. Na ndio maana kitabu cha zaburi ni maisha ya Bwana Yesu mwenyewe mwanzo mwisho.

Tunaona pia Daudi alipokuwa anapitia tabu na kuonekana kama hakuna msaada wowote alisema, Mungu wangu! Mungu wangu mbona umeniacha? (zaburi 22) ..alisema pia "hutaucha mwili wangu uone uharibifu(akiwa na maana kuwa kutokufa)",.aliposalitiwa na watu wake wa karibu alisema "aliyekula mezani pangu amenigeuzia kisigino chake "...alisema pia, "wameyapigia kura mavazi yangu.." na maneno mengine mengi...Na mengi ya hayo tunaona yakijirudia kwa Bwana Yesu alipokuwa anapitia tabu kama za Daudi katika maisha yake, na alipokuwa msalabani. Ukiwa ni mchunguzaji wa maandiko utaona mambo hayo.

Hivyo ukitaka kufahamu maisha na tabia ya BWANA YESU alipokuwa duniani kabla na baada ya huduma kuanza rudi katika historia ya ukoo wake, utayaona mwanzo mwisho jinsi alivyoishi hapa duniani. Ndio maaana alipokuwa anaondoka aliwaambia wanafunzi wake..Luka 24: 44 " Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima YATIMIZWE YOTE NILIYOANDIKIWA KATIKA TORATI YA MUSA NA KATIKA MANABII, NA ZABURI.
45 Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko.
46 Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu;
47 na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu".

Umeona hapo maisha ya Bwana yaliandikwa katika TORATI, ZABURI na MANABII ukizingatia kusoma hizo utamwona Yesu lakini kwa kawaida maisha yake yatabakia kuwa fumbo machoni pa mtu.Kwa mfano utatafuta katika biblia yote mahali pameandikwa masihi atakufa na kufufuka siku ya tatu hutaona kwasababu mambo hayo yameandikwa katika mafumbo ambayo yanahitaji msaada wa Roho kuyafahamu.

Mahali pengine kwenye zaburi Daudi katika taabu zake alisema ;

Zaburi 69: 7 Maana kwa ajili yako nimestahimili laumu, Fedheha imenifunika uso wangu.
8 Nimekuwa MGENI KWA NDUGU ZANGU, NA MSIKWAO KWA WANA WA MAMA YANGU.
9 Maana WIVU WA NYUMBA YAKO UMENILA, Na laumu zao wanaokulaumu zimenipata.
10 Nilipolia na kuiadhibu roho yangu kwa kufunga, Ikawa laumu juu yangu.
11 Nilipofanya gunia kuwa nguo zangu, Nikawa mithali kwao.
12 Waketio langoni hunisema, Na nyimbo za walevi hunidhihaki.
13 Nami maombi yangu nakuomba Wewe, Bwana, Wakati ukupendezao; Ee Mungu, Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, Katika kweli ya wokovu wako.
14 Uniponye kwa kunitoa matopeni, Wala usiniache nikazama. Na niponywe nao wanaonichukia, Na katika vilindi vya maji.

"Ndio sababu Bwana Yesu aliitwa mwana wa Daudi japokuwa YESU ndiye aliyekuwa Bwana wake

Ukichunguza maandiko utaona maneno hayo pia yalimuhusu Bwana. Yeye hata ndugu zake hawakumwamini kama anaweza mtu kama yeye kuwa MFALME wa Israeli, alionekana kama mgeni katikati ya ndugu zake, kisa tu ameamua kutenda mapenzi ya baba yake, japokuwa alikuwa ni mtu wa dua nyingi akiwaombea maadui zake kwa kufunga na kulia (Waebrania 5:7), marafiki pia wasingeweza kukaa naye kwasababu alionekana kama mtu wa itikadi fulani za kidini ngumu, maana kama angekuwa na marafiki bila shaka hao hao marafiki zake wangeweza kuja kuwa wanafunzi wake...

Biblia inasema pia alikuwa hana UMBO LA UZURI kama wengi tunavyodhani (Isaya 53:3-4)..ni mtu ambaye asingeweza kulinganishwa na vijana wengine kwa uzuri. Lakini mbele za Mungu alikuwa ni mzuri kuliko watu wote duniani...Alifikia umri wa kuoa lakini hakuoa kuwa mke ni kitu cha maana sana kwake zaidi ya kumtazama Baba yake kila wakati. Maisha yake yalikuwa hivyo hivyo siku zote, kabla ya kuanza huduma, tafakari hata nyumba yake binafsi alikuwa hana, wala kiwanja, kwa dunia ya sasa watu wangeweza kusema mtu asiyekuwa na malengo...Lakini alikuwa ni mtu mwenye malengo makubwa kuliko watu wote duniani na ndio maana tunasoma habari zake mpaka leo. kazi yake,chakula chake, kuishi kwake ilikuwa ni KUTENDA MAPENZI YA MUNGU TU!! na kuzingatia utakatifu wa hali ya juu..Na ndio hapo baada ya Mungu kumuhakiki kwa muda mrefu wa miaka 30 ...Ndipo akaona huyu ndiye mwana wake pekee aliyempendezwa naye akampa vyote na kumtangaza hadharani..HUYU NDIYE MWANA WANGU, MPENDWA WANGU NILIYEPENDEZWA NAYE...HALELUYA....

Unaona hapo Bwana Yesu hakumpendeza Mungu baada ya kuanza huduma, hapana bali kabla ya kuianza..japokuwa maisha yake mbele za watu yalidharaulika lakini ulipofika wakati Mungu alimtukuza na kumweka juu ya vitu vyote.Vivyo hivyo na sisi Mungu hatuangalii tunapokuwa wahubiri bali anataka tumpendeze katika maisha tunayoishi siku zote sasa katika hali yoyote tunayopitia, katika kutengwa, au kupendwa, katika kuradhaulika au kukubalika... JE! TUNAISHI SAWASAWA NA MAPENZI YA MUNGU KATIKA UTAKATIFU WOTE?.

Je! tunampenda Mungu wetu kwa akili zetu zote na mioyo yetu yote kama Yesu alivyofanya?. Tukifanya hivyo basi BABA atapendezwa na sisi na kutupa vyote kabla hata hatujaanza kumtumikia katika viwango vingine.Hivyo ndugu huu ni wakati wa kuanza kuchukua uamuzi katika hatua tulizopo na kuyatenda mapenzi ya Mungu..usiongoje uwe muhubiri au mtumishi anza sasa, na Bwana akishakwisha kukushuhudia atakutukuza. MUNGU ATUSAIDIE SOTE.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali share kwa wengine ujumbe huu na Mungu atakubariki.

No comments:

Post a Comment