"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, May 5, 2018

JIHADHARI NA ROHO ZIDANGANYAZO.


Mathayo 24:23-28

23 Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki.
24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.
25 Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele.
26 Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki.”

Luka 17: 23 “Tena watawaambia, Tazama, kule! Tazama, huku! Msiondoke mahali mlipo, wala msiwafuate;
Bwana alipoykuwa anayazungumza maneno hayo alimaanisha kabisa kwamba kuna wakati wa hatari utafika ambapo mtoto yeyote wa Mungu atalazimika kubaki mahali alipowekwa kwa usalama wa roho yake, kwasababu alisema watatokea manabii wengi wa uongo na makristo wa uongo kudanganya watu yamkini hata walio WATEULE. Kumbuka wateule ni watu waliosimama katika imani kweli kweli ndio katika siku za mwisho watakaokuja kujaribiwa na sio tu kila mtu wa ulimwengu hao walishadanganyika siku nyingi..

Hivyo ni muhimu sana kujua ni wapi tulipoonywa tubaki tusiondoke?. Ni dhahiri kuwa patakuwa ni sehemu moja, Kumbuka alipokuwa anazungumza hizi habari kwa wanafunzi wake hapo mwanzo aliwaambia; kama zilivyokuwa katika siku za Nuhu ndivyo itakavyo kuwa katika siku za kuja kwake mwana wa Adamu. Sasa tujifunze kidogo siku za Nuhu zilikuwaje..

Tunasoma habari kwamba kabla ya gharika kuanza Nuhu na familia yake waliambiwa na Mungu waingie ndani ya SAFINA, na walipomaliza kuingia tu wote, Mungu mwenyewe ndiye aliyeufunga mlango, ikiwa na maana kuwa hakutakuwa na mazingira ya mtu yeyote kutoka mpaka utakapofikia wakati wa Mungu mwenyewe kuufungua tena, kutokana na hatari iliyopo nje. Kwa lugha rahisi alikuwa anamaanisha kuwa WASITOKE MAHALI WALIPO mpaka utakapofika wakati wa Mungu mwenyewe kuwafungulia mlango watoke.

Lakini tunakuja kuona baadaye mara baada ya mvua kuacha kunyesha na maji kuanza kupungua Nuhu alishawishika kufungua mlango ambao BWANA hakumwambia aufungue..Ni Yeye mwenyewe kwa kuwaza kwake, alikisia tu kwamba nje kutakuwa kumeshaanza kuwa salama, matokeo yake alipofungua tu madirisha yale Mungu aliyoyafunga ZIKATOKA ROHO MBILI.

Na hizi roho ni zipi?

Si nyingine zaidi ya KUNGURU na NJIWA. Kwa ufupi hizi roho zilitoka ili kuwaongoza katika njia waliyotaka kuiendea. Tunasoma alitoka kwanza Kunguru, na hakurudi tena, kuashiria kwamba huko nje ni SALAMA KABISA, chakula sasa kipo tele nje, maji yamekauka, ardhi ni kavu kabisa hivyo ni wakati wa kutoka na kuanza kufurahia nchi, pengine wakina Nuhu walishaanza kujiandaa kutoka wakidhani kuwa nje ni salama, kumbe ile ilikuwa ni roho idanganyayo, maana kama mfano wangetoka nje,wasingeweza kurudi tena katika safina pengine wangekutana na tope kubwa sana ambalo lingewazamisha ndani yake, na pia wasingekutana na jani lolote kama walivyotegemea kutoka katika ile injili ya kunguru hivyo wasingeweza kuishi kwa namna yoyote..Lakini Bwana kwa huruma zake na rehema zake hakupenda Nuhu aangamie akaruhusu Roho nyingine iwatangulie nje nayo ni NJIWA.

Lakini kama tunavyoisoma habari, yule njiwa hakuona mahali pa kutua na kurudi safinani, kuashiria kuwa huko nje hakuna maisha, Hivyo Nuhu akalazimika kungojea tena siku saba nyingine, na yule njiwa alipotoka tena, akarudi na TAWI LA MZEITUNI mdomoni mwake kuashiria kuwa nje ni salama kijani kimeshatokea..sasa huo ndio wakati wa KUTOKA. (Mwanzo 8).
 

Habari hii ni ya siku hizi za mwisho kama Kristo alivyosema, Bwana kwa kuiona hatari iliyopo katika majira haya alitangulia kutufungia mahali fulani ili tukae huko mpaka wakati wetu na majira yaliyokusudiwa yafike. Na kifungo hicho ni NENO LA MUNGU (Biblia). Kumbuka unapokuwa mkristo na umezaliwa kweli mara ya pili, Mungu analazimika kukufunga katika misingi ya Neno lake kwamba udumu huko usitoke. Na yule njiwa ni Roho Mtakatifu(Waefeso 4:30) na yule kunguru ni mfano wa roho zidanganyazo zinazotenda kazi katika siku hizi za mwisho kuwadanganya yamkini hata walio wateule.

Kumbuka unapofungua mlango ambao Mungu alishaufunga kwako unaruhusu roho zidanganyazo zilizofananishwa na yule kunguru kukuongoza. Na roho hizi zitakuhubiria huko nje hakuna shida siku zote ni raha, kuna amani, kuna maisha, hakuna tena gharika, Mungu kashaibariki nchi, hizi roho zitakuwa zinakuambia njoo!! njoo!! njoo!! zinakuita sana ujiunge nazo kuliko zenyewe kukuletea chakula, mfano ya yule kunguru, zitakufundisha dunia haiishi leo wala kesho, zitakwambia chakula kipo tele cha kukutosha huku nje!! .Ndugu yangu na kama hutadumu katika maagizo ya NENO LA MUNGU hakika zitakuchukua.

Tunaishi katika kizazi kile alichokisema Bwana cha kuzuka kwa makristo na manabii wengi wa uongo, wanaohubiria watu injili nyingine, na Yesu mwingine, ambaye hakuhubiriwa na mitume. Mitume walihubiri watu watubu, wakabatizwe kwa jina la Yesu kristo kwa ajili ya ondoleo la dhambi zao na wapokee Roho Mtakatifu. lakini wao hilo halina maana sana kwao, unaweza ukawa na Yesu tu(umeokoka) hata ukiwa unavaa nguo za nusu uchi,unapaka wanja,lipstick, unaabudu sanamu, n.k. Mungu haangalii mavazi anaangalia moyo. Biblia pia inasema Yesu ndiye njia kweli na uzima, wao wanasema zipo njia nyingi za kumfikia Mungu kipimo ni upendo tu, unaweza ukawa dini nyingine na ukaenda mbinguni bila hata kumwamini Bwana Yesu, Injili zao siku zote ni za kumfariji mtu katika hali ya dhambi aliyopo. Hazilengi kumwelekeza mtu mbinguni, bali zinalenga kumwelekeza mtu kufanikiwa tu katika mambo ya mwilini, hazihubiri hukumu inayokuja kwa watu ambao wapo kwenye dhambi zinafundisha mtu ambaye hajafanikiwa ndio kipimo halisi cha kulaaniwa na Mungu..n.k.

Hizi zote ni roho za kunguru zinazotangulia kudanganya watu wa kweli wa Mungu. Lakini Roho wa Mungu kwa mfano wa yule njiwa anakuletea tumaini ukiwa ndani ya safina yako akiwa na TAWI LA MZEITUNI mdomoni mwake. Huo ndio utakuwa uthibitisho tosha kuwa nje ni salama. Yule njiwa Hatakupigia kelele nenda sehemu fulani,yeye ndio yupo, bali atakuambia tazama ufalme wa Mungu haupo kule wala huku, bali upo ndani yako.
 

Ndugu yangu hili kanisa tunaloishi ndilo la mwisho linaloitwa LAODIKIA,(ufunuo 3) na ndilo Bwana alilolitolea habari hizo na kusema;

"Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele wakiwaambia Tazama, kule! Tazama, huku! Msiondoke mahali mlipo, wala msiwafuate"; Usizifuate hizi roho bali dumu katika kile BIBLIA inasema, na sio kile DINI au DHEHEBU,au MCHUNGAJI, au NABII au mtu yeyote anachosema kwasababu hizi ni nyakati za hatari sana. Itafika wakati Bwana mwenyewe atatoa ishara kwa watu wake kutoka..na ndio maana wanafunzi wake wakamuuliza Bwana... "Wapi, Bwana? Akawaambia, Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai”.

Utakuja wakati ambao ni hivi karibuni, karibia na unyakuo nao utakuwa ni mfupi sana, kwa wale wateule wa Mungu kutoka, utapita UAMSHO WA ROHO MTAKATIFU duniani kote,ambao utakuwa wa kipekee sana, mfano wa yule njiwa alipolileta tawi la mzeituni kwa Nuhu na kumpa IMANI KAMILI ya kutoka nje ya SAFINA, kadhalika Roho Mtakatifu ataachilia UFUNUO FULANI WA KIPEKEE KWA WATU WAKE TUU (ndiyo zile ngurumo 7 ambazo hajifanuliwa bado kwa kanisa (ufunuo 10:4)) ndizo zitakazokuja kumpa IMANI bibi-Arusi wa Kristo ya kwenda kwenye UNYAKUO. Kumbuka hii ni IMANI ile Bwana Yesu aliyoiulizia kwamba akija je! ataiona? katika luka 18:8.

Hivyo ndugu hizi ni siku za mwisho, JE! UMEOKOLEWA!, NI NANI ANAYEKUONGOZA SASA, NJIWA AU KUNGURU?. biblia inasema Roho Mtakatifu ndio Muhuri wa Mungu , na wote wasio na Roho wa Mungu hao sio wake(warumi 8:9). TUBU sasa mgeukie Yesu Bwana aliye mkuu wa uzima wako.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali washirikishe na wengine ujumbe huu.

No comments:

Post a Comment