"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, June 16, 2018

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 29.

SWALI 1: Ni sahihi mkristo kujipulizia pafyumu na kujipaka mafuta ya marashi ndugu?

JIBU: Mungu anaangalia sababu ya mtu kufanya hivyo ni nini?. Kwa mfano kupaka pafyum fulani isiyokuwa na harufu kali kwaajili ya kuzuia harufu ya jasho, au harufu fulani sio tatizo, suala la muhimu ni iwe pafyumu ya kawaida tu, isiyokuwa na maudhui ya kishetani, kwa mfano pafyumu nyingine zinaitwa lucifa, au demon,dragon au wengine wanajipulizia pafyumu kwa ili kuvutia kupendwa au kutamaniwa kama vile makahaba wanavyofanya, unakuta pafyumu nyingine zinatoa harufu kali, njia nzima mpaka zinakuwa ni kero kwa watu wengine, ...Sasa hiyo ni dhambi na hitakiwi kwa mtoto wa Mungu..Lakini kama ni kwa ajili ya kujiweka katika utanashati tu wa kawaida, au kutoa harufu mbaya mwilini haina shida, Biblia inasema yule mwanamke alimwendea usiku Bwana akamwagia marhamu kichwani pake yenye thamani kubwa na Bwana akambarikia kwa tendo lile Na pia kuna sehemu nyingine Bwana alisema

Mathayo 6:16 Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao.
17 Bali wewe ufungapo, JIPAKE MAFUTA KICHWANI, UNAWE USO;
18 ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi"...

Unaona hapo BWANA aliruhusu watu wafungapo wajipake, mafuta kichwani, na wanawe uso sababu kuu sio wavutie wapenzi, au waonekane na watu hapana bali sababu ni ili wasionekane na watu kama wamefunga, kadhalika na mtu unapopulizia pafyumu, au kupaka mafuta fulani ni muhimu jichunguze nia yako ya ndani kwanini unafanya hivyo.

SWALI 2: Hivi ndugu Mwanamke anapaswa aziache nywele zake bila kuzikata ziwe ndefu mpaka huko zitakapofika zenyewe? kulingana na 1Wakoritho 11:15 ?JIBU: Biblia inaposema mwanamke asikate nywele zake haimaanishi kwamba kiwembe, au mkasi visifike kabisa kichwani mwake, hapana ina maanisha kuwa mwanamke asizikate nywele zake zikawa fupi kama za mwanaume, kiasi kwamba tofauti yake na mwanamume haionekani, hivyo mwanamke nywele zake zinapokuwa ndefu kupita kiwango fulani anapaswa azipunguze na kuziweka kiwango fulani labda cha kufika mabegani au juu kidogo au chini kidogo, lakini zisivuke shingo na kuwa kipara, na pia hakuna sharti lolote juu ya nywele za mwanamke kuburuza chini, labda iwe ni kwa mapenzi yake tu, hivyo anapaswa azimudu tu zisifike chini sana wala zisipungue sana..

Kadhalika nywele za kiafrika ni za katani, hivyo hata ukuaji wake huwa ni wa shida kidogo hivyo huyu ndiye hapaswi kukata kwasababu hata aziache vipi haziwezi zikawa nyingi za kumzidi kiwango..Lakini kama zikukua vivyo hivyo yeye naye anaruhusiwa kuzipunguza.

SWALI 3:
Kwanini nyie mnaitwa Wingu La Mashahidi ndugu? Siku moja nilidhania labda nyie ni wa wale Mashahidi wa Yehova.


JIBU: Ubarikiwe swali zuri, kwanza sisi sio mashahidi wa Yehova wala wingu la mashahidi. Tulipofungua hizi account za facebook,website na blog ndizo tulizoziita wingu la mashahidi, na sababu ya kuita wingu la mashahidi ndio ile ile ya kuliita group jina "tukue toka imani hata imani"..

Kwahiyo neno "wingu la mashahidi" linapatikana katika kitabu cha waebrania 12:1" Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na WINGU KUBWA LA MASHAHIDI namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,"

Kumbuka safari ya ukristo inafananishwa na riadha, hivyo watu wanaposhindana kwenye riadha huwa wanaweka chini vitu vizito ili wawe wepesi katika kukimbia, kadhalika wanajizuia na mambo mengi,wakidumu katika mazoezi makali, wengine wanajizuia hata kula, wengine wanajizuia na wanawake, wengine anasa,n.k. ilimradi tu waweze kujiweka kwenye chat (wasishuke viwango).

kadhalika na sisi tupo mbioni katika riadha zetu za rohoni na ndio hapo biblia inatuambia, "tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu", kwakuwa tumezungukwa na wingu kubwa la mashahidi walioshindana mbio kwa uaminifu na kuzishinda, sasa hili wingu la mashahidi ni akina nani?? Ukirudi sasa kwenye waebrania sura ya 11 yote utawaona hawa wingu la mashahidi ni wakina nani? utawaona ni wakina Habili,Musa, ibrahimu, henoko, Isaka, Yakobo n.k..Hao ndio wingu la mashahidi wametuzunguka sisi, katika ulimwengu wa Roho, vivyo hivyo tunapaswa tupige mbio kama wao. Ili na sisi tuwe washirika wa hilo wingu kubwa la mashahidi linalotuzunguka... Kasome waebrania 11 yote na 12 utaelewa vizuri.

SWALI 4:
Ule mfuko wa fedha Yuda Iskariote aliokua anaubebaga, zile fedha kule mfukoni walikua wanazipata wapi?

JIBU: walikuwa wanazipata katika michango iliyokuwa inatoka kwa watu..Luka 8: 1 "Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, 2 na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, 3 na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, WALIOKUWA WAKIMHUDUMIA KWA MALI ZAO". Unaona hapo wapo waliokuwa wanamuhudimia Bwana kwa mali zao wale walioguswa na Roho.

SWALI 5: Wakati Nabii Samueli alipoenda kumpaka Daudi mafuta ili daudi awe mfalme wakati ule."Yale mafuta yalikua ni mafuta ya aina gani ndugu?"

JIBU: Ni mafuta ya mti unaoitwa wa  mizeituni, unastawi zaidi maeneo ya mashariki ya kati (Israeli, Palestina, Jordani na nchi za kandokando)..mafuta hayo yalitumika kama ishara tu ya nje! lakini Daudi alitiwa mafuta rohoni na Mungu..

SWALI 6: Wakristo tunaruhusiwa kuwapaka mafuta wagonjwa?Na ni mafuta ya aina gani?

JIBU: Unampaka hayo mafuta kwa makusudi gani?. watu wengi siku hizi wanatumia mafuta, maji, chumvi, sabuni, odongo, n.k. kana kwamba vyenyewe ndio nyenzo pekee ya mtu kupokea uponyaji wakishikilia ule mstari wa Yakobo 5: 14 "Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. 15 Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa". ..

Lakini si kweli, kinachomponya mtu ni Imani katika Jina la YESU. Hivyo vingine ni maagizo yanayoweza kuambatana na imani, na hayana fomula fulani maalumu ya kufuata kwamba kila mgonjwa apakwe mafuta, au atumie maji au chumvi..Hapana hiyo ni kwa jinsi mtu atakavyoongozwa na Roho, na ndio maana mahali pengine Bwana Yesu alioongozwa na Roho awaponye vipofu kwa kuwapaka matope, wengine kwa kuwatemea mate, n.k. lakini kuna wengine alikuwa anawaponya pasipo maagizo yoyote..Hivyo ni kulingana na uongozo wa Roho, na sio tu kila tatizo ni mafuta au maji au chumvi kama wengi wanavyofanya sasa hivi..hiyo ni sawa na ibada za sanamu.

Ubarikiwe.

No comments:

Post a Comment