"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, June 7, 2018

UFUNUO: Mlango wa 3

Sehemu ya kwanza.

Bwana na mwokozi wetu YESU KRISTO atukuzwe daima. Karibu katika mwendelezo wa uchambuzi wa kitabu cha Ufunuo, Leo tukiliangalia lile kanisa la TANO kati ya yale makanisa SABA, na Ujumbe aliopewa Mtume Yohana ayapelekee. Kanisa hili linaitwa SARDI. Tunasoma.

Ufunuo 3:1 "Na kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa".

Kumbuka hapa Bwana anajitambulisha kama "yeye mwenye hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba". Katika kanisa hili hakujitambulisha kama "yeye mwenye macho kama mwali wa moto au yeye mwenye huo upanga mkali utokao kinywani mwake n.k." bali alijitambulisha kama yeye mwenye hizo Roho saba, akifunua asili yake ya ndani, Sasa Hizi Roho saba, sio kwamba Mungu anazo Roho 7 na kila moja inajitegemea kivyake hapana, bali ni Roho ile ile moja isipokuwa inatenda kazi katika nyakati tofauti tofauti saba. Mfano tuna siku 7 katika juma, na kila siku tunaona jua likichomoza na kuzama, sasa hatuwezi tukasema kwa wiki tuna ma-jua 7, hapana tunafahamu kuwa jua ni lile lile moja isipokuwa limetenda kazi katika siku saba tofauti, na ndivyo ilivyo kwa Roho wa Mungu. Kwanza ni vizuri kufahamu Mungu ni Roho, na ni mmoja, na Roho yake ni moja, kadhalika na nafsi yake ni moja. Kwahiyo hapo ni ile ile Roho moja ikitenda kazi katika nyakati tofauti tofauti saba za Kanisa.

Kwahiyo kwanini Bwana alijitambulisha kama yeye mwenye Roho 7, ni kwasababu "Roho ndiyo inayotia uzima". Na ndio iliyokuwa inatia UZIMA kwa makanisa yote 7 kuanzia la kwanza mpaka la mwisho. Ikiwa na maana kuwa kanisa hilo la SMIRNA lilihusiana na kupungukiwa na Roho wa Mungu. Hivyo kama tunavyofahamu mtu akikosa Roho wa Mungu ni sawa na kakosa uzima,na Kinachobakia ni kifo. Wakati fulani Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake katika

Yohana 6: 63 "ROHO NDIYO ITIAYO UZIMA, mwili haufai kitu; MANENO HAYO NILIYOWAAMBIA NI ROHO, TENA NI UZIMA".

Unaona hapo anasema ni Roho tena ni uzima. Hivyo kanisa hili limehusiana na kuacha maneno ya Bwana ambayo ndio Roho yenyewe itiayo uzima kwao. Na ndio maana Bwana anasema anayajua matendo yao ya kwamba “wana jina lililohai lakini WAMEKUFA”.

Tulichunguze kidogo hili kanisa la SARDI; Tafsiri ya neno SARDI ni "WALE WALIOTOROKA"..Na kanisa hili lilianza mwaka 1520WK na kuisha mwaka 1750WK, Kanisa hili halikudumu kwa muda mrefu sana kama Kanisa lililopita la Thiatira ambalo lenyewe lilidumu kwa muda wa zaidi ya miaka 900. Kipindi hichi cha kanisa hili kinajulikana maarufu kama "wakati wa matengenezo ya kanisa", Ni wakati ambao lile giza ambalo lilikuwa limetanda duniani kutoka katika nyakati za kanisa la nne lilianza kumezwa na Nuru ya kweli ya Mungu kidogo kidogo baada ya kanisa kuharibiwa kwa muda mrefu na mafundisho ya dini ya uongo (Katoliki).

Hivyo Mungu akaanza kunyanyua watumishi wake waaminifu ambao waliyashika yale maneno ya Bwana aliyosema katika lile kanisa la Nne lililotangulia kwamba "wanamridhia yule mwanamke YEZEBELI". Hivyo hawa baada ya kuzijua fumbo za shetani na kwamba makao yake makuu yapo katika dini ya uongo inayofanana sana na ukristo (Katoliki), hawakumridhia kama watu wa kanisa la nne walivyofanya.. Hivyo wakaanza kunyanyuka na kwenda kinyume na kuyapinga mafundisho yake kwa kuhubiri UKWELI WA NENO kwa watu wote pasipo kumwogopa. Ndipo tunakuja kuona Mungu akamnyanyua mtu kama "MARTIN LUTHER", Ambaye yeye ndiye aliyekuwa mjumbe/Malaika wa kanisa hilo (SARDI), na wengine pia kama wakina Calvin, Zwingli, na wengineo..Wote hawa kwa pamoja hawakumridhia yule mwanamke YEZEBELI. Na kama vile tafsiri ya jina la Kanisa hili lilivyo (Sardi=wale waliotoroka), hivyo hawa wakristo wa nyakati hii walifanikiwa kutoroka kwa sehemu kutoka kwa yule mwanamke Yezebeli.

Tunaona Martin Luther ambaye mwanzoni alikuwa ni kasisi wa kikatoliki, baada ya kuona njia ya kanisa Katoliki haiendani na kweli ya Mungu, aligeuka na kuyapinga mafundisho ya kanisa hilo, siku moja katika safari yake ya kuutafuta ukweli, alisikia sauti ikimwambia.."Mwenye haki ataishi kwa Imani" (Warumi 1:17). Hivyo baada ya kupokea ufunuo huo akaanza kuyakataa mafundisho yote ya "wanikolai" ya "Balaamu" na ya "Yezebeli" kwamba mtu hatapitia kwa kuhani fulani au Padre fulani au Papa ili amfikie Mungu, Bali kwa IMANI kwa Mungu kila mtu atamfikia yeye na kumpendeza..kwamba mtu anasamehewa dhambi zake kwa IMANI kwa Mungu, na sio kwa kupitia mwanadamu yoyote, kadhalika na uponyaji na mahitaji na mambo mengine yote...


Hivyo kuanzia huo wakati Martin Luther alizidi kupinga kwa Nguvu mifumo ya kanisa Katoliki siku moja aliandika HAYA 95 zinazopinga mfumo wa kipapa na kuzigongelea kwenye mlango wa ngome ya kanisa kubwa la kiKatoliki lililokuwepo huko wittenberg Ujerumani mwaka 1517. Na ndipo uprotestant ulipoanzia ikasababisha uamsho mkubwa wa roho, watu wengi wakaanza kutoka kwenye hiyo dini ya uongo kwa kupitia injili za hawa wana matengenezo.

Biblia zikaanza kutafsiriwa jambo ambalo hapo kwanza zilikuwa zinasomwa tu na makuhani wa kikatoliki, Hivyo ndivyo nuru ya kweli ilivyoanza kurejeshwa kidogo kidogo.

Lakini ilifikia wakati miaka kadhaa baada ya wale wajumbe kuondoka, watu wakaanza kujisahau, na kuanza kujiundia dini badala ya kuuendeleza uamsho wa Kweli ya Mungu, badala ya kuendelea kujitakasa kutoka katika yale mafundisho ya uongo zaidi na zaidi wakajiundia ngome, nao pia wakaanza kujiita Walutheran, wacalvism, wabrownist, wamennonite n.k. watu wakaanza kujivunia wanadamu na dini, badala ya kujivunia Kristo hivyo ikawafanya wasahau kabisa ule msingi wa uprotestant ambao haukuwa na lengo la kuanzisha dini nyingine bali ulikuwa na lengo la kuwatoa katika uongo wa yule mwanamke Yezebeli (Katoliki) na kuwarejesha watu kwenye NENO LA MUNGU.

Jambo ambalo Mtume Paulo alilikemea pia kwa nguvu katika...


1wakorintho 1: 11 "Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu.
12 Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu kusema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo.
13 Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo? "


Hivyo mbele za Mungu hawa watu wa Sardi ambao mwanzoni walianza vizuri kwa nje walionekana kama wapo hai, lakini kwa ndani walikuwa WAMEKUFA kwasababu Roho ya uhai, na UZIMA haikuwa tena ndani yao, ya kuwafanya waweze kuuendeleza ule UAMSHO walioanzana nao hapo mwanzo.

Tukiendelea kusoma tunaona...

"2 Uwe mwenye kukesha, ukayaimarishe mambo yaliyosalia, yanayotaka kufa. Maana sikuona matendo yako kuwa yametimilika mbele za Mungu wangu.
3 Basi kumbuka jinsi ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia; yashike hayo na kutubu. Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako".

Unaona hapo waliambiwa wakeshe, na wayaimarishe mambo yaliyoyasalia, (yaani kumalizia kuondoa mafundisho yote ya Yezebeli ndani ya Kanisa), na kwamba wasipofanya hivyo (yaani kukesha) atakuja kwao kama mwivi na wala hawatajua hiyo saa atakayokuja.

Swali ni saa gani hiyo anayoizungumzia atalijilia hilo kanisa? Angali wakati wa hilo kanisa ulishapita na unyakuo haujatokea?

Ni muhimu kufahamu kwamba kila kanisa Bwana alikuwa na wakati wake wa kulijilia kanisa hilo, na kujiliwa huko kulikuwa ni UAMSHO fulani wa kipekee ambao ni mahususi kwa kuwavusha watu katika hatua nyingine ya kiimani inayofuata na huo Uamsho huwa unakuja karibu na mwishoni kabisa mwa nyakati wa kanisa husika..Hivyo kwa kanisa la kwanza baada ya kuacha upendo wao wa Kwanza Bwana aliwajilia kwa kupitia uamsho wa Irenio mjumbe wa kanisa la pili hivyo kwa ile jamii iliyoweza kumtii Kristo kwa ujumbe wa wakati waliokuwa nao(Wa mtume Paulo) waliweza kuchukuliana na ujumbe wa nyakati iliyofuata..Hivyo kwao Bwana anakuwa amewajilia lakini sio kama mwivi kwasababu Roho wa Mungu hajazimishwa ndani yao, lakini wale waliokataa, kwao inakuwa kama mwivi ndio unakuta watu wanaishia kuupinga ule ujumbe wa kuwaua, Na kuishia kuchukuliwa na mafundisho ya shetani.

Kadhalika na kwa nyakati ya pili, kujiliwa kwao kulikuwa ni mwishoni kabisa mwa nyakati, jamii ya watu waliodumu na mafundisho ya Irenio (Mjumbe wa kanisa la pili) waliweza kuchukuliana na uamsho wa mjumbe anayefuata..Vivyo hivyo na kwa kwani la nne, la tano.

Sasa katika hili la tano saa ya kujiliwa kwao ilikuwa ni wakati wa uamsho wa kanisa lililofuata ambalo Bwana alimtumia Mjumbe wa Kanisa lile JOHN WESLEY kuja na ujumbe wa UTAKASO KWA DAMU YA YESU, na utakatifu Hivyo kwa wale wachache ambao waliruhusu Roho wa Mungu awatoe kutoka hatua moja hadi nyingine ya IMANI, na kukaa mbali na mifumo ya yule kahaba Yezebeli walipewa neema ya kuuamini na kuupokea ujumbe wa John Wesley na huko ndiko kulikokuwa kujiliwa kwao. Lakini wale wengine waliokuwa wanaonekana wapo hai lakini wamekufa kwa kujiundia "majina" na kutengeneza madhehebu, Bwana alipokuja na uamsho wa Roho wa Wesley hawakujua chochote Sasa hiyo ndiyo kujiliwa kama mwivi, walibaki na dini zao na madhehebu yao.wakawa hawataki kufahamu jambo lingine la ziada ya ulutheri, ucalvinism, umennonite n.k. wakati lile kundi dogo ambalo lilikuwa tayari kwenda na Roho wa Mungu lilipokea uvuvio mpya wa Roho. Kwamba kuhesabiwa haki kwa Imani peke yake hakutoshi bali pia na Utakatifu ambao hakuna mtu atakayemwona Mungu asipokua nao (Waebrania 12:14)

Kadhalika na kwa kanisa la sita Filadelfia vile vile Bwana alilijia na wale waliokuwa wanadumu katika mafundisho ya mjumbe wa kanisa la sita John Wesley ilipofika wakati kujiliwa waliweza kupewa neema ya kuonja Uamsho uliofuata lakini wale ambao waliridhika na kuchukulia ujumbe wa Wesley kama dini, walibakia katika madhehebu yao wakajifungia katika Umethodisti na wakati wa Pentekoste ya Bwana ulipokuja mwaka 1906 huko Asuza Marekani, hawakujua chochote, wengine waliishia kupinga na kusema hicho kitu ni cha shetani na wengine hawakuelewa ni kitu gani.. Kwamba kuhesabiwa haki kwa imani pamoja na utakaso havitoshi bali pia Ubatizo wa Roho Mtakatifu ndio ukamilifu wa mambo yote. (Waefeso 4:30) kwamba huo ndio muhuri wa Mungu.

Vivyo hivyo na kwa kanisa la mwisho tunaloishi linaloitwa Laodikia, wale wote watakaoupokea ujumbe wa mjumbe wa kanisa hili WILLIAM BRANHAM wakidumu katika kujitenga na mafundisho ya yule kahaba mkuu YEZEBELI na kuruhusu Roho ya Mungu ya uhai ifanye kazi ndani yao, Na kukua kutoka hatua moja kwenda nyingine kila siku, Sasa hawa Bwana atakapokuja watajua kwasababu Roho wa Mungu anatenda kazi ndani yao, na taa zao zinawaka, lakini wale wengine hawatajua chochote, wataishia aidha kupinga, au kutokuelewa juu ya huo uamsho wa mwisho unaokuja. na kwa vile hakuna nyakati nyingine zaidi ya saba..Umsho huo utakuwa ni kwa ajili ya unyakuo wa kanisa. Na zile ngurumo 7 kwenye ufunuo 10 (zilizobeba siri ambazo hazijaandikwa mahali popote ), hizo ndizo zitakazoleta uamsho wa mwisho zitakazomvusha bibi-arusi wa Kristo kutoka katika nyakati ya saba, na kuingia katika umilele. Na ndio maana Bwana alisema...

Marko 13: 33 "Angalieni, kesheni, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo.

34 Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe.
35 Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jimbi, au asubuhi;
36 asije akawasili ghafula akawakuta mmelala.
37 Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni".


Na utaona maneno haya haya aliliambia hili kanisa la SARDI...


Ufunuo 3: 3 "Basi kumbuka jinsi ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia; yashike hayo na kutubu. Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako". ...

Lakini pamoja na hayo walikuwepo wachache katika kanisa hilo, walioweza kuenenda kwa uongozo wa Roho na kujitenga na yule mnyama hao ndio Bwana aliowaambia wataenda naye katika uvuvio wa Roho utakaokuja wa John Wesley.

"4 Lakini unayo majina machache katika Sardi, watu wasioyatia mavazi yao uchafu. Nao watakwenda pamoja nami hali wamevaa mavazi meupe, kwa kuwa wamestahili.
5 Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake.
6 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa".

Anasema yeye ashindaye jina lake halitafutwa katika kitabu cha uzima, na zaidi ya yote yale mavazi meupe yanawakilisha usafi wa hali ya juu, 'heri wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu (Mathayo 5:8) inasema hivyo"..Hivyo kundi hili katika umilele unaokuja watakuwa na nafasi ya karibu sana na Mungu kuliko watu wengine.

Hivyo ndugu Ujumbe huo pia unatuhusu hata sisi watu wa kizazi hichi tunachoishi, wa kanisa hili la mwisho la laodikia. Je! unakesha? na taa yako inawaka? je! Roho wa Mungu bado yupo hai ndani yako?. au una jina lililo hai lakini ndani yako umekufa?..Kumbuka huu ni wakati wa jioni, ondoka katika madhehebu na vifungo vya dini kama umeupokea ujumbe wa wakati wako halafu unaugeuza kuwa kama dini au dhehebu huu ni wakati wa kugeuka. Hivi karibuni Bwana ataenda kuachilia uvuvio wa mwisho nao utakuwa ni wa kipindi kifupi sana, utakaompa bibi arusi imani ya kwenda kwenye unyakuo.

Luka 12: 35 "Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka;

36 nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara".

Ubarikiwe sana.

Tafadhali share ujumbe huu kwa wengine na Mungu atakubariki.

 

No comments:

Post a Comment