Sehemu ya nne.
Shalom! mwana wa Mungu, karibu tujifunze Neno la Mungu, leo tukiwa katika mwendelezo wa kitabu cha Ufunuo. Hii ni sehemu ya nne, inayozungumzia juu ya lile kanisa la nne kati ya yale saba aliyoyachagua Bwana (Ufunuo 1:11), linaloitwa THIATIRA. Katika sura hii ya pili tulishayaona makanisa matatu ya mwanzo, tukaona ni jinsi gani yalivyokuwa yanaenenda na tabia zake kulingana na nyakati hayo makanisa yaliyopitia. Na leo tutamalizia sehemu ya mwisho ya sura hii ya pili, ambayo tutaliona kanisa hili la Thiatira na ujumbe wake waliopewa kutoka kwa BWANA.
Ufunuo 2:18 "Na kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika; Haya ndiyo anenayo Mwana wa Mungu, yeye aliye na macho yake kama MWALI WA MOTO, na miguu yake mfano wa shaba iliyosuguliwa sana".
Hapa tunaona Bwana ananza na utambulisho kama yeye azungumzaye ni “yule mwenye macho kama mwali wa moto, na miguu yenye mfano wa shaba iliyosuguliwa sana”..Kama tulivyojifunza kila utambulisho unaotangulia kabla ya ujumbe,huwa una mahusiano makubwa sana na ujumbe wenyewe wa kanisa husika. Mfano tuliona katika lile kanisa lililopita alijifunua kama "yeye aliye na huo upanga mkali ukatao kuwili utokao katika kinywa chake", na tunajua upanga unaashiria vita, na tulipokuja kusoma tuliona alikuja kufanya vita na wale wote ambao hawakutubia matendo yao maovu ndani ya kanisa. Kadhalika na hapa Bwana anakuja kama mwenye macho kama mwali wa moto na miguu iliyosuguliwa, mfano wa shaba. Tunajua kuwa macho kazi yake ni kuona. Na kama yanatoka moto inamaana kuwa anachokiona kinastahili moto. Hivyo hapa katika hili kanisa vile vile anakuja kwa hukumu kwa kile anachokiona. Swali ni kitu gani alichokiona ambacho kinastahili hukumu?..Tutakuja kukiona mbeleni.
Tukiendelea kusoma..
"19 Nayajua matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza".
Kwa historia fupi kanisa la Thiatira lilianza mwaka 606WK hadi mwaka 1520WK, na mjumbe wake aliitwa KOLUMBA, Ni kanisa lililodumu kwa kipindi kirefu kuliko makanisa yote saba, takribani miaka 914. Kipindi hichi kinajulikana kama kipindi cha giza ni wakati ambao nuru ya NENO la Mungu lilikuwa imefifia sana kutokana na mafundisho ya kipagani kuongezeka na mambo mengine kama uchawi, na umaskini vilikuwa vimekithiri sana duniani. Lakini kulikuwa pia na kuna kundi dogo la wateule wa Mungu ambao walikusudia kutokujitia madoa na mambo maovu, walidumu katika Imani yao pasipo kujali mateso waliyoyapitia, walidumu katika upendo, na uvumilivu wa hali ya juu, na wenye bidii katika kujisafisha kila siku, wakihama kutoka utukufu hata utukufu na zaidi ya yote walikuwa na bidii sana ya kumtumikia Mungu(huduma), wakihubiri huku na kule mpaka kufikia Bwana kuwaambia matendo yao ya mwisho yamezidi yale ya kwanza, (je na sisi tunaweza tukafika hatua ya kuambiwa hivyo?)
Lakini pamoja na kwamba watu wa kanisa hilo ni watu waliokuwa na bidii nyingi na upendo na uvumilivu na subira lakini Bwana alikuwa na Neno moja juu yao ambalo ndilo lililomfanya aonekane mbele zao kama "mwenye macho kama mwali wa moto"...Unaona hapo na sisi tunaweza tukawa tunafanya mema na bidii lakini Bwana bado akawa na Neno juu yetu..tusome..
"20 Lakini nina neno juu yako, ya kwamba WAMRIDHIA YULE MWANAMKE YEZEBELI, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu.21 Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake.22 Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake;23 nami nitawaua watoto wake kwa mauti. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake".
Tunaona pamoja na kwamba kanisa hili lilitenda mema mengi kiasi cha kusifiwa lakini kilionekana kikwazo ndani yao na hicho si kingine zaidi ya yule MWANAMKE YEZEBELI kama tunavyomsoma.
YEZEBELI NI NANI?
Yezebeli tunamwona katika agano la kale alikuwa ni mke wa mfalme Ahabu wa Israeli. Kumbuka mwanamke huyu hakuwa binti wa kiyahudi, bali Ahabu alimtoa katika mataifa ya kipagani,(huko Lebanoni) ingekuwa heri kama angebadilishwa imani yake na kuwa myahudi kama ilivyokuwa kwa Ruthu, lakini haikuwa hivyo kwake, yeye alitoka huko nchi za mataifa ya kipagani, akiwa na dini yake, ya kuabudu miungu mingi pamoja na Baali, na kibaya zaidi hakuja peke yake, bali alikuja na manabii wake wengi wa kumsaidia kufukiza uvumba kwa miungu yake akiwa Israeli hivyo akawa kikwazo kikubwa kwa Israeli kwasababu hakufanya hizo ibada za sanamu peke yake bali pia aliwafundisha na kuwalazimisha watu wote hata wale waliokataa kuiabudu miungu yake kufanya hivyo (1Wafalme 19).
Hivyo Bwana alilifananisha hili kanisa la Thiatira na Israeli kipindi cha Mfalme Ahabu. Kumbuka tafsiri ya neno THIATIRA ni "MWANAMKE ANAYETAWALA"..Hivyo kama Israeli kwa wakati ule kulikuwa na mwanamke anayetawala Yezebeli, Kadhalika na katika kanisa hilo yupo mwanamke anayetawala mwenye tabia zinazofananishwa na za Yezebeli. Na huyu si mwingine zaidi ya “KANISA KATOLIKI”., mwanamke huyu huyu tunamwona pia katika ile sura ya 17, ambayo tutakuja kuzisoma kwa undani habari zake hapo baadaye, ..
Ufunuo 17: 3 "Akanichukua katika Roho hata jangwani, nikaona MWANAMKE, ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, mwenye kujaa majina ya makufuru, mwenye vichwa saba na pembe kumi.
4 Na mwanamke yule alikuwa amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake.
5 Na katika kipaji cha uso wake alikuwa na jina limeandikwa, la siri, BABELI MKUU, MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI.
6 Nikamwona yule mwanamke amelewa kwa damu ya watakatifu, na kwa damu ya mashahidi wa Yesu. Nami nilipomwona nikastaajabu ajabu kuu. "
Sasa kumbuka kwenye lile kanisa la kwanza, shetani alianza kujipenyeza kama "matendo ya wanikolai", na katika kanisa la tatu na kuendelea akakomaa yale matendo yakabadilika na kuwa "mafundisho" ..Tunaona pia roho ile ile iliyokuwa kwa wanikolai ndio hiyo hiyo ilitenda kazi kwa Balaamu katika kanisa la tatu, na ndiyo hiyo hiyo inatenda kazi ndani ya Yezebeli katika Kanisa hili la Nne. Konstantini alisimama kama Balaamu, na Kanisa Katoliki linasimama kama mwanamke Yezebeli. Nao wote hawa ukiangalia kazi yao ilikuwa ni moja ni kuwakosesha watu wa Mungu wazini na kula vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu. Hivyo Kanisa katoliki liliwakosesha watakatifu wa wakati ule wamkosee Mungu kwa kufanya uasherati wa kiroho. Na uasherati wenyewe ni upi?. Ni dhahiri kuwa waliyapokea mafundisho mengine ambayo hawakukabidhiwa na Mungu tangu awali kupitia mitume wake watakatifu kwa kulichanganya Neno la Mungu na desturi za kipagani, kwamfano ibada za sanamu, kuomba kwa wafu, ibada za miungu mitatu, sala za mapokeo ya kipagani, ubatizo wa vichanga n.k.
Hivyo pamoja na kwamba walikuwa ni watakatifu, wanajitahidi kufanya mambo mema, na kutenda kazi ya Mungu kwa bidii lakini bado Mungu alikuwa anaona kasoro ndani yao, kwamba WAMEMRIDHIA yule mwanamke Yezebeli. Maana ya "kuridhia" ni kuvumilia / kukubaliana /kuchukuliana naye..Hivyo wale watakatifu wa kipindi hicho waliopewa macho ya kumtambua kwa kupitia Mjumbe wa Mungu aliyemteua kwa wakati huo (KOLUMBA) walimridhia yule mwanamke na kuchukuliana na mafundisho yake. Hivyo Bwana akawaonya watubu na kwamba wasipotubu atawaua kwa mauti na makanisa yote ndipo yatakapojua ya kuwa Bwana anachunguza viuno(fahamu za watu) na mioyo ya watu wote, kwamba yale macho yake yaonayo mpaka sirini na hakuna jambo lolote linalositirika kwake!
Kanisa Katoliki nalo Bwana alilipa muda wa kutubu, lakini halikutaka kutubu, kama tulivyoona hapo juu, hata hivyo (Yeremia 51: 9 ilishatabiri habari zake na kusema ..“Tungependa kuuponya Babeli, Lakini haukuponyeka; Mwacheni, nasi twendeni zetu, Kila mtu hata nchi yake mwenyewe; Maana hukumu yake inafika hata mbinguni, Nayo imeinuliwa kufikilia mawinguni. "
Na ndio maana Bwana Yesu alisema .." 21 Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake.
22 Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake;
23 nami nitawaua watoto wake kwa mauti. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake. "
Kumbuka Yezebeli alikuwa anao watoto, na mmoja wapo aliitwa "ATHALIA" (2Wafalme 9). Huyu naye alienda kuolewa na Mfalme wa Yuda na mambo yale aliyoyafanya mama yake aliyafanya na yeye vilevile na mabaya kuliko hayo. Aliutwaa ufalme kwa nguvu,na kutawala Israeli kwa muda wa miaka 7 jambo ambalo lilikuwa ni machukizo makubwa kwa Israeli taifa la Mungu kutawaliwa na mwanamke. Alidiriki pia kuuangamiza uzao wa Daudi kwa kuwaua wazao wote wa kifalme lakini mpango wake haukufanikiwa. Na zaidi ya yote aliwakosesha watu wa Yuda kama mama yake alivyowakosesha watu wa Israeli kwa kuabudu miungu migeni.
Hivyo kama Yezebeli alivyokuwa na binti anayefanana na yeye kitabia kadhalika Kanisa Katoliki (Yezebeli wa rohoni), amezaa mabinti wanaofanana na yeye kitabia na ndio maana anajulikana kama mama wa makahaba, na mabinti zake ni madhehebu yote yanayofanana na yeye. Na watu wanaoshikamana nayo Bwana atakuja kuwaua kwa mauti ( katika lile Ziwa la moto.)
Tukiendelea kusoma mistari inayofuata....
"24 Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wo wote wasio na mafundisho hayo, wasiozijua FUMBO ZA SHETANI, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine.25 Ila mlicho nacho kishikeni sana, hata nitakapokuja”.
Unaona hapo? Bwana anasema kuna watu wasiojua "FUMBO ZA SHETANI" na walikuwa katikati ya kundi la Mungu..Hivyo shetani naye anazo fumbo zake, nazo zinahitaji hekima kuzitambua. Ikiwa na maana kuwa anajua namna ya kumdanganya mtu kulingana na jinsi anavyoenenda, ukiwa ni mwovu atakudanganya kwa njia ya uovu, na ukiwa mtakatifu atakuja kwa kivuli cha utakatifu. na ndio maana biblia inasema yule mwanamke jina lake limeandikwa kwa SIRI, kumbuka sio kwa wazi bali kwa siri, BABELI MKUU MAMA WA MAKAHABA, NA MACHUKIZO YA NCHI.. Hapo ndipo kiti cha enzi cha shetani kilipo..Yeye pamoja na watumishi wake wanajigeuza kuwa kama malaika na watumishi wa nuru. Hivyo ni kujichunguza na kujihakiki kila siku je! tupo kwenye NENO? hiyo ndiyo njia pekee ya kulifumbua fumbo la shetani na kumshinda. Lakini tukipuuzia mambo kama hayo yatatukuta kama hayo ya kanisa la Thiatira Bwana atatuua kwa mauti.
Unakumbuka watu wa kanisa hili waliambiwa matendo yao mema yamezidi hata yale ya kwanza, walijitahidi sana kuwa wakamilifu lakini walikosa kuzitambua mbinu za shetani, Kadhalika na sisi wa kanisa la mwisho tulilopo, Yule mwanamke YEZEBELI na MABINTI zake wapo, na wanazidi kuwakosesha watu na kuwapeleka mamilioni ya watu kuzimu (hususani wakristo), Kwahiyo kiini cha ujumbe ambao Bwana alikuwa anataka kuwaambia ni kwamba katika ukamilifu na utakatifu wao waongezee tu kumtoa yule mwanamke kahaha na uzinzi wake katikati yao kwa kutokuridhia mafundisho yake, na sisi vivyo hivyo katika bidii yetu yote tuliyonayo kwa Mungu katika upendo subira, uvumilivu, huduma tumalizie kwa kujitenga na yule kahaba Babeli mkuu (Katoliki) pamoja na mabinti zake wote (madhehebu).
Ufunuo 18:4 "Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, ENYI WATU WANGU, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.
5 Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake".
Kwahiyo wote walioshinda katika kanisa hilo kwa kujitenga na yule mwanamke Yezebeli na kudumu katika Neno Bwana aliwaahidia thawabu..
" 26 Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa,27 naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyanzi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea kwa Baba yangu.28 Nami nitampa ile nyota ya asubuhi.29 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. "
Thawabu hizi ni katika ulimwengu unaokuja, Bwana atakapokuwa MFALME WA WAFALME, ni dhahiri kuwa atatwaa wafalme wachache chini yake ili yeye awe Mfalme wa Wafalme na ndio watakaokuwa watu wa kanisa hili, hawa ndio watakaopewa mamlaka juu ya mataifa, na hiyo fimbo ya chuma itakuwa ni kutoa amri na kutekelezwa. Na ile nyota ya asubuhi ina maana kuwa utukufu wao utakuwa ni wa kipekee tofauti na wengine, kumbuka nyota ya asubuhi ndio nyota pekee yenye kuangaza hata wakati wa mchana, wakati nyingine nguvu zao za kung'aa zinakuwa ni usiku tu. Hivyo kule katika mbingu mpya na nchi mpya watang'aa milele na milele pamoja na Bwana Yesu. Hivyo ndugu kwanini ukose mambo hayo yote mazuri?..Tafuta kwanza ukamilifu (UTAKATIFU) mpe Bwana maisha yako leo, kisha malizia kwa kujitenga na yule mwanamke kahaba, na mabinti zake kwa kudumu katika NENO LA MUNGU TU!.na sio katika mapokeo na dini.
Ubarikiwe sana.
Tafadhali "share" kwa wengine ujumbe huu, na Mungu atakubariki. Usikose mwendelezo huu wa kitabu cha Ufunuo.
No comments:
Post a Comment