"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, July 10, 2018

KITABU CHA UKUMBUSHO


Yapo maswali kadha wa kadha umekuwa ukijiuliza kama mkristo (tukisema mkristo tunamaanisha mtu aliyegeuka na kudhamiria kwa gharama zake zote kubeba msalaba wake na kumfuata Kristo). Wakati mwingine unajikuta aidha ndani ya moyo wako au nje na maswali unayokosea majibu!!.

Kwamfano pengine unasema tangu nilipompa Bwana maisha yangu ni kweli ndani ya moyo wangu nilipata amani kubwa ya ki-Mungu lakini nje! Naona mambo mengi hayapo sawa, nilipojaribu kuishi maisha matakatifu marafiki na ndugu wakanitenga , nilipojaribu kuacha usengenyaji ndipo nilipoanza kuonekana mbele ya marafiki zangu ninajidai, nilipoacha rusha ndipo visa vikainuka kazini na kupelekea kuongeza idadi ya watu wanichukiao, niliposaidia watu badala ya kupokea shukrani ndio napokea lawama, nilipoanza kufunga na kuomba badala ya matatizo kupungua ndio yaliendelea kuwa vile vile, nilipoanza kufanya kazi ya Mungu ndipo matatizo ya kiuchumi yakanyanyuka zaidi,

Mpaka unafikia hatua ya kusema mbona huku kuishi maisha ya kujinyima na mambo ya dunia hakuna faida yoyote ninayoipata, zaidi ya kuwa vile vile tu siku zote!, mbona wale wasiomcha Mungu wana raha siku zote, ni matajiri pamoja na kwamba wanamkana Mungu, wanazidi kufanikiwa katika mambo yao,mbona wazinzi ndio wanao afya nzuri?. Mimi pamoja na utakatifu wangu wote na wema wangu wote, Mungu kama hanioni na kunipa raha kama hao wengine, japo ninafanya mema kushinda wao?, kwani ni laana gani ninayo hadi yanipate hayo yote, au wao wana kitu gani cha ziada cha kushinda mimi mpaka wao wayapate hayo yote?,..Kumbuka Hayo ni mawazo yaliyopo ndani ya watakatifu wengi wa Mungu, Hata Daudi naye pia alizungumza maneno kama hayo tusome katika:
Zaburi 69: 7 “Maana kwa ajili yako nimestahimili laumu, Fedheha imenifunika uso wangu.
8 Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, Na msikwao kwa wana wa mama yangu.
9 Maana wivu wa nyumba yako umenila, Na laumu zao wanaokulaumu zimenipata.
10 Nilipolia na kuiadhibu roho yangu kwa kufunga, Ikawa laumu juu yangu.
11 Nilipofanya gunia kuwa nguo zangu, Nikawa mithali kwao.
12 Waketio langoni hunisema, Na nyimbo za walevi hunidhihaki”.
 
Zaburi 73:1 "Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli, Kwa hao walio safi mioyo yao.
2 Nami miguu yangu ilikuwa karibu na kupotoka, Hatua zangu zilikuwa karibu na kuteleza.
3 MAANA NALIWAONEA WIVU WENYE KUJIVUNA, NILIPOIONA HALI YA AMANI YA WASIO.4 Maana hawana maumivu katika kufa kwao, Na mwili wao una nguvu.
5 Katika TAABU YA WATU HAWAMO, Wala hawapati mapigo pamoja na wanadamu.
6 Hivyo kiburi kimekuwa mkufu shingoni mwao, Jeuri huwavika kama nguo.
7 Macho yao hutokeza kwa kunenepa, Wameipita kadiri ya mawazo ya mioyo yao.
8 Hudhihaki, husimulia mabaya, Husimulia udhalimu kana kwamba wako juu.
9 Wameweka kinywa chao mbinguni, Na ulimi wao hutanga-tanga duniani.
10 Kwa hiyo watu wake hugeuka huko, Na maji yaliyojaa humezwa nao.
11 Nao husema, Mungu ajuaje? Yako maarifa kwake aliye juu?
12 Fahamu, ndivyo walivyo wasio haki, Na kwa kustarehe sikuzote wamepata mali nyingi”.

Zaburi 42: 3 “Machozi yangu yamekuwa chakula changu mchana na usiku, Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako”.

Kama tunavyosoma Daudi pamoja na wema wake wote wa kuwaombea watu wengine fadhili mbele za Mungu kwa kufunga na wakati mwingine kwa machozi lakini bado alionekana kuwa kama ni kituko na mgeni mbele zao. Mpaka kufikia hatua ya kuwaonea wivu watu waovu.

Kadhalika na mambo haya haya yanawazwa na watakatifu walioko leo duniani , Wanasema aidha kwa midomo yao au kwa mioyo yao: Mungu wetu yuko wapi? Mbona hatuoni faida yoyote ya kumtumikia, mbona hatuoni faida yoyote ya kuacha kuvaa vimini, hereni, suruali, kuacha kupaka lipstick na wigi, wale wanaoendelea kufanya hivyo hao ndio wanaolewa kwa harusi nzuri, wana watoto wazuri lakini mimi bado nipo vile vile tu!.Utasema mbona sioni faida yoyote ya kuacha pombe na sigara, mbona sioni faida yoyote ya kuacha uasherati, disco, anasa,na kucheza kamari na ku-bet, wenzangu wanafanikiwa kirahisi mimi nipo vile vile tu, Mbona sioni faida yoyote ya kuacha kula rushwa, zile pesa nilizokuwa ninapata mwanzoni sizioni tena nikizipata sasahivi, wale wenzangu tuliokuwa tunakula nao rushwa zamani wanazidi kunawiri na kusomesha watoto wao na kujenga majumba makubwa na mimi nimebaki katika hali ile ya kawaida tu!.n.k.

Haya yote yamekuwa ni maswali ya WATAKATIFU tangu zamani, Lakini Bwana naye aliyasikia na kuyatolea majibu yake: Kama tunavyosoma katika Malaki 3 Bwana anasema.

Malaki 3:13 “Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno juu yako kwa namna gani?
14 MMESEMA, KUMTUMIKIA MUNGU HAKUNA FAIDA; na, TUMEPATA FAIDA GANI KWA KUYASHIKA MAAGIZO YAKE, NA KWENDA KWA HUZUNI MBELE ZA BWANA WA MAJESHI? 15 Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao.
16 Ndipo wale waliomcha Bwana waliposemezana wao kwa wao. NAYE BWANA AKASIKILIZA, AKASIKIA; na KITABU CHA UKUMBUSHO KIKAANDIKWA MBELE ZAKE KWA AJILI YA HAO WAMCHAO BWANA, NA KULITAFAKARI JINA LAKE.
17 Nao watakuwa wangu, asema Bwana wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; naam, watakuwa hazina yangu hasa; nami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye.
18 Ndipo mtakaporudi, nanyi mtapambanua kati ya wenye haki na waovu, na kati ya yeye amtumikiaye Mungu na yeye asiyemtumikia”.

Unaweza ukaona hapo?. Hakuna wema wowote wa mtakatifu atakaoufanya ukapita bure bure tu! , mbinguni kuna KITABU CHA KUMBUKUMBU kimewekwa kwa watu maalumu, kinarekodi mambo yote mema watakatifu wanayoyafanya kila siku huku duniani. Na kama ni kitabu basi inaamanisha ili kiwe kitabu kamili ni lazima kiwe na kurasa nyingi na sio chache, na kitabu hichi cha watakatifu, ni matendo mema tu ndio yanayoandikwa huko, na sio kingine. Kwahiyo wingi wako wa kumcha Mungu na matendo yako mema mbele za Mungu kila siku yanarekodiwa katika kitabu kile na ndio yatakayoelezea wingi wa thawabu utakazopewa mbinguni katika siku ile ya mwanakondoo.

Hivyo ndugu/dada ukiwa ni mkristo kweli kweli uliyedhamiria kusimama katika Imani huu sio wakati wa kudhani kumtumikia hakuna faida yoyote,Faida zipo nyingi sana utazijua kwa marefu na mapana utakapofika katika urithi uliowekewa na Mungu wako. Mambo ya ulimwengu huu sio urithi wetu, wewe upate usipate, uwe tajiri uwe maskini, uwe una afya usiwe na afya, vyovyote wewe endelea kumcha Mungu bila kujali lolote lile ukijua siku ile ni Mungu wako aonaye taabu yako ndiye atakayekulipa, maadamu unajiona upo sawa na Mungu wako usikwamishwe na kitu kingine chochote,songa mbele! endelea kuliweka Kumbukumbu lako sawa mbinguni, usidanganyike na mafundisho ya watumishi bandia kwamba kuwafanikiwa au kutokufanikiwa kifedha ndio uthibitisho kwamba Mungu yupo na wewe au Mungu amekuacha, hapana uthibitisho pekee ni maisha unayoishi ya kumpendeza Mungu wako sikuzote, kwasababu kitabu cha kumbukumbu kipo mbinguni.

Ongeza bidii, ikiwa umekataa rushwa endelea kuipinga, ukiwa umekataa uasherati endelea kufanya hivyo kwa bidii zaidi, ikiwa umekataa kuenenda kama mfano wa watu wa ulimwengu huu kuvaa vimini, suruali endelea hivyo hivyo kumbukumbuku lako kila siku linawekwa na thawabu yako ya siku haitapita bure..Bwana aliyeumba macho anaona yote!. Lakini ukisema nitafanya hivyo nikifika umri fulani au wakati fulani, hujui kesho yako itakuwaje, na utakosa kumbukumbuku bora siku ile wakati wenzako wanafarijiwa kwa mambo mazuri yasiyoelezeka ya umilele na wewe haupo.Usiwaige watu waovu katika njia zao?

Na ni kwasababu gani Mungu anaruhusu waovu wafanikiwe sasa? .
Ni kwasababu urithi wao upo katika dunia ya sasa iliyoharibika na hawana sehemu yoyote katika urithi katika ulimwengu unaokuja. Hivyo faraja yao ipo katika mambo ya ulimwengu wa sasa kule hawana sehemu ndio sababu Bwana karuhusu wapate faraja yao hapa.

Bwana alimwambia Daudi..Zaburi 92:7 “WASIO HAKI WAKICHUPUKA KAMA MAJANI NA WOTE WATENDAO MAOVU WAKISTAWI. NI KWA KUSUDI WAANGAMIZWE MILELE”
 
Kwahiyo sababu pekee ya waovu kufanikiwa sio kwasababu wanampendeza Mungu, ni ili waangamizwe milele, je! Na wewe unapenda kuwa miongoni mwao?, unafanikiwa katika rushwa yako ili uje uangamizwe milele?, unafanikiwa katika uasherati wako,na ulevi wako, na biashara yako haramu ili uje uwe miongoni mwa hao watakaoangamizwa milele? Unafanikiwa katika utapeli wako na kamari yako na betting yako, ili uje uangamie milele?? Biblia inasema ITAKUFAIDIA NINI UPATE ULIMWENGU MZIMA, NA KUPATA HASARA YA NAFSI YAKO?, itakufaidia nini uonekane ni wakisasa kuliko watu wote duniani, kwa kujichora, kwa kuvaa vimini, na suruali na mawigi na kisha upate hasara ya nafsi yako? Ndugu KUMBUKUMBU LA WENYE HAKI LINAANDIKWA MBINGUNI kamwe usitamani mambo yao wala njia zao, kama hujampa Kristo maisha yako ni vema ukafanya hivyo sasa angali wakati upo, kabla mlango wa Neema haujafungwa.
 
Mungu akubariki.

Tafadhali “share” kwa wengine ujumbe huu, na Mungu atakubariki.

No comments:

Post a Comment