"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, July 13, 2018

MASWALI NA MAJIBU:SEHEMU YA 32

 SWALI 1: Je! Ni sahihi kwa mkristo kuoa/kuolewa na mtu wa imani nyingine?.

JIBU: Kwanza sio sahihi kwa mtu aliyeamini kwenda kutwaa mke au mume asiye wa imani yake ya kikristo, kwasababu moja tu! nayo ni KUEPUKA KUGEUZWA MIOYO!..

Kumbuka jambo mojawapo ambalo Mungu aliwakanya sana wana wa Israeli hata kabla ya kufika nchi ya Ahadi ni suala la kuoa/kuolewa na watu wa jamii nyingine tofauti na wayahudi, na sio kwasababu labda ni wabaya, au hawavutii hapana, ni kwasababu moja tu! Watageuzwa mioyo yao wasiambatane na Mungu wa Israeli kinyume chake wataambata na miungu migeni. Na Mungu siku zote ni Mungu mwenye wivu!.

Tukisoma Nehemia 13:25 “………… nikawaapisha kwa Mungu, nikasema, Msiwaoze wana wao binti zenu, wala msiwatwae binti zao ili waolewe na wana wenu, wala na ninyi wenyewe.
26 Je! Sulemani, mwana wa Daudi, hakufanya dhambi kwa kutenda hayo? Lakini katika mataifa mengi hapakuwa na mfalme mwingine mfano wake. Tena alipendwa na Mungu wake, naye Mungu akamfanya mfalme juu ya Israeli; walakini WANAWAKE WAGENI WALIMKOSESHA HATA YEYE.
27 Basi, na sisi, je! Tuwasikilize ninyi kutenda neno hili baya, hata kumhalifu Mungu wetu kwa kuwaoa wanawake wageni?.

Unaona hapo? Mfalme Sulemani pamoja na hekima zake zote nyingi za kuweza kupambanua mambo lakini aligeuzwa moyo, na wale wanawake wa mataifa mpaka kufikia hatua ya kuivukizia uvumba miungu migeni, Unadhani itashindanaje kwa mkristo mwingine yeyote wa kawaida?.
Unaweza ukasema aa! Mimi nitaweza kumtawala, lakini hilo haliwezekani Mungu sio mwongo, akisema atakugeuza, ni kweli atakugeuza,.Mwanzoni utaona kama inawezekana lakini mwisho wa siku utajikuta unaangukia katika shimo kama Sulemani.

Vivyo hivyo ukimsoma Mfalme Ahabu alikoseshwa na Yezebeli mchawi, Samsoni naye alikoseshwa na Delila. Wote hawa wake zao walikuwa ni wanawake wa kimataifa n.k.

Kwahiyo unapokuwa mkristo unapaswa umtafute mtu mwenye imani moja na yako ya kikristo, au kama sio basi umgeuze kwanza amgeukie Kristo ndipo umuoe au uolewe naye, vinginevyo utakuwa unajiweka mwenyewe katika hali ya hatari kubwa ya kumkosea Mungu, na kuishia katika majuto…

Lakini kama ikitokea mlishaoana tayari huko nyuma na mtu mwingine kabla wewe hujawa mkristo, na wewe baadaye ukaja kuamini na Yule mpenzi wako hajaamini lakini bado anaona vema kuishi na wewe hapo biblia inasema haupaswi kumuacha, unatakiwa ukae naye katika hali yake hiyo hiyo pengine wakati ukifika kwa matendo yako mema ya kikristo yatambadilisha na yeye naye aamini…Lakini kama akichukizwa na uamuzi wako wa wewe kuwa mkristo na anataka kuondoka…Hapo haufungiki, anaweza kwenda, na biblia inaruhusu kutwaa mke/mume mwingine ila katika Bwana tu ambaye ni mkristo mwenye imani moja na wewe.

Soma. 1Wakoritho 7: 12 “Lakini watu wengine nawaambia mimi, wala si Bwana, ya kwamba iwapo ndugu mmoja ana mke asiyeamini, na mke huyo anakubali kukaa naye asimwache.
13 Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe.
14 Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe; kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi; bali sasa ni watakatifu.
15 Lakini yule asiyeamini akiondoka, na aondoke. Hapo huyo ndugu mume au ndugu mke hafungiki. Lakini Mungu ametuita katika amani.
16 Kwa maana wajuaje, wewe mwanamke, kama utamwokoa mumeo? Au wajuaje, wewe mwanamume, kama utamwokoa mkeo?”

Kwahiyo hairuhusiwi kuoa mtu ambaye sio wa IMANI moja nawe kulingana na maandiko.


 SWALI 2: Manabii walisema “Neno la Mungu likanijia” ..nataka kufahamu hili Neno liliwajiliaje?.

JIBU: Kujiliwa na Neno la Mungu ni sawa sawa na kufunuliwa ujumbe unaomuhusu mtu au jamii fulani, na ujumbe huu Mungu anamshushia mtu aidha kwa njia ya ndoto, au maono, au sauti, au kutembelewa na malaika, au njia nyingine yoyote ya ki-Mungu.

Kwahiyo unaposoma mahali popote kwenye biblia,unakutana na sehemu inasema Neno la Mungu lilimjia Isaya, au Yeremia au Yona, hap ni sawa na kusema, ujumbe utokao kwa Mungu umemfikia Isaya, au Yeremia au Yona awapelekee watu.

Kadhalika hata sasa hivi Neno la Mungu, huwa linawajilia watu kwa njia mbalimbali, mt anapofunuliwa Neno lolote kwa njia ya ndoto, au maono au kuzuriwa na malaika, au katika biblia, na Neno hilo limebeba ujumbe wa kwenda kuwapelekea watu wengine, hiyo ni sawa tu na Neno la Mungu limemjia mtu huyo.

Kadhalika unaposikia ndani wito wa kwenda kuwashuhudia wengine habari njema, hapo ni sawa na lile Neno linalosema “Marko 16:15 Enendeni ulimwenguni kote mkahubiri injili kwa kila kiumbe ” limekujia, hivyo unapaswa ukauwasilishe huo ujumbe kwa wakati.

Na kuna hatari za kutokutii Neno la Mungu linalokujia, na hatari zenyewe ndio kama zile zilizompata Nabii Yona na zile alizoonywa Nabii Ezekieli zikisema..

Ezekieli 3: 17 “Mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi wa nyumba ya Israeli; basi, sikia neno hili litokalo katika kinywa changu, ukawape maonyo haya yatokayo kwangu.
18 Nimwambiapo mtu mbaya, Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.
19 Lakini ukimwonya mtu mbaya, wala yeye hauachi ubaya wake, wala njia yake mbaya, atakufa katika uovu wake; bali wewe umejiokoa roho yako.
20 Tena mtu mwenye haki aiachapo haki yake, na kutenda uovu, nami nikiweka kikwazo mbele yake, atakufa; kwa sababu hukumwonya, atakufa katika uovu wake, wala matendo yake ya haki aliyoyatenda hayatakumbukwa; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. “

SWALI 3: Habari nilikuwa naomba unifafanulie maandiko kutoka katika Marko 2:2-12 Kwanini pale Bwana Yesu alichukua hatua ya kusamehe dhambi kwanza badala ya kumponya yule kiwete?.

JIBU: Ubarikiwe dada tuisome kwanza habari yenyewe..

Marko 2: 1 “Akaingia Kapernaumu tena, baada ya siku kadha wa kadha, ikasikiwa ya kwamba yumo nyumbani.
2 Wakakusanyika watu wengi, isibaki nafasi hata mlangoni; akawa akisema nao neno lake.
3 Wakaja watu wakimletea mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne.
4 Na walipokuwa hawawezi kumkaribia kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo; na wakiisha kuivunja wakalitelemsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza.
5 Naye Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.
6 Na baadhi ya waandishi walikuwako huko, wameketi, wakifikiri mioyoni mwao,
7 Mbona huyu anasema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu?
8 Mara Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi mioyoni mwenu?
9 Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende?
10 Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza),
11 Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako uende nyumbani kwako.
12 Mara akaondoka, akajitwika godoro lake, akatoka mbele yao wote; hata wakastaajabu wote,wakamtukuza Mungu, wakisema, Namna hii hatujapata kuiona kamwe”

.....Kama ukichunguza utaona kuwa jambo la kwanza Bwana aliloliona ni ile Imani yao kwake, aliona ndani yao walikuwa na kitu cha ziada zaidi ya imani ya kuponywa, nayo ni Imani kwa Yesu Kristo.....Na tunajua kitu cha kwanza kilichomleta Bwana Yesu duniani ni kuokoa dhambi za watu, na vitu vingine baadaye… Ukisoma Yohana 8:24 Bwana aliwaambia makutano ..“Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu”....Unaona hapo?...Inakupasa uamini kwanza. Na ndio maana jambo la kwanza alilolitamka yeye kama mkuu wa uzima wa roho za watu mara baada ya kuona Imani yao kwake, akamwambia yule aliyekuwa amepooza..UMESAMEHEWA DHAMBI ZAKO…..Ni Neno zuri na la neema kiasi gani!!!

Lakini wale wengine mawazo yao yalikuwa tofauti, wao walitazamia tu, Bwana amponye yule mtu kisha amwambie nenda zako, halafu yule mtu akaendelee kuishi maisha ya dhambi kisha mwisho wa siku afe aishie kupata hasara ya nafsi yake!..na uponyaji wake wa mwili usimfaidie kitu baada ya maisha ya hapa.

Sasa Ukiendelea kusoma pale utaona Bwana anawauliza tena wale watu, Marko 2:9 “Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende?, Sasa kwa namna ya kawaida kwa mtu mwenye akili za rohoni atagundua kuwa ni afadhali usipone ugonjwa wako, lakini dhambi zako ziwe zimesamehewa…kuliko kuponywa halafu dhambi zako ziendeleee kubaki! Na ndio maana Bwana alimchagulia fungu lililo jema la kusamehewa dhambi zake kwanza, kisha baadaye amponye…

Na ndivyo tunavyopaswa na sisi kama wakristo kufanya sasahivi, tunakimbilia kuwaombea watu magonjwa ,wapokee miujiza, na mafanikio na huku tunasahamu kuwafundisha watu habari za msamaha wa dhambi ambao ndio msingi wa Imani ya kikristo.. vyepesi ni vipi??? Ni heri tukamuhubirie mtu habari za msamaha na toba, aokolewe roho yake hata kama hatapokea uponyaji kuliko kuhubiri kila siku mimbarani miujiza na uponyaji na huku bado watu wanakufa katika dhambi zao. Au ni afadhali kufanya vyote kuliko kutupilia mbali habari za msamaha wa dhambi, na kushikamana na miujiza tu.

Ubarikiwe dada.

No comments:

Post a Comment