"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, October 25, 2018

MAISHA YETU NI MILKI YA YESU KRISTO.

Kanisa linafananishwa na mwanamke, Bwana ndio kapenda kulifananisha kanisa lake na mwanamke, akifunua kwamba kama vile mwanaume ampendavyo mkewe ndivyo Kristo anavyolipenda kanisa lake. Na kama ijulikanavyo huwa kuna hatua zinafuatwa kabla ya mwanamume kumtwaa mwanamke awe mkewe, na moja ya hatua muhimu sana inakuwa ni MAHARI. Mahari kazi yake ni kumwongezea ujasiri mwanamume kwamba hakumpata mke wake kirahisi, amemgharimia. Na baada ya kulipa mahari ,ni ndoa kufungwa,hapo Yule mwanamke anahama kwao na kuhamia kwa mume wake, na zaidi ya yote jina lake la ukoo linabadilika, Jina la ukoo linabadilika kuonyesha kwamba kuanzia huo wakati na kuendelea yeye sio milki ya ukoo wa wazazi wake tena, bali anakuwa milki ya ukoo mwingine wa mume wake.

Sasa Bwana aliruhusu huo utamaduni uendelee kuwepo mpaka leo katikati ya wanadamu, ili kuufanya wokovu ueleweke kirahisi kwetu, kwa kulinganisha namna mwanamke anavyotwaliwa kutoka kwa wazazi wake, mpaka anapotolewa mahari, mpaka anapokuwa mke halali wa mwanaume tutapata picha namna kanisa la Kristo navyo lilivyotawaliwa kutoka katika dunia.


Hatua ya kwanza Kristo anawahubiria watu wake watoke katika ulimwengu kwa ishara na miujiza mingi, kama vile mwanamume amshawishivyo mwanamke katika hatua za awali, kisha baada ya hapo Bwana Yesu ni kulipia mahari, na Mahari anayolipa ni damu yake aliyoimwaga pale Golgotha ambapo alitoa nafsi yake kama fidia kwa mkewe (YAANI KANISA), Gharama hii aliyoingia ilimfanya yeye awe na uhalali wa kulimiliki kanisa asilimia 100%.

Na hatua ya mwisho ni mtu kubadilishwa jina na kupewa jina lipya la mumewe, kama vile jina la mwanamke la ukoo linavyobadilika na kuhamia moja kwa moja kwa mumewe. Sasa mwanamke au mwanamume asipopitia hatua zote hizo ndoa yeke inakuwa sio halali.

Sasa mimi na wewe, ili kwamba tuweze kuwa wake halali wa Bwana wetu Yesu Kristo, sharti lazima tukubali kumwamini na kumgeukia yeye na kuacha wazazi wetu waliotuzaa, yaani kuuacha ulimwengu na mambo yake yote, sharti lazima tumtii kwa kutubu na kumaanisha kabisa kuacha dhambi na maisha ya nyuma ya anasa na kufanyika viumbe vipya.

Kisha hatua inayofuata baada ya kumkubali Yesu moyoni mwetu, Ni Bwana Yesu mwenyewe kutusafisha kwa maji na kwa damu kwa gharama aliyoingia pale Golgotha, Na ndio maana pale Golgotha wale askari wa kirumi walipomchoma mkuki ubavuni, kulitoka maji na damu, ambayo ile ni kama ishara ya mahari kwetu, kwamba tunasafishwa kwa maji na damu.
1 Yohana 5: 6 Huyu ndiye aliyekuja KWA MAJI NA DAMU, Yesu Kristo; si katika maji tu, bali katika maji na katika damu. Naye Roho ndiye ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli”.

Hatua hii inamfanya mtu kuwa mke halali aliyetwaliwa kwa gharama, Bwana anakusafisha dhambi zako zote, na kukuweka kuwa huru na dhambi. Na Neno lake ndio maji yanayotusafisha na Neno lake linasema...
Matendo 2: 37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, TUBUNI MKABATIZWE KILA MMOJA KWA JINA LAKE YESU KRISTO, MPATE ONDOLEO LA DHAMBI ZENU, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu”.

Unaona hapo? namna mke halali wa Yesu Kristo anavyoandaliwa?...sio kwa kujiunga na dhehebu au kanisa bali ni kwa KUTUBU, Na KUBATIZWA KATIKA JINA LA YESU KRISTO, na kupokea kipawa cha Roho. Na kuanzia huo wakati jina lako linabadilika, na kuitwa Mkristo au wa-Yesu Kristo. Kwasababu umebatizwa kwa hilo jina, na Huwezi kuwa mkristo kama hujapitia hizo hatua.


Huwezi kuitwa wa Yesu Kristo kama haujabatizwa kwa hilo jina, sehemu zote kwenye maandiko watakatifu walibatizwa kwa hilo jina, yaani jina la Yesu, ukisoma mistari ifuatayo utaona jambo hilo {Matendo 2:38. Matendo 8:12, Matendo 8:16, Matendo 10:48 na Matendo 19:5}


Kwahiyo kama tu mwanamke aliyeolewa,anakuwa hawezi kujiamulia tu mambo, kwamba anaweza akalala popote atakapo, au akafanya chochota atakacho juu ya mwili wake, bali anakuwa ameingia kama kwenye kifungo Fulani, ambacho hakimpi uhuru wa kuwa na mahusiano ya karibu na kila mtu. Vivyo hivyo na kwa mkristo aliyempa Bwana maisha yake kwa kutubu na, na kubatizwa kwa jina lake Yesu Kristo, anakuwa ni milki halali ya Yesu Kristo, hana ruhusa ya kujiamulia mambo tu, au kufanya chochote anachojisikia akiwa katikati ya mahusiano yake yeye na Bwana.. Na ndio maana Biblia inasema katika
1 Wakoritho 6: 19 Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? WALA NINYI SI MALI YENU WENYEWE;
20 maana MLINUNULIWA KWA THAMANI. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu”.

Unaona hapo, biblia inasema “SISI SI MALI YETU WENYEWE” ikiwa na maana kwamba ni “sisi tuliozaliwa mara ya pili ni milki ya mtu mwingine” na huyo si mwingine zaidi ya YESU KRISTO, hivyo hatuwezi kujiamulia chochote katika miili yetu, au katika aina ya maisha tunayotaka tuishi, Kwasababu yeye (Yesu Kristo) alitununua kwa thamani, nyingi maandiko yanasema hivyo.


Kwahiyo Bwana anao uhalali wa kutufanya chochote endapo tukijihusisha na mambo yoyote katika maisha yetu au katika miili yetu yatakayomtia wivu, au kumuudhi au kumhuzunisha. Kama bibli inavyosema katika..
1 Wakoritho 3: 16 “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?
17 KAMA MTU AKILIHARIBU HEKALU LA MUNGU, MUNGU ATAMHARIBU MTU HUYO. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi”.

Sasa tukiliharibu hekalu la Mungu yaani miili yetu, Bwana naye atatuharibu, kwahiyo tunapokuwa wakristo sio suala la kujichagulia maisha hapana ni suala la kuchaguliwa maisha na yeye aliyetutolea mahari sisi, Wivu wa Bwana unakuwa kwa wale aliwatolea mahari yaani wale aliowasafisha dhambi zao kwa damu yake, Maovu makubwa yanayomchukiza sio ya watu waliomkataa, hapana bali ni yale ya watu walio wake na bado wanafanya dhambi,(wanakuwa vuguvugu) katika maisha ya kawaida hakuna mwanamume yeyote aonaye wivu akiona mwanamke mwingine asiye wake anafanya uasherati, lakini ataona wivu zaidi endapo akimwona mke wake aliyemtolea mahari na kumwoa anamsaliti na kufanya uasherati. Na ndio maana Bwana baada ya kuwatoa wana wa Israeli Misri aliwapatia amri 10 wao tu! Hakuwapa zile amri kumi watu wote wa ulimwengu mzima, au watu wa Misri. Kwanini? Ni kwasababu Misri hakuwa mke wake halali bali Israeli.


Dada/kaka unayesoma ujumbe huu, kama kweli umeamua kumfuata Bwana na umepita hizo hatua tatu, yaani KUTUBU, na KUBATIZWA KATIKA JINA LA YESU na kupokea ROHO MTAKATIFU. Na bado unajiamulia maisha, nakushauri usifanye hivyo tena, badilisha mtazamo wako, usiwe kama mwanamke mpumbavu aliyeingia kwenye ndoa na asijue mikataba na makubaliano ya hiyo ndoa, kama umeamua kuwa mkristo mwili wako ni hekalu ya Roho Mtakatifu, usilichore tattoo, usifanye uasherati, usiunyweshe pombe, wala usiuvutishe sigara, usiuvalishe nusu uchi, wala usiuvalishe mavazi yasilolipasa ya jinsia nyingine, wala usiufanye usiwe katika hali yake ya asili. Kwasababu mwili huo sio milki yako mwenyewe ni Milki ya mtu mwingine ambaye anaweza kukufanya lolote endapo ukiuharibu na hautapata mtetezi.

Zipo faida leo ukidumu katika uaminifu wako kama bibi-arusi wa Kristo, asiye na hila wala mawaa, kwasababu biblia kama inavyosema katika mbingu mpya na nchi mpya Uje mji mtakatifu wa Mungu yaani YERUSALEMU mpya ushukao kutoka mbinguni ndio bibi-arusi wa Kristo(Ufunuo 21), Mungu atakaa ndani yake, Na katika huo (ambao ndio sisi) Mungu ndio atafanya maskani kumbuka hatafanya maskani kwa kila mtu tu atakayekuwepo huko hapana, bali kwa bibi-arusi tu.. Hivyo tukaze mwendo kama bibi-arusi wa kweli wa Kristo.

Ubarikiwe.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine, na Bwana akubariki.

No comments:

Post a Comment